Castro and Cuba

Comred Mbwana Allyamtu

JF-Expert Member
Jun 28, 2016
348
847
KWAO CASTRO ALIKUWA CUBA NA CUBA ILIKUWA CASTRO.

Na.Comred Mbwana Allyamtu
Thursday -30/8/2018

Fidel Alejandro Castro Ruz alifariki usiku wa saa 4:29 siku ya tarehe 25/11/2016 huko Havana Cuba na mwili wake kuchomwa moto siku iliyofuata ya tarehe 26/11/2016 na kisha kuzikwa kwa heshima ya kitaifa tarehe 3/12/ 2016 katika eneo la mji wa Santiago, eneo ambalo ndio kitovu cha harakati za uhuru wa Cuba mwaka 1890 zilizo ongozwa na mwasisi wa taifa hilo Jose Mart, Lakini eneo hilo pia ndipo harakati za Castro za kuuangusha utawala wa Fulgencio Batista zilianzia.

Ukweli ni kwamba Castro ndio mjamaa pekee ambaye aliendelea kusalia madarakani hata pale tawala za kijamaa zilipoanguka kote duniani, lakini Castro aliendelea kupeperusha bendera nyekundu karibu na maadui wake wakubwa, Marekani.

Kiongozi huyo mwenye utata alisifiwa na wafuasi wake kama mwanamapinduzi mwenye haiba ya Jose Marti baba wa taifa la Cuba aliyeikomboa taifa hilo miaka ya 1890 kutoka mikononi mwa Uhispania pia Castro hutazamwa kama kiongozi wa ujamaa mwenye ushupavu kama Simion Bolivar mwasisi wa mapinduzi ya Latin Amerika anaye heshimiwa mno Amerika ya kusini ambaye ndie baba wa mataifa ya Venezuela, Colombia, Panama, Peru, Ecuador na Costa rica.

Castro ni askari na mwanasiasa ambaye hutazamwa kama kiongozi na baba wa taifa hilo ambaye alilijenga taifa hilo la kijamaa, lakini pia wapinzani wake walimuona kama dikiteta ambe alikabiliwa na shutuma kwa kuwazima wapinzani wake kwa njia ya mateso kwa kuazisha sera ambazo ziliporomosha uchumi wa Cuba kwa takribani miaka 50 ya utawala wake.

Fidel Alejandro Castro Ruz alizaliwa tarehe 13 Agosti 1926, nje ya ndoa ya familia ya mkulima bwanyenye , Angel María Bautista Castro y Argiz, ambaye alihamia Cuba kutoka Uhispania.Mama yake Castro alitwa Lina Ruz González alikuwa kijakazi aliyefanya shughuli za shamba ambaye baadae alikuwa mpenzi wa baba yake na baadae baada ya kuzaliwa kwa Fidel akawa mkewe halali kwa kufunga ndoa yao huko Habana (Havana kwa sasa).

Castro alisoma katika shule ya kikatoliki mjini Santiago kabla ya kujiunga na chuo kinachoendeshwa na makasisi wa Jesuit kilicho eneo la El Colegio de Belen jijini Havana.Hata hivyo Castro alishindwa kimasomo na badala yake alipendelea kutumia muda wake mwingi katika shughuli za michezo.

Ilikuwa wakati anasomea sheria katika Chuo Kikuu cha Havana kati kati ya miaka ya 1940s ndipo alipokuwa mwanaharakati wa siasa, na kuimarisha ujuzi wake wa kuzungumza hadharani. Malengo yake yalikuwa ni pamoja serikali ya Cuba, iliyoongozwa na Ramon Grau, ambayo ilikumbwa na shutuma za ufisadi wakati huo. Ghasia za maandamano ya upinzani ziligeuka kuwa maisha ya kila siku na Castro akajipata akilengwa na polisi kwa shutuma mbalimbali za uchochezi.

Pia alikuwa miongoni mwa watu waliopanga njama za mapinduzi ya kumg'oa mamlakani Rafael Trujillo, kiongozi wa mrengo wa kulia wa Dominican Republic, lakini jaribio hilo lilishindwa baada ya na Marekani kuingilia kati. Huku mnamo mwaka 1948 Castro alimuoa Mirta Diaz-Balart, mwanae mwanasiasa tajiri nchini Cuba. Mbali na kumtia msukumo wa kujiunga na wasomi wa nchi aligeuka kuwa na itikadi za Leninst- Kimaxist. Castro aliamini matatizo ya Cuba ya kiuchumi yalikuwa ni matokeo ya ubepari usioweza kudhibitiwa ambao unaweza kutatuliwa tu kwa mapinduzi.

Baada ya kuhitimu masomo Castro alizindua shughuli za kisheria lakini zilishindwa kufanikiwa na aliendelea kuingia katika mzozo wa madeni. Castro alisalia kuwa mwanaharakati wa kisiasa, akishiriki katika misururu ya maandamano ya mara kwa mara ya ghasia. Mnamo mwaka 1952 Fulgencio Batista alifanya mapinduzi ya kijeshi yaliyomg'oa madarakani rais wa Cuba , Carlos Prío.

Sera ya Batista ya uhusiano wa karibu na Marekani na kukandamiza mashirika ya kijamaa vilikuwa pingamizi kwa imani za msingi za siasa za Castro. Baada ya kushindwa katika shughuri za kisheria, Castro alibuni shirika lililoitwa The Movement lililoendesha shughuli zake kisiri kwa lengo la kuung'oa madarakani utawala wa Batista. Cuba palikuwa mahala pa watu matajiri kujivinjari, na nchi iliongozwa na kiasi kikubwa na magenge ya wahalifu . Ukahaba ,wacheza kamali na walanguzi wa mihadarati vilikithiri.

Mwezi Julai 1953 Castro alipanga shambulio dhidi ya kituo cha kijeshi cha Moncada ambacho kipo karibu na Santiago ili kupora silaha kwa ajili ya kuzitumia katika harakati za kivita. Shambulio lilishindwa na wanamageuzi waliuawa ama kukamatwa .

Castro alikuwa mmoja wa wafungwa kadhaa waliofikishwa mahakamani mnamo mwezi Septemba 1953. Castro alitumia muonekano wake mahakamani kutangaza maasi yaliyotekelezwa na jeshi jambo ambalo baadae lilimpatia umaarufu, hususan miongoni mwa waandishi wa habari wa kigeni ambao waliruhusiwa kuhudhuria kesi hiyo.

Fidel Castro alihukumia kifungo cha miaka 15 jela, Baadae aliachiliwa huru kufuatia tangazo la msamaha wa raisi wa jumla mnamo mwezi Mei 1955 baada ya kutumikia kifungo hicho kwa miezi 19 pekee katika mazingira bora kiasi. Katika kipindi hiki kifupi gerezani alimtaliki mkewe na kujiimarisha zaidi katika sera za kimaxist. Kutokana na Batista kuendela kuwa kamata wapinzani wake Castro alitorokea Mexico kuepuka kutiwa nguvuni . Huko alikutana na mwana mageuzi kijana aliyeitwa Ernesto "Che" Guevara.

Huyu Ernesto "Che" Guevara anatajwa kama mtu mwingine muhimu sana katika mapinduzi ya Cuba ya mwaka 1959 ni mwanamapinduzi na mzaliwa wa Argentina ni mmoja wa wakombozi wa Cuba. Ernesto "Che" Guevara ni moja ya wanadamu waliojitoa mhanga kupambana dhidi ya ubeberu kote duniani. Katika maisha yake aliwahi kupita Tanzania na kushiriki kwenye vikao na vyama vya ukombozi kusini Mwa Afrika.

Tanzania iliunganishwa na Che kupitia Zanzibar. Vijana wa Zanzibar walipelekwa mafunzoni Cuba Kwa ajili ya ukombozi. Mwaka 1962 wakati wa mgogoro wa Oktoba 1962 kule Cuba, vijana wa kizanzibari waliokuwa mafunzoni Cuba walijitolea kupigana bega Kwa bega na waCuba dhidi ya Marekani. Jambo hili liliwafungua macho wacuba kuhusu Afrika na Kwa hakika Afrika yao ilikuwa Zanzibar.

Watu kama Mzee Ali Sultan Issa na Komred Shaaban na Dkt. Salim Ahmed Salim wakati huo akiwa Mkuu wa Ofisi ya Zanzibar kule Havana, Cuba. Pamoja na AbdulRahman Mohamed Babu, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Zanzibar na baadaye Waziri wa zamani wa Uchumi wa Tanzania alikuwa mtu wa karibu sana na Che Guevara na kupitia hawa Che aliiona Afrka kama nyumbani.

Che Jina lake kamili aliitwa Ernesto Che Guevara alisomea udaktari, lakini baadae alikuwa mwanamapinduzi wa kijamaa (marxist). Uraia wake ulikuwa wa taifa la Argentina. Che Guevara alizaliwa June 14 1928 na Kufariki dunia mnamo October 9, 1967 huko katika nchi ya Bolivia katika milima ya "La heguera". Chanzo cha kifo chake ni kuuwawa kwa kupigwa risasi na maasikari wa Bolivia kwa ushilika wa karibu kabisa na maafisa wa CIA kutoka Marekani.

Miaka ya 1950 akiwa anasoma udaktari huko Mexico, Che Guevara alikutana na Fidel Castro na Raul Castro ambapo watatu hao walipanga mapinduzi ya kumgoa raisi wa Cuba wakati huo Fulgencio batista ambaye alikuwa na uhusiano wa kimaslahi na America, Che akapata nguvu na uaminifu mkubwa kutoka kwa Fedel Castro na kupandishwa kuwa kiongozi wa wanamgambo (guerilla insurgents). Punde tu baada ya Fulgencio Batista kukimbia CUBA,Che alihusika kama mtu muhimu katika serikali ya Cuba iliyoongozwa na Fidel Castro, akiwa kama Gavana wa benki kuu ya Cuba na waziri wa fedha wa Cuba ambapo saini yake ilianza kutumika katika noti za Cuba na baadae kama waziri wa kilimo wa Cuba.

Mnamo mwezi Novemba 1956, Castro alirejea Cuba akiambatana na wanajeshi 81 pamoja na Che kwenye ndege iliyokuwa na uwezo wa kuwabeba watu 12 pekee. Makao makuu ya chama yalitafuta hifadhi katika milima ya Sierra Maestra . Kutoka kwenye ngome hii Castro alizindua vita vya msituni dhidi ya utawala wa Havana.

Tarehe 2 Januari, 1959, jeshi la waasi likaingia katika mji mkuu wa Cuba Havana na Batista akatoroka. Mamia ya wafuasi wa zamani wa Batista walinyongwa baada ya kesi ambazo wageni wengi waliziona kuwa hazikuwa za haki. Castro ralijibu kwa kusisitiza kwamba " Haki ya mageuzi haina misingi ya kisheria ya kubadili tabia ama mawazo , bali inazingatia uwajibikaji wa maadili”. Serikali mpya ya Cuba iliahidi kurejesha ardhi kwa watu na kulinda haki za maskini.

Baada ya fidel kutwaa madaraka kwa kumpindua Batista ndani ya siku 100 za mwanzo alifanya mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na kutwaa baadhi ya mashamba ya miwa, kusogeza huduma za jamii karibu, kupiga marufuku ubaguzi wa rangi nk.. Lakini mara moja serikali ilianza kulazimisha mfumo wa chama kimoja cha kisiasa . Mamia ya watu walitupwa jela na kwenye kambi za kutumikisha kazi za sulba kama wafungwa wa kisiasa. Maelfu ya waCuba hususan wenye kipato cha kadri wakalazimika kuikimbia nchi yao. Castro alisisitiza kwamba fikra zake zilikuwa ni bora zinajali kwanza maslahi ya watu wa Cuba. Fidel Castro alisema "hakuna ujamaa au umaxist , bali uwakilishi wa demokrasia na haki ya kijamii katika mpango bora wa uchumi ," alisema wakati huo.

Nchi ya Cuba ilikuwa na idadi kubwa ya watu ambao hawajasoma zaidi ya asilimia 60 ya watu wake walikuwa hawajui kusoma na kuandika, chini ya Castro akaanzisha utaratibu wa wale wachache wanaojua kusoma na kuandika wawafundishe wale wasiojua, wakasambaa kote nchini chini ya msemo maarufu wa “kama hujui jifunze ujue na kama unajua fundisha”.

Kupitia mpango huo watu wengi wa Cuba wengi walijua kusoma na kuandika na elimu ilitolewa bure. Pia nchi hiyo wakati wa Fidel anaingia madarakani ilkuwa na jumla ya madaktari 6000 tu na wengi walikuwa hapoHavana, kule vijijini huduma zilikuwa hakuna na watoto wengi walikufa kwa kukosa huduma. Castro akawaambia madaktari wale waliorundikana mjini wasambae mpaka vijijini wakatoe huduma. Wengi waligoma na kukimbia nchi, ndio chanzo cha wengi kwenda miami na pia watu wengi waliokuwa na uchumi mzuri ambao mali zao zilitaifishwa walimchukia Fidel na kuikimbia nchi, ndio hao walokuwa wakishangilia wakati wa kifo cha Castro.

Nikipindi hicho Marekani ilitangaza ofa ya uraia na kitita cha dola kibao kwa Mcuba yoyote atakaye fanikisha kuondoka Cuba na kwenda Marekani, kupitia hiyo uhasama wa kidipromasia baina ya Cuba na Marekani uliongezeka maradufu kujibu hilo Castro mnamo mwaka 1960 Fidel Castro aliwapatia uraia wamarekani woote waliokuwa wanamiliki biashara katika kisiwa hicho. Kujibu hatua hiyo, utawala wa Washington ulimuwekea vikwazo vya kibiashara vilivyo tarajiwa kudumu kwa karne nzima ya 21st.

Nchini kwake Castro alipania kuleta huduma za afya karibu Fidel alianzisha vyuo vitatu maalum kwa ajili ya kupambana na uhaba wa madaktari na alifanikiwa sana, vifo hasa vya watoto vilipungua sana kuliko baadhi ya miji huko USA wakati huo. Maadui wa Castro waliongezeka toka nje na ndani ya nchi, CIA walitumia mbinu chafu za kumuondoa Fidel duniani na mipango mingi iliwahusisha wacuba wengi waliokimbia nchi hasa waliokuwa wakiishi Miami.

Casto alipambana na mbinu hizo kwanza kwa kuunda kitengo cha ujasusi ambacho kilikuwa chini yake, kiliitwa DGI(Director General of Intelligence) na kitengo hiki kilikuwa kama mali binafsi ya Fidel, wengi wa waliofundishwa walikuwa ni vijana wadogo hasa walioungana nae huko kwenye milima ya Ciera Maestra wakati wakipambana na Batista na vijana hawa walikusanywa na mama mmoja aliyekuwa karibu sana na Fidel, aliitwa Celia Sanches, mama huyu alikufa kwa Saratani mwaka 1980.

Vijana hawa asilimia 95 walifanya kazi ya kijasusi bure bila malipo na wakati mwingine walichukuliwa vijana wadogo sana na kupelekwa "shambani" ambako walipewa elimu ya ujasusi wa hali ya juu sana, na pia walikuwa wazalendo sana kwa nchi yao na watiifu kwa Fidel.

Kwani kupitia kitengo hiki hakuna CIA officer aliyeingia Cuba bila kufahamika, mipango ya mauaji iliyopangwa kumuondosha Fidel iligundulika haraka kwani Fidel alifanikiwa kupenyeza vijana wengi kwenda USA hasa Miami na Florida na huko waliishi wakifuatilia kila Wamarekani wanachokipanga juu ya Fidel na wengi wa vijana hawa bila CIA kufahamu kwamba ni majasusi waliwatrain tena ili kufanikisha mipango yao ya kumuua Fidel Castro, vijana hawa walibaki watiifu kwa Fidel na hivyo mipango yote waliyopanga ilimfikia el Comandante Fidel Castro Ruz bila wasiwasi.

Moja ya njama ya kumuua Castro iliyolatibiwa na CIA ni ile mbinu maarufu ya mwaka 1961 ambayo ilielezwa na Marita Lorenz ambaye alisafiri kutoka Miami kwenda New York akiwa na Alex Rorke kuwatembelea mama yake pamoja na makachero wawili Frank Lundquist na Frank O'brien. Katika safari hiyo ndipo alisikia kwa mara ya kwanza mpango wa kumuua Fidel Castro. Marita Lorenz alieleza mpango huu kwenye kitabu chake alichoandika cha “The spy who loved Castro” katika kitabu hichi Marita Lorenz Anaeleza kuwa wakati wakiwa Manhattan ndiko alisikia mpango huo. Alex Rorke alikuwa shushushu mwenye sifa za kilokole. Alichanganya vyote viwili kama njia ya kuhamasisha na kutekeleza mikakati.

Ni kama mtaalamu wa teolojia wa nia ovu. Alitumia uwezo wake wa "ucha Mungu" kumsisitizia Marita Lorenz umuhimu wa kujilinda na kutekeleza mipango ya dola (nchi). Marita anasema hakumbuki idadi ya vikao vilivyofanyika na mawakala wa CIA na FBI iwe ofisini au nyumbani kwake kwa shabaha ya kuyakatisha maisha ya Castro ukweli Castro aliwanyima usingizi Marekani.

Baada ya John F. Kennedy kuwa Rais wa Marekani alimkabidhi ndugu yake aliyeitwa Robert Kennedy jukumu la kumuua Fidel Castro kwa kupitia Counter Intelligence na Double Agent. Vijana wa Fidel waligundua njama hizo na zikafika mezani kwa el comandante Fidel Aljandro Castro. Kwani zaidi ya majaribio 633 ya kuuwawa kwa Castro yalibainika na kuteguliwa. Kwani maafisa wa ujasusi wa Marekani CIA walijaribu kumuua , katika kisa kilichojulikana kama Operation Mongoose ambapo mbinu mojawapo ilikuwa ni apewe sigara iliyokuwa imesheheni vilipuzi.

Mbinu nyingine zilikuwa za kushangaza sana ikiwemo mojawapo ya kumfanya ndevu zake zianguke ili kumfanya awe na sura ya kuto heshimika. Akihojiwa na mwandishi wa Reuters, Fidel alitahadharisha Marekani kwa kusema jaribio lolote la kumuua kiongozi wa Cuba litakuwa na madhara kwa Marekani na wasitishe mipango yao, Wamarekani walisikia lakini walikaidi na Robert Kennendy akaendelea na mipango ya kumuua Castro.

November 22 mwaka 1963 Lee Oswald alimpiga risasi Rais wa Marekani John F. Kennedy na baada ya saa moja ikatangazwa raisi ameuawa, inaaminika Castro alifahamu mipango hiyo japo alikanusha sana. Uhasama wa Cuba na Marekena pakubwa ulichochewa na Kennedy raisi wa 35 wa Marekani kwani Kennedy aliwaagiza CIA wahakikishe Fidel ana ondolewe madarakani hii ni baada ya Fidel kutaifisha mali nyingi zilizokuwa zikimiliwa na Wamarekani na pia alianza kuagiza bidhaa toka Soviet.

