Bawacha: Taarifa kwa umma kuhusu mauaji ya watoto Njombe

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Mar 9, 2015
14,243
34,899
BARAZA LA WANAWAKE WA CHADEMA (BAWACHA)

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MAUAJI YA WATOTO NJOMBE.

Kwa kipindi cha takriban mwezi mmoja sasa kumekuwa na habari za kutisha kutoka mkoani Njombe ambapo vyombo vya habari mbalimbali vimeripoti kuwepo kwa mfululizo wa mauaji ya watoto wapatao 10, ambao wametekwa na kuuwawa kwa kuchinjwa katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Mji wa Njombe na Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.

Imeelezwa kupitia taarifa hizo kuwa wanaosadikiwa kuwa watekaji na wauaji wa watoto hao wamekuwa wakikata baadhi ya viungo, kama vile, meno, sehemu za siri na macho, na kuondoka navyo kabla ya kuitelekeza miili hiyo.

Katika hali ya masikitiko na majonzi makubwa ya taarifa hizo za ukatili wa kinyama dhidi ya watoto wetu, BAWACHA Taifa tunatoa salaam za pole na rambirambi kwa familia na ndugu wa watoto hao waliotekwa na kuuwawa kikatili. Tukiwa akina mama, tunatambua wakati mgumu wa maumivu makali yasiyo na mfano ambayo familia hizo zimelazimishwa kupitia kutokana na matendo ya kifedhuli ya baadhi ya wanajamii wenzetu.

Tunaungana na wanawake wenzetu wa Njombe na maeneo mengine nchi nzima kuwalilia watoto hao ambao uhai wao umekatizwa kikatili, bila hatia yoyote.

BAWACHA Taifa, kupitia taarifa hii, tunalaani vikali mauaji hayo na wote wanaohusika na unyama huo dhidi ya watoto ambao ni mojawapo ya makundi maalum katika jamii yetu yanayostahili kulindwa, kupendwa na kuthaminiwa, si kufanyiwa ukatili wowote ule.

Taarifa zinasema kuwa mauaji hayo yanachochewa na imani za kishirikina hasa kwa ajili ya kutafuta mafanikio ya utajiri, kupandishwa vyeo kazini na kuondoa nuksi. BAWACHA tunasema wazi kuwa hakuna sababu yoyote inaweza kukubalika ndani ya jamii ya iliyostaarabika na inayotambua haki za binadamu, kuhusu mauaji hayo.

Tunaitaka Serikali, kupitia vyombo vya dola, kama ilivyotoa kauli kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ndani ya Bunge, ichukue hatua zote zilizoko ndani ya mamlaka yake kisheria, kukomesha vitendo hivyo vya ukatili kwa watoto mara moja, kwa kuwasaka wahusika na kudhibiti kabisa mtandao unaohusika na mauaji hayo.

Tunasisitiza suala la kudhibiti mtandao wa wahusika, kwa sababu katika miaka ya hivi karibuni Watanzania wameshuhudia kuongezeka kwa vitendo vya utekaji, mauaji na kutelekezwa kwa miili ya watu waliouwawa, lakini hawaoni hatua madhubuti za kukomesha hali hiyo kutoka kwa mamlaka husika, hususan vyombo vya dola. Badala yake, matukio hayo yanazidi kujirudia, kushamiri na kusambaa sehemu mbalimbali za nchi yetu.

Tunaitaka Serikali kuchukua hatua za haraka, za muda mfupi na mrefu na kuutarifu umma, ili kuondoa hofu iliyowakumba watoto wa Njombe na wazazi wao kwa sasa na hivyo kuishi bila amani na utulivu kutokana na tishio kubwa la haki yao ya kuishi.

Tunatoa wito kwa jamii yetu kutambua kuwa watoto wanastahili haki ya kulindwa dhidi ya ukatili wowote na mahali popote iwe ni nyumbani, shuleni au maeneo mengine yoyote wanapokuwa. Hili linapaswa kuwa jukumu adhimu kwa kila mmoja wetu katika jamii.

Halima Mdee (Mb)
Mwenyekiti wa BAWACHA Taifa
Januari 31, 2019
 
Back
Top Bottom