Barua ya wazi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Songuo

Member
Sep 28, 2012
9
1
BARUA YA WAZI KWA MH. RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO TANZANIA


Mheshimiwa Rais;

Naomba kwanza nikupongeze na nikupe pole kwa kazi kubwa na nzuri unayoifanya ya kuliongoza taifa letu kwa moyo wa wa ujasiri na upendo mkubwa. Kwa ujumla kazi yako ni njema sana. Sisi watanzania tunajisikia furaha sana kuwa na kiongozi wa aina yako. Pamoja na pongezi, tunakuombea sana kwa mwenyenzi Mungu azidi kukupa afya njema, akupe nguvu zaidi, hekima nyingi na busara ili uishi maisha marefu, uendelee kutuongoza vema huku ukituwekea misingi imara itakayosaidia kuwa na taifa zuri la watu wanaoipenda nchi yao, wenye bidii ya kuchapa kazi kwa moyo kwa manufaa yao wenyewe, jamii na taifa kwa ujumla. Mungu akulinde mama yetu.

Pili naomba nilete ombi kwako mh rais. Kuna jambo amablo linaumiza watumishi wa umma hususani madaktari bingwa (specialists) wa magonjwa ya binadamu. Ni kuhusu ANDIKO (Published article) kutumika kama kigezo mojawapo cha LAZIMA kwa daktari bingwa kupandishwa daraja kwenye utumishi wa umma. Na kama hiyo haitoshi, ili andiko likubaliwe unapaswa kuwa mwandishi wa kwanza (first author) kwenye hilo andiko sio wa kushirikishwa. Nje na hapo unakuwa moja kwa moja umepoteza sifa ya kupandishwa daraja na hivyo huwezi kupanda daraja kwenye utumishi.

Kigezo hiki ni kizuri, muhimu na chenye nia njema kabisa kwa manufaa yetu wenyewe na taifa kwa ujumla. Mimi binafsi nina imani na mtizamo chanya juu ya kigezo hiki na ninajua wapo wengine pia wana mtizamo chanya.

Baadhi ya faida zake ni:-

Kwanza, hizi tafiti zitasaidia sana kupata takwimu na taarifa (research findings) za kwetu kutoka kwa watu wetu wa maeneo yetu halisi ambazo zitaweza kuwasaidia sana waandaa sera na miongozo (policies and guidelines) kwa kutumia local research findings.

Pili itasaidia kupata takwimu na taarifa (local data) bila kutumia gharama kubwa sana.

Tatu, utatusaidia sisi kama wataalam kujiendeleza wenyewe pamoja na wale walio chini yetu kwenye eneo la tafiti.

Pamoja na faida zake zikiwemo nilizozitaja hapo juu, kigezo hiki Mh Rais kina MADHARA kwa wataalam wenyewe, jamii wanayoihudumia na kwa taifa kwa ujumla. Hii ndiyo sababu kubwa nimeona niandike waraka huu, hivyo inafaa na nashauri kitazamwe upya.

CHANGAMOTO:-

Kwanza kigezo hiki kimetumika kuwanyima haki ya kupanda daraja watu wenye vigezo vingine vyote. Kuna ambao kimewaathiri, wengine kinawaathiri sasa hivi na kuna wengine wengi wataendelea kuathirika mwaka hadi mwaka. Jambo hili linawaumiza na kuwavunja moyo sana wataalam hali ambayo inaweza kuiathiri pia jamii wanayoihudumia na taifa.

Tatizo kubwa lililopo ni UWEZESHAJI (FUNDING) ya hizo tafiti. Inafahamika wazi kuwa hakuna utafiti usiokuwa na gharama, haupo.

Na ili utafiti wowote uweze kutoa majibu sahihi (VALID RESULTS) ni lazima gharama kubwa itumike sio chini ya shilingi million 20 za kitanzania (TZS 20m). Pia ni lazima kuwepo na kujitoa/kujituma kwa mtafiti mwenyewe.

Ukiangalia kiuhalisia, mazingira ya kufanyia kazi Tanzania mbali na mshahara duni anaolipwa daktari utaona kabisa hiki kigezo ni kandamizi chenye nia ya kufanya watu washindwe kukidhi vigezo ili washindwe kupanda daraja. Hii sio sawa hata kidogo.

Tanzania kuna mikoa ina specialist mmoja tu wa idara moja tu na kwingine hawapo kabisa. Kuna idara nyingi utakuta kwenye mkoa mzima hazina hata specialist mmoja wa idara hizo.
Kwa mfano.

Ni mikoa mingapi Tanzania ina daktari bingwa wa magonjwa ya ndani (physicians) zaidi ya mmoja?

Ni mikoa mingapi Tanzania ina daktari bingwa wa upasuaji (general surgeon) zaidi ya mmoja?

Ni mikoa mingapi Tanzania ina daktari bingwa wa mifupa (orthopaedic surgeon) zaidi ya mmoja?

Ni mikoa mingapi Tanzania ina daktari bingwa wa watoto (paediatrician) zaidi ya mmoja?

Ni mikoa mingapi Tanzania ina daktari bingwa wa sikio, pua na koo (ENT surgeon) zaidi ya mmoja?

Ni mikoa mingapi Tanzania ina daktari bingwa wa macho (opthamologist) zaidi ya mmoja?

Mh Rais; Specialists wa kada mbalimbali ni wachache kwenye mikoa mingi Tanzania. Majukumu anayokuwa nayo huyu daktari katika kuhudumia jamii ni mengi sana yakiwemo ya kutibu wagonjwa na mengine ya kiuongozi ambayo hayakwepeki, na kipato chake ni duni halafu kwenye kipato hichohicho aweze kugharamia utafiti wa shilingi milioni 20, 30, 40, 50 nk. Kwa kweli hataweza.

MAPENDEKEZO

Mh rais,
naomba nipendekeze yafuatayo:-

Kwanza nashauri kigezo hiki kwa sasa kiondelewe na kisitumike kuamua nani apandishwe daraja na nani asipandishwe mpaka kifanyiwe maboresho. Badala yake viendelee kutumika vigezo vingine kama vile muda wa utumishi ambao mtumishi ametumika katika ngazi hiyo, idadi ya wagonjwa aliowahudumia kliniki na wodini, idadi na aina ya operesheni alizofanya akiwa katika ngazi husika, kazi nyinginezo alizofanya akiwa katika ngazi hiyo, idadi ya CPD points alizojikusanyia akiwa katika ngazi husika nk.

Pili nashauri serikali itenge fedha kwenye bajeti yake kwa ajili ya kuwezesha tafiti hizi na iziwekee utaratibu. Serikali itoe angalau shilingi milioni 20 kwa kila specialist kwa kila miaka mitatu au mitano kwa ajili ya kufanya tafiti na kuchapisha/kuzipublish. Au itoe shilingi milioni 50 kwa watu watatu watatu, ili waweze kushirikiana na kufanya tafiti nzuri na zenye tija.

Tatu, nashauri serikali itengeneze mfumo rasmi wa kusimamia utekelezaji wa zoezi hili mfano kupitia MCT na ielekeze jarida ambamo tafiti hizi zinaweza kuwa published.

Mwisho nikushukuru tena Mh Rais, na nikutakie baraka za mwenyenzi Mungu na afya tele. Madaktari na watanzania tupo nyuma yako!

Ni mimi katika utumishi wa umma,
Dr Kimambo ELISONGUO
Department of Obs &GYN
Mbeya Zonal Referral Hospital
 
Hili suala mtu wa mwisho ni Waziri wa Wizara husika na Kamati Tendaji za vyama vya madaktari na wauguzi.

Rais kumtwisha mzigo huu ni kumuonea. Mumuache Rais wetu atafakari suala la Bandari zetu kwa mapana yake.
 
Back
Top Bottom