CAG 2019/20: Mapungufu katika Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
Mamlaka ya Serikali za Mitaa zinajukumu la kusimamia idadi kubwa ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini. Miradi hii yenye lengo la kutoa huduma za kijamii, hutekelezwa kwa fedha za ruzuku inayotumwa kutoka Serikali Kuu na kiasi fulani huchangiwa na mapato ya ndani ya Halmashauri husika pamoja na wananchi. Hata hivyo, utekelezaji wa miradi hiyo umekuwa na kasoro zifuatazo;

1. Mamlaka ya Serikali za Mitaa 152 hazikupokea TZS 410.4 bilioni sawa na asilimia 46 ya fedha za miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2019/20. Mamlaka ya Serikali za Mitaa 73 ziliathirika zaidi kwa kutopokea zaidi ya asilimia 50 ya bajeti iliyoidhinishwa kama inavyoonekana katika jedwali Na. 1. Halmashauri ya Mji wa Ifakara haikupokea fedha yoyote ya ruzuku ya miradi ya maendeleo kwa mwaka 2019/20.

2. Hazina na washirika wa maendeleo hawakutoa fedha za miradi ya maendeleo kiasi cha TZS 53.4 bilioni sawa na asilimia 22 ya bajeti iliyoidhinishwa. Fedha hizo zilitakiwa kutekeleza miradi 10 katika sekta za maji, kilimo, afya na elimu inayotekelezwa na watekelezaji wa miradi 144.

Hii imetokana na watekelezaji kushindwa kuwasilisha kwa wakati taarifa za utekelezaji wa miradi kwa Wizara ya Fedha na Mipango. Hii ni kinyume na makubaliano baina ya watekelezaji na Wizara (Hazina).

Kutotolewa kwa fedha za miradi ya maendeleo, kuliwasababishia watekelezaji kushindwa kupewa fedha. Mfano, sekta ya maji haikupokea kiasi cha TZS 20.8 bilioni sawa na asilimia 16 ya bajeti iliyoidhinishwa ikifuatiwa na sekta ya afya kwa kiasi cha TZS 19.5 bilioni sawa na asilimia 23 ya bajeti iliyoidhinishwa kwa sekta husika.

3. CAG alibaini zaidi ya miradi ya maendeleo 68 yenye thamani ya TZS 18.3 bilioni ilikuwa imekamilika lakini haitumiki. Miradi hii ilitekelezwa kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa 40 ikihusisha miradi ya ujenzi wa masoko, ujenzi wa hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati, ujenzi wa miundombinu ya shule (nyumba za walimu, vyoo na madarasa) na ujenzi wa maeneo ya machinjio.

Athari
1. Halmashauri kushindwa kukamilisha miradi ya maendeleo kwa wakati na mingine kutotekelezwa kabisa. Mfano kwa mwaka 2019/20, jumla ya miradi ya maendeleo 266 yenye thamani ya TZS 184 bilioni katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa 101 haikukamilika.

Vilevile, zaidi ya miradi ya maendeleo 76 iliyopangwa kutekelezwa kwenye Halmashauri 6 (Halmashauri za Wilaya Sumbawanga, Kyela, Mvomero na Tarime, Halmashauri ya Mji Tarime na Halmashauri ya Manispaa ya Musoma) yenye thamani ya TZS 4.4 bilioni haikutekelezwa kutokana na kutopokea fedha za miradi ya maendeleo kutoka Hazina

2. Kutokukamilika kwa miradi kwa wakati hukosesha wananchi kupata huduma zilizokuwa zimekusudiwa endapo miradi hiyo ingekamilika kwa wakati, na

3. Miradi yote ya Serikali hufanywa kwa malengo mahususi ya kuwapatia wananchi huduma. Kutokutumika kwa miradi iliyokamilika kunawanyima wananchi kupata huduma iliyokusudiwa na kutokuwepo kwa thamani ya fedha.

Ushauri:

Ili kutatua kasoro zilizoainishwa, WAJIBU inashauri yafuatayo;

1. Serikali kuziwezesha Halmashauri kukamilisha miradi iliyokwisha anza kabla ya kuanza miradi mipya. Hii ni pamoja na kuhakikisha kwamba, miradi yote iliyokamilika inapatiwa vifaa wezeshi pamoja na rasilimali watu ili iweze kuwahudumia wananchi

2. Wizara ya Fedha na Mipango (Hazina) na watekeleza miradi wafuate makubaliano waliojiwekea na washirika wa maendeleo kwa kuwasilisha kwa wakati taarifa za utekelezaji wa miradi ili fedha ziweze kutolewa kwa wakati

3. Mamlaka ya Serikali za Mitaa ziendelee kuimarisha ufuatiliaji na usimamizi wa mifumo ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuimarisha ushirikishwaji wa wananchi katika kupanga, kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo ili kuleta umilikishwaji na uendelevu wa miradi hiyo

4. Waheshimiwa Madiwani na Menejimenti za Halmashauri zifuatilie na kuhakikisha gharama za uendeshaji wa miradi inayokaribia kukamilika zinaingizwa kwenye bajeti ya mwaka unaofuata ili miradi hiyo itakapo kamilika kusiwe na visingizio vya kutokuwepo kwa bajeti ya uendeshaji.

WAJIBU INSTITUTE
 
Back
Top Bottom