Tanzania na Canada zaanza mjadala wa kulinda Uwekezaji wa Wakanada
KLH News
Serikali ya Canada imeanza mchakato wa mazungumzo ya kuingia makubaliano na serikali ya Tanznia ili hatimaye serikali hizo mbili ziingie kwenye Mkataba wa Kupromoti na Kulinda Uwekezaji wa Kigeni ili wafanyabiashara na wawekezaji wa kigeni kutoka Canada waweze kuwa na utaratibu wa kisheria unaoongoza na kulinda mitaji na miradi yao nchini.
Mazungumzo hayo ambayo yamekuwa yakifanyika kwa miezi kadhaa sasa haijulikani ni lini yatakamilika na kuanza kutekelezwa na ni kwa kiasi gani Bunge letu ambalo linajukumu la kutoa baraka zake kwenye mikataba ya serikali linahusika.
Mkataba huo wa Kupromoti na Kulinda Uwekezaji wa Kigeni ujulikanao kwa kiingereza kama "Foreign Investment Promotion and Protection Agreement" (FIPA) utakuwa ni mkataba wa pili kuingiwa na serikali ya Canada na nchi ya Kiafrika. Mkataba kama huo uliingiwa kati ya Canada na Afrika ya Kusini mwaka 1995, ingawa bado haujaanza kufanya kazi.
Kwa mujibu wa taarifa za Taasisi ya Mambo ya Nje na Biashara ya Canada, makubaliano ya FIPA yana malengo makubwa ya kumlinda mfanyabiashara au shirika la Kikanada linapofanya biashara katika nchi ya kigeni. Kwa mujibu wa taasisi hiyo "Makubaliano ya FIPA yanamhakikishia mwekezaji wa Kikanada kuwa atakuwa na nafasi sawa ya ushindani katika biashara sawa sawa na washindani wengine wa nje au wa ndani ya nchi husika".
Kwa maneno mengine endapo Mkataba kama huu utaingiwa basi wawekezaji wetu wazalendo watapaswa kushindana na Taifa kubwa na wafanyabiashara wakubwa wa Kikanada kana kwamba wako sawasawa kwa mitaji, uzoefu, raslimali na uwezo.
Zaidi ya yote makubaliano ya FIPA yanahakikisha kuwa unapotokea mzozo wa kibiashara mahakama za ndani zinawekwa pembeni na zaidi kukimbilia kwenye mahakama za kimataifa. Kwa uamuzi kama huo mahakama hizo nyingi za Kimataifa ziko tayari kwenye nchi za magharibi na mara nyingi zimekuwa zikitetea na kusimama upande wa nchi za Kibepari za Magharibi. Kwa kukwepa kutumia mahakama na sheria zetu, mkataba wa FIPA unaweza kabisa kutuingiza katika wavu wa kisheria kama uliotukuta wakati wa mkataba wa IPTL.
Endapo mkataba wa FIPA utaingiwa siyo tu utaifunga serikali kuu bali pia utafunga kwa masharti hayo hayo tawala za mikoa na serikali za mitaa.
Siku chache zilizopita tovuti hii na vyombo vingine vya habari kufunua habari za kushindwa kwa kampuni ya Barrick toka Canada kuwashawishi wabunge wa Muungano kutokukubali mapendekezo ya Kamati ya Bomani iliyoundwa kutoa ushauri kuhusu sekta ya madini.
Kampuni hiyo ikipigwa tafu na Balozi wa Kanada nchini ilijitahidi kwa karibu wiki nzima kuwashawishi wabunge mbalimbali kubadili misimamo yao ili hatimaye baadhi ya mapendekezo ambayo yanaigusa kampuni hiyo yasipokelewe. Hata hivyo baada ya kushindwa katika kujipigia debe, njia ambayo sasa inataka kutumiwa ni ile ambayo kimsingi itaifunga Tanzania katika makubalianao ambayo itakuwa ni vigumu sana kujitoa hapo baadaye.
Tunaendelea kufuatilia ili kujua kwa undani ni jinsi gani makubaliano haya yatakapoingiwa yataathiri uwekezaji wa kampuni za Kanada hasa katika sekta ya madini. Unaweza kusoma na kujifunza zaidi kuhusu FIPA kupitia hapa:
http://www.international.gc.ca