Amani Girls Organization
Member
- Feb 17, 2024
- 23
- 11
Waswahili wanasema, “Ukiona vyaelea, vimeundwa.”Hivyo ndivyo, wanafunzi wa shule ya msingi ya Mnane na Kikio, Mkoani Singida wanavyoandaliwa mazingira mazuri ya kujifunza kuhusu kilimo na lishe bora. Shirika la Amani Girls (AGO) kwa kushirikiana na walimu wa mazingira na wanafunzi wa shule ya msingi Mnane na Kikio, wamekuwa wakilima na kuzihudumia bustani za mboga za majiani (mfano loshuu, mchicha, spinachi) kama mfano wa kujifunza kwa vitendo.
Bustani hizi zimekuwa zikitunzwa kwa zamu na wanafunzi wa darasa la 6 katika shule hizi mbili. Kwa wastani darasa la 6 lina wanafunzi takribani 76, ambapo hulima matuta, kumwagilia kwa kuweka ndoo ambazo hutoa maji kidogo kidogo kwenye matuta hayo. Ndoo hizi zimefungwa kwa ustadi kwa kuunganishwa na mipira maalum yenye matundu madogo madogo ambayo yanapitisha maji ili kumwagilia matuta haya ya mboga. Ndoo hizi huwekwa maji kila siku asubuhi na jioni (kabla na baada ya masomo).
Bustani hizi zinalenga kuwapa wanafunzi, ujuzi na mbinu ambazo zitawasaidia kuandaa bustani kama hizo majumbani kwao ili basi familia zipate lishe iliyo bora. Pia, ujuzi huu utawasaidia pale watakapoanza kilimo kwa siku za baadae, kuweza kuyahudumia vyema mashamba yao na kupata mavuno bora.
Mradi huu unatekelezwa Mkoani Singida na Shirika la Amani Girls kwa kushirikiana na Stromme Foundation Tanzania.
#AmaniGirls