Asubuhi ya kwanza Dar es Salaam

Asubuhi ya kwanza Dar es Salaam

Jokajeusi

JF-Expert Member
Joined
Jun 1, 2018
Posts
6,336
Reaction score
10,896
Habarini Wakuu!!

Moyo ulikuwa unapwita pwita kwa shauku. Furaha si Furaha, hamasa si hamasa. Nilikuwa siamini kama siku yenyewe ndio imefika. Siku ambayo machungu na shurba zote zingekoma. Tabu na vurugu zingeyeyuka. Kadhia za kijiji nilizipa mkono wa baibai. Sitaenda tena kuchunga ng'ombe na mbuzi. Sitaenda tena kukata kuni wala kulima Kwenye Mashamba ya mzee Joka. Nilijisemea moyoni huku uso wangu ukifunikwa na ukungu wa tabasamu.

Basi lilitia moto tayari kwa safari. Niliangaza macho huku na huko mule ndani na kuona jinsi teknolojia ilivyokuwa kwa kiwango cha juu. Ndani ya Basi kulikuwa na Luninga karibu kila kiti. Nilikumbuka vile vigari vya kijijini kwetu nikabaki tuu kucheka. Mule ndani pia kulikuwa na AC iliyozidisha kaubaridi kenye kuleta mvuto zaidi. Yote ningeyapata wapi mimi mtoto wa shamba niliyezoea kupigwa na upepo wenye vumbi. Kama si hii safari nauliza JokJeusi ningepata wapi kupulizwa na AC.

Jirani yangu aliketi mwanadada ambaye sura yake haikufahamika mara moja kutokana na kubadilika badilika kila mara. Alikuwa kila baada ya dakika kumi anatoa Mekapu(Make up) na kuanza kujiremba. Jamani Nauliza Joka ningepata wapi kuona mambo haya kama si safari hii. Nilikumbuka wasichana wa kijiji chetu walivyokuwa wamevubaa kwa vumbi na moshi wa kuni. Niliona nimefanya maamuzi muhimu sana katika maisha tangu kwani nilijinasua kwenye mtego mbaya wa jinamizi la shamba.

Nilishangaa kila mmoja mule ndani ya Basi akipewa Soda. Sikuamini si macho mpaka nilipopewa na mimi. Alikuja Dada mmoja mrembo aliyeumbika haswa akiwa ndani ya sare. Aliniuliza natumia soda gani, ndipo Joka nikacheka si kwa kufurahi, hasha bali ni kwa kuhamanika tuu. Nilipewa Cocacola. Lakini yule Dada alikataa kupewa. Nilitamani nimwambie yeye achukue lakini kama hanywi nitakunywa mimi. Nilimuongalia kwa jicho la kifedhuli ungedhani ninamdai. Nauliza ningeyapata wapi haya yote kama si hii safari wakati kijijini kwetu Soda unainywa kipindi cha Sikukuu au harusi za vibopa.

Nilitamani gari ipae kwa spidi ya Kilohaz Frikwensi Megamix ili nifike Dar. Nikatabasamu kwa kitambo baada ya kukumbuka Bashite yangu ya Fizikia. Mambo hayo nilimuachia Aizaki NYutoni.

"Nikifika Dar lazima nimuone Kanumba" NIliwaza kwa sauti ya moyoni. KIla nililowaza nililipa Tiki ya tabasamu. "Nikifika Dar lazima nimuone Joti" wazo hilo lilifuatiwa na tabasamu. "Nikifika Dar Nitaenda kuogelea beach" Halikadhalika nilitabasamu. "Nikifika Dar lazima nimuone Dr. Shika" hapa nilicheka kwa sauti kidogo watu waliokaribu yangu wakanitazama. Niliona aibu kama mtu aliyejamba Ukweni. Hata hivyo nilipuuzia.

Mfukoni nilikuwa na shilingi milioni moja nilizozipata baada ya kuuza ng'ombe mbili nilizomuibia Baba yangu Mzee Joka. Niliziona ni nyingi sana za kunikimu mpaka nitakapopata kazi.

