Wapendwa wanajamvi salaam kwenu,
Nimekuwa nikitatizwa sana na sera ambazo serikali imekuwa ikizitekeleza bila mpangilio maalumu. Kwa muda kidogo ilikuja na mpango wa kurejesha programu ya kupeleka wahitimu wa kidato cha sita kupata mafunzo ya JKT. Tatizo hasa linalonitatiza ni kile ambacho kimekuwa kikitolewa kama sababu ya kurudisha programu hiyo. Yamekuwepo masuala mbalimbali ambayo yamepelekea na kusababisha serikali ianzishe tena programu hii. Nadharia zipo nyingi sana lakini hizi mbili zimepata kuwa maarufu; kurejesha uzalendo kwa nchi na vijana wa sasa ni legelege hivyo tunahitaji kuwafanya kuwa wakakamavu.
Nitajadili nadharia mojamoja na wale ambao wana hoja madhubuti pamoja nao wale ambao ni wazamani kidogo enzi zile za program kama hii ilipokuwapo watasaidia kuniweka sahihi maana mi bado kijana mdogo ndo kwanza nimemaliza form six.
Nadharia ya uzalendo; Inashangaza kuona watu wenye akili timamu tunadhani uzalendo waweza kujengwa kwa mazoezi makali na ya mateso ya miezi sita kwa wahitimu wa kidato cha sita na wiki tatu kwa wabunge walio tayari na uzalendo kama Zitto Kabwe(Japo na yeye ni kati ya wafuasi wa mpango huu). Uzalendo ni hali ya kuwa na mapenzi ya dhati kwa taifa hasa katika kutetea rasilimali za taifa an maaslahi ya watu waliowengi katika taifa husika. Uzalendo hujengwa kwa misingi imara na mfumo wa kizalendo katika jamii ambamo mhusika amelelewa. Japokuwa mara nyingine uzalendo huweza kujengwa na matamanio ya mtu kuinasua jamii yake kutokana na uonevu wanaoupata kutoka kwa mtawala flani. Kwa misingi hiyo sidhani kama kuwapeleka raia ama vijana katika kambi za jeshi kwa mafunzo haya kupandikiza uzalendo litafanikiwa. Nalazimika kukumbuka nukuu hii wakati maamuzi kama haya yanapochukuliwa kwa minajili ya kurejesha uzalendo
No abounding of military training shall avail us if our spiritual senses atrophy. The foes of our own household will surely prevail against us unless there be in our people an inner life which finds its outer expression in a morality like unto that preached by the seers and the prophets of God
Nadharia ya ukakamavu kwa vijana; Wakati naanza shule ya msingi tulikuwa na utaratibu wa kukimbia mchakamchaka asubuhi mwendo kama wa kilometa moja. Utaratibu huu wa kukimbia mchakamchaka ulikuwapo hata shuleni niliposoma o-level. Mi nadhani kuliko kupoteza rasilimali na pesa nyingi katika kuandaa camp za mafunzo na kuendesha hayo mafunzo yenyewe serikali ingefanya yafuatayo;
- Kwa shule za msingi na sekondari iwe ni lazima wanafunzi kukimbia mchakamchaka na kujihusisha moja kwa moja na kazi za nje kama kupalilia, kufyeka na kujihusisha na mazoezi ya viungo kwenye pindi za P.E( Physical education) hii itasaidia sana watoto kuanza kuondokana na uvivu na uzembe taratibu .
- Majeshi yetu kutuma vijana wake kama walivyofanya enzi za miaka ya themanini pale Tabora Boys kuwapa vijana angalau Short term training wakiwa bado wapo skuli. Ni vizuri pia kama wanaweza kupatiwa mafunzo ya mgambo kwani yanaweza kutolewa shuleni kama ambavyo wanawapa mazoezi na mafunzo watoto wa halaiki.
- Shule zenye mashamba (hizi ni nyingi mikoani) kuwashirikisha wanafunzi kwa kiasi fulani katika uzalishaji kwa muda ambao hautaathiri masomo yao.
- Wanafunzi washiriki shughuli kama kuwa scouts na uwekwe utaratibu wajaichanganye na jamii katika usafi wa miji na kazi nyingine za kujitolea.
Ni matumaini yangu kuwa njia hizo zinaweza kuwafanya vijana wawe wakakamavu na kujenga mazoea ya kufanya kazi hasa kama watazoezwa tangu wakiwa wadogo. Kwa mtazamo wangu hakuna sababu ya msingi kutenga pesa ambazo nchi ingeweza kutenga kunzisha miradi ambayo ingeweza kutoa ajira kwa vijana hao hao pindi watapomaliza vyuo.Katika mazingira ambayo taifa lina unemployment rate of about 10.7% nilitegemea mabilioni hayo ya pesa yangetumika hata kuanzisha viwanda vya kati ambavyo ni labour-intensive ili kuondoa bomu ambalo Mr. Lowassa humkumbusha Jakaya kila anapopata wasaa.
Nadharia ya kuongeza nguvu kazi JKT ; Hii ni nadharia ambayo imekuwa inaongelewa kwa chini kwamba wanafunzi hawa watapelekwa JKT kusaidia na kuongeza rasilimali watu katika programu zinazotekelezwa na JKT. Japo hii haisemwi sana lakini inaweza kuwa ni mkakati wenyewe hasa ikizingatia kwamba KILIMO KWANZA inaonekana imekuwa ni sera inayotekelezwa na JKT kwa bidii.
Kwa wale ndugu zangu wakubwa wa zamani ningependa mtujuze nini kilipelekea programu hii ya JKT kufutwa mwanzoni mwa miaka ya tisini? Na pili serikali wakati ilipoanzisha programu hii ilipata makusudio iliyoyatarijia hadi ilipofutwa? Lakini la mwisho utekelezaji wake kwa formula ya miaka hiyo utaweza kufanikiwa kwa kizazi hiki cha watoto mdebwedo, wazembe na wasiojua kilimo maana wengi wa mjini siku hizi.( Hapa namaaanisha mtoto wa Kariakoo au Masaki ashinde kwenye kazi ngumu kila siku miezi sita ) pamoja na masharobabies kama wajiitavyo wenyewe bila kuzimiazimia sana?
Naomba kuwasilisha.