APRILI 30, mwaka huu, Ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kulifanyika kongamano la miaka 44 ya Azimio la Arusha.
Ni kongamano lililoandaliwa na Sauti ya Vijana Tanzania-Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (SAVITA UDSM), kwa kushirikiana na Klabu ya Falsafa chuoni hapo.
Kongamano lilihudhuriwa na wengi, baadhi wakiwa mashuhuda wa kuzaliwa kwa Azimio hilo. Mashuhuda hao ni pamoja na Ibrahim Kaduma, Waziri wa zamani katika Serikali ya Mwalimu Nyerere pamoja na Mzee Hashim Mbita.
Profesa Issa Shivji, ambaye naweza kumtambua kama wakili wa Azimio la Arusha lililohujumiwa bila hatia, aliongoza tafakuri ndani ya kongamano hilo.
Kauli mbiu ilihusu; Tafakuri ya kina juu ya Azimio la Arusha. Je, lina nafasi katika mjadala wa Katiba mpya?
Kwa kauli mbiu hii, ni dhahiri Azimio lilipuuzwa na hatimaye kuhujumiwa bila hatia, misingi yake sasa inahitajika nchini.
Ni misingi ya utu inayokataa suluhu na viongozi wanaojilimbikizia mali kwa kutambua kuwa utu haulindwi kwa mitutu bali uongozi bora wenye miiko.
Hadi mwisho wa kongamano, ilidhihirika Azimio halikuwa na hatia yoyote mbele ya wanyonge isipokuwa liliwakera baadhi ya viongozi tu.
Madhara yamezidi kujianika. Kwa sasa, si tu viongozi wamejilimbikizia mali; bali wanaitumia mali hiyo kuharibu mifumo nyeti nchini, ikiwamo ya kupata uongozi bora. Wamegeuza, kwa mfano, mchakato wa uchaguzi kuwa gulio la kuuza na kununua kura.
Hujuma dhidi ya Azimio zimeibua viongozi mafisadi. Hakika, Azimio halikuwa na hatia. Ni dhahiri waliolipuuza na kuhujumu ndiyo wenye hatia.
Halikuwa na hatia kwa sababu lililinda maslahi ya wanyonge na kutoa si tu mwongozo, bali pia mwelekeo kuhusu mustakabali wa uongozi bora nchini.
Wananchi mashambani, sokoni, safarini, majumbani na hata ofisini walikuwa na uhakika kuhusu kiongozi gani anastahili kuwajibishwa, kwa sababu gani na kwa wakati gani.
Walikuwa na fursa ya kufahamu hivyo kwa sababu Azimio lisilokuwa na hatia kwao, liliwapa fursa ya utambuzi huo kutokana na kusimika miiko ya uongozi kitaifa, kimkoa, wilaya, kata hadi kijiji au mtaa.
Uongozi ulitengwa na kuwekewa mkondo usiopenyeza wanunuzi au walanguzi wa kura kama ilivyo sasa ndani na nje ya vyama vya siasa.
Naunga mkono mawazo yaliyoibuka kwenye kongamano kwamba; ni wakati muafaka misingi ya Azimio la Arusha isimikwe kwenye Katiba mpya na hasa miiko ya uongozi.
Naunga mkono kwa sababu, hatupaswi kuacha suala la miiko ya uongozi liamuliwe kwa kuzingatia utashi wa vyama vya siasa au sheria za hapa na pale zinazotungwa kwa kuzingatia hisia za serikali au Bunge.
Hatupaswi kuliacha suala la miiko katika hali hiyo. Hatupaswi kutelekeza suala hili nyeti kwa Taifa. Lazima tuwe na masharti ya uongozi na yabainishwe sasa katika Katiba mpya.
Kuna tofauti kubwa ya kiuongozi kati ya enzi zile za utekelezaji wa Azimio la Arusha na miiko ya uongozi na enzi hizi za uongozi bila miiko. Kwa sasa, tunashuhudia kiwango cha juu cha kuvumilia uhuni, ufisadi na uchafu mwingine katika uongozi wa kitaifa.
Tunashuhudia suala la uhuni wa kiuongozi likiachwa kushughulikiwa kwa mujibu wa utashi wa kiongozi mkuu badala ya mfumo ambao ungekuwa bora na imara zaidi kama ungeimarishwa katika misingi ya Azimio la Arusha; yaani miiko ya uongozi.
Bado tunahitaji zaidi misingi ya Azimio la Arusha ambalo pengine si sahihi sana kudai limeuawa. Si busara kusema limeuawa kwa sababu Azimio la Arusha limejikita zaidi katika fikra (hasa fikra sahihi).
