CCM itakuwa na Wabunge Wanawake 117 kwenye Bunge jipya

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) leo inatarajiwa kutoa orodha ya wabunge wa viti maalumu katika Bunge la 12 la Tanzania. Bunge la 11 la Tanzania lilikuwa na wabunge 113 wa viti maalumu.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ally alisema jana kuwa, katika mchakato huo CCM imepata wabunge 94 ambao ukijumlisha na wabunge wanawake 23 waliopatikana kwenye majimbo chama hicho kitakuwa na wabunge wanawake 117 kwenye Bunge la jipya.

Alisema miongoni mwa wabunge hao, 94 wabunge 22 wamepatikana kutoka katika jumuiya zake wakiwemo walemavu watatu, wazazi wawili, vijana 10, wasomi wawili, watatu kupitia asasi za kiraia na wawili kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)

Kwa mujibu wa Dk Bashiru idadi hiyo ya wabunge wanawake 117 kupitia haijawahi kutokea katika Bunge lolote tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

"Hii ni ishara njema kwa wanawake wote kwa kuwa Bunge lijalo litakuwa na idadi kubwa ya watetezi wa masuala yao, hii ndiyo maana tunasema CCM ni chama kinachojali maslahi ya wote" alisema Dk Bashiru.

Taarifa ambazo hazikuthibitishwa zilidai kuwa, kwa kuzingatia idadi ya kura walizopata wagombea ubunge kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), chama hicho kimepata wabunge 19 wa viti maalumu.

Awali Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC Dk Charles Mahera, alilieleza gazeti hili jana kuwa, wabunge waliopitishwa viti maalumu ni kutoka CCM na CHADEMA.

Alisema mchakato wa kuwapata wabunge hao ulianza juzi kwa vyama kuwasilisha majina ya wabunge walioteuliwa katika vyama vyao.

Dkt. Mahera alisema, baada ya kuchambua kwa kina majina NEC itatoa orodha tayari kwa ajili ya kuendelea na mchakato wa kuwaapisha na wabunge wenzao bungeni jijini Dodoma.

“Lakini hadi hivi sasa bado hatujapokea majina ya walioteuliwa kutoka Chadema, nilisikia leo (jana) watakuwa na mkutano wao wa ndani kujadiliana kuhusu majina hayo, matumaini hadi kufikia jioni yatakuwa yametufikia ili kwa pamoja kesho tuweze kuyatangaza” alisema Dk Mahera.

Alisema utaratibu wa kupata idadi ya wabunge kutoka kwa vyama hivyo viwili pekee umezingatia taratibu iliyopo katika Ibara ya 78-(1) ya Katiba ya Tanzania, kwa madhumuni ya uchaguzi wa wabunge, wanawake waliotajwa katika ibara ya 66(1) (b), vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi, kwa kufuata utaratibu uliowekwa, vitapendekeza kwa tume majina ya wanawake.

Kwa mujibu wa Dkt. Mahera, vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi, kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa, vitapendekeza kwa tume majina ya wanawake kwa kuzingatia masharti ya uwiano wa uwakilishi baina ya vyama vilivyoshinda uchaguzi katika majimbo na kupata viti bungeni.

Alisema kwa mwaka huu CCM na Chadema wamekidhi matakwa ya kutoa wabunge kulingana na utaratibu wa kuwapata wabunge wanawake wa viti maalumu.

Dkt. Mahera alisema, wabunge hao wanapatikana kwa kuchukua jumla ya kura zote halali za ubunge ambazo chama kimepata na kuzidisha kwa idadi ya viti maalumu vyote ambavyo tume itatoa na kugawanya kwa idadi ya kura halali za ubunge kwa vyama vilivyopata angalau asilimia tano ya kura zote halali za ubunge.

