Athari za mabadiliko ya tabianchi kamwe hazitaisha kama dunia haikuchukua hatua kwa pamoja

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,034
Na Pili Mwinyi

VCG31N1350886400.jpg

Ukame, mafuriko, moto wa msituni, ukosefu wa chakula, kutoka nchi zenye mapato madogo hadi zenye mapato makubwa duniani, athari za mabadiliko ya tabianchi zimekuwa zikishuhudiwa kila siku katika sayari hii. Kati ya mwaka 1998 na 2017, hasara iliyotokana na hali mbaya sana ya hewa duniani ni kama $174 bilioni kila mwaka.

Kwa mujibu wa ripoti ya umasikini, ukosefu wa usawa na mabadiliko ya tabianchi iliyotolewa na Umoja wa Mataifa, watu wanaoishi kwenye umasikini ndio wanashuhudia zaidi makali ya mabadiliko ya tabianchi na kupata hasara kubwa kuliko hata wale wanaoishi kwenye mataifa tajiri.

Lakini si mataifa hayohayo tajiri ndio yenye jukumu la kubadilisha mwelekeo huu?

Nchi mbalimbali za Afrika hivi sasa kila siku zimekuwa zikiripoti kuwepo kwa dhoruba kali ya upepo, ongezeko la joto na mafuriko, kwani kila inaponyesha mvua kubwa kwenye baadhi ya maeneo basi yanafuata mafuriko. Nchini Uganda mwaka uliopita (2020) kiwango cha maji katika Ziwa Victoria ambalo ni kubwa katika Afrika, kilikuwa juu kuliko kawaida na maji yalifurika katika maeneo ya karibu na ziwa hilo. Mafuriko ya Uganda yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi yamesababisha watu kama 200,000 hivi kupoteza makazi yao, kwani nyumba nyingi zimeharibiwa. Mbali na mafuriko pia maporomoko ya udongo na tope yanashuhudiwa nchini humo.

‘Uhaba wa mvua’ hili ni tatizo kubwa zaidi ambalo sasa linaziathiri nchi za Afrika Mashariki zikiwemo Kenya na Tanzania. Kutokana na mabadiliko ya tabianchi sasa mvua zimekuwa haziwezi kutabirika. Hivi majuzi Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwenye utabiri wake wa msimu huu wa mvua, ilibainisha kuwepo viashiria vya uhaba wa mvua mpaka chini ya wastani kwa mikoa ambayo ni muhimu na vinara kwenye uzalishaji wa chakula nchini humo. Hivyo kuzua hofu na wasiwasi wa kuwepo upungufu mkubwa wa chakula Tanzania.

Nako nchini Kenya Rais Uhuru Kenyatta tarehe 8 Septemba 2021, alitangaza ukame unaoathiri maeneo mengi nchini humo kuwa ni janga la kitaifa, na mamlaka za hali ya hewa nchini humo zimekadiria kuwa idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa kali itakuwa na kufikia milioni 2.4 katika msimu wa mvua chache wa Oktoba hadi Disemba. Hizi si hadithi bali ni hali halisi zinazoshuhudiwa katika maeneo ya nchi mbalimbali. Juhudi za lazima zisipochukuliwa, kweli dunia inaweza kuangamia, na mwishowe tukabakiwa na majuto tu.

Hivi sasa dunia imekuwa ikitegea sikio na kusubiri kupata majibu ya maswali mengi yanayozunguka kwenye vichwa vya watu kuhusu ufumbuzi wa athari na matatizo yote haya ya mabadiliko ya tabianchi. Mkutano wa wiki mbili wa mabadiliko ya tabianchi (COP26) ulioendelea wikiendi hii katika jiji la Glasgow, nchini Scotland ndio jukwaa kubwa linalotia watu matumaini ya kuleta suluhu ya mabadiliko ya tabianchi hasa kwa nchi zinazoendelea zikiwemo za Afrika zinazokabiliwa na tishio kubwa.

Moja ya ahadi walizotoa ili kupata suluhu ya tatizo hili ni kwamba viongozi wa kundi la nchi 20 (G20) wamekubaliana kusitisha ufadhili wa uzalishaji wa makaa ya mawe katika nchi za nje na kuwekeza kwenye nishati safi na endelevu, ikimaanisha kuwa zinapaswa kutumia teknolojia zaidi. China ikiwa mstari wa mbele kutekeleza ahadi zote inazotoa kwenye majukwaa ya kimataifa, hivi majuzi tu serikali yake ilitangaza kusitisha ufadhili wowote wa miradi mipya ya makaa ya mawe katika nchi za nje, lengo likiwa ni kukomesha kuongezeka kwa joto ulimwenguni. Ahadi hiyo imesifiwa kama hatua muhimu ya kukwamua changamoto za ongezeko la joto duniani. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Wakulima Afrika Mashariki, Steve Muchiri anasema nchi nyingine zinafaa kuiga mfano wa China wa kuongoza kwa vitendo.

“China inaongoza katika kushughulikia mabadiliko ya tabianchi, imefanya juhudi za kutosha, tunaomba nchi nyingine pia zifanye hivyo, na ziweke bayana vile namna zitakavyofanya, hata nchi za Afrika pia zina jukumu la kuhakikisha kwamba zinazingatia mambo ya mabadiliko ya tabianchi kuanzia sasa na kuendelea hadi siku za mbele.”

Kusitisha matumizi ya makaa ya mawe na utoaji wa hewa ya ukaa kunaonekana kufanikisha ahadi ya makubaliano ya Paris ya kupunguza ongezeko la joto duniani na kuwa chini ya nyuzi 2 hadi 1.5C. Hii ni muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kama vile dhoruba kali, mafuriko, moto wa msituni na udongo kutokuwa na unyevu kutokana na uhaba wa mvua ambao huleta upungufu wa mazao na kusababisha baa la njaa.
 
Na Caroline Nassoro

VCG111356147057 (1).jpg


Mkutano wa Nchi zilizosaini Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) uliofanyika Glasgow, Uingereza, umemalizika hivi karibuni. Katika mkutano huo, suala la nchi tajiri kutimiza ahadi zao za kutoa dola za kimarekani bilioni 100 kila mwaka kuzisaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi lilipewa kipaumbele.

Nchi zinazoendelea, zikiwemo za Afrika, zimekuwa ni wahanga wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi. Majanga ya asili kama mafuriko, maporomoko ya udongo, na ukame yameleta athari kubwa kwa watu wa nchi hizo. Uhaba wa mvua umeshuhudia mavuno hafifu yasiyotosheleza mahitaji ya familia na hata mataifa husika, na kusababisha baa kubwa la njaa.

Mwaka 2009, wakati wa mkutano wa 15 wa Nchi Zilizosaini Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadilko ya Tabianchi, (COP15) uliofanyika Copenhagen, Denmark, nchi tajiri duniani ziliahidi kutoa dola bilioni 100 za kimarekani kila mwaka kwa nchi maskini ili kuzisaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kupunguza ongezeko la joto.

Ahadi hiyo iliyotolewa miaka 12 iliyopita, mpaka sasa bado haijatimizwa, na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi zimeongezeka kwa kasi.

Marais wa nchi za Afrika waliohudhuria mkutano wa COP26 walitoa wito kwa nchi tajiri kutimiza ahadi yao hiyo. Rais wa Misri, Abdel-Fattah al-Sisi alisema, kuna pengo kubwa kati ya fedha zilizoahidiwa na fedha zilizopo, na pia kuna vikwazo vingi ambavyo nchi hizo zinakumbana navyo katika kupata fedha hizo.

Lakini wakati nchi zinazoendelea zikisubiri fedha hizo, kuna hatua ambazo zinaweza kuchukuliwa ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi katika nchi husika.

Moja ya mambo muhimu yanayotakiwa kupewa kipaumbele ni kulinda misitu na kuacha kukata miti hovyo. Kuna wakati nchini Tanzania kulianzishwa kampeni ya ‘kata mti, panda mti,’ ambako kwa kila mti unaokatwa, miti mingine miwili ilipandwa. Jambo lingine la kuzingatia ambalo nchi zinazoendelea zinaweza kufanya ni kulinda vyanzo vya maji. Tumeshuhudia binadamu wakivamia maeneo ya vyanzo vya maji na kuendeleza shughuli za kibinadamu, jambo linalosababisha aidha kupungua kwa maji, ama majanga ya kiasili kutokea.

Waswahili husema, tunza mazingira yakutunze. Tutakapoanza kutunza mazingira yetu kwa nia thabiti, kuacha kutupa ovyo taka, kuacha kukata miti ovyo, kupunguza utoaji wa hewa chafu, na kuanza kutumia nishati mbadala, ni wazi kuwa hali ya hewa ya dunia itarejea kuwa nzuri, na binadamu wataishi kwa masikilizano na mazingira yanayomzunguka.
 
Back
Top Bottom