Baada ya pressure kubwa toka kwa CIA, Rais kenedy akaidhinisha kuondolewa madarakani kwa Fidel Castro na katika mpango huo Kennedy alisema hataki ijulikane kuwa Marekani ndio imehusika na mpango huo kwa hiyo akawataka CIA wahakikishe wanakamilisha mpango huo bila kuacha alama ya mhusika mkuu. CIA wakaanza mpango huo kwa kuwahusisha wacuba waliokimbia nchi hasa wale waliokuwa Miami, jumla yao ilikuwa 1400 na kikosi cha watu hao kikapewa jina la kikosi 2506, wakapelekwa eneo maalumu na kuanza kupewa mafunzo ya kwenda kumwondoa madarakani El commandante Fidel Castro.

Mazoezi ya anga, majini na ardhini yalifanyika katika kundi hilo la wakimbizi waliokuwa wakipewa mafunzo walikuwepo maagent wa Fidel waliokuwa wakipenyeza taarifa zao havana. Mazoezi yalipokamilika zilipangwa hatua tatu za mashambulizi ambazo Rais Kennedy alizipitisha, njia ya kwanza ilikuwa ni kutumia ndege za kivita kuzipiga air base zote za Jeshi la Anga la Fidel, walitaka kushambulia na kuzimaliza ndege zote.

Njia ya pili ilikuwa ni kwenda kumalizia mabaki yoyote ya ndege ambayo haikulipuka kwenye mpango wa kwanza na njia ya tatu ilikuwa ni kuingia kwa hao wakimbizi wa Cuba waliopewa mafunzo kwenda kushambulia na kumwondoa Fidel madarakani. Njia ya kwanza ikaanza kutumika, marubani wavamizi walipewa ndege, ndege zile za kivita zilibadilishwa rangi na kufanana sana na zile za Jeshi la Cuba na pia zilipakwa matope ili zikiwa angani zionekane ni chakavu, jamaa wakaenda wakashambulia kambi ya anga ya Fidel na waliangamiza asilimia 80 ya ndege za Castro, Jeshi la Anga la Castro lilibakiwa na ndege sita tu na marubani saba, ilikuwa big loss kwa comrade.

Baada ya njia ya kwanza kuleta matokea chanya kwa Wamarekani, huko New York kiongozi wa Cuba Umoja wa Mataifa akaitisha kikao, akaituhumu Marekani, Marekan ikakataa katakata kuhusika, wakadai ndege zilizoshambulia ni za Wacuba wenyewe walioasi Jeshi. Balozi wa Cuba akasema ndege za Jeshi la Cuba sio zilizoshambulia, ndege zilizoshambulia zina mngurumo tofauti na ndege za Cuba, ndege zilizoshbulia ni za Marekani ila mmezibadilisha rangi zifanane na za Cuba ila mmeshindwa kubadili muungurumo.

Hapo rais Kennedy akaingiwa na ubaridi na akasitisha njia ya pili iliyokuwa imepangwa, Maafisa wa CIA walichukia sana kuona rais amekataa njia ya pili kutumika. CIA wakaenda njia ya tatu ya kuwa deploy wale 1400 ili wavamie Cuba, kule Cuba Fidel mwenyewe aliingia front na kusema hii ni kazi ya Marekani na Cuba will respond shambulizi hili. Baada ya kauli hiyo Fidel alizihamisha zile ndege sita zilizosalia na pia akaandaa mpango mkakati wa kujibu.Wale wavamizi 1400 wa mara ya kwanza ilikuwa imepangwa waingie Cuba kupitia Trinidad lakini baada ya Kennedy kuigomea njia ya pili, Maafisa wa CIA nao wakabadili njia ya kuingia Cuba kwa hawa wavamizi, wakaelekezwa waingie cuba kupitia hapo the bay of pigs ambapo jaribio hili la uvamizi lilishindwa vibaya.

Kwani katika mwambao wa Pigs,vikosi vya Cuba vilikabili majeshi ya uvamizi, na kuwauwa wengi huku 1,000 wakikamatwa. Fidel Castro alikuwa ameonja malaka kwa njia ya damu kwa hivyo asingeweza kuwasamehe. Kufatia kuongezeka kwa vitisho vya serekali ya Washingtoni dhadi ya ile ya Havana Castro aliamua kutafuta ushilikiano wa karibu na taifa la Usovieti, ingawa Castro alidai kuwa alilazimishwa kuingia katika mikono ya muungao wa Usovieti na kiongozi wake, Nikita Khrushchev, ila baadhi ya wachanganuzi na wabobezi walisema aliingia katika muungano huo USSR kwa utashi wake mwenyewe.

Iwe ni kwa sababu yoyote ile, taifa la Cuba liligeuka kuwa uwanja wa mapamabano ya vita baridi vya dunia. Mwaka mmoja baadae, ndege za uchunguzi za Marekani ziligundua makombora ya Usovieti wakati zilipokuwa njiani kuelekea maeneo ya Cuba. Dunia ilishtushwa na uwezekano wa kutokea vita vya nuklia vya dunia."msururu wa maeneo yenye makombora ya masafa marefu ya kivita sasa yanaandaliwa katika kisiwa kilichofungwa. Lengo la ngome hizi za makombora haliwezi kuwa lingine zaidi ya kutoa uwezo wa kufanya mashambulio ya nuklia dhidi ya mataifa ya magharibi ," alionya rais John F Kennedy.

Mataifa yenye nguvu duniani yalibaki kushuhudia kinachoendelea lakini ni rais Khrushchev pekee ambaye aliweza kuchukua hatua kwanza na kuondoa makombora yake nje ya Cuba baada ya Marekani kukubali kuondoa kisiri silaha zake kutoka Uturuki. Fidel Castro, hata hivyo, alikuwa tayari ni adui wa Marekani namba moja. Maafisa wa ujasusi wa Marekani CIA walijaribu kumuua mara nyingi zaid bila mafanikio.

Kufatia vikwazo vya kiuchumi vilivyo wekwa na Marekani ili kuidhofisha Cuba kiuchumi iliifanya Muungano wa Usovieti imwage pesa ndani ya Cuba. Ilinunua mavuno ya sukari inayozalishwa kisiwani humo na meli zake kurejea na zimesheheni na bidhaa nyingine, kama vile chakula kilichokua kinahitajika ili kukabiliana na vikwazo vya Marekani vya biashara nchini Cuba. Licha ya utegemezi wa msaada kutoka mataifa ya Usovieti , Castro aliiongoza Cuba kuwa taifa jipya lisilokuwa na mafungamano yoyote.

Kufatia kuimalika ujamaa Cuba Castro aliegamia hasa Afrika, ambako alituma majeshi kuunga mkono wapiganaji wa msituni waliokuwa na sera za kimaxist katika nchi za Angola na Msumbiji ili kufanya ukombozi. Lakini katikati ya miaka ya 1980, siasa za dunia zilianza kubadilika na mabadiliko hayo zilibadili mkondo wake wa siasa. Ilikuwa ni enzi ya Mikhail Gorbachev kule USSR, sera za glasnost na perestroika, zilidhihirika wazi kuwa kinyume na mageuzi ya Castro. Kufatia hilo Utawala wa Moscow ukakata uhusiano wa kiuchumi na Cuba kwa kukataa kata kata kununua sukari ya Cuba. Mtikisiko huo ulianza kuikumba Cuba Castro kiwa bado chini ya vikwazo vya Marekani na kukatwa kwa huduma muhimu za mataifa ya Sovieti uhaba wa huduma na bidhaa na ukosefu wa akiba ya bidhaa vilidhihirika ndani ya Cuba

Taifa ambalo Fidel Castro aliita lililoendelea zaidi duniani, hali ya maisha ilikuwa mbaya. Kwani katika kati ya miaka ya 1990s, waCuba wengi walikuwa wamechoshwa na hali nchini mwao. Maelfu walianza kutoroka kupitia njia ya maji hadi Florida wakiwa na ndoto ya kuishi maisha bora zaidi. Wengi walikufa maji. Hata hivyo Cuba ilirekodi baadhi ya mafanikio ya kufurahisha ndani ya nchi. Huduma bora za matibabu zilitolewa bure kwa wote , na viwango vya vifo vya watoto wachanga kwani vililinganishwa na vile vya mataifa tajiri duniani.

