Baharia; (Ujasusi, Mapenzi na Upelelezi wa kutisha)

RIWAYA; BAHARIA

NA; BAHATI MWAMBA

SIMU; 0758573660


SEHEMU YA NNE



Hakuamini macho yake, aliona gari la baba yake mzazi likiwa linaingia barabara kubwa likiwa linatokea pale kwake.

“aah ina maana nyumbani nao wanajua nimekufa hadi wafuate nguo zangu?” Alijiuliza huku akiwa ameweka mikono kichwani.

Vedi hakujua afanye nini katika dakika zile ili kuondoa uongo ule ambao ulikuwa unasambaa kwa kasi kama moto wa kifuu.

****
Vedi aliona kama utani,ila ndivyo ilikuwa; vyombo vyote vya habari vililiripoti tukio lile kwa marefu na mapana huku sababu ya binti kujiua ikihusanishwa na wivu wa kimapenzi.

Habari zingine zilisema Vedi alijiua kwa kuwa hakupenda kuona rafiki yake akiolewa na bilionea kijana kabisa alieitwa Boneka.

Vedi habari zote alizipata akiwa kwenye kituo cha internet ya kulipia.

Alijifuta machozi kisha akachukua mkoba wake na kwenda kupanda gari kuelekea kwa dada yake aliekuwa akiishi Tabata bima. Alihitaji kujua kinachoendelea kabla hajafika nyumbani kwao ambako aliamini kabisa watakuwa wanaomboleza kifo chake.

Licha ya jambo hilo kumpata ila hakutaka kulihusanisha na tukio aliloshuhudia usiku ndani ya meli. Aliamini pengine walichanganya taarifa tu na alijua kabisa ataliweka sawa akifika nyumbani kwa dada yake.

Vedi akamfikiria Mama yake.

Hakujua ni vipi Mama yake atakuwa amepagawa na taarifa za kifo chake bandia.

Wakati akifikiria hayo kuna kitu kilimjia kichwani pake.

Kwanini ndugu zake wamefanikiwa kuamini uvumi haraka kiasi kile kiasi wakaharakisha kufuata nguo zake kwake?.

Akajifuta chozi lililoanza kumwanguka.

Akarudia tena kuwaza kitu kile.

Akaguna!!

Inamaana kama wamefanikiwa kupata taarifa za kifo chake basi wataitwa hospitali kuutambua mwili ule na je baada ya kutambua ndio wakaamua kufuata mizigo yake kule kwake?.

Hata! .

Kuna namna ipo.
Haiwezekani iwe rahisi kiasi hicho.

Wakati akiwaza yote hayo alikuwa mbali na kuikumbuka simu yake ambayo iligoma kufanya kazi kabisa hadi wakati huo ambao alikuwa ndani ya gari kuelekea tabata kumuona dada yake.

Hatimae safari yake ilikomea kituo cha bima kisha akachepuka upande wa pili na kuelekea mashariki ambako aliishia kwenye vichochoro kadhaa kisha akakunja tena na kwenda hadi kwenye nyumba iliokuwa na geti jekundu.

Kikawaida Vedi amezoea kufika kwa dada yake na kusukuma kigeti kidogo na kuingia bila kugonga hodi,alijua mazoea ya dada yake ya kuacha geti lile wazi huku akisema hapendi kusumbuliwa na hodi nyingi.


Aliona geri la dada yake likiwa limeegeshwa nje huku mlangoni kukionekana viatu vyeusi alivyopenda kuvivaa dada yake.

Mara nyingi Vedi alipenda kujikaribisha mwenyewe kwa dada yake. Hata siku hii pia aliingia na kukaa kwenye sofa huku akimsikia dada yake akivuta kamasi chumbani kwake.

Hakujua kama analia ama anafanya kitu gani, yeye aliendelea kukaa.

Dakika kadhaa badae alisikia mtu akilia huku anaukaribia mlango wa kutokea chumbani.

Mara dada yake akatokeza akiwa amejifunga ushungi huku machozi yakimtiririka.

Ebana ee!

Tofauti na matarajio ya Vedi; dada yake aliruka kwa woga na kupamia mlango wa chumbani kwake huku akitoa kilio cha woga na licha ya kupamia mlango ila bado hakufanikiwa kuingia ndani hivyo akabaki akisota kwa matako chini na kizuizi kilibaki ni mlango.
.
Macho ya dada ake Vedi yalimtoka mithili ya mtu aliepigwa ngeta.

Vedi alishindwa hata kuongea, akasimama.

“Tafadhali usiniue… .usiniue!!”

Eeh!

Vedi alishangaa,akageuka kutazama nyuma yake pengine ataona mtu anaeambiwa maneno hayo.

Hakuona mtu, na hivyo iliashiria maneno yale yalimlenga yeye.

Ajabu hii!!.

“Dada unakichaa kwani!” Vedi aliuliza kwa mshangao.

Bado dada yake aliendelea kutoa macho huku akiomba asiuliwe n mara hii alizidi kutetemeka..

“Dada mi ni Vedi”

“No! Mdogo wangu kafariki na nimemuona mwenyewe hospitali,wewe sio Vedi” Dada wa Vedi aliongea huku akiwa amefumba macho kama alieona jini mbele yake.

Vedi akazidi kupagawa kwa tukio lile.

“Dada mi ni mzima kabisa nipo hapa” Alijitetea Vedi.

Bado Dada yake aliendelea kulia kama bwege pale chini alipodondokea.

Vedi akapiga hatua ili amfikie dada yake amshike.

Ohoo!

Dada yake akasota kwa nguvu na kuusukuma mlango kisha akaingia ndani kwake na kufunga haraka.

Vedi alijikuta akishindwa kuamua, ama alie ama acheke kwa tukio lile.

“Jamani mi nimekufa?” Alijiuliza bila kupata jibu na hapo akakumbuka kauli ya dada ake ya kuwa amemuona akiwa amekufa hospitalini na hapo ndipo alijua kwa nini walifuata nguo zake nyumbani kwake.

Haiwezekani bwana!

Alijisemea Vedi huku akipiga hatua kuelekea kwenye mlango ili atoke nje.

Mara akasita gafla!

Kuna wazo lilipita kichawani mwake.

“au kweli nimekufa, mana wanasemaga roho huwa zinahagaika kabla ya maziko” Alijisemea huku akijifinya kwa kucha zake ili asikie maumivu.

Maumivu aliyapata!

“Sijafa bwana!” Alisema huku akipiga hatua ndefu kuuendea mlango akiwa na lengo la kuelekea nyumbani kwao.

Alivuka kichochoro cha kwanza na kabla hajafikia kichochoro kingine alikutana na mtu mmoja aliekuwa amevaa koti mtelezo jeusi.

Mtu yule alikuwa amejikunja kuwasha sigara yake.

Vedi alimpita.

Mtu yule nae aligeuka na kuanza kumfuata Vedi.

Vedi hakujali kufuatwa mana Dar kila mtu mambo yake.

Aliendelea kusonga hadi alipofika barabarani na kungojea daladala.

Akiwa amesimama na mtu yule nae alisimama mbali na kituo huku akindelea kuvuta sigara yake.

Gari ilifika na Vedi akapanda huku mtu yule nae akigeuka na kutoka pale alipokuwa amesimama.

Kwao Vedi ilikuwa ni mabibo na alielekea huko.

****

Baada ya foleni za hapa na pale, hatimae alishushwa kwenye kituo alichohitaji na baada ya hapo akaanza kutembea hatua za kivivu kuelekea nyumbani kwao.

Akiwa amebakiza mita chache ili afike kwao; Vedi aliona umati wa watu ukiwa nje ya nyumba yao huku magari nayo yakiweka jamu kwenye barabara na baadhi ya majumba ya jirani na pale kwao.

Mwili ulimsisimka kuona amewekewa msiba ilihali yeye ni mzima wa afya.

Akaona kupita lango kuu la kuingilia kwao ni kuzua taharuki isio na sababu ni bora atumie geti la dharura ili aingie ndani na azungumze na ndugu zake na waweke sawa lile jambo.

Akachepuka kwa tahadhari ili watu wasimuone na akapita kichochoro kimoja na kujikuta akiwa nyuma ya nyumba yao.

Akasikia sauti za wamama zikitokea upande ule na alipotizama aliona moshi ukipepea angani kuashiria mapishi yalikuwa yakiendelea upande ule.

Akajitazama mavazi aliovaa.

Hayakuweza kumsitiri vyema asifahamike, yeye alivaa suruali na T-shirt ya zambalau na mkononi alibeba mkoba ambao haukuwa na mtandio isipokuwa ulikuwa na vipodozi vichache na taulo za kike kwa ajili ya dharura na pia kulikuwa kuna kitabu cha kumbukumbu alichokitoa ndani ya meli.


Akapiga moyo konde na kuusogelea mlango ule wa dharura.


Ilikuwa ni bahati mbaya kwake,kwani wakati anataka kusukuma geti ili aingie ni wakati huo ambao geti lilifunguliwa na mwanamke alietaka kumwaga maji machafu nje.

Yule mwanamke alipiga mweleka wa nguvu baada ya kukutana na Vedi kisha akarudi mbio huku akipiga kelele za woga na kitendo hicho kilifanya wamama wengine nao watake kujua kulikoni huko getini.

Aah!

Hawakuamini wanachokiona.

Walishuhudia Vedi akiwa amesimama getini kama sanamu la kariakoo.

Nani abaki sasa!

Kukaibuka kitimutimu cha ajabu ambapo kila mtu alikuwa anaokoa roho yake kwa kuona mzimu wa Vedi ambae wamethibitisha amefariki na taratibu za mazishi zinaendelea vije tena mtu aonekane mzima getini.

Wamama walipiga kelele na kukumbilia mbele kulikokuwa na watu wengine wakiwa wamekaa.

Wababa nao hawakuwa nyuma kuungana na wamama kutimka kutoka nje ya geti huku wale wanene wakilaani dhahama ile wasioijua, kelele za jini jini, zilisikika kila kona huku vilio vya woga vikitamalaki eneo zima la nyumba ya Mzee Mashimo.

Wanaume baadhi walisalia na kutaka kuona kilichotokea na wakaungana japo kiuoga kuelekea kule walikotokea wale wamama.

Wakaelekea huko na hakuna walichoshuhudia.

Walirejea na jibu moja ya kuwa hakuna jini wala zimwi waliloliona huko nyuma ya nyumba.

Akaitwa yule mama alieanzisha sekeseke lile.

Nae kwa uhakika kabisa alisema amemuona Vedi akiwa amesimama getini,hoja yake ikaungwa mkono na wamama wengine waliokuwa katika upishi kule nyuma, nao wakaeleza wazi ya kuwa walimshuhudia Vedi akiwa amesimama getini akiwatizama.

Watu wa imani wakaita mchungaji wa kanisa alilosali Vedi;akaombea pepo baya linaloanza kundama nyumba ile.

Ndugu wa karibu walioguswa na msiba ule baada ya tukio lile wakaanza kulia upya ni kama walitoneshwa vidonda vyao ambavyo havikupona.

Wengi walilia ila kuna mtu mmoja ambae hakuwa akilia kabisa na alikuwa kimya jambo ambalo lilifanya kuzuke minong’ono miongoni mwa waombolezaji waliokuwa wamekusanyika ndani ya nyumba kufariji wafiwa.

Alikuwa ni mama Msangu;Mama wa Vedi na Msangu binti yake mkubwa ambae alimkimbia Vedi kule Tabata alikokuwa akiishi.

Msangu alifika nyumbani kwao na kuelekea alipokuwa amekaa mama ake.

Kama wengine nae alianza kulia huku akimsimulia namna alivyotokewa na muzimu wa Vedi.

Mama yake akamtazama kwa machungu sana kisha akamwambia
“Sina hakika kama mwanangu kafariki, sijauona mwili wake ila nafsi yangu inakataa kabisa kukubaliana na suala hili”

Msangu alikaa kitako huku akifuta machozi na kumtazama mama yake na asielewe kabisa.

“Mama nimeitwa kuhakikisha maiti ile na pasi na shaka ni Vedi yule, namjua mdogo wangu” Alisema Msangu kwa sauti ndogo ili wengine wasisikie maongezi yao.

“Mwanangu wewe hujazaa, ila ukizaa utajua kwanini nayasema haya, yani mwanao hata akifinywa uko nae mbali mwili wako utakupa taarifa ya maumivu yake sembuse kifo?” Alisema mama Msangu.

“Yani hata nikijilazimisha kulia bado machozi hayatoki kabisa mwanangu hajafa” Alizidi kusisitiza mwanamke yule.

Punde akaingia mzee Mashimo na kumuita mkewe chumbani.

“Mke wangu umesikia yalitokea huko nje?” Alihoji Mzee Mashimo.

“Kwa hiyo na wewe unaafiki ya kuwa watu wameona muzimu?” Alihoji Mama msangu bila kujibu alichoulizwa.

“Unamaana gani kusema hivyo Mke wangu”

“Vedi hajafa, mwanangu yupo hai kabisa na hajafa eti”

Aya!!

Mzee Mashimo alikodoa macho kwa kutoamini anachosikia kutoka kwa mkewe.

“Mke wangu unaanza kuchanganyikiwa kwa kifo hiki ngoja niite mchungaji ak..”

“Nipo mzima kabisa wala sijaugua na naomba tusitishe msiba huu Baba Msangu”

“Mama Msangu unakufuru sasa!” Mzee Mashimo aliwaka kwa hasira na kisha akatoka ndani na kuelekea nje bila kutia neno zaidi na aliona kama mkewe ameanza kuchanganyikiwa na msiba ule.

Maongezi yao yalikuwa yanasikiwa vyema na mdada aliekuwa amamekaa karibu kabisa na chumba walichokuwamo wazee wale alikuwa ameshika simu janja yake akionekana kuperuzi ila alikuwa anatuma ujumbe mahali na ujumbe ule uliibua jambo lingine tena katika familia ile ya mzee Mashimo.

Jambo ambalo kamwe hawatakaa walisahau katika maisha yao yote.

****


Nb; Maoni yako ni muhimu kwa kila sehemu unayosoma ili kuboresha sehemu inayofuata.
Soma na shusha utabiri wako kwa kitakachofuata, kosoa sifia ili uandishi uwe mzuri zaidi.

Karibunj
 
Mkuu Nina buku au hata Kama utanipunguzia Bei na hizo riwaya zako nyingine nipo tayari kuchukua kea ajili ya kujisomea na sio biashara.nakupataje?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom