Ballon d'Or haitupi Mchezaji bora mara zote

Ballon d'Or haitupi Mchezaji bora mara zote

marcoveratti

JF-Expert Member
Joined
Sep 21, 2017
Posts
1,110
Reaction score
1,951
Kila mwaka, Dunia ya soka husimama kwa dakika chache. Sio kwa sababu kuna fainali ya Kombe la Dunia, Sio kwa sababu kuna Clasico, wala sio kwa sababu kuna usiku mwingine wa kichawi wa Ligi ya Mabingwa ulaya.

Ni kwa sababu kuna tuzo, usiku ambao furaha ya mmoja hugeuka hasira ya mamilioni ya wengine.
Ni usiku ambao mitandao ya kijamii hujaa mabishano. Wengine hushangilia. Wengine huapa kwamba soka limekufa. Na wengine huanza kuhesabu mabao, pasi za mwisho na mataji kana kwamba mchezo huu unaweza kufungwa ndani ya jedwali la takwimu.

Lakini kila mwaka huwa najiuliza swali moja, Je, kweli kuna tuzo inayoweza kumtaja mchezaji bora duniani?
au kuna tuzo inayomtaja mchezaji ambaye alikuwa na mwaka bora zaidi?

Kwa sababu hayo ni mambo mawili tofauti, Historia ya soka imejaa majina ambayo hayakuwahi kushika Ballon d'Or, lakini hakuna anayethubutu kusema hayakuwa makubwa na bora.
  • Paolo Maldini alijenga ukuta ambao washambuliaji waliuota vibaya usiku.
  • Xavi Hernández alifundisha Dunia kwamba mpira unaweza kukimbia zaidi kuliko mchezaji.
  • Andrés Iniesta alifunga bao lililobadilisha historia ya Hispania, lakini mara nyingi jina lake lilikuwa nyuma ya wengine.
  • Thierry Henry aliwahi kutawala England kwa namna ambayo mabeki walitamani ratiba isiwapeleke Emirates au Highbury.
Je, hawa hawakuwa bora? au walikuwa na bahati mbaya ya kuishi kwenye kipindi ambacho macho ya dunia yalikuwa yanaangalia sehemu nyingine?

Hapo ndipo ugumu wa Ballon d'Or ulipo, kwa sababu mpira si riadha.
Hakuna mstari wa kumalizia unaosema huyu amefika wa kwanza ndio mshindi.
Hakuna kipimo kinachosema pasi moja ni nzito kuliko nyingine.
Hakuna hesabu inayoweza kupima hofu ambayo beki huipata kila anapomuona mpinzani fulani akianza kukimbia na mpira.

Soka lina hisia, na hisia hazina fomula.
Ndiyo maana mwaka mmoja Luka Modrić aliushinda ulimwengu kwa akili yake.
Mwaka mwingine Karim Benzema alikumbusha kwamba mshambuliaji anaweza kuchelewa kung'aa, lakini akiwaka anaweza kuangaza kuliko wote.
Na kuna miaka ambayo watu waliinuka kutoka kwenye viti vyao wakiamini kwamba safari hii haki itatendeka.
Haikutendeka.

Lakini je, hilo lilibadilisha ubora wa mchezaji? Hapana.
  • George Weah hakuhitaji Ballon d'Or kuthibitisha alikuwa mchezaji mkubwa wa Afrika.
  • Ronaldinho hakuhitaji tuzo nyingine ili watu wakumbuke tabasamu lake na uchawi wake.
  • Iniesta hakuhitaji kabati lililojaa Ballon d'Or ili watoto wengi waanze kupenda kucheza kiungo.
Kwa sababu kuna tofauti kati ya tuzo na urithi, Tuzo hutolewa usiku mmoja.
Urithi hujengwa kwa miaka, na mara nyingi urithi hushinda.
Labda tatizo letu si Ballon d'Or, Labda tatizo ni sisi.

Tumefika mahali ambapo tunataka tuzo itoe jibu la mjadala ambao hauna jibu.
Tunataka kipande cha dhahabu kiamue kitu ambacho watu wataendelea kubishana hata baada ya miaka hamsini.

Haiwezekani.
Kwa sababu uzuri wa soka uko kwenye kutokubaliana.
Utamkuta mmoja akisema Zidane alikuwa mataamu kuliko wote.
Mwingine atasema Ronaldinho hakuwahi kuwa na mpinzani.
Mwingine atasema Messi alifanya vitu ambavyo havikupaswa kufanywa na binadamu.
Na mwingine atasimama na kusema Cristiano Ronaldo ndiye mfano halisi wa kazi, nidhamu na ushindi.

Hakuna atakayemshawishi mwenzake, na hilo ndilo uzuri wa mchezo huu.
Ballon d'Or inaweza kumchagua mshindi, Lakini haiwezi kumaliza mjadala,

Kwa sababu mchezaji bora haishi ndani ya kura.
Anaishi ndani ya kumbukumbu za waliomwangalia.
Anaishi kwenye watoto waliovaa jezi yake.
Anaishi kwenye mabeki waliokesha wakijiuliza namna ya kumzuia.
Anaishi kwenye viwanja vilivyosimama kwa makofi baada ya kufanya kitu ambacho hakikutarajiwa.

Hayo hayaandikwi kwenye tuzo.
Hayo huandikwa kwenye historia, ndiyo maana kila mwaka tutabishana.
Tutakasirika.
Tutashangilia.
Tutahesabu mabao.
Tutahesabu mataji.

Lakini mwisho wa siku, Ballon d'Or itaendelea kufanya kile ilichokuwa imekusudiwa kufanya.
Kumtangaza mshindi.
Sio kumaliza mjadala wa nani alikuwa bora kuliko wote.

Kwa sababu katika soka, kuna mambo mawili ambayo hayajawahi kuwa sawa.
Kushinda tuzo.
Na kuwa hadithi.
Mara nyingi vinaenda pamoja.
Lakini si kila mara.

1783948157532.png

1783948180822.png
 
Dhumuni la ballon d or ni kumtunuku tuzo mchezaji ambae alikua na mwaka bora. Ingawa michuano ya world cup kwa miaka mingi imekua na ushawishi zaidi katika kuamua mshindi wa balon d or

Kwa haraka haraka nakumbuka Zidane, ronaldo de lima, canavaro na messi walishachukua ballon d or miaka ambayo walichukua world cup. Modric alichukua hii tuzo ingawa alipoteza fainali.

Hili suala limekua likihojiwa kwanini mashindano ya mwezi mmoja yatumike kama determinant factor kwenye tuzo ambazo zinajumuisha mwaka mzima. Tuzo za ballon d or zilianza kuhojiwa zaidi nyakati za utawala wa ronaldo na messi. Katika kilele cha ushindani wao hawa jamaa wawili world cup haikua na nguvu katika kuamua mshindi. Lakini wakati messi anachukua tuzo yake ya 8 kikatumika kigezo cha world cup kumpa tuzo, ingawa perfomance yake ya mwaka mzima haikua nzuri.

Nafikiri ronaldo na messi ndio walifanya hizi tuzo ziwe questioned kuhusu uadilifu wake. Binafsi naona katika tuzo 5 za ronaldo kuna moja hakustahili. Ilitakiwa iende kwa frank ribery. Katika tuzo 8 za messi kuna tatu hakustahili. Zilitakiwa ziende kwa iniesta, sneidjer na halaand.

Na kama FIFA itawapendeza nafikiri makipa wawe na balon d or zao binafsi. Maana ni ngumu kumzidi kura mchezaji wa ndani. Maajabu ya watu kama buffon, neur, oliver kahn wangeyafanya wakiwa wachezaji wa ndani wangekua na balon d or.
 
Back
Top Bottom