Nilifurahishwa na namna nchi yetu ilivyo nzuri yenye kuvutia. Niliyaona mabonde mazuri yenye rutuba ambayo yangefaa kwa kilimo. Lakini ni nani alime ikiwa Hata Joka Jeusi nimekimbia jembe. Wanasema mfupa uliomshinda fisi. Pia niliona mashamba makubwa ya Mkonge yaliyopandwa wka mistari misari na kufanya muonekano mzuri. Njiani tulikutana na makundi makundi ya mifugo yakivuka barabara hivyo gari letu lilipunguza mwendo kuruhusu mifugo ile ipite. Lakini kila nilipokumbuka adha ya kuchunga ng'ombe nilitamani dereva azigonge tuu.

karibu watu wote ndani walikuwa wamelala kasoro mimi na Wamasai wawili ndio tulikuwa macho tukitizama luninga. Watu wa mikoani utatujua tuu. Safari yote ni kushangaa nje na kuangalia luninga. Lakini usinilaumu bhana, sio kosa langu, nyumbani kwetu hakuna Luninga.

Niliingia Jiji la Dar saa kumi jioni nikiwa nimechoka kama Ostadhi wakisunni aliyefunga Ramadhani.
Nilishuka nikiwa sijui niende wapi. Nilichukua boda boda nikamuamrisha dereva anipeleke Manzese. Alinipeleka kwa elfu tano. Nilichukua Gesti ya elfu kumi na tano nikapaki begi na kuondoka kwenda kuzurura. Unaambiwa Jogoo la shamba haliwiki mjini lakini kauli hiyo nilitaka kuifuta rasmi. Nilitembea kwa kudunda ungedhani ni wale magensta wa Arusha. Hii yote ili nami nionekane ni Mtoto wa Mujini.

"io hapo shi,ngapi Mshikaji wangu" Niliongea kidarisalamu huku nikitafuna Big G. Moyoni nilijicheka lakini nitafanya nini na nitatenda kitu gani. Ndio hivyo sasa nimekuwa mwanagenzi wa MJI wa kibashite.

Nilipitia Bar kupata Fanta painepo, na huko nilikutana na warembo wa kila rangi, umbo na mapozi tofauti. Nilijikuta katika tamaa ya ngono. Nilichukua manzi mmoja wa Kisingapori ati ni ndugu yake Sepenga. Nilienda nae Kwenye Ile Guesti kwa makubaliano ya kumlipa elfu thelathini. Kweli Dar ni Dar tuu. Kumbe ndio maana Jiwe anafukuza watu lakini watu wameng'ng'ania hawataki kuondoka.

Asubuhi ilifika Joka nikaamka. Ilikuwa Asubuhi ya kwanza katika jiji la Bashite. Watu wanaongea kibashite, huku watu hutembea Kibashite, Kuvaa kibashite yaani Kila kitu ni Ubashite. Watu wa mji huu hujivunia ubashite. Nasikia bila maisha ya kibashite Mji huu unaweza kukushinda. Basi Joka kuangalia pembeni simuoni Yule Mrembo niliyemtoa huko kwenye vilabu vya pombe.

kengele ya hatari ililia kichwani. Nilitazama begi langu nikakuta nguo na vitu vingine nje ya begi. Tayari nilikuwa ni mhanga. Mapigo ya moyo yalipiga na kukimbia mbio sana. Nilianza kuhema kama panya aliyekoswa koswa na paka. Oooh!! Salale Jokajeusi nitafanya nini. Milioni na kitu zimepaizwa na Kidosho wa Mujini.

Nilianza kutoa laana ya kibashite kwa wale wote watakaoitumia hela yangu. Iwe ni yule mdada au yeyote tuu. Ilimradi Dua la kuku raundi hii limpatae mwewe.

Wasalaam!!
 
Back
Top Bottom