Bila tume huru hakuna uchaguzi huru

RAKI BIG

JF-Expert Member
Apr 26, 2020
394
456

(Hotuba ya Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Ndugu Maalim Seif Sharif Hamad,Mwenyekiti wa Chama Taifa Kuhusu Masuala ya Msingi Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2020)

Ndugu Watanzania,
Kama inavyofahamika, 2020 ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu. Tanzania inatarajiwa kufanya uchaguzi wa madiwani, wabunge, wawakilishi na urais tarehe 25 Oktoba 2020.

Ulimwenguni kote, kipindi cha uchaguzi mkuu ni kipindi cha kipekee cha kuamua kuijenga nchi au kuibomoa nchi. Uchaguzi unaoiacha nchi salama ni lazima ufanyike kwenye mazingira ya uhuru na haki. Kinyume chake, chaguzi huzaa uhasama, chuki na machafuko katika Taifa. ACT Wazalendo tungependa uchaguzi wa mwaka 2020 uwe wa kuijenga badala ya kuibomoa Tanzania.

Kwa bahati mbaya, ikiwa imesalia miezi miwili tu kuelekea kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu, mazingira ya kisiasa nchini hayatoi taswira ya uchaguzi unaoweza kuiacha nchi yetu salama. Tunakwenda kwenye uchaguzi tukiwa hatuna maridhiano ya kisiasa ambayo yangefanikisha uchaguzi kufanyika kwa amani. Vyombo vinavyosimamia uchaguzi, Tume za Taifa za Uchaguzi (NEC na ZEC) na vyombo vya dola kwa ujumla wake haviendeshwi katika namna itayolivusha Taifa salama kwenye uchaguzi wa mwaka huu. Dalili zipo wazi kuwa kama hali ya sasa itabaki kama ilivyo, bila shaka, Tanzania itaingia kwenye machafuko.

Kwa msingi huo, ACT Wazalendo tunawasilisha hoja kwa wadau wa uchaguzi kuhusu mapungufu yaliyopo na mapendekezo yetu kuhusu masharti ya lazima kwa uchaguzi kuwa huru na wa haki.(Minimum reforms for free and fair election)
Mapungufu Yaliyopo Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2020

1. Serikali haijayafanyia kazi mapendekezo yetu ya kuufuta Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 2020. Uchaguzi huo umesababisha kuwepo kwa viongozi wa vijiji na mitaa ambao hawana uhalali wa kisheria wala wa kisiasa kwa sababu hawakuchaguliwa na wananchi. Katika kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu, ni wakati muafaka kwa mamlaka zinazohusika kutathmini kosa hili la kihistoria. Ni dhahiri kuwa hakuna maendeleo ya maana na yanayoaminika yanayoweza kusimamiwa na watu hawa kwa sababu umma hauwezi kuwaunga mkono.

2. Tume za Uchaguzi si huru. Kwa muundo wake, Tume zetu zote mbilizinaonekana kuwa Tume za Rais badala za Tume Huru ya Uchaguzi. Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar wanateuliwa na Marais (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar) ambao pia ni Mwenyekiti wa CCMna Makamu wake kwa upande wa Zanzibar. Pia, katika ngazi ya Halmashauri, Wasimamizi wa Uchaguzi ni Wakurugenzi wa Halmashauri ambao kwa sehemu kubwa ni makada wa CCM. Ni jambo la kustaajabisha kuwa hata makada wa CCM kama vile Omar Ramadhan Mapuri ambaye amekitumikia Chama Cha Mapinduzi katika nyadhifa mbali mbali mpaka kuwa Katibu Mwenezi wake wameteuliwa kuwa wajumbe wa Tume ya Uchaguzi. Katika hali hii vipi unaweza kufikiria kuwa tunaweza kuwa na Uchaguzi huru na wa haki?

3. Hujuma kwenye uandikishwaji wa wapigakura Zanzibar.
Hivi sasa kwa upande wa Zanzibar, ZEC wanaendelea na zoezi la Uhakiki wa Wapiga kura wakongwe na kuandikisha Wapiga kura Wapya. Zoezi hili limetawaliwa na njama za makusudi zinazoratibiwa kati ya ZEC, Ofisi ya Usaijili wa Matukio ya Kijamii inayoandikisha Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi na CCM. Hujuma hizi zinalengo la kuhakikisha kuwa wananchi wa Zanzibar kwa maelefu wananyimwa haki yao ya msingi ya kupiga kura. Hadi sasa ambapo ZEC wameshakamilisha zoezi la uandikishaji kwa upande wa Pemba takwimu zinaonyesha kuwa ZEC imeandikisha jumla ya wananchi 109, 567. Ukilinganisha na wananchi walioandikishwa mwaka 2015 ambao ni 145,066 utagundua kuwa wananchi 35,499 kwa Mikoa miwli ya Pemba pekee wameachwa nje ya daftari kwa makusudi ili kuwanyima haki yako ya kuchagua viongozi wanaowataka. Hali hii haiwezi kutoa taaswira ya kuwa tunaweza kuwa na Uchagzi huru na wa haki.

