Born Too Soon: Unayopaswa Kujua kuhusu Watoto Njiti

Sildenafil Citrate

JF-Expert Member
Jan 29, 2021
573
2,555
Unjiti ni hali ya Mtoto kuzaliwa kabla ya Wiki ya 37 ya Ujauzito kutokana na Sababu Mbalimbali ikiwemo Mjamzito kupata Uchungu wa Mapema.

Watoto hawa huzaliwa na Changamoto nyingi zinazohitaji Uangalizi wa karibu ili kuwaepusha na Vifo au Ulemavu wa Maisha.

Ripoti ya Born Too Soon
Kwa Mujibu wa Takwimu, Katika kila kundi la Watoto 10 wanaozaliwa, Mtoto 1 huwa na hali hii.

Unjiti unatajwa kuwa sababu namba moja ya Vifo vya Watoto wenye umri chini ya Miaka 5. Mwaka 2020, 9.9% ya Watoto wote waliozaliwa duniani walikuwa Watoto Njiti.

Takriban 45% ya Watoto Njiti walitokea Nchi 5 pekee. India ilikuwa na idadi kubwa zaidi (3,016,700) ikifuatiwa na Pakistan (914,000), Nigeria (774,100), China (752,900) na Ethiopia (495,900)

Hali ya Ujiti inaweza kusababisha Changamoto za Muda mrefu zinazohusisha mfumo wa Upumuaji na Moyo. Baadhi ya Watoto hukabiliwa pia na ukuaji hafifu wa Mfumo wa Neva za Fahamu unaoweza kuathiri tabia za baadae ikiwemo Kujifunza.

Uwepo wa Uangalizi na huduma Sahihi za Kimatibabu wakati na baada ya Kuzaliwa husaidia kuepusha Changamoto hizi na kuboresha hali ya Maisha ya Mtoto.

Sonona ya Uzazi na Msongo wa Mawazo
Wanawake wanaojifungua Watoto Njiti huwa kwenye hatari kubwa ya kupatwa na Sonona ya Uzazi na Msongo wa Mawazo unaoweza kuathiri Malezi ya Mtoto kuliko Wanawake Wanaojifungua kwenye Muda sahihi

Kupunguza athari hizi, Shirika la Afya Duniani (WHO) hushauri Wiki 6 za Mwanzo baada ya Kujifungua zitumike Kufuatilia kwa Ukaribu Afya ya Mama na Mtoto

Ufuatiliaji huu husaidia pia kushughulikia Changamoto za Kiafya zinazomkabili Mtoto na Kuepusha Vifo visivyo vya lazima

Kuboresha Mfumo wa Rufaa
Kama Sehemu ya Mipango ya kupunguza Vifo vitokanavyo na Uzazi pamoja na vile vinavyohusisha Watoto Njiti, Mifumo ya Utoaji wa Rufaa kwenye Vituo vya Afya inapaswa kuboreshwa.

Hii itarahisisha upatikanaji wa Haraka usio na Mchakato mrefu wa Huduma za Msingi zinazoweza kuokoa Uhai wa Mama na Mtoto.

Uwekezaji Mkubwa wa Vifaa Tiba vya Kisasa na Kuongeza Wigo wa Upatikanaji wa Dawa Muhimu kwenye Vituo hivyo unapaswa pia kufanyika.

Ukosefu wa Tafiti Mpya
Miaka 10 iliyopita imeshuhudia Jitihada Ndogo za kupunguza Idadi ya Watoto Njiti wanaozaliwa kila Mwaka Duniani japokuwa baadhi ya Sababu zinazopelekea kuzaliwa kwao zinafahamika.

Pia, Tafiti Mpya za Kiuchunguzi zenye lengo la kubaini Sababu zisizojulikana zinazopelekea Kuzaliwa kwa Watoto hawa Hazijafanyika kwa Kiwango Kikubwa.

Tafiti zaidi za Watoto Njiti zinapaswa Kufanyika ili zisaidie kuongeza Uelewa wa Mambo yanayowahusu na jinsi wanavyoweza Kuzuiliwa.

Uwekezaji wa huduma za Afya ili kuongeza Uwezekano wa kuishi
Watoto Njiti wanaopatiwa Huduma Bora za Afya, hata kama Wamezaliwa wakiwa na Wiki 28, huwa na Uwezekano wa Kuishi kwa zaidi ya 95% huku wanaozaliwa kwenye Mazingira duni yasiyo na Huduma Bora wakiwa na uwezekano wa Chini ya 5% za Kuishi

Vifo hivi vinaweza kupunguzwa kwa kufanya Uwekezaji Mkubwa kwenye Sekta ya Afya pamoja na Kuanzisha Vitengo vya Huduma ya Watoto Wachanga kuanzia ngazi ya Vijijini

Uwekezaji huu lazima uwaweke katikati Wanawake na Watoto ili kufanikisha Haki zao za Msingi za kupata Huduma zinazojali Utu, Shirikishi na zenye Ubora wa hali ya juu.

Ndoa za Utotoni Chanzo cha Watoto Njiti
Ndoa za Utotoni huwaweka Wasichana kwenye hatari ya kukutana na Ukatili wa Kijinsia unaoweza kuchangia Kuzaliwa kwa Watoto Njiti.

Huongeza pia idadi ya Watoto Wanaozaliwa wakiwa na Uzito mdogo na wale Wanaofariki kabla ya Kuzaliwa.

Ndoa hizi zinapaswa Kukomeshwa ili kupunguza Vifo vitokanavyo na Uzazi pamoja na Idadi ya Watoto Wanaozaliwa wakiwa na Changamoto mbalimbali zikiwemo za Unjiti.

Madhara ya Mabadiliko ya Tabianchi
Ni Muhimu kuchukua hatua za kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi ili kulinda Afya na Ustawi wa Watoto Njiti.

Hatua hizi ni pamoja na kupunguza uzalishaji wa Gesi chafu, Kuongeza ufikiaji wa huduma bora za Lishe na kuimarisha utayari wa kukabiliana na Majanga ya Asili.

Hii itasaidia kupunguza Changamoto mbalimbali za Kiafya zinazoweza kuchangia Ongezeko la Vifo na Ulemavu wa Kudumu.

Chanzo: Born Too Soon
 
Back
Top Bottom