Baraza Jipya La Mawaziri: Tafsiri Yangu (Makala, Raia Mwema) | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Baraza Jipya La Mawaziri: Tafsiri Yangu (Makala, Raia Mwema)

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by maggid, May 11, 2012.

 1. m

  maggid Verified User

  #1
  May 11, 2012
  Joined: Dec 3, 2006
  Messages: 1,084
  Likes Received: 397
  Trophy Points: 180
  Na Maggid Mjengwa,
  NIMEPATA kusimulia kisa cha kijana aliyehangaika sana kuusaka ukweli. Katika pitapita zake akaliona duka. Kibao kimeandikwa dukani; “Hapa tunauza ukweli”.


  Dukani hapo ukweli unauzwa kwa kilo. Bei ya robo kilo ya ukweli imeandikwa, vivyo hivyo, bei ya nusu kilo ya ukweli. Lakini, mwenye duka hakuandika bei ya ukweli mzima, kwa maana ya kilo nzima ya ukweli.

  Kijana yule akauliza; “Mie nataka ukweli kilo nzima, mbona hujaandika bei?”

  “Alaa, unataka kilo nzima ya ukweli?” aliuliza mwenye duka. “Naam” Akajibu kijana yule.

  “Basi, zunguka uje ndani nikuambie bei yake”.

  Alipoingia ndani dukani, kijana yule akaambiwa; “Kijana, hatukuandika bei, maana, gharama ya ukweli mzima ni uhai wako. Je, uko tayari kulipa?”

  Kijana yule akatimua mbio. Nyuma aliacha vumbi. Hakuwa tayari kulipa gharama ya ukweli mzima.

  Yumkini ukweli utakaousema mwanadamu waweza usiwafurahishe wachache, walakini, ukawa wenye kuleta tija, furaha na matumaini kwa walio wengi.

  Mimi nitasena hapa ukweli wangu, kuwa Baraza jipya la mawaziri ni mabadiliko ya sura ya Baraza lakini si mabadiliko ya mfumo uliosababisha udhaifu wa kiutendaji ikiwamo ‘madudu’ yale tuliyoyaona bungeni hivi karibuni. Na kauli za baadhi ya mawaziri zinathibitisha hilo; wengi wameahidi kuanzia na yanayotokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ( CAG).


  Hakika, tatizo letu kubwa ni la kimfumo. Unaanzia na tunavyompata Rais wa nchi, unakuja na tunavyowapata wabunge wetu, unaendelea na mawaziri wetu wanavyopatikana na hata baadaye watendaji wetu.

  Katika nchi hii Rais ana wakati mgumu sana. Maana, mfumo unamtaka awachague mawaziri kutoka miongoni mwa wabunge wa chama chake. Si ajabu juzi hapa Rais amewateua wabunge wapya kutoka kwenye nafasi zake kumi na kuwafanya kuwa mawaziri hata kabla ya kuapishwa bungeni. Ilikuwa dhahiri, kuwa Rais aliwaona mawaziri wake wa kumsaidia miongoni mwa majina yale mapya ya wabunge aliowateua.

  Kwa mantiki hiyo basi, mfumo ulio nafuu kwetu ni kumpa Rais uwezo wa kuchagua mawaziri nje ya Bunge. Kwamba Katiba ijayo iweke wazi kuwa mawaziri wasiwe wabunge kwa wakati mmoja. Kama Rais ataamua kumteua mbunge kuwa waziri, basi, mbunge huyo ajiuzulu kiti chake cha ubunge. Maana, mbunge ni mwakilishi wa wananchi ambaye moja ya majukumu yake bungeni ni kuisimamia Serikali. Mwanadamu huwezi kupanda farasi wawili kwa wakati mmoja.


  Tuna tatizo jingine hatuliweki wazi lakini lipo na linakomaa; uteuzi wa Baraza la Mawaziri katika mfumo wetu wa sasa unaangalia pia jiografia ya nchi yetu. Inaangaliwa kama katika Baraza jipya Mbeya wamepata mawaziri? Dodoma? Mwanza….


  Na tukitoka hapo tunakuja ni wangapi kwa kila mkoa? Ni mfumo mbaya unaozoeleka. Maana, mitaani watu wa Singida wanaweza kuhoji? Mbona sisi tumesahaulika kwenye Baraza jipya? Kana kwamba ni Baraza la mikoa wakati ni la taifa.

  Na hii inatokana na tabia iliyojengeka ya baadhi ya mawaziri kuonyesha wazi wazi kuwa wanatumia uwaziri wao kuvutia maendeleo kwao- kwenye majimbo yao badala ya kuangalia nchi nzima. Waziri anakuwa waziri wa jimbo badala ya nchi nzima.

  Ni katika mazingira haya, hata kama mbunge wa chama kilichotoa rais ni mgonjwa, lakini anakubalika sana kwenye jimbo, wilaya na hata kanda anayotoka, Rais anaweza kushauriwa ampe chochote kile ilimradi cheo cha ‘Mheshimiwa Waziri’ kisifutike. Maana, kikifutika hicho, basi, kuna kura nyingi za chama zitakazofutika kwenye uchaguzi ujao!

  Ukabila na ukanda umeanza kunukia badala ya utaifa. Tumesahau kuwa miaka hiyo nchi hii imepata kuwa na wabunge na hata mawaziri wazungu na wahindi. Ni akina Derek Brysson, Leader Sterling, Al Noor Kassam, Ameir Jamal na wengine. Hawa walionekana kwanza kama Watanzania wazalendo.

  Tatizo jingine la mfumo tulio nao sasa ni Rais wa nchi kushauriwa kufanya teuzi zinazoendana na mikakati ya siasa za vyama. Kwa mantiki hii, hata CUF au CHADEMA wakiingia madarakani kesho, na kwa mfumo huu huu, nao, kwa kiasi kikubwa, watafanya hivi hivi. Ndio maana ya kusisitiza, kuwa, tulilo nalo sasa ni tatizo la kimfumo ambalo ndiyo chimbuko la utendaji mbovu wa kuanzia mawaziri na walio chini yao. Ni mfumo unaomfanya waziri, awajibike zaidi kwa chama chake badala ya taifa kwa ujumla wake.


  Na ni katika mfumo huu ambapo chama kinabeba jukumu la kumlinda waziri hata katika maovu. Ni kwa tafsiri hii, mathalan, wabunge wa CCM wakimwangusha Waziri aliyefanya maovu, huamini kuwa wamekiangusha chama chao na Rais, ambaye ni mwenyekiti wao na ndiye aliyemteua waziri husika. Hilo husababisha kujengeka kwa hofu miongoni mwa wabunge wa chama tawala katika kumjadili waziri na hata kumwajibisha.


  Na hofu hiyo huimarika zaidi kutokana na mfumo wa chama tawala ambao yumkini Waziri anayejadiliwa aweza pia kuwa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama. Ni Kamati ambayo hupitisha uamuzi muhimu kwa chama ikiwamo kupitisha majina ya wagombea nafasi mbalimbali ndani ya chama ikiwamo ubunge. Kuna wabunge wenye kuhofia kuukata mkono unaowalisha. Hatima yake? Ni madudu kama yale tuliyoyaona kwenye ripoti ya CAG.


  Na kwa vile mfumo uliosababisha madudu yale ungalipo, basi, yumkini madudu yale yatatafuta namna nyingine ya kuishi, badala ya kutambaa sakafuni, yataanza kujichimbia zaidi. Dawa mujarab ya madudu yale tuliyoyaona kwenye ripoti ya CAG ipikwe na kuchanganywa vilivyo kwenye Katiba yetu mpya tunayokwenda kuitengeneza.


  Na tatizo la mfumo tulionao tutaliona pia kwenye teuzi za wakuu wa wilaya ndani ya mwaka huu. Maana, katika mfumo wetu huu, wakuu wa wilaya ni makada wa chama tawala.

  Wakuu wa wilaya katika mfumo ulio nafuu wangepaswa wabaki ‘kiserikali’ zaidi kuliko ‘kichama’. Kwenye maeneo yao wangesimamia masuala ya maendeleo bila kutanguliza maslahi ya chama ikiwamo kulinda maovu kwa kukiogopa chama kilicho madarakani.


  Ni makosa, katika dunia ya sasa, pale mfumo unapofikiria kumpeleka DC wilayani aende akadhoofishe upinzani badala ya kusimamia maendeleo na kuhakikisha wadau wote wilayani, bila kujali tofauti zao za itikadi, wanashirikishwa katika kuinua uchumi wa wilaya, na hivyo kuiletea wilaya na wananchi maendeleo. Kubadilisha mfumo inawezekana.  0788 111 765 Mjengwa Blog::Habari,Picha,Matangazo
   
 2. M

  Mkulima aka peazant Member

  #2
  May 11, 2012
  Joined: Dec 18, 2011
  Messages: 21
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  well said tushirik vyema katika kuandika katiba tunayoitaka.
   
 3. N

  NasDaz JF-Expert Member

  #3
  May 11, 2012
  Joined: May 6, 2009
  Messages: 11,308
  Likes Received: 1,651
  Trophy Points: 280
  majjid,
  Umeutaja ukweli wako ambao bila shaka unaamini ndio tatizo msingi. Hata mimi, nakubaliana na wewe lakini sikubaliani nawe kwa asilimia mia moja. Sikubaliani na wewe kwa asimilia mia moja kwavile umeuacha kuuleza ukweli wa msingi wa tatizo la nchi yetu. Ukweli ulioueleza wewe ni matawi tu ya ukweli halisi. Na kama ukweli uliousema ni mkubwa sana basi unaishia tu kwenye ukubwa wa shina na katu si ukubwa wa mzizi! Ukweli ambao umeuacha ni UKOSEFU WA MAADILI MIONGONI MWA WATANZANIA! Huu ndio msingi, ama mzizi wa tatizo kuu la nchi yetu. Hata kama Rais angeweza kuteua Mawaziri nje ya wabunge, bado tatizo lingebaki paleple kwavile Ukosefu wa maadili umeenea kwenye kada zote za jamii yetu! Kwangu, mzizi wa tatizo ni ukosefu wa maadili na shina ni Utawala Bora! Mfumo wa Utawala Bora ni mzizi wa tatizo letu. Utawala Bora ndani ya Jamii isiyo na maadili ni kansa! Mfumo wa Utawala Bora ni mzuri sana lakini kweye jamii yenye maadili! Nguzo mojawapo ya Utawala Bora ni Utawala wa Sheria....Mtuhumiwa atabaki kwamba ni mtuhumiwa unless proved otherwise, tena beyond any reasonable doubt! Huo ndio Utawala wa Sheria, Nguzo kuu ya Utawala Bora!! Kutokana na hilo, mara zote Utawala Bora unaonekana kuwa ni kichaka cha wezi, wala rushwa, wakosefu wa uwajibikaji na kansa zingine ndani ya jamii ya kistaarabu! Na ndio maana leo hii, viongozi wengi barani Afrika wanaupigia chapuo mfumo huu kwavile wanafahamu hiki ndio kichaka muafaka cha uovu wao! Kichaka chenye jina zuri na kuvutia huku kikiwa kimezungushiwa maua ya jasmini, ambayo ni mujarabu kwa harufu yake!! Wazungu nao, au labda tuite mataifa ya magharibi si kwamba hawafahamu kwamba mfumo waliotuletea ni kichaka cha wahalifu, la hasha! Sina shaka yoyote ile kwamba wanafahamu. Hata hivyo, kichaka hiki ni muafaka pia kwa maajenti wao wanaokuja Afrika kwa kofia ya uwekezaji! Leo hii hata JK akimteua majjid kuwa waziri bado ni kazi bure kwavile uovu wa majjid utalindwa na utawala bora/utawala wa sheria labda tu majjid mwenyewe awe mwadilifu! Leo hapa tumesikia, kwamba fulani ni mla rushwa, fulani ni fisadi....ni nani basi mwenye jeuri ya kuwapeleka watu hao mahakamani wakati atatakiwa kuthibitisha madai yake?! Huo ndio Utawala Bora, shina la matatizo la nchi yetu!

  Suluhisho ni nini basi! Kama ulivyosema, ni katiba mpya! Hata hivyo, katiba mpya ni kielelezo tu; jambo la msingi ni katiba mpya inayotambua pasi na shaka yoyote kwamba jamii yetu ina ukosefu mkubwa wa maadili. katiba itakayotambua wazi kwamba Watanzania wengi sio waaminifu. Hilo likishafahamika, basi katiba bora kwetu ni ile itakayolenga ukirudisha jamii ya Kitanzania katika mstari! Leo hii ukiniuliza ni katiba ya namna gani basi sitasita kusema Katiba ya Kidikteta na kama ni suala la utawala bora, basi urithiwe na Approved Dictatorship Governance! Nieleweleke vizuri hapa, hatuhitaji Kiongozi Dikiteta bali ni Utawala wa Kidikteta ambao umekuwa approved na katika katiba. Katiba ambayo, itatamka wazi kwamba kiongozi kuwa na utajiri usioendana na mapato yake halali anapaswa kufikishwa kortini mara moja na ni yeye ndie athibitishe kwamba utajiri wake ni halali na sio kwamba upande wa mashitaka ndio uthibitishe kwamba utajiri wake sio halali!

  Tunahitaji Katiba ya Kidikteta ambayo itatamka wazi kwamba ile tu kutuhumiwa na mamlaka halali (kama vile CAG) kwamba kuna ufisadi kwenye ofisi fulani, basi watendaji na wafanyakazi wote wa ofisi husika wafikishwe mahakamani bila kuchelewachelewa kama ilivyo sasa!!