Na ukweli ni kwamba, ni vigumu na pengine haiwezekani kuua fikra sahihi ndani ya Azimio la Arusha. Tunaweza kuua mtu mwenye fikra sahihi, lakini hatuwezi kuua usahihi wa fikra zake.
Kwa mantiki hiyo ya uwezekano wa kuua mtu mwenye fikra sahihi lakini kamwe kutoweza kuua usahihi wa fikra zake, nahimiza wazalendo wote ndani na nje ya nchi, kuamini kuwa Azimio la Arusha na hasa misingi yake, ni suala la kifikra zaidi, tena fikra sahihi.
Kama ilivyoelezwa katika kongamano, misingi ya Azimio la Arusha ilikuwa ni utu uliowekewa mipaka ya nidhamu kiuongozi. Hizi ni fikra sahihi. Ni fikra hai kuliko msimu wa uhai wa binadamu.
Azimio lilibainisha nani awe kiongozi na nani asiwe kiongozi. Kazi ya kumtafuta kiongozi haikutupwa au kutelekezwa mikononi mwa wapiga kura wenye kuhangaikia tonge la siku kiasi cha kukosa muda wa kupima kwa busara nani kiongozi bora.
Kazi ya kumtafuta kiongozi bora, na hivyo kujenga uongozi bora nchini ilirahisishwa ndani ya Azimio la Arusha kupitia miiko ya uongozi.
Mgombea alijipima ubavu kama atamudu kuongoza bila kujilimbikizia mali, kama atazingatia misingi ya utu na hasa kwa vitendo kwamba; binadamu wote ni sawa.
Mgombea hakupewa fursa ya kujipima kwa kutazama kigezo cha fedha au ukubwa wa biashara zake. Alilazimishwa kujipima kwa kigezo cha miiko ya uongozi kwa mujibu wa Azimio la Arusha lisilo na hatia kwa wanyonge.
Ndani ya Azimio la Arusha, kutokujilimbikizia mali halikuwa suala la kwenda kuamuliwa mahakamani ambako si ajabu hata baadhi ya majaji au mahakimu wakawa ni sehemu ya wenye hatia.
Kwangu, kongamano hili lilinipa nafasi ya kuwatambua waliohujumu Azimio la Arusha bila hatia kuwa ni sawa na walioshiriki mauaji ya wanafunzi ya Soweto, Afrika Kusini.
Wanafunzi wale walijitokeza kuandamana Juni 16, 1976 wakipigania utu na haki kama ambavyo Azimio la Arusha lilivyokuwa likijinadi. Walipigania msingi wa utu kwa kupinga ubaguzi. Lakini bila hatia, maisha yao yalizimwa. Wakauawa.
Waliandamana kudai haki na misingi ya utu, uongozi bora usio wa kibaguzi. Kwa wakati huo, Azimio la Arusha lilikuwa likiishi bila kuhujumiwa. Tanzania iliyokuwa ikiisaidia Afrika Kusini, kwa hali na mali, kupinga ubaguzi wa rangi pia ilikuwa ikiishi katika falsafa ya Azimio la Arusha lililotambua binadamu wote ni sawa.
Ilikuwa katika mitaa ya Soweto, wanafunzi takriban 20,000 wa shule mbalimbali walijitokeza kwa ujasiri mkubwa kutetea haki na utu. Hawakujua mwisho wa uamuzi wao huo, baadhi yao 176 waliuawa.
Hata hivyo, waliouawa na ambao hawakuuawa, kwa pamoja hawakujua kitakachowapata, lakini walijua wanapigania haki.
Kwa hali ilivyo na hasa katika kupigania urejeshwaji wa miiko ya uongozi, ni lazima tuwe na upande. Tuchague upande. Wanaounga mkono wajitokeze, wanaopinga pia tuwajue. Wasiokuwa na upande tutawaweka kundi moja na wanaopinga urejeshwaji wa miiko ya uongozi.
Nimalizie kwa kunukuu mtazamo wa mmoja wa raia wa Marekani waliopata kuwa watetezi wa Ujamaa, Max Eastman aliyepata kusema:
People who demand neutrality in any situation are usually not neutral but in favor of the status quo.
Max, aliyezaliwa Januari 4, 1883 na kufariki Machi 25, 1969 anajenga mantiki kwamba; wanaojidai hawana upande katika masuala ya msingi, si kweli kwamba hawana upande, isipokuwa wananufaika na hali ilivyo.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika