Rubawa
JF-Expert Member
- Dec 25, 2015
- 2,055
- 3,266
BARAZANI
Na Ahmed Rajab
SIKU moja, siku yenyewe hasa nimeisahau,lakini ilikuwa Juni mwaka 1973, nilijikuta ndani ya lifti iliyojaa watu kwenye jengo la Bush House, katikati ya jiji la London. Hii leo jengo hilo ni hoteli lakini miaka hiyo lilikuwa makao ya matangazo ya nchi za nje ya idhaa za Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), ambalo enzi hizo nilikuwa mmoja wa watangazaji wake.
Miongoni mwa waliokuwa ndani ya lifti alikuwa Robin White, mtangazaji na baadaye mhariri wa kipindi cha redio cha “Focus on Africa” kilichokuwa kikivuma miaka hiyo. Pia alikuwemo mgeni wake aliyekuwa anakwenda naye studio kumhoji.
Huyo mgeni alikuwa sababu ya mimi kuwemo ndani ya hiyo lifti kwani alikuwa amekwishanitafuta niwe naye kwa wakati huo. Ghafla nikahisi mkono unatoka kwenye mfuko wa kulia wa suruali yangu. Sijui mkono huo uliingiaje mfukoni mwangu bila ya mimi kuhusu. Nilichohisi ni kitu kilichoachwa humo. Kisa hicho kilikuwa cha kufumba na kufumbua macho na sitokisahau kamwe. Hakuna mwengine aliyeshuhudia yaliyojiri.
Niliponyanyua kichwa changu nilimuona mgeni wa Robin akinikodolea macho huku akitabasamu. Alikuwa Marcelino dos Santos, aliyefariki dunia Maputo, Msumbiji Jumanne ya wiki iliyopita akiwa na umri wa miaka 90 na cheo cha kijeshi cha umeja-jenerali.
Alichowacha mfukoni mwangu ilikuwa ni bahasha ikiyokuwa na waraka ulioandikwa jela na Abdulrahman Babu, waziri wa zamani wa Tanzania na kiongozi wa chama cha zamani cha Umma Party cha Zanzibar ambaye wakati huo alikuwa mfungwa wa Rais Julius Nyerere.
Babu aliiandika barua yake kwa mkono jela ikahaulishwa na kumfikia aliyekuwa mkewe na komredi mwenzake Ashura Hilal (maarufu Ashura Babu). Yeye ndiye aliyempa Marcelino anifikishie.
Marcelino, aliyekuwa mshairi na mwanamapinduzi, alikuwa miongoni mwa wanasiasa washupavu wa Kiafrika wa mrengo wa kushoto waliotusaidia chini kwa chini katika kampeni yetu ya kumpigania Babu pamoja na makomredi wengine waliokuwa wamefungwa Zanzibar na Tanzania Bara. Baadhi yao walikuwa wamehukumiwa kifo.
Halikuwa jambo la ajabu kwa Marcelino kuwa na msimamo huo. Alikuwa mpigania haki kote kulikokosekana haki.
Ni sahihi kabisa kusema kwamba Marcelino dos Santos alikuwa kiongozi wa kihistoria si kwao Msumbiji tu bali Afrika nzima. Alizaliwa Lumbo, mji wa bandari ulio kaskazini-mashariki kwenye mwambao wa Msumbiji mkabala na Bahari ya Hindi.
Hata hivyo, Marcelino alikuwa mtoto wa mjini kwa sababu alikulia Maputo, siku hizo za utawala wa Kireno ikiitwa Lourenço Marques.
Alipokuwa kijana mdogo alikuwa akimuona baba yake Firmino do Santos, aliyekuwa ameajiriwa kuendesha gazeti moja la Msumbiji, akizikumbatia siasa akiwa mwanaharakati wa Jumuiya ya Kiafrika ya Msumbiji, iliyokuwa kwa hakika jumuiya ya kisiasa. Hapo ndipo Marcelino, aliyechanganya damu ya Kireno na ya Kimsumbiji, alipoanza kuuonja utamu wa siasa, utamu anaokuwa nao mtu anapokuwa anapigania haki.
Marcelino aliondoka Msumbiji kwenda Ureno kwa masomo ya juu akiwa na miaka 18. Jijini Lisbon ndiko siasa zilipozidi kumkolea. Huko alikutana na wanafunzi kutoka makoloni mengine ya Ureno barani Afrika. Walikuwa wakikutana kwenye nyumba moja iliyokuwa ikiitwa “Casa dos Estudantes do Império” (CEI).
Nyumba hiyo ilikuwa maskani ya wanafunzi kutoka makoloni ya Ureno waliokuwa wakisoma kwenye vyuo vikuu katika miji ya Lisbon, Coimbra na Oporto. CEI, iliyofunguliwa mwaka 1944, ilikuwa muhimu sana kwa mwamko wa kisiasa wa wanafunzi hao. Wakiwa humo wanafunzi wakijihisi kuwa wako huru kama walikuwa kwenye chemchemi ya demokrasia na uhuru.
Miongoni mwa wanafunzi aliokutana nao huko Marcelino walikuwa pamoja na Agostinho Neto, Eduardo Mondlane, Amilcar Cabral, Mário Coelho Pinto de Andrade, Francisco Tanreiro na Lúcio Lara. Wao na wenzao walikuwa wakikutana na kupanga shughuli za kisiasa wakitumia nyenzo za kitamaduni na kazi za kifasihi zilizokuwa zikiupinga ukoloni. Ndio maana miongoni mwao kukachomoza waandishi wa riwaya na washairi.
Wanafunzi wa CEI walijiunga na vyama mbalimbali vya upinzani vya Ureno. Waliunda pia Vuguvugu la Wanafunzi wa Kiangola, “Movimento dos Estudantes Angolanos” (MEA).
Vuguvugu hilo la MEA lilitayarisha na kutekeleza ule uitwao mpango wa “fugas dos 100”, mpango wa kuwatorosha wanafunzi 100 wa Kiafrika kutoka Lisbon na sehemu nyingine za Ureno na kuwapeleka Paris, Ufaransa. Inahitaji tuandike kitabu kizima kuhusu kutoroshwa kwa wanafunzi hao hadi Ufaransa. Naitoshe tu hapa tukisema kwamba vijana hao walisaidiwa, kwa mujibu wa mwandishi mmoja, na Baraza la Dunia la Makanisa ya Kiprotestanti, Jumuiya ya Wanafunzi wa Kiprotestanti (Cimade) yenye makao yake Paris, majasusi watatu wa Shirika la Ujasusi la CIA na serikali ya Ufaransa.
Kulikuwa na mshikamano mkubwa baina ya wanafunzi wa Kiafrika waliokuwa Lisbon na Paris. Walikuwa kitu kimoja wakiupiga vita ukoloni wa Kireno. Ni wao walioliasisi vuguvugu la mwanzo la kupinga ukoloni wa Kireno — “Movimento Anti-colonialista” (MAC) — mnamo mwaka 1957, Marcelino akiwa Paris. Viongozi wakuu wa vuguvugu hilo walikuwa Amilcar Cabral (akiwakilisha Guinea-Bissau na Cape Verde), Marcelino dos Santos (Msumbiji), Guilhermino de Espírito Sante (São Tomé e Principe), Mário de Andrade, Lúcio Lara na Viriato da Cruz (wote kutoka Angola).
Kufikia mwaka 1950 Agostinho Neto kutoka Angola alikuwa amekamatwa na Eduardo Mondlane kutoka Msumbiji alikuwa amekwishaondoka Ureno na kuhamia Marekani.
Kina Marcelino na wenzake 99 walilazimika kukimbia kutoka Ureno kwa sababu walikuwa wamekwishaanza kuandamwa na vyombo vya ulinzi vya Ureno, hususan idara yake ya usalama ya PIDE iliyokuwa hailali wakati wa utawala wa dikteta António de Oliveira Salazar. Ukatili wa PIDE ulipindukia ule wa uhayawani, watesaji wake wakitesa kinyama.
Alipowasili Paris Marcelino alijiunga na Chuo Kikuu maarufu cha Sorbonne ambako alihitimu shahada ya sayansi ya uchumi na elimu-jamii.
Wakati huo huo alikuwa akiogolea katika duru za wasomi waliokuwa wakifungamana na lile jarida la kifasihi la “Présence Africaine”. Marcelino alikuwa akichanganyika zaidi na waandishi na wasanii.
Alipokuwa Paris ndipo pia alipojiunga na tawi la huko la Uniao Democratica Nacional de Moçambique (UDENAMO), moja ya makundi ya Msumbiji ambayo baadaye yaliungana kuunda Frelimo mwaka 1962.
