Feedback
JF-Expert Member
- Mar 14, 2011
- 7,988
- 4,514
- Asema mwenendo wa wabunge si mzuri
- Umepotezea Bunge mvuto kutokana na vituko
Makinda alisema hayo wakati akimkaribisha Mbunge wa Dole (CCM), Sylvester Mabumba, kuongoza mjadala wa wabunge kuhusu bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012, baada ya yeye (Spika Makinda) kubanwa na shughuli nje ya ukumbi wa Bunge. Alisema hivi sasa taswira ya Bunge imekuwa si nzuri kwa watu wanaofuatilia shughuli zake kutokana na baadhi ya wabunge kuongea bungeni bila kufuata utaratibu. Spika Makinda alisema kitendo hicho kimekuwa kikisababisha kero kwa watu na hivyo kushindwa kufuatilia shughuli za Bunge.
Napigiwa simu nyingi na kuandikiwa ujumbe, image (taswira) yetu mbele ya jamii siyo nzuri. Kuongea bila utaratibu tunatumia muda, ambao wachangiaji wangekuwa wengi, alisema Spika Makinda. Aliongeza: Jamani tuendelee kukua, tusiendelee kuwa kero kwa watu. Walikuwa wanapenda sana kuangalia sana kipindi hiki, lakini sasa wengine wanakereka sana kwa tabia zetu. Kwa hiyo tubadilike, muwe watu waheshimiwa kama tunavyoheshimiwa na watu waliotuchagua.
Kauli ya Jumatano iliyopita aliyoitoa wakati akitoa matangazo na ufafanuzi wa masuala mbalimbali bungeni akieleza kusikitishwa kwake na mwenendo wa wabunge ndani ya Bunge kwa kufanya mambo kinyume cha kanuni zinazokubalika, alifananisha hali hiyo na kama watu wako Kariakoo. Awali Makinda alisema kuwa alichokuwa amefanya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Rasmi Bungeni, Freeman Mbowe, kwa kutaka mwongozo wa Spika baada ya kupata majibu yasiyoridhisha kutoka kwa Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu, alikuwa sahihi na si kama wanavyofanya wabunge wengine wanaopiga tu kelele za kuomba mwongozo wa Spika wakati mzungumzaji akiwa bado anaendelea kuzungumza kama wako Kariakoo. Makinda alisema kimsingi, mwongozo wa Spika unaomwa mara tu baada ya tukio husika kumalizika ndani ya Bunge, kama ambavyo alikuwa amefanya Mbowe.
Ni katika muktadha huo, Spika aliwataka wabunge kuacha kufanya mambo ya ovyo wanapokuwa katika vikao vya Bunge kwani wanatia aibu kwa watu wanaowatazama na wameligeuza Bunge kama Kariakoo. Vile vile, aliwaasa wasome vizuri bajeti ili watakapochangia wachangie vitu vya msingi badala ya kuzungumza mambo yasiyohusu bajeti. Alisema alisikitishwa na hali iliyotokea Jumanne wiki iliyopita katika kikao cha jioni kilichokuwa kikiongozwa na Mwenyekiti wa Bunge, George Simbachawene. Alisema katika kikao hicho wabunge walifanya vituko vya ajabu kiasi cha yeye (Makinda), kushindwa kuendelea kuangalia mwenendo wa kikao hicho.
Hii ni aibu kubwa na sijui kwa nini mnajidharaulisha kwa wananchi, mnajua watu huko nje wanawaheshimu sana, sasa mkifanya mambo ya ovyo wanawadharau na mjue haya yote yanayofanyika humu yanaonekana, mimi mwenyewe nilikuwa naangalia, lakini nikashindwa kuendelea kwani nilikuwa naona vitu vya ajabu ajabu, alisema Makinda na kuongeza kuwa:
Hapa bungeni kuna utaratibu wa kuzungumza, mtu akiwa anazungumza wengine mnapaswa kumsikiliza, lakini jana (Juzi) mtu mmoja anachangia na wengine wanazungumza utadhani mko Kariakoo.
Katika kikao kilichoongozwa na Simbachawene, wabunge walikuwa wakiwasha vipaza sauti vyao na kutoa maneno ya vijembe kwa wenzao na wengine wakizomea wachangiaji. Hali hiyo ilimpa wakati mgumu Simbachawene, ambaye alikuwa akilazimika kuwakatisha wabunge waliokuwa wakiomba mwongozo ili kuwabana wazungumzaji walioonekana kuwakejeli wengine.
Waheshimiwa wabunge tutumie muda wetu kujadili huu mpango ulio mbele yetu, nikiruhusu kila mtu asimame atoe mwongozo muda wote tutakuwa tumeupoteza bure, naomba tuwe makini, alisema Spika Makinda. Baada ya kurusha kombora kwa watu wa Kariakoo, mchana Makinda alilazimika kuomba radhi kutokana na tafsiri iliyoonekana kuwakera baadhi yao. Kauli kwamba wabunge wasizungumze kama wako Kariakoo ilionekana kuwakera baadhi ya watu waliomtumia ujumbe wakimweleza kuwa amewadhalilisha na kwa kuonyesha kuwa eneo hilo halina maana.
Nawaomba radhi waliokwazika na kauli yangu, lakini sikumaanisha kuwadharau watu wa Kariakoo, nilichokuwa na sema ni kwamba watu watofautishe kati ya kuzungumza bungeni na mitaani, hapa bungeni kuna taratibu zake za kuzungumza, mtu mmoja akizungumza wengine mnapaswa kumsikiliza tofauti na sehemu kama sokoni Kariakoo ambapo mtu mmoja anaweza kuwa anazungumza na wengine wanazungumza wakati huo huo.
Ijumaa iliyopita, wakati wa kuchangia bajeti, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alijikuta katika wakati mgumu kwa kukatishwa kuzungumza na Mwenyekiti, Jenista Mhagama. Kwanza alimtaka kufuta kauli yake kuwa serikali inaua watu akitolea mfano mauaji ya watu watano katika mgodi wa North Mara na ya watu watatu waliouawa mjini Arusha wakati wa maandamano ya Chadema Januari 5, mwaka huu. Safari ya pili alimkatiza akimwekekeza kuwa kanuni za Bunge zinakataza kuwataja wabunge wengine kwa majina na badala yake azungumze na kiti. Alisisitiza kwamba utamaduni na kanuni za Bunge zinataka mzungumzaji yeyote kuzungumza na kiti na si kujibishana na mbunge mwingine au waziri.
Baada ya maelekezo hayo Msigwa aliendelea kuchangia hoja bajeti, na alipomaliza alisimama Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher ole Sendeka, akitaka Mwenyekiti asaidia kuwasilishwa kwa maelekezo kwa wabunge juu ya maadili ya kuzungumza bungeni kwa kuwa Msigwa alikuwa ameongea maneno ya kuudhi kwa kuifananisha serikali ya Tanzania tangu uhuru sawa na mtoto wa miaka miwili anayelialia tu.
Sendeka alisema kuwa Tanzania imekuwa na wasomi bora na mabingwa, wako katika nchi mbalimbali duniani, wanaongoza taasisi kubwa duniani kama Umoja wa Mataifa na kwingineko; imekuwa na marais watatu, akiwamo Mwalimu Nyerere ambaye anahesimiwa duniani; Rais Ali Hassan Mwinyi. Rais Benjamin Mkapa na sasa Rais Jakaya Kikwete. Alisema serikali zote hizo zimefanya kazi vizuri, zinaaminika na kuheshimiwa na mataifa yote duniani.
Kwa maana hiyo, alisema hata kuwako kwa Msigwa ndani ya Bunge ni mafanikio ya serikali hizo, kwa maana hiyo kuifananisha na mtoto wa miaka miwili ni maneno ya kuudhi. Alimtaka Mwenyekiti Mhagama kutoa mwongozo ama kwa kumshauri spika atoe mwongozo kwa wabunge jinsi ya kuzungumza kwa wabunge bungeni na jinsi ya kuhesimu serikali yao. Mhagama alikubaliana na Sendeka na kusema kuwa atawasiliana na Spka ili aone kama anaweza kufanya nini ikiwa ni pamoja na uwezekano kurekebisha kanuni za Bunge.
Kabla suala hilo halijapo, aliibika Waziri wa Nchi, Ofisi Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, kumwomba mwenyekiti wa bunge amtake mbunge huyo athibitishe kauli yake juu ya Waziri Mkuu kwenda na ndege mbili Iringa na magari 50. Kabla ya kutoa uamuzi, Mhagama alimweleza Msigwa athibitishe madai yake au ayafute. Katika mtafaruku huo ndani ya Bunge, Kambi ya Upinzani Rasmi Bungeni kupitia kwa Mnadhimu Mkuu, Tundu Lissu, Ijumaa iliyopita ilitangaza kwamba itamshitaki Makinda katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kanunu za Bunge, kwa madai kuwa anapindisha kanuni kwa kuwapendelea mawaziri na wabunge wa CCM na kuwakandamiza wapinzani.
Kambi ya Upinzani Rasmi inaundwa na wabunge wa Chadema. Jana NIPASHE ilifuatilia malalamiko ya Upinzani kama yamefikia wapi, lakini John Joel, Kaimu Katibu wa Bunge, alisema kuwa Upinzani haujawasilisha malalamiko yao dhidi ya Spika. Wakati hayo yanajiri, leo wabunge wanatarajiwa kupitisha bajeti ya serikali iliyowasilishwa Juni 8, mwaka huu na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo. Kulingana na mwenendo wa uchangiaji wa mjadala wa bajeti, huenda wabunge wa upinzani wataibana serikali kuhusiana na mambo kadhaa, kubwa likiwa ni suala la kutaka posho za wabunge kuhudhuria vikao zifutwe.