3. Hujuma kwenye ugawaji majimbo Zanzibar
ZEC imetangaza dhamira yake ya kutaka kupitia upya mipaka ya majimbo ya Uchaguzi na kukata upya Majimbo. Ni jambo la kushangaza sana. ZEC hii imekata Majimbo mwaka 2015 ambapo iliongeza Majimbo kutoka 50 na kuwa na Majimbo 54. Si jambo lililotarajiwa hata kidogo kuona kuwa ZEC watafikiria kukata Majimbo baada ya miaka mitano tu tokea kukata Majimbo hayo. Tunafahamu kuwa kinachoisukuma ZEC kukata majimbo ni pressure kutoka CCM inayozidi kufifia kila uchao kule Zanzibar ya kuiona vipi inaweza kukwepa hasira za Wananchi kupitia visanduki vya kura. Hivyo ZEC kwa kushirikiana na CCM wamepanga kukata upya Majimbo ili kuisaidia CCM. Taarifa tulizonazo mipango ya ZEC kwa kushirikiana na CCM inalenga kupunguza Majimbo kutoka 54 waliyoyaongeza mwaka 2015 na kurudi kuwa na majimbo 50 kama ilivyokuwa kabla ya mwaka 2015. Katika kufanikisha hili, wanalenga kupunguza Majimbo Mawili Pemba na Majimbo Mengine mawili katika Wilaya za Mgharibi. Suala tunalowauliza ZEC, Pemba hakukuongezwa Jimbo hata moja mwaka 2015 inakuwaje kuhusike kupunguzwa. Hivyo ZEChawajui wapi waliongeza Majimbo mpaka wapotoe kuyatafuta walikoyaongeza. Hii yote inathibitisha njama ovu zinazoratibwa na ZECkatika kuhakikisha kuwa Uchaguzi unahujumiwa mapema na hivyo kuufanya uchaguzi wa mwaka huu kukosa sifa za kuwa Uchaguzi huru na haki.

5. Hujuma kwenye kanuni za uchaguzi. Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (NEC) imeanza mchakato wa mabadiliko ya Kanuni za Uchaguzi. Kwa mujibu wa Rasimu za Kanuni hizo, kukaribisha waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa ni suala la hiyari. Pia, mawakala wa vyama vya siasa hawatapewa nakala za viapo ambazo miaka yote zimetumika kama sehemu ya utambulisho wao katika vituo vya kupigia kura. Pia, haki ya mawakala kupewa nakala za matokeo limefanywa kuwa ni suala la hiyari. Msimamizi wa Uchaguzi anayo hiyari ya kuwapatia mawakala nakala za matokeo iwapo zitakuwepo za kutosha. Kanuni hizi, bila shaka, zitahatarisha amani na utulivu kwenye uchaguzi mkuu 2020.

6. Hujuma za Vyombo vya Dola. Vyombo vya dola, hasa Jeshi la Polisi ambalo lina dhamana ya kutenda haki kwa raia wote, linajidhihirisha kuegemea upande wa Serikali. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Jeshi la Polisi limetumika kuhujumu mikutano na shughuli za vyama vya upinzani. Katika miaka ya hivi karibuni, Maafisa wa Jeshi la Polisi wameonekana waziwazi kwenye shughuli za CCM au za umma wakiimba nyimbo au kutoa kauli za kuibeba CCM. Kwa mwenendo huu wa Jeshi la Polisi, ni dhahiri kuwa haviwezi kutenda haki kuelekea uchaguzi mkuu.
Hatua za Kuchukua Kabla ya Uchaguzi Mkuu 2020
Kutokana na udhaifu mkubwa tuliouainisha, ACT Wazalendo tunapendekeza masuala yafuatayo ya kufanyiwa maboresho (minimum reforms) kabla ya kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu 2020;

1. ACT Wazalendo tunarejea rai yetu kuwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2020 ulikosa uhalali wa kisiasa na kisheria. Mosi, Serikali itafakari upya nafasi ya viongozi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji waliopo. Pili, Serikali ihakikishe kuwa yale yaliyojitokeza kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hayajitokezi kwenye Uchaguzi Mkuu. ACT Wazalendo, kwa kushirikiana na wenzetu katika upinzani, tumejipanga kuhakikisha kuwa tunadhibiti hujuma zozote kama zile zilizojitokeza kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

2. Serikali ipeleke Muswada kwa hati ya dharura kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na Sheria ya Uchaguzi ili kuifanya Tume ya Uchaguzi iwe huru. Vifungu kwenye Katiba na Sheria ya Uchaguzi vinavyompa mamlaka Rais kuteua Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Uchaguzi vibadilishwe. Uteuzi ufanywe na chombo huru. Katika ngazi ya Halmashauri, uchaguzi usimamiwe na watendaji wa Tume Huru ya Uchaguzi badala ya Wakurugenzi wa Halmashauri ambao wengi ni makada wa CCM. Marekebisho yanayopendekezwa pia yaruhusu matokeo ya uchaguzi wa Rais kuhojiwa mahakamani.

