CCM ya JANA na ya LEO

Mzee wa Gumzo

Senior Member
Apr 21, 2008
197
5
Wanajukwaa,
Nimeona ni wakati muafaka kuwapa nafasi ya kusoma na kutoa maoni yenu juu ya mtizamo huu wa mtanzania mwenzetu kuhusu mustakabali wa taifa hili lenye umri wa miaka 47 ya kujitawala na raia wapatao zaidi ya milioni 36.
**********************************
Wengi wetu tumekulia katika mazingira ya chama kimoja. Tulifundishwa na
kuaminishwa itikadi ya CCM. Nikiri kwamba mimi ni muumini sana wa itakadi za
TANU/CCM. Siifahamu iliyokuwa itakadi ya ASP. Ninavyoifahamu CCM ni chama chenye
itakadi murua, inawezekana kupita vyama vyote barani Africa, uongozi imara na
inayoamini kwenye umoja wa Tanzania na Afrika kwa ujumla. Nasema ‘probably’
CCM ndicho chama imara zaidi barani Africa kutokana na kuweza kujenga umoja na
upendo kwa wananchi wake. Nakumbuka juzi nilisikiliza hotuba ya mwalimu katika
kipindi cha wosia wa baba akiwa anahutubia kikao cha UWT, aliuliza:
“Nionyesheni nchi yeyote Afrika yenye amani, upendo na umoja kama
Tanzania?”. Jibu lilikuwa hakuna. Aliendelea kusema Tanzania tunaweza tukawa
maskini wa mali lakini kwa upande wa amani, umoja, kuvumiliana na kuheshimiana
hakuna kama Tanzania.

Hicho ndicho chama changu, CCM. Chama kilichokuwa hakina uvumilivu kuhusu
rushwa. Chama kilichokuwa haki ‘compromise’ kuhusu mambo ya nchi. Nakumbuka
hata Mh. Jumbe alipothubutu kuhatarisha umoja wa nchi aliombwa kama alivyoombwa
Tabu Mbeki ajiuzulu. Hiyo ndio CCM.

Leo najiuliza, hivi kile chama changu ndicho hiki au limebaki jina tu? Napata
wasiwasi kuwa hiki si kile chama changu. Nahisi kama chama kimetekwa na mbwa
mwitu waliokusudia kuwala wanakondoo. Yafuatayo yananifanya nikione chama changu
kama si kile nilichokiamini na kama vile kuna “leadership crisis”.

(ii) Kifo cha Wangwe na Kampeni za Tarime. Msiba wa Wangwe ulipokelewa kwa
hisia tofauti. Wengine waliamini ameuawa na CHADEMA. Kwa vile kiongozi mkuu wa
CHADEMA ni Mchagga na anayetuhumiwa pia kuuwa ni Mchagga basi baadhi ya magazeti
yakaandika “ Wachagga washambuliwa Tarime”. Kukawa na kampeni chafu na
uchochezi wa kutisha. Baadae familia ya marehemu wakatoa taarifa ya daktari
waliemwamini, kifo cha Wangwe kilisababishwa na ajali. Mimi nikadhani yaliisha.
Kampeni ya kiti cha ubunge Tarime ikaanza. CCM ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti
Mzee Msekwa, katibu mkuu na baadhi ya Mawaziri wakampa jukwaa ndugu yake Wangwe
nao wakiwa wamekaa wakimsikiliza. Wangwe aliuawa na CHADEMA, angalia Mwenyekiti
wake mchagga, mtuhumiwa mchagga. Wakuu hawa wa chama wakamshangilia, anawasaidia
kupata kura. Nikajiuliza. Hivi chama changu hiki kina wabunge wangapi? Hivi
kinahitaji kujenga chuki za ukabila na kichama, damu imwagike, amani itoweke ili
mradi tu tupate kiti cha
ubunge? Hiki si chama changu . Chama kinaongozwa na watu wanaomiliki hadi
funguo za mbinguni, wakimfungia mtu duniani hata mbinguni amefungiwa? Hii si ile
CCM yangu. Kama kweli Wangwe aliuawa, kwanini sheria isichukue mkondo wake?
Kwanini Mbowe asikamatwe?

Mwandishi mmoja alimuuliza Mwalimu Nyerere kama angeulizwa angetoa ushauri gani
kuhusu kudumisha amani iliyopo. Alijibu: Amani ni sawa na mti. Ukiumwagilia maji
na kuweka mbolea utastawi. Ukiunyima maji na mbolea utanyauka. Sioni kama hawa
wanaochochea chuki huku wakishangiliwa na viongozi wakuu wa chama wanaweka
mbolea na maji kwenye huu mti.

(ii) EPA. Swala la EPA limezungumzwa sana. Lakini tunaweza kusema tu kwamba
Rais ameshindwa kuilinda katiba aliyoapa kuilinda na kuitetea. Watu wote ni sawa
mbele ya sheria. Iweje wahalifu wabembelezwe? Jibu ni kuwa tukiwakamata fedha
zetu zitapotea. Hivi ni kwanini tulimkamata kasusura? Kwanini tulimkamata Prof
Mahalu? Wezi wa mabenki, na wahalifu wengine? Kwanini tusingewapa muda
wakarudisha fedha walizotuibia? Nikisema Tanzania hatufuati utawala wa sheria
nitakuwa nakosea? Nijuavyo mimi Rais anaweza kumsamehe au kumpunguzia adhabu mtu
aliyehukumiwa na mahakama na si mtuhumiwa? Mamlaka ya kujadiliana na wahalifu
ameyapata wapi? Nadhani historia itatuhukumu. Hiki si kile chama changu.

(iii)Sakata la Zanzibar si chi. Nani asiyejua Tanganyika ilizikwa mwaka 1964?
Hivi Rais anapotuambia leo ndani ya Tanzania kuna nchi inaitwa Tanganyika
tumwelewe vipi? Kuna mtu anaweza kunionyesha neno “Tanganyika ‘ ndani ya
katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977? Rais anaogopa kuitetea na
kuilinda katiba ya nchi aliyoapa kuilinda na kuitetea. Hiki si kile chama
changu.

Kuna mengi yanayoweza kusemwa lakini nathubutu kusema nchi kwa sasa ina tatizo
la uongozi. Najiuliza, akina Kingunge, Warioba, Msekwa, Kawawa na wengine wengi
waliokuwa wanafunzi watiifu wa Mwalimu wako wapi? Hivi wako tayari kuona
watanzania tunachinjana Tarime kwa ajili ya kiti cha ubunge? Wako tayari kuwaona
watanzania wakigawanywa kwenye makundi ya wanyonge na wakubwa? Mkubwa aliyekomba
mabilioni anabembelezwa, aliyedai rushwa ya shilingi elfu 15 amesekwa miaka kumi
gerezani. Sijui nini kimewasibu!. Hiki si kile chama changu

Watanzania tupo wapi? Nadhani tunalojukumu. Nchi inapokosa umakini katika
uongozi lazima tuzungumze, tutoe maramko hata kama hatutasikilizwa tubaki kwenye
record. Na ili kufanikisha hili tusiwe washabiki wa siasa. Tufikiri, tutafute
ukweli na tuuseme ukweli. Nchi ikiyumba sisi tutalaumiwa zaidi. Hapa ndipo
nauona umuhimu wa Mwalimu. Ni kama baba aliyekufa akawaacha watoto wake . Watoto
hawajui wafanyeje, hawana wa kuwaongoza tena. Kabla ya kifo chake alitamka: “
Bila ya CCM imara nchi itayumba”. Maskini Tanzania, maskini CCM, chama changu
nilichokipenda sana.
 
Back
Top Bottom