Askofu Chiwanga: Magufuli awaambukize ukali watendaji wa chini

cheusimangala_

Senior Member
Dec 1, 2018
114
174
pic+askofu.jpg



Jina la Askofu Simon Chiwanga (81) si geni masikioni mwa wengi, hasa waliokula chumvi kiasi.
Aliwahi kuwa mwalimu, mwanasiasa na mjumbe wa kamati kuu CCM, Mkurugenzi Shirika la Elimu la Kibaha na amemaliza utumishi akiwa Askofu wa Kanisa la Anglikana akiwa ndiye mwanzilishi wa Dayosisi ya Mpwapwa.

Mwananchi ilimtembelea nyumbani kwake Mpwapwa na kufanya mazungumzo kuhusu miaka minne ya uongozi wa Rais John Magufuli. Endelea.

Swali: Rais John Magufuli ametimiza miaka 4 madarakani, kuna kitu chochote ungependa kuzungumza juu yake?

Jibu: Yapo mengi lakini jambo la msingi ni kumshukuru Mungu. Kabla sijataja jambo lolote, napenda Watanzania wafahamu kuwa kila awamu ya uongozi tangu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Mungu amekuwa akituongoza kumchagua Rais kwa mahitaji ya wakati husika.Lakini kwa awamu ