CCM yatoa msisitizo na maelekezo kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi

SautiYaMnyonge

JF-Expert Member
May 13, 2018
439
742
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MSISITIZO NA MAELEKEZO YA CHAMA KWA SERIKALI KATIKA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI

SEKTA YA MIFUGO

Chama Cha Mapinduzi CCM kimetoa pongezi kwa Wizara ya kilimo na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitisha makadirio na matumizi ya Wizara hiyo kwa ufanisi, maboresho na ustadi wa hali ya juu huku ikizingatia mahitaji ya wananchi kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 - 2025.

Aidha Chama Cha Mapinduzi kinaipongeza Wizara ya Kilimo kwa utekelezaji mzuri wa maelekezo ya Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo aliyo yatoa tarehe 20/05/2021 Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo alitoa maelekezo kwa Wizara ya Kilimo, Wizara ya ardhi, Wizara ya Nishati wakaizingatie Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025. Wakati wa kuwasilisha bajeti ya Serikali na mpango wa Taifa wa maendeleo wa miaka mitano kwa mwaka wa fedha 2021- 2022 Chama Cha Mapinduzi kimetoa maelekezo na msisitizo kwa Serikali katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi Ili kuleta mabadiliko makubwa na ya kisayansi katika Ufugaji, CCM kupitia Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020-2025, CCM inailekeza serikali kuhakikisha shughuli za ufugaji nchini zinakuwa za kisasa na kibiashara, zenye kuzingatia kinga, tiba na utafiti wa mifugo ili kuzalisha ajira nyingi zaidi hasa kwa vijana na kuinua mchango wa sekta katika pato la Taifa na kuleta ustawi wa wananchi.

Aidha chama kinailekeza Serikali kushughulikia kwa kasi zaidi, migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi ili kupata ufufumbuzi. Hivyo CCM imeelekeza Serikali katika bajeti hii ya mwaka 2021/2022, kujikita katika kuboresha maeneo yenye matokeo chanya kama ifuatavyo.

1. SHUGHULI ZA UGANI NA UTAFITI

I. Chama kimeelekeza Serikali katika bajeti hii, kuhakikisha kunakuwepo na maafisa ugani angalau kila kata na kijiji na kuwezeshwa usafiri wa magari au pikipiki zitakazowezesha kuwafikia wafugaji kirahisi zaidi na kuongeza tija zaidi.

II. Chama kimeelekeza serikali uanziashwaji wa mashamba darasa ya mifugo katika Halmashauri mbalimbali nchini ili wafugaji wajifunze ufugaji wa kisasa na kibiashara kwa vitendo. Aidha ili kwenda sambamba na maendeleo ya sayansi na teknolojia Serikali inaelekezwa kuandaa mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya uratibu wa utoaji wa huduma za ugani nchini.


III. Chama kimeelekeza Serikali kuviwezesha vituo vyote vya utafiti nchini kama vile Taasisi ya utafiti wa mifugo (TALIRI) na Wakala wa Maabara ya Vetenari (TVLA) ili kufanya kazi zao za utafiti na kuhakikisha tafiti hizo zinafanywa kwa kufuata ajenda ya kitaifa ya utifiti wa mifugo na kanuni zake. Pia kuhakikisha tafiti hizo zinawanufaisha wafugaji, wadau wa mifugo na Taifa kwa ujumla.

2. UZALISHAJI WA MIFUGO NA MASOKO

I. Ili kuwa na maziwa na nyama bora ya kutosha, kukidhi soko la ndani na nje, ufugaji wa kisasa na wakibiashara ni Muhimu. Hivyo basi, Chama kimeelekeza Serikali katika bajeti hii, Kuimarisha vituo vyote vya uhimilishaji nchini kufikia angalau ng’ombe Milioni moja 1,000,000. Aidha Chama kinaielekeza Serikali kuhakikisha, inawajengea uwezo wahimilishaji katika Halmashauri zote nchini ili kuwarahisishia wafugaji kupata huduma hii kwa urahisi.

II. Sambamba na uhimilishaji, Chama kinaielekeza Serikali kununua mitamba bora angalau 500 kwa ajili ya mashamba ya kuzalisha mifugo ya serikali ili kuboresha uzalishaji wa mitamba katika mashamba hayo. Pia Chama kimeelekeza Serikali, katika mwaka huu wa fedha, itoe mitamba angalau 2000 kutoka kwenye mashamba ya serikali kwenda kwa wafugaji kwa bei ya ruzuku bila upendeleo. Hatua hii itasaidia kuongeza fursa ya upatikanaji wa mitamba bora kwa wafugaji wetu nchini.

III. Kutokana na changamoto kubwa ya upatikanaji wa vifaranga bora vya kuku nchini ambavyo vinaathiri ubora wa kuku na mayai, Chama kimeelekeza Serikali kupitia taasisi ya Mifugo ya TALIRI iendeleze tafiti za uzalishaji wa kuku wa kienyeji. Hatua hii itasaidia kuondokana na utegemezi wa mbegu bora za kuku kutoka nje ya nchi na kuongeza kiwango cha uzito kwa kuku na utagaji wa mayai.

3. BIASHARA YA MIFUGO NA MAZAO YAKE

I. Nchi yetu imebarikiwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo Afrika ikiwemo Ng’ombe, Mbuzi, Kondoo, Kuku n.k, hivyo Kutokana na uhitaji mkubwa wa kuwa na soko la ndani na nje kwa mazao yatokanayo na mifugo, Chama kimeelekeza serikali, kujenga na kukarabati minada ya mifugo ya upili kama vile Weruweru-Kilimanjaro, Bariadi-Simiyu, Kishapu-Shinyanga, Pugu-Dar es salaam, pamoja na kujenga minada ya kimkakati mipakakani ikiwemo mipaka ya Namanga, Misenyi, Loliondo na Sirari. Hatua hii itasaidia kuongeza pato la taifa, kipato kwa wafugaji na kuzalisha ajira.

II. Chama kimepokea malalamiko kutoka kwa wadau wa biashara ya mifugo kuhusu changamoto za biashara ya mifugo nje ya nchi. Hivyo, Ili kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na kuongeza mauzo ya mazao ya mifugo, Chama kimeelekza serikali kufanya mapitio ya ada na tozo mbalimbli hususani tozo ya thamani ya mizigo (FOB value) na kuondoa tozo zisizo za lazima kwa nyama zinazouzwa nje ya nchi na ada ya ukaguzi wa mifugo. Hatua hii itachochea biashara ya uuzaji wa mazao yao ya mifugo bila usumbufu na kwa tija.

III. Ili kuongeza ubora na thamani ya mazao ya mifugo hususani ngozi, Chama kimeelekeza serikali kuhakikisha ngozi zote zinachakatwa na kupangwa katika madaraja stahiki kabla ya kuuzwa.

IV. Kutokana na kuwepo kwa mifugo ya kutosha nchini (malighafi ya ngozi), Chama kimeelekeza Serikali, kuhakikisha inaongeza uwekezaji wa ujenzi wa viwanda vikubwa vya bidhaa za ngozi kutoka vitano vilivypo sasa, mpaka kumi (5-10) unatiliwa mkazo ili bidhaa kama vile viatu, mikanda, mikoba n.k viendelee kuzalishwa nchini, ili kukidhi soko la ndani, kuongeza ajira na kipato kwa wafugaji.

V. Chama kimepokea malalamiko mengi yahusuyo sheria ya biashara ya ngozi nchini, hivyo Chama kimeelekeza Serikali kufanya mapitio ya sheria na kanuni zinazohusu biashara ya ngozi ili kuleta tija katika biashara hiyo na kupunguza malalamiko ya wafugaji na wadau wengine wa biashara hiyo.

VI. Kutokana na kukua kwa biashara ya nyama nchini na ili kukidhi ushindani wa soko la nje, Chama Cha Mapinduzi, Kimeelekeza serikali kuhakikisha inaboresha na kuimarisha machinjio yote nchini yakiwemo machinjio makubwa ya Dodoma na Vingunguti-Dar es salaam na machinjio ya kati na madogo kama vile Tanganyika packers za Shinyanga na Mbeya, machinjio ya Halmashauri za Manispaa ya Iringa na Mbeya, Kigamboni, na Ruvu-Pwani, na maeneo mengineyo nchini.

VII. Kutokana na uhitaji mkubwa wa maeneo ya kuogeshea mifugo kwa wafugaji wengi nchini, Chama Chama Mapinduzi kimeelekeza serikali kujenga na kukamilisha majosho ya Njombe DC, Kisarawe-Pwani, Musoma-Mara, Geita Tc, Igunga-Tabora, Uyui-Tabora, Simanjiro-Manyara, Uvinza-Kigoma na Mpwapwa-Dodoma

VIII. Ili kuongeza mapato yatokanayo na uuzaji wa nyama ndani na nje ya nchi, Chama kimeelekeza serikali kuhakikisha Kampuni ya NARCO inaendelea kuongeza uzalishaji wa ng’ombe bora wa nyama katika ranchi za Kongwa, Ruvu n.k ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi, na ranchi hizo ziwe mfano kwa wafugaji wa pembezoni mwa ranchi hizo.

4. MALISHO NA MAJI

I. Zipo Changamoto za malisho na maji kwa ajili ya mifugo maeneo mbalimbali nchini, hivyo Chama kimeelekeza Serikali kushirikiana na mamlaka za Serikali za Mitaa, kutenga maeneo kwa ajili ya malisho, kuimarisha/kujenga miundombinu ya maji kama malambo na visima virefu katika maeneo yenye ukame na uhitaji mkubwa wa maji kama vile Dodoma, Singida, Manyara, Shinyanga, Tabora na Arusha.

5. MIGOGORO BAINA YA WAFUGAJI NA WATUMIAJI WENGINE WA ARDHI

I. Kutokana na kuwepo kwa migogoro mingi naya muda mrefu, baina ya Wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi kama vile wakulima na hifadhi katika maeneo ya Kiteto na Simanjiro-Mnyara, Kilindi-Tanga, Kilosa, Mvumero na Kilombero-Morogoro, Kondoa naKongwa-Dodoma, Ngorongoro-Arusha na Serengeti na Tarime-Mara, Hivyo Chama Cha Mapinduzi kimeelekeza Serikali kuhakikisha inapatia ufumbuzi wa kudumu migogoro kwa kuzingatia haki na maslahi ya pande zote.

SEKTA YA UVUVI

Sekta ya uvuvi inayo nafasi kubwa katika kuchangia pato la taifa, kukuza ajira, kukuza ustawi wa watu na utoshelevu wa mahitaji ya samaki nchini. Hata hivyo mchango wa sekta hii katika maeneo tajwa hapo juu bado umekuwa ni wa kusuasua. Hivyo kupitia Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020-2025 fungu la 43, Chama kimeelekeza serikali katika bajeti ya mwaka 2021/2022 kufanya yafuatayo.

1. KUJENGA MIUNDOMBINU YA UVUVI

I. Chama Cha Mapinduzi, Kimeelekeza Serikali kuanza mipango ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi katika ukanda wa Pwani, bandari hii itawezesha meli za uvuvi kutia nanga ili kufaulisha na kuuza samaki, ukamilishaji wa Bandari hii utazalishaji ajira zaidi 30 elfu na kipato kwa wananchi.

II. Chama kimeelekeza serikali, kuanzisha ujenzi wa vituo vipya vya ukazaji viumbe maji katika mikoa ya mwambao wa bahari ya Hindi kama vile Tanga, Dar es salaam, Lindi na Mtwara, hatua hii itaimarisha ufugaji wa samaki, kambamiti, Kaa,chaza wa lulu, majongoo bahari na kilimo cha mwani. Pia chama kimeelekeza serikali ikarabati na kupanua vituo vya kuongeza uzalishaji wa vifaranga vya samaki katika maeneo ya, Nyengendi-Lindi, Ruhila-Ruvuma, Kingorwira-Morogoro, Mwamapuli-Tabora na Rubambagwe-Geita.

2. ELIMU NA MAFUNZO KWA WAVUVI

I. Kutokana na changamoto ya uvuvi haramu unaoathiri uendelevu wa rasilimali ya mazao ya bahari,maziwa,mabwawa na mito na malalamiko ya wavuvi kwa serikali kutumia nguvu kupita kiasi katika kukabiliana na suala hili, ikiwemo kuwapiga wavuvi, kuharibu zana za uvuvi, kama vile vyavu, mitumbwi n.k Chama kimeelekeza serikali kuhakikisha upatikanaji wa zana bora za uvuvi kwa wingi na kwa gharama nafuu, kutoa elimu na mafunzo ya matumizi ya zana bora za uvuvi. Hatua hii itasaidia uvuvi kuwa endelevu na wenye tija kwa vizazi vya sasa na vijavyo na kupunguza malalamiko ya wavuvi.

ANGALIZO.

Katika mwaka huu wa fedha Bajeti kwa ajili ya Ufugaji na Uvuvi, hasa katika ya Sekta ya Uvuvi imetengewa bajeti ndogo sana ya shilingi Bilioni 62,550,000,000 fedha za ndani kwa ajili miradi ya maendeleo, licha ya kuwa fedha imeongezwa toafauti na mwaka wa fedha wa 2020/2021 ingawa mwaka huo ni 35% tu sawa na shilingi bilioni 4.6 tu kutoka bilioni 13.1 ya bajeti ya maendeleo. Hivyo kwa mwaka huu Hakuna miradi mikubwa ya maana iliyotengewa fedha, mathalani

I. Hakuna fedha wala mipango kwa ajili bandari ya uvuvi kama iliainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020 – 2025 Fungu la 43 (a)

II. Uimarishaji wa miundombinu ya uvuvi kwa kujenga mialo katika maziwa ya Viktoria, Tanganyika na Nyasa Chama Cha Mapinduzi kimeshauri bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi hasa katika Sekta ya Uvuvi iangaliwe upya kwa sababu hakuna vipaumbele vinavyomgusa mvuvi moja kwa moja. Kama ilivyoeelekeza katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020 -2025

Shaka Hamdu Shaka
KATIBU WA H/KUU YA TAIFA UENEZI
DAR ES SAALAM.
26/05/2021


IMG-20210520-WA0021.jpg
 
Back
Top Bottom