WANAZUONI wa Kiislamu nchini wameipa siku tatu Chadema Taifa kulaani kitendo cha wafuasi na viongozi wake kulidhalilisha vazi tukufu la hijab na kumwomba radhi Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario, kwa kumvua sitara yake.
Wamesema iwapo chama hicho kitapuuza kufanya hivyo na kupita muda huo wanazuoni hao na Waislamu wataiona Chadema kama chama chenye sera na madhumuni ya kuhujumu Uislamu na Waislamu wa Tanzania na kuhimiza Waislamu kukiepuka kama ukoma.
Kauli hiyo iko kwenye tamko la Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania (HAY-AT) lililosomwa jana na Naibu Katibu Mkuu wa Sekretarieti Kuu ya Umoja huo, Shehe Sherali Hussein Sherali na kusema siku tatu hizo zilianza jana.
Wanazuoni hao zaidi ya 10 wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Shehe Suleimani Kilemile, walitoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari na kusema baada ya hapo umoja huo utakaa na kutafakari hatua stahiki za kukabiliana na dharau hizo na kuelekeza Waislamu cha kufanya.
Sherali alisema ifahamike, kwamba shambulio lolote dhidi ya hijab ni dhidi ya Uislamu na Waislamu wote, haliwezi kuvumilika na watakabiliana na yeyote anayetaka kuidhalilisha amri ya hijab iliyo katika Quran sura ya 33:59.
Tunataka ifahamike, kwamba yeyote atakayelidharau vazi la hijab kwa kauli au vitendo, atakuwa amewachokoza Waislamu na sisi kamwe hatukubali hilo liendelee na kukaa kimya, tutachukua hatua stahiki na ikibidi tutalazimika kuondoa munkari kwa mikono yetu wenyewe, kama dini yetu inavyotuelekeza, alisema.
Aliongeza kuwa wanalaani na kupinga kitendo kilichofanywa na wanaodaiwa kuwa wafuasi na viongozi wa Chadema kumvua nguo Mkuu huyo wa Wilaya na kumwacha bila sitara.
Alisema Kimario ni Mwislamu anayefuata mafundisho ya Uislamu yanayomtaka kila
mwanamke ajisitiri kwa vazi la hijab, hivyo kumvua ni kumdhalilisha kwa wanajamii kama mwanamke wa Kiislamu, mama mwenye watoto na kiongozi wa Serikali.
Tumetafakari tukio hili kwa undani na tunalichukulia kama shambulio la wazi na la maku