Alisema Ibara hiyo ya Katiba inaendelea kueeleza kuwa, iwapo NEC itaridhia kuwa mtu yeyote aliyependekezwa ana sifa za kuwa Mbunge itamtangaza kuwa amechaguliwa kuwa Mbunge, na masharti ya ibara ya 83 ya Katiba ya Tanzania itatumika kuhusu kuchaguliwa kwa mtu huyo kuwa Mbunge.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, jumla ya wapiga kura milioni 29,754,699 walijiandikisha kwenye daftari la wapiga kura na waliopiga kura Oktoba 28 mwaka huu walikuwa milioni 15,091,950 na kati ya hizo kura halali ni milioni 14,830,195.

Katika uchaguzi huo jumla ya wabunge wa majimbo waliochaguliwa ni 264 na kati ya hao, 214 ni wa majimbo ya Tanzania bara na 50 wa Zanzibar.

Aidha, jumla ya vyama 19 vilishiriki uchaguzi huo na kati ya hivyo vyama vilivyopata wabunge ni CCM majimbo 256, Chama Cha Wananchi (CUF) watatu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) (1) na Chama Cha ACT-Wazalendo (4).

Wakati Dkt. Mahera alisema baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 NEC iliteua wabunge 113 wa viti maalumu kutoka vyama vitatu.

Ili kuwapata wabunge hao NEC, ilichukua jumla ya kura zote halali za ubunge ambazo chama kilipata na kuzidisha kwa idadi ya viti maalumu vyote ambavyo tume ilitoa na kugawanya kwa idadi ya kura halali za ubunge kwa vyama vilivyopata angalau asilimia tano ya kura zote halali za ubunge.

Katika utaratibu huo, CCM ilipata wabunge 66 wa viti maalumu, Chadema 37 na CUF 10.

Kwa upande wa wabunge wa majimbo katika uchaguzi wa mwaka 2015 CCM ilipata wabunge 206, CUF 29, Chadema 26, ACT-Wazalendo na NCCR-Mageuzi wakipata mbunge mmoja mmoja.
 
Kama kila Jimbo linae Mbunge aliechaguliwa na Wananchi Basi hao Wabunge wanaosadikika ni viti maalumu hakuna haja ya kuwepo kwani ni Wanasababisha Matumizi mabovu tu ya pesa za Wananchi.

Mmewaacha kina; Zitto, Mbowe, Lema, Heche, Sugu na miamba mingine yenye hoja za kuichalenji serikali, Mmetujazia Wasaka tonge wa kusifu na kuimba mapambio 24/7 kwa mgongo wa haki sawa.

Binafsi; Sikubaliani kabisa na huu upuuzi wa Wabunge wa viti maalamu. Kiti maalumu ndo mdudu gani kwanza.
 
Rais amejinasibu kubana matumizi..ili kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo..tambua eneo lingine kubwa linalofuja pesa za watanzania ni bunge..jicho lako la kubana matumizi naomba litazame na huku...mana kwakua wakwamisha maendeleo hawapo bungeni nadhani ukipeleka hii hoja haitapingwa.

#MaendeleoHayanaChama
 
Hakuna jipya, wameshaua upinzani wamebaki wanatapatapa tu.
 
  • Thanks
Reactions: PNC
Inapendeza, ila idadi kubwa sana...



Cc: mahondaw
Hata wawe 500 wanamsaada gani kwa wanawake?? Hao wabunge wanaume na wingi wao wote huo, wameshawahi kutanguliza lini masilahi ya wanachi? Walikuwa wanazidiwa na wapinzani 40?!!! Mpinzani mmoja kama zitto/msigwa ni wabunge 200 wa ccm!!
 
MNAENDA KUCHOCHEA UMALAYA NDANI YA DODOMA.

NIKIKUMBUKA JINSI NDOA YA BHONA KALUA ILIVYOVUNJIKA SINA HAMU NA BUNGE HILO.

NI NGONO MWANZO MWISHO NA KUITIKIA TU NDIOOOO!!!
 
Back
Top Bottom