Katika miaka iliyofuata Castro alionekana mtulivu hivi. Mwaka 1998 alitembelewa na Papa John Paul II, jambo ambalo halingeweza hata kufikiriwa miaka mitano ya awali. Wakati huo Papa aliilaumu Cuba kwa ukiukaji wake wa haki za binadamu na kumuaibisha Castro mbele ya vyombo vya habari vya dunia. Pamoja na hivyo Fidel Castro alikuwa amebuni utambulisho wake kama mjamaa wa Caribbean ambao kwa miaka kumi iliyopita, alilazimika kuukumbatia, pole pole alianzisha mabadiliko machache ya biashara huria ili kulinda mageuzi yake ya sera ya ujamaa.

Tarehe 31 Julai 2006, siku chache tu kabla ya maadhimisho ya mwaka wake wa 80 wa kuzaliwa, Castro alikabidhi mamlaka ya muda kwa Raul baada ya kufanyiwa upasuaji wa dharura wa utumbo. Afya yake iliendelea kudhoofika. Mapema mwaka 2008, Castro alitangaza kwamba hatakubali nyadhifa za urais na amiri jeshi mkuu katika mkutano mkuu ujao wa kitaifa. Katika barua iliyochapishwa katika gazeti rasmi la kijamaa, alikaririwa akisema kuwa "Ni kudanganya nafsi yangu kuchukua majukumu yanayohitaji kutembea na kujitolea, wakati siko katika hali ya kimwili inayoniruhusu kufanya hivyo ."

Alijiondoa kwa kiasi kikubwa katika maisha ya umma, huku akiandika taarifa zilizochapishwa katika vyombo vya habari vya kitaifa chini ya kichwa cha habari “Tathmini ya maisha ya Amir Jeshi Fidel”. Alijitokeza tena hadharani mwezi Julai 2010, alipoonekana mbele ya umma tangu augue, akiwasalimia wafanyakazi na kuhojiwa na televisheni ambapo alijadili kuhusu hali ya wasi wasi baina ya Marekani na Iran pamoja na Korea kaskazini.

Mwezi uliofuatia Castro alitoa hotuba yake ya kwanza katika bunge la taifa baada ya miaka minne, akiitaka Marekani kuacha kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran au Korea Kaskazini akionya kutokea kwa maafa ya nuklia ikiwa uhasama utazidi. Alipoulizwa ikiwa Castro anaweza kuingia tena katika serikali, waziri wa utamaduni Abel Prieto aliiambia BBC "nadhani wakati wote amekuwa katika maisha ya siasa za Cuba lakini hayuko serikalini. Wakati wote amekuwa makini kwa hilo. Vita vyake vikuu ni kuhusu masuala ya kimataifa."

Tangazo la rais Obama la Disemba 2014 la mwanzo wa kumalizika kwa vikwazo vya Marekani vya biashara na vinginevyo nchini Cuba ilionekana kama matumaini katika kile kilichokuwa “uadui wa nusu karne wa uhusiano baina ya nchi hizo mbili". Castro mwenyewe aliafiki hatua hiyo aliyoielezea kuwa "hatua nzuri ya kutafuta amani ya kikanda", lakini hakuiamini serikali ya Marekani maana aliwaona Marekani kama jinamizi lenye lengo ya kuitafuna Cuba.

Wakati waCuba kadhaa bila shaka walionekana kutokumpenda Castro, wengine wengi walimpenda kwa dhati. Walimuona kama David ambaye aliweza kukabiliana na Goliath wa Marekani.

Hakika “Kwao Castro alikuwa Cuba na Cuba ilikuwa Castro”.


Email- mbwanaallyamtu990@gmail.com
IMG_20190507_102739_449.jpeg
 
Back
Top Bottom