  Utawala Bora, panahitajika ushahidi usio na shaka yoyote ile na katika kuhakikisha watuhumiwa hawasalimiki moja kwa moja ndipo utakuta anayetolewa kafara inapaswa kupewa kesi ya matumizi mabaya ya ofisi! Hii ni kwavile, uking'ang'ana kwenye rushwa au wizi, unaweza kukosa ushahidi na mtuhumiwa kuwa huru! Hivyo basi, tunahitaji Katiba ya Kidikteta itakayotamka wazi kwamba Matumizi mabaya ya ofisi nao ni ufisadi sawa na ufisadi mwingine wowote ule! Katiba itakayotamka wazi kwamba matumizi mabaya ya ofisi ni Uhujumu wa Uchumi na hivyo, hukumu yake iendane na kiwango cha hasara (in fact ni wizi) aliyosababisha! Itamke wazi kwamba, Hasara ya Shilingi Milioni moja hukumu yake ni Jela mwaka mmoja; hivyo aliyeitia hasara serikali kwa shilingi milioni mia moja basi nae aende jela miaka mia moja na akafie huko huko shenzo taipu zake!

  Tunahitaji katiba ya kidkteta itakayotamka wazi kwamba DPP, DCI na TAKUKURU ni nguzo muhimu za kuvunja ufisadi nchini. Hivyo, ikiwa mwaka unapita bila kuwa na kesi yoyote ya ufisadi mkubwa wakati bado mazingira yanaonesha wazi kwamba ufisadi bado upo basi waheshimiwa hawa watatakiwa kutoa maelezo ya kina kwanini hakuna kesi hata moja....pasipo na maelelezo ya kutosha, basi hapo hapo wanakuwa branded kama CORRUPTION AGENTS na kuchukuliwa hatua stahili.

  Tunahitaji katiba ya kidikteta ambayo itatamka wazi kesi za ufisadi, ni kesi zinaposwa kupewa kipaumbele katika uendeshaji wake na hivyo kesi za namna hiyo hazipaswi (kwa mujibu wa katiba) kuchukua muda mrefu! Tunaweza kuanzisha hata Night Courts kwa ajili ya kushughulikia kesi kama hizi. Lengo, ni kutoa hukumu mapema!

  By the way, yote hayo yakifanyika bado tutakuwa hatujatoka kwenye mstari wa Utawala Bora!!! Nguzo kuu ya Utawala Bora ni Utawala wa Sheria. Mama wa sheria zote, ni Katiba iliyotokana na wananchi. Katiba ya Kidikteta itakuwa imepitishwa na wananchi. Hivyo, kuitekeleza kwake itamaanisha tunatekeleza utawala wa sheria ambao ndio msingi wa utawala wa bora.

  Narudia, tunahitaji Katiba ya Kidikteta itakayotulea Approved Dictaroship Governence (ADG) ambayo itaturudisha watanzania kwenye mstari. Mstari wa maadili. Mstari wa Uaminifu! Mstari wa Uwajibikaji! Mstari wa Huruma dhidi ya wengine! Haidhuru, tunaweza kuipamba kwa mashada ya maua na kuipulizia manukato kwa kuiita TRANSITIONAL DICTATORSHIP CONSTITUTIONAL! Tukiulizwa WHY TRANSITIONAL, tutajibu Transition TOWARDS CIVILLIZED AND GOOD GOVERNANCE!
   
 4. N

  NasDaz JF-Expert Member

  #4
  May 11, 2012
  Joined: May 6, 2009
  Messages: 11,308
  Likes Received: 1,651
  Trophy Points: 280
  LABDA iwe ni Katiba ya Kidikteta!
   
 5. qq.com

  qq.com JF-Expert Member

  #5
  May 11, 2012
  Joined: Jan 9, 2012
  Messages: 370
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 0
 6. J

  JokaKuu Platinum Member

  #6
  May 11, 2012
  Joined: Jul 31, 2006
  Messages: 12,751
  Likes Received: 4,968
  Trophy Points: 280
  ..Majjid unajidanganya.

  ..hakuna mfumo usio na matatizo.

  ..hata huo mfumo wenye checks and balance unaoupigania mara nyingine huwa abused na wanasiasa na kuikwamisha serikali iliyoko madarakani.

  ..nakuhakikishia wapo maraisi wanaolilia mfumo tulio nao ili waweze kufanikisha shughuli za maendeleo ktk mataifa yao.

  ..chama au raisi aliyeshindwa ktk mazingira na mfumo tulio nao Tanzania hawezi kufanikiwa ktk mfumo wowote ule. ni sawa sawa na mfanyabiashara aliyeshindwa wakati ana monopoly aanze kudai akiletewa ushindani ataweza biashara.

  NB:

  ..JK amekuwa kwenye chama miaka zaidi ya 10.

  ..amekuwepo serikalini miaka zaidi ya 20.

  ..amejiandaa na kufundwa kuchukua Uraisi kwa miaka 10.

  ..kwanini ameshindwa?

  ..kwa mtizamo wangu ni kwasababu hana uwezo na nafasi hiyo.
   
Loading...