Marcelino alihusika na kuasisiwa kwa Mkutano wa Jumuiya za Kizalendo za Makoloni ya Ureno (CONCP) uliofanywa Casablanca mwaka 1961. Kwenye mkutano huo alichaguliwa awe mratibu wa harakati za kizalendo. Kwa vile alikuwa mtu fasaha Marcelino alifanikiwa pa kubwa katika kuuelezea ulimwengu dhamira na shabaha za CONCP.
Baada ya kuuawa Mondlane, Rais wa mwanzo wa Chama cha Ukombozi wa Msumbiji, Frelimo, jijini Dar es Salaam Februari 3, 1969, Marcelino alichaguliwa awe mjumbe wa Baraza la Urais wa Frelimo lililokuwa na wajumbe watatu. Wenzake walikuwa Uria Simango na Samora Machel. Mwaka 1970, Samora alipoibuka Rais wa pekee wa Frelimo, Marcelino alikuwa makamu wake. Aliushika wadhifa huo hadi 1977. Mwishoni mwa mwongo wa 1977 alichaguliwa waziri wa maendeleo ya kiuchumi na katika miaka ya 1980 alichaguliwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Kisiasa ya Frelimo aliyesimamia uchumi. Alikuwa Spika wa Bunge kuanzia 1987 hadi 1994 na kwa muda wa miaka mingi baadaye aliendelea kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Frelimo.
Maisha yake yote alikuwa mrengo wa kushoto wa Frelimo akiendelea hadi alipofariki kuushikilia uzi wake ule ule wa itikadi ya Umarx na Ulenin japokuwa Msumbiji imeukumbatia ubepari kwa miongo kadhaa sasa.
Akiamini kwamba ubepari ulikuwa unapita njia tu Msumbiji na ulihitajika ili nchi yake ipate msaada wa madola ya Magharibi kupambana na waasi wa Renamo. Akiamini pia kwa dhati kwamba baadaye hali za mambo zitageuka na Msumbiji italazimika iifuate itikadi ya kisiaa itayoleta usawa katika jamii.
Juu ya hayo Marcelino alifariki akiwa amevunjika moyo kwa jinsi ufisadi ulivyosambaa Msumbiji na zaidi katika Angola, nchi nyingine aliyoipenda na aliyokuwa na matumaini makubwa nayo.
Marcelino alikuwa chanda na pete na Rais wa mwanzo wa Angola, Agostinho Neto. Siku Neto alipotangaza uhuru wa Angola huko Luanda, Marcelino alikuwa ubavuni mwake.
Washairi hao wawili na wanamapinduzi walikuwa wandani wakubwa tangu ujanani mwao walipokuwa Ureno, ingawa Neto alimzidi umri Marcelino kwa miaka saba.
Wakati wa harakati za ukombozi walijikuta wakiishi Dar es Salaam kulikokuwa makao ya Kamati ya Ukombozi wa Afrika katika miaka ya 1960 na 1970. Familia zao zikiingiliana sana pamoja na ya Babu na makomredi wengine kutoka Zanzibar.
Nitamkumbuka Marcelino kwa ucheshi wake, ile kadhia ya kwenye lifti na kwa mashairi yake.
Marcelino dos Santos alijibandika majina mengine mawili aliyoyatumia alipokuwa akiyachapisha mashairi yake. Mashairi yake ya mwanzo aliyaandika akitumia majina ya “Kalungano” na “Lilinho Micaia”. Yamo kwenye diwani iitwayo “O Brado Africano” (tafsiri isiyo rasmi: Kilio cha Kiafrika}.
Mashairi yake mengine yamo kwenye diwani mbili zilizochapishwa na CEI, huko Lisbon. Akitumia jina la uandishi la Lilinho Micaia alichapisha diwani moja Urussi na mwaka 1987 alichapisha diwani nyingine akitumia jina lake rasmi. Diwani hiyo, iliyochapishwa Msumbiji, inaitwa “Canto do Amor Natural” (tafsiri isiyo rasmi: Wimbo wa Mapenzi Asilia).
Serikali ya Maputo ilifanya vyema kumtunukia nishani ya Ushujaa wa Kitaifa mwaka 2015 alipokuwa bado yu hai badala ya kungoja mpaka alipofariki. Na alipofariki bendera za Msumbiji zilipepea nusu mlingoti kwa siku saba ikiwa ishara ya kuombolezwa na taifa.
Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab