........Naye Meya Lyimo, alipoulizwa kuhusiana na uteuzi wa kumpata Naibu Meya wa Chadema Estomiah Mallah, alisema kuwa uteuzi ulifuata sheria na taratibu zote za vikao halali vya halmashauri, alisema mazungumzo yao yalikuwa yanaendelea kwa miezi miwili na mwafaka ulifikiwa baadaye na maamuzi ya kikao kilichosimamiwa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Raymond Mushi.
Meya Lyimo alisema baada ya kikao hicho kila upande ulipeleka taarifa katika chama chao.
"Kura katika kikao hicho zilipigwa na wajumbe walikuwa 25 na kati ya hizo kura tatu ziliharibika na kura moja ilisema hapana, hivyo tukamwapisha na sasa wanaendelea na vikao vya kamati mbalimbali, mfano leo (jana) tupo katika kikao cha kamati ya mipango miji," alisema Lyimo.
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Estomiah Chang'ah, alisema hakuna tararibu zilizokiukwa na walifuata taratibu zote za halmashauri za uchaguzi na kwamba anayo barua ya Chadema ya kumteua kuwa diwani wake kuwa naibu meya.
Naye Naibu Meya wa Chadema, Estomiah Mallah, alisema hatajiuzulu.
"Mimi siwezi kujiuzulu kwa sababu ni naibu meya halali na nimepita kwa kufuata taratibu zote na kanuni za halmashauri na siwezi kumsikiliza mtu mmoja anayeibuka na kunikataa," alisema.
Chini ya makubaliano, Chadema kitashika wadhifa wa unaibu meya hadi mwaka 2014 na TLP litashika nafasi hiyo hadi 2015 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo.
Mbali na kuwekeana vipindi vya kushika unaibu meya, nafasi za wenyeviti wa kamati za baraza la madiwani pia zimegawanywa.
Kamati ya Uchumi, Elimu na Afya itaongozwa na diwani wa Chadema; kamati ya Fedha na Utawala ikiwa na wajumbe tisa, wanne kutoka Chadema na mmoja wa TLP, huku CCM ikiwa na wajumbe wanne tu, itakuwa chini ya Meya (CCM) na kamati ya Mipango Miji na Mazingira itaongozwa na diwani wa CCM.
Taarifa za mwafaka huo ziliwekwa hadharani Juni 20, mwaka huu katika mkutano wa Baraza la Madiwani wa Jiji la Arusha ukihusisha madiwani wote wa CCM, Chadema na TLP.
Mgogoro wa umeya uliibuka Disemba mwaka jana na kuzua uhasama kati ya CCM na Chadema kutokana na uchaguzi uliomweka madarakani Meya Lyimo kudaiwa kujaa utata.
Mwenyekiti wa vikao hivyo, Michael Kivuyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Sokoni One kwa tiketi ya TLP, wiki iliyopita alikiambia kikao maalum cha Baraza hilo kuwa mgogoro wa kutomtambua Meya Lyimo, umemalizika baada ya vikao vilivyokuwa vimefanyika mfululizo kwa kipindi hicho.
Alisema katika vikao hivyo, vyama vitatu vya CCM, Chadema na TLP vilikuwa vikitafuta suluhu kuhusu mgogoro huo na sasa wamefanikiwa.
Wiki iliyopita akiwa mjini Dodoma Lema alipotakiwa na NIPASHE kuzungumzia habari za mwafaka huo alisema kwa njia ya simu alikuwa hajapata taarifa ya maamuzi ya kikao hicho, lakini anawaamini waliokuwa katika kamati ya usuluhisi.....
SOURCE: IPP MEDIA.