3. Huwezi kuwa na uchaguzi huru na wa haki ambao wananchi wake kwa maelfu wanalalamika kunyimwa haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowataka. Hivyo basi tunaitaaka ZEC ihakikishe kuwa hakuna Mzanzibari anayekoseshwa haki yake hii kwa makusudi. ZEC iaandae utaratibu wa utakaowapa nafasi wanachi hawa wanaoachwa kuandikishwa kwa hila katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura ili ukifika wakati waweze kutumia haki yao hii. Kwa kufanya hivi ndio tunaweza kuwa na uchaguzi huru na wa haki.

4. Uchagzu Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu 2020 unapaswa kuonekana kuwa ni uchaguzi huru, wa haki, wa wazi na wenye kuaminika. Hivyo basi ni lazima ZEC na NEC ziandae mazingira rafiki yatakayoruhusu Waangalizi wa Kimataifa wa muda mrefu na mfupi wanapata fursa ya kuungalia na kuupima uchaguzi huu. Wakati huo huo Jumiya ya Kimataifa iwaunge mkono waangalizi wa ndani ili nao waweze kushiriki kuupima Uchaguzi huu.

5. NEC ishirikishe wadau vya kutosha katika utungaji wa Kanuni za Uchaguzi. Kanuni za Uchaguzi zihakikishe ushiriki wa waangalizi wa kimataifa na mawakala wa vyama vya upinzani. Kanuni za Uchaguzi ziweke pia sharti kwa vyama vya upinzani kupewa nakala daftari la wapigakura mapema kabla ya kampeni kuanza.

6. Vyombo vya dola kama vile Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa na Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar vifanye kazi yake kwa weledi bila kuonesha upendeleo wa wazi kwa CCM.

7. Kuungana na Wananchi wa Zanzibar katika kuhakikisha kuwa Chaguo lao linaheshimiwa hivyo basi Mshindi wa Uchagzi wa mwaka 2020 anapata fursa ya kuunda serikali bila mizengwe na hila kama ambayo Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 inavyotaka. Huu utakuwa ni uchaguzi wa 6 tokea kuanzishwa kwa Mfumo wa Vyama Vingi mwaka 1992. Wananchi wa Zanzibar wameshuhudia kila aina ya hila zikifanyika kuzuia chaguo lao kupata nafasi ya kuendesha nchi. Yaliyoafanyika yameshafanyika vya kutosha. Tunataka watawala wajue kuwa jaribio lolote la kuwanyima tena wananchi wa Zanzibar fursa ya kuongozwa na kiongozi wanayemtaka ACT Wazalendo itasimama na umma wa Wazanzibari kuzuia jaribio hilo. Watawala wajaindae kisaikolojia kuwajibika na matokeo ya jaribio hili. Nimesema na narudia tena kuwa sasa basi. Imetosha.

8. Vyombo vya habari vya umma vinapaswa kutoa fursa sawa kwa vyama vyote vya siasa bila upendeleo wa aina yoyote. Vyombo vya habari vinamchango mkubwa katika kuhakikisha kuwa Uchaguzi unakuwa huru na wa haki. Hali ilivyo hivi sasa inasikitisha sana. Hivi sasa sote ni mashahidi kuwa vyombo vya habari vya umma vimekuwa ndio mdomo wa CCM. Vimeshaanza kazi ya Kampeni kabla hata wakati wa kampeni kuanza. Vipi vyote vinavyoandaliwa hivi sasa vinafanya kazi moja tu ya kukitangaza Chama cha Mapinduzi na kwa upande mwenngine vinajuzuia kabisa kutoa habari yoyote inayotolewa na vyama vya upinzani. Wito wetu vyombo hivi vinapaswa kubadilika kwa kutoa fursa sawa kwa vyama vyote bila upendeleo wowote. Kwa kufanya hivyo ndio tunaweza kuhakikisha kuwa tunakuwa na uchagzi huru na wa haki.
Mwisho:

ACT Wazalendo tunaamini kwa dhati kuwa wadau wa uchaguzi wanaweza kutumia muda uliobaki kabla ya kuanza kwa kampeni kuzifanyia kazi kasoro zilizoainishwa na kujenga maelewano mazuri yatakayoweza kuiepusha nchi yetu machafuko. ACT Wazalendo tunayasema haya tukiamini kuwa tunatimiza wajibu wetu kama wadau muhimu katika ustawi wa nchi yetu na watu wake. tunao muda. Tukiamua kuutumia vizuri tunaweza kufanya mambo makubwa kwa mustakabali wa nchi yetu. Mapendekezo haya yanatekelezekwa kwa muda uliobakia kama kuna nia njema na kwamba sote tunatamani kuiona nchi yetu ikiendelea kuwa ni ya amani na utulivu na kwamba kila mmoja kati yetu anajivunia kuwa Mtanzania.


SOURCE

ACT Wazalendo


103543298_3332099370146957_8816902019972398850_n.jpg
 
Back
Top Bottom