Dotto C. Rangimoto
JF-Expert Member
- Nov 22, 2012
- 1,985
- 1,286
Assamaleikum!
Wajua baada ya kugundua sina weledi wa kutosha wa kuandika makala hasa za kisiasa, niliashamua siku nyingi sana kuacha kuandika, na badala yake nimekata shauri, fikra na mawazo yangu niwe nayaandika kwa kifupi sana kwa kutumia lugha ya kishairi. Nahisi hilo walau nalimudu.
Hata hivyo, wakati mwingine hujikuta naamua kandika kama nikikuta jambo ambalo nahisi laenda kombo na kisha sioni mtu kwa wakati huo akilitupia jicho. Nami kwa wakati huo huenda sina mistari au nachelea ujumbe kutofika kama ninavyotaraji, basi hapo navunja uamuzi wangu kwa kuamua kuandika japo sina weledi kama nilivyo sema hapo juu.
Katika pitapita zangu katika mitandao nimeona wanachama wa CUF wengi wao wa Zanzibar na wanachama wa CHADEMA wakishabikia kukusimamishwa uanachama kwa wabunge wawili wa CUF, na kwakuwa hawakuwepo kwenye kikao cha baraza kuu kilichofikia uamuz huo, hivyo wakaishia kusimamishwa na si kufukuzwa kabisa. Kwa hali ilivyo, siku yoyote CUF ikiwasikiliza hawa wabunge, basi ndio kufukuzwa kwao na ndio kupoteza ubunge wao.
Ninasikitika sana kwa CUF kufikiria kuwafukuza wanachama ambao wamewadhamini kwa wananchi na kwa NEC. Ninasikitika kwa wanachama na wapenzi wa vyama vya upinzani kushabikia hili, ninasikitika sababu kwa sheria zetu mbunge kupoteza uanachama ndio kupoteza ubunge.
SABABU ZA SIKITIKO LANGU.
Mosi: Kukanyaga msingi mkubwa wa demokrasia.
NCCRA-MAGEUZI, UKAWA, UKUTA, nk yote haya kwa namna moja au nyingine ni matokeo ya watanzania kupigania demokrasia inayo kandamizwa na CCM chini ya mwavuli wa serikali. Demokrasia ni pamoja na kuheshimiwa maamuzi na mamlaka ya umma juu ya nani auwakilishe huo umma katika serikali na bunge.
Wananchi wa Kaliua pamoja na watanzania wengine walimchagua Magufuli ili awe rais wao, yaani aunde serikali kwa niaba yao na serikali hiyo itunze, itumie, na igawanye rasilimali za nchi kwa usawa katika huo umma kwa njia ya huduma za jamii.
Wananchi wa Kaliua walimchagua Sakaya ili awe mwakilishi wao katika bunge. Serikali iliyo undwa na rais walio mchagua watu wa Kaliua na watanzania kwa ujumla lazima ifanye kazi yake kwa utaratibu ambao wananchi hao wanataka.
Kwahivyo mbunge mara baada ya kujua nini watu walio mtuma wanataka, kwa kushirikiana na wabunge wenzake na huku wakizingatia maslahi ya ujumla ya nchi, wanatunga sheria ambazo rais na timu wake wanatakiwa wazifuate wakati wakiwa wakitumia na kugawanya rasilimali za umma.
Demokrasia tunayo ipigania imewapa WANANCHI mamlaka hayo, na kwa wananchi kupewa mamlaka hayo ndio maana Abram Lincoln alisema demokrasia ni serikali ya watu, iliyopata mamlaka kutoka kwa watu kwa faida ya watu hao. Rais Magufuli apoteze urais kisa tu kavuliwa uanchama na CCM huko ni kuwadharau watu walio mchagua na kuikanyaga demokrasia, walau mamlaka hiyo ibaki kwa bunge tu ambalo lenyewe lina wawakilishi wa wananchi.
Alkadhalika kwa mbunge, diwani na mwenyekiti wa mtaa, kijiji na kitongoji, ni kukanyaga demokrasia kwa viongozi hawa kupoteza nyadhifa zao kisa tu wamevuliwa uanachama kwa vyama vyao.
Pili. Kuishi kivitendo.
Mimi nadhani vyama vyote vya upinzani isipokuwa ACT na chama tawala havijui sababu za uwepo wao au vimeacha kufuata sababu za uanzishwaji wao. Ndio maana Prof Kitila alisema nchi inahitaji chama mbadala wa CHADEMA(kama chama kikuu cha upinzani) na CCM(kama chama tawala). Kwa vyovyote vile alimaanisha nchi inahitaji mbadala wa CHADEMA utakao kwenda kuwa mbadala wa CCM kwa kushinda uchaguzi katika ngazi yoyote.
CCM yenyewe inadhani lengo la kuundwa kwake ni kuongoza nchi na kubaki madarakani, ndio maana iko radhi kufanya lolote(hata kwa goli la mkono) kubaki madarakani. Tunataka chama dola kinachojua kimeundwa si kuwa chama dola bali kimeundwa kwaajili ya kuwaridhisha wananchi, na ya kwamba wenye nchi wasiporidhika wanaweza kukiadhibu kwa kukitoa madarakani.
Vyama vyote vya upinzani na wanachama wao wanadhani wako pale kuchukua dola, yaani kuitoa CCM madarakani. Na kwa kujipa jukumu hili, ndio maana wanatumia nguvu kubwa na fedha nyingi na hila za rangi mbalimbali kuitoa CCM madarakani huku watanzania wakizidi kutaabika kwa hali mbaya ya maisha na uduni wa huduma za kijamii.
Vyama vya siasa vinatakiwa kujipa jukumu la kuhakikisha hali ya maisha ya wananchi inakuwa bora, watekeleze jukumu hilo wakati wakitafuta dola na baada ya kupata dola, na vifanye hivyo katika ngazi ya mtaa na kitongoji ambapo ndipo walipo watanzania na wapiga kura.
Mathalani, mtaani kuna makaravati yameziba maji ya mvua yanapoteza uelekeo, kuna vichaka au maboma yenye vichaka ambavyo vinaweza kutumika kama maficho ya wahalifu, kuna baadhi ya njia muhimu kwa mtaa au kijiji hazipitiki au hakuna kabisa njia. Watoto wetu watoro shuleni lakini mtaani kuna banda la video au pool table ambapo watoto wetu wanashida hapo, mtaani kuna vijiwe vya wacheza kamari na wavuta bangi, nk
Hali ikiwa hivyo mtaani au kijijini, katika kijiji hicho au mtaa, tuna uongozi wa BAVICHA, NGOME YA VIJANA ACT na JUMUIYA YA VIJANA YA CUF, zote ngazi ya kijiji au mtaa.
Hawa ni vijana wa namna gani wanashindwa kutenga siku katika mwezi kwaajili ya kushughulikia matatizo hayo. Kwanini vijana hawa wasishinikize uongozi wa mtaa uitishe mkutano mkuu wa dharula wa mtaa ili upitishe azimio la kufunga mabanda ya video na pool table nyakati za masomo na kazi? Kwani kufanya haya yanahitaji uwe na serikali? Au hawa ni vijana hewa?
Lengo si kuwatoa katika mada yangu, lengo ni kuwatanabaisha kuwa tunaweza kufanya mabadiliko bila kuingia ikulu, na mabadiliko hayo ndio turufu ya kuingia ikulu lakini mbwembwe zote za kampeni na mambo ya kufananayo ni garasa tu ambalo halafui dafu kwa turufu.
Tuje, kwenye demokrasia huku ukizingatia mifano yangu hiyo ya uwajibikaji wa ngazi ya mtaa na kijiji kwa jumuiya zetu za chama. Vyama upinzani vinataka serikali na CCM iheshimu demokrasia, hata rasimu ya Warioba wanayo itetea wapinzani ni kwasababu rasimu hiyo imetambua misingi ya kidemokrasia. La kushangaza vyama vyetu vinapigania hilo huku venyewe vikikanyaga demokrasia tena mchana wa jua la utosi.
Baada ya Mh Sakaya kusimamishwa uanachama, na baada ya kujulikana kutokusikilizwa ndio sababu pekee iliyo mfanya aendelee kuwa mwanachama, ndugu Zitto alisema japo kwa lugha ya mafumbo kuwa CUF inadai demokrasia lakini yenyewe inaikanyaga hiyo demokrasia.
Demokrasia ambayo Zitto alisema CUF inaikanyaga si ile iliyotumika kumsimamisha uanachama Sakaya, bali ni ile ya kuingilia mamlaka ya wananchi ya kuchagua kiongozi wanaye mtaka. Ikumbukwe Tanzania hatuchagui chama bali tunachagua mtu, hata kama shuruti huyo mtu atokane na chama. Mtu hawi mbunge kwa kura za wanachama wa chama chake tu!
Ingekuwa tunachagua chama kusingekuwa na haja kwa chama kuweka wagombea, badala yake tungechagua nembo za chama katika karatasi za kupigia kura, kisha chama kilichoshinda kwa kupitia utaratibu wao wa ndani ya chama watupatie kiongozi kwa jimbo waliloshinda, na rais kama chama hicho kimechaguliwa kutoa rais.
Kwakuwa mbunge akipoteza uanchama ndio amepoteza ubunge, na kwakuwa utaratibu huu unaingilia mamlaka ya wananchi, na kwakuwa CUF kupitia rasimu ya Warioba walipinga na wanaendelea kupinga utaratibu huu, hivyo basi CUF na vyama vyote vya upinzani vinavyo amini juu ya rasimu ya Warioba havitakiwi hata kidogo kumfukuza mwanachama wao ambaye ni kiongozi wa kuchaguliwa na wananchi. Wanachotakiwa ni kumvua vyeo vyake vyote isipokuwa uanachama wake tu.
Wakifanya hivi kutakuwa na faida zifuatazo.
1. Jambo kubwa chama kitakuwa kimewaheshimu wapiga kura na wananchi. Kuna dhana kuwa chama kikimvua uanachama kiongozi mwenye matatizo chama hicho kitaonekana kina uthubutu wa kuwashughulikia wanachama wake bila kujali nyadhifa zao, na hivyo chama kupata HESHIMA.
Mimi nawaambia, mbunge anaweza kushughulikiwa na chama chake na wananchi wakajua kuwa mbunge wao kashughulikiwa na chama chake bila hata ya mbunge huo kuvuliwa uanachama. Mafano, chama kinaweza kumuondoa mbunge huyo kuwa mjumbe wa kokasi ya chama hicho, kama ana vyeo vya chama kuvuliwa vyeo vyake vyote, wanaweza kumpiga marufuku kufanya kazi za chama jimboni, nk Yanaweza kufanyika haya na chama kupata heshima yake inayostahili na wananchi kuendelea kuwakilishwa na mtu waliye mchagua.
2. Mbunge aliyetengwa na chama, kwa kipindi chote alichotengwa anapata muda mzuri zaidi wa kutafakari vitendo vyake na hasara alizopata au anazopata baada ya kutengwa. Jambo hili linaweza kumrudisha katika mstari huenda hata kabla ya uchaguzi unao fuata.
Lakini pia chama kinapata nafasi nzuri ya kuzidi kujitafakari kwa uamuzi unaotaka kuuchukua kwa mwanachama wake. Wakati mwingine fukuzafukuza hutawaliwa na hasira zaidi kuliko busara, lakini siku zikienda na hasira hupungua, na kwa kupungua chama kinaweza kuona makosa yake au kinaweza kuona mbunge wao amerudi katika mstari, na hivyo basi kumsamehe na mambo yakesha!
3. Chama kinakuwa kimetekeleza kwa vitendo yale inayo yaamini na kuyapigania. Sababu ni ajabu sana kwa CUF kulalamika kuwa Jecha kaingilia mamlaka ya wananchi kwa kitendo chake cha kuvuruga uchaguzi wa Oct 2015 lakini CUF hiyohiyo inafanya kitendo ambacho athari zake ni pamoja na kupoteza ubunge kwa mbunge aliyechaguliwa kihalali na wananchi wa jimbo la Kaliua. Hivi kwa kitendo hichi, Maalim Seif na Jecha tafauti yao ipi hasa?
4. Wananchi wataona kwamba chama kinaanza kutekeleza mambo inayo yaamini na kuyapigania kabla hata chama hicho kwenda ikulu, jambo hili litaleta imani kubwa sana kwa wananchi kwa chama husika.
Mathalani CHADEMA ina sera ya serikali kupunguza matumizi kwa kuachana na anasa zisizo lazima. Hivi kwa mfano, wabunge wote wa CHADEMA katika bunge lilopita katika kutekeleza sera hii kivitendo, wangekataa posho kwa kuzielekeza hizo posho kwenye miradi ya maendeleo katika majimbo yao, hivi unafikiri jambo hilo lingetuma ujumbe gani kwa watanzania?
Badala ya kutekeleza hilo, tukaona sinema ya vituko ya Mbowe pale mchana alipokataa gari la serikali alilopewa kama KUB, na kisha usiku akenda kulichukua kama kigagula. Mbaya zaidi wabunge hawa wa CHADEMA tukaona wakipanga foleni za kutetea posho za makalio na huku Lema akisema posho hazitoshi na ya kwamba uzalendo sio umaskini.
Jambo baya kabisa wabunge hawa wapinzani walianza kumsumbua na kumsakama mbunge pekee aliyekuwa anapinga na kukataa kupokea posho kivitendo.
La haula, kumbe wenzetu wanataka kutajirika na si kutupigania? Huu ndio ujumbe uliokwenda kwa watanzania na hii ndio moja ya sababu ya KUSHINDWA KWA CHADEMA. Chama hiki kimeshindwa kuyaishi yale inayo yapigania na kuyaamini.
CUF ifanye uhuni huu wa kutoyaishi inayo yaamini, alafu utakuja kuona kuporomoka kwa CUF, kitu pekee kitakacho wabeba ni vile vinasaba vya siasa za mwaka 1963, na vinasaba ambavyo huku bara havipo, na kwakuwa havipo huu uhuni ndio mwanzo wa mwisho wa CUF bara.
5. Wananchi watajiona kweli wao ndio wenye mamlaka ya kuuweka na kuutoa uongozi madarakani. Wananchi wataona hivyo endapo wakiambiwa kuwa kwa makosa aloyafanya mbunge wao ilibidi afukuzwe chama kabisa, lakini kwa kujua kuwa kumfukuza chama ndio kumvua ubunge inabidi aachiwe uanachama wake.
Vyama hivi katika majukwaa vinasema umma ndio una mamlaka ya kuuweka na kuutoa uongozi madarakani, hivi watanzania wataamini vipi kama wanamamlaka ya kuitoa CCM madarakani ikiwa wanaona mbunge aliyechaguliwa kwa kura 30,000 anatolewa bungeni kwa kikao cha kamati kuu chenye wajumbe 30 au baraza kuu lenye wajumbe 300? Ndio maana wapo watanzania ambao hawataki kabisa kupiga kura kwa kudhani kura yao haina mamlaka ta kuuweka au kuutoa UONGOZI.
MWISHO.
Kishindo jana nilipata kusema wanachama wa chadema ni mbumbumbu, lakini leo niseme wanachama wa CUF zenji ni mbumbumbu, sababu wako tayari kuingia barabarani kupinga serikali kukanyaga demokrasia, lakini wakiwa ndani ya chama chao wanampigia makofi Sultani anaye kanyaga demokrasia na kudharau wananchi walio tumia haki yao ya kidemokrasia kuchagua mbunge wao, huku wananchi hao wengi wao si wanachama wa CUF bali wa vyama vingine au hawana chama kabisa!
Kwanini watu ambao sio CUF waathirike au waumie kwa maamuzi ya CUF? hii ndio demokrasia tunayo ipigania? Hii ndio "HAKI SAWA KWA WOTE?
Nikipata wasaa nitakuja kuwaelezea ACT tunavyofanya katika kuyaishi yale tunayo yaamini. Sababu naamini kila chama huku kikizingatia itikadi na falsafa yake, kikiyaishi inayo yaamini, wanachama wao na watanzania kwa ujumla tutafaidika na huu utitiri wa vyama vya siasa ambavyo tunavyo.
Dotto Chamchua Rangimoto(Njano5)
Call/whatspp 0622845394 Morogoro.