Rev. Kishoka
JF-Expert Member
- Mar 7, 2006
- 4,526
- 1,529
Tatizo kubwa liko kwenye kipengele (d) Ujamaa ni Imani:
Kinasema: Lakini Ujamaa hauwezi kujijenga wenyewe. Kwani Ujamaa ni imani. Hauna budi kujengwa na watu wanaoamini na kufuata kanuni zake .. Wajibu wa kwanza wa mwana-TANU na hasa kiongozi wa TANU ni kutii kanuni hizi za Ujamaa hasa katika maisha yake mwenyewe. Na hasa mwana-TANU kiongozi hataishi kwa jasho la mtu mwingine au kufanya jambo lolote ambalo ni la kibepari au kikabaila.
Kipengele hicho kinamalizia na: Utimizaji wa shabaha hizo na nyinginezo zinazofuatana na siasa ya Ujamaa unategemea sana viongozi kwa sababu Ujamaa ni imani na ni vigumu kwa viongozi kujenga siasa ya Ujamaa ikiwa hawaikubali imani hiyo.
Viongozi wengi hawakuwa waumini wa dhati ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Walikuwa wanafiki na wabinafsi. Hawakulipenda Azimio la Arusha tangu mwanzo kwa sababu waliona linawabana. Pia wapo wengine ambao walikuwa ni bendera tu yafuata upepo. Hao ndio wale ambao hawakuweza hata kujifunza Siasa ya Ujamaa maana yake ni nini. Kwa hiyo, hawakuweza hata kuwafundisha ama kuwaeleza wananchi kinaganaga juu ya manufaa ya Siasa ambayo Chama chao kilikuwa kikifuata.
Wapo wengine ambao walikuwa na imani kubwa na Mwalimu Nyerere kutokana na msimamo aliokuwanao wa kujali sana maslahi ya wanyonge. Wapo pia ambao kwa kutokuwa na elimu ya kutosha na uelewa mdogo wa mambo ya Siasa, walikuwa wakifuata tu alichosema Mwalimu Nyerere bila kuelewa yale kiongozi wao aliyokuwa akiyasimamia. Hawa ndio wale waliokuwa wakiimba kama kasuku Zidumu Fikra .. Ukiwauliza ni fikra gani hawajui, hawana cha kueleza.
Lakini kuna kundi lingine ambalo walimchukia Mwalimu kwa kuwa aliwazidi kwa akili na kuwa na upeo mkubwa wa kufikiri na kuelewa mambo. Wengine walikuwa na chuki binafsi kwa kuwa pengine Mwalimu katika kutekeleza kazi zake za uongozi aliwahi kuwachukulia hatua kali ama kuwaumiza wao au jamaa zao. Kundi hili kwa chuki tu, liliweza kubeza na kupinga hata yale mazuri Mwalimu aliyoyasimamia. Wapo na wengine ambao walijiona kwamba hata wao walikuwa na mawazo mazuri kuzidi ya Mwalimu, lakini Mwalimu hakuyatilia maanani ama aliyapinga na akayajengea hoja ya kwake yeye, na kuibuka mshindi wa hoja; ama kwa sababu ndiye aliyeshika rungu la uongozi, kulazimisha yake aliyoyaamini yeye.
Matokeo yake, katika kujadili kushindwa kwa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, na Azimio la Arusha, wakawepo watu ambao bila kujua kwa undani madhumuni ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea iliyozaa Azimio la Arusha, ama kwa sababu nyingine yoyote waliamua kwamba Siasa hiyo ndiyo iliyoliletea umaskini nchini, na Azimio halikuwa muhimu wala halikuwa na manufaa kwa Taifa.
Hivi sasa, viongozi wa vyama vya Siasa, wasomi na wananchi wasioridhika na jinsi Serikali ya CCM inavyoendesha shughuli za nchi, hususan kwenye masuala ya ufisadi na matabaka yaliyojitokeza dhahiri ya Matajiri wa kutupa na Maskini wasiojua kesho watakula nini na watoto wao, na kadhalika, wamegundua kwamba kumbe Azimio la Arusha lilikuwa na mantiki. Pia, wapo wanaogundua kwamba Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea haikuwa na ubaya wowote, isipokuwa viongozi wa TANU na CCM waliopaswa kuwa mstari wa mbele katika kuijua, kuitetea na kuitekeleza hawakufanya hivyo kwa dhati. Kutokana na ubinafsi wao, hawakuwa na waumini wa kweli wa Itikadi waliyoamua wenyewe kuifuata!
Ili tuendelee tunahitaji Watu, Ardhi, Siasa Safi na Uongozi Bora!
Kwenye waraka wangu niliongelea haya:
Kurudisha na kuimarisha Heshima, Utu na Uadhi ya Mwananchi na Taifa la Tanzania
Kurudisha na kuimarisha Heshima, Wajibu na Hadhi ya kazi na kufanya kazi kwa Watanzania wote, vijijini na mijini
Kuelimisha Wananchi haki zao kama raia, wajibu wao na sehemu yao katika Taifa na Serikali yao kupitia Katiba, Serikali Kuu, Bunge na Mahakama
Kuimarisha Ufanisi na Ustawi wa Jamii katika kupiga vita Ujinga, Umasikini, Njaa na Maradhi
Kuhakikisha kuwa Katiba, Sheria na Kanuni zilizowekwa zinatekelezeka kutokana na nyakati zilizopo, zinafuatwa ipaswavyo na vyombo vyote husika; Serikali, Bunge, Mahakama na Wananchi wenyewe. Aidha kuweka maamuzi na mipango ya Serikali wazi kwa wananchi wote ili kuhakikisha uadilifu na uwajibikaji wa Serikali haufanyiki kwa siri na na kuwapa wananchi wote haki kwa kuwa wao ndio waliotoa dhamana ya kuwepo kwa Serikali na kuruhusu Uongozi uliopo uongoze nchi
Kubuni mbinu za kiuchumi ili kumpunguzia mzigo mwananchi wa kawaida hasa wale wa kipato cha chini na wakulima ili kujenga nguvu kubwa ya taifa kuwa katika Tabaka la kati (middle class)
Kuhakikisha kuwa njia kuu za Uchumi na uzalishaji mali zinaboreshwa na kutumika kwa manufaa ya kila Mtanzania na taifa la Tanzania linanufaika kwanza
Kuhamasisha na kuhakakisha kuwa Uzalishaji mali (kilimo, viwanda, uvuvi, ufugaji, biashara, madini , utalii, biashara, sanaa, michezo, huduma na maofisini) unafanyika kwa dhatgi, kisayansi, kiushindani, kiuwajibikaji, kiufanisi na kwa ubora wa hali ya juu kwa kutumia tija, kuongezeka kwa juhudi na maarifa ya uzalishaji mali huu
Kuhakikisha kuwa huduma za msingi zinaboreshwa na kupewa kipaumbele na kufikishwa kwa wananchi ili kujenga maendeleo ya kweli kwa jamii na Taifa;- Afya, Elimu, Maji safi, Chakula, Uchukuzi na Nishati
Kuhakikisha kuwa vita dhidi ya Rushwa, Ubadhirifu, Udini, Ukabila, Uzembe, Ufisadi, Uhujumu, Uvivu, Uzururaji na Kutowajibika au kutokujituma kwa watendaji wa Serikali na taasisi zake (wakuteuliwa au kuchaguliwa), waajiriwa , wafanyakazi na wakulima ni vita vya Taifa zima na linahitaji ushiriki na kushirikisha Wananchi wote. Wananchi wote bila kujali kabila, rangi, jinsia, umri, elimu au mwelekeo wa kisiasa ni wajibu wao kushiriki katika vita hii
Pamoja na kuwa haya ni kuhusu Mwananchi, lakini ni Uongozi pekee ulio mahiri, adilifu, bunifu, nyenyekevu na chapa kazi unaweza kufanikisha hili.
Nikaendelea kuyasema haya
Kazi tuliyonayo sasa si tofauti na ile ya mwaka 1967, ni ile ile na sana sana ni kulenga Nyenzo kuu za maendeleo yetu kama Taifa na kibinafsi kwa kupitia milango miwili. Ili tujikwamue kutoka hali hii mbaya tuliyonayo kama Taifa, ni wajibu wa kila mmoja wetu kuwajibika na kuwa na nia ya kweli kuyafanya yafuatayo;
Uchumi wetu hauwezi kujengeka kwa kutegemea misaada au wawekezaji kutoka nje kuja na kusukuma gurudumu la uzalishaji mali ili kutuongezea kipato. Aidha uchumi wetu hautajengeka kuwa madhubuti kwa kuanzisha mipango mipya au kufanya makosa yaleyale ya kale yaliyofanyika wakati wa Azimio la Arusha, Mipango ya kufufua uchumi 1985-2000 au mipango ya kuchochea Uwekezaji na kuvutia wageni washike hatamu za Uchumi ya 1992-2010.
- Kujenga Uchumi imara na madhubuti. Hili litatusaidia katika vita dhidi ya Umasikini, Ujinga, Maradhi na Njaa
- Kuwa na Uongozi mahiri na fanisi. Utawala na uongozi wa nchi unahitaji na unategemea Uongozi mahiri kutekeleza sera na mipango, wenye ufanisi kuhamasisha uzalishaji mali na uwajibikaji na wenye kuwa wanyenyekevu na kuheshimu dhamana walizopewa
Na mwisho nikatoa vipaumbele vya Uongozi bora
Uwezo wa Tanzania kuwa na maendeleo ya kweli utaanza na Uongozi bora.
Uongozi bora ni ule;
· wenye mapenzi ya kweli na dhati na kujivunia Utaifa wake
· wenye kujali na kulinda maslahi ya Taifa lake na watu wake
· wenye uwezo wa kupanda mbegu imara ya Uzalendo kwa kila mwananchi bila kujali itikadi, rangi, kabila, dini, elimu, umri au jinsia
· wenye uwezo wa kuhamasisha na kuchochea juhudi za maendeleo ya jamii, umma na Taifa
· wenye nidhamu, watiifu, kuwajibika, tija, ufanisi, kujituma na ufuatiliaji wa hali ya juu
· wenye usikivu, uungwana na unyenyekevu kukiri makosa, kukubali kukosolewa na kupokea na kufanyia kazi maoni ya wengine
· wenye uwezo wa kufanya kazi, kufikiri, kuwa na upeo na wepesi wa kukabili na kufanya maamuzi magumu
· usiolea uzembe, ubaguzi, unyanyasaji, uhujumu, ubadhirifu, rushwa, kudharau, kudhalilisha, kujuana au kulinda maslahi ya wachache au kikundi Fulani
Wajibu wetu kama Taifa na haki yetu kama wapiga kura kuchagua viongozi kutuongoza unabidi uachane na mfumo duni tulioujenga wa kuangalia sura na chama na tuangalie wagombea wetu wa uongozi kwa vigezo hivyohapo juu ili kuunda tabaka jipya la viongozi ambao ni wachapakazi na watakuwa manahodha wazuri kutuongoza katika safari yetu ya kulijenga Taifa.
Sasa kilichotokea ni kuwa Viongozi wengi walikuwa wakihubiri "Juhudi na Maarifa, Ujamaa na Kujitegemea" lakini wengi wao Juhudi na Maarifa yalikuwa ni kujineemesha matumbo yao na kupiga domo na si kufanya kazi na kuwa mfano wa kuigwa. Ni hao hao ambao badala ya kutumia nyenzo ya kujitegemea na kujiimarisha kuwa huru an kujitegemea, wakaitegemea Serikali kwa kila kitu mpaka karatasi za chooni kwa jina la Uongozi.
Azimio bado ni hai kwa wale wenye imani na ambao wakao tayari kulifanyia kazi.
Niko mstari wa mbele kutamka rasmi kuwa naamini Azimio la Arusha kwa 85% bado ni hai na ni muhimu kufanyiwa kazi kw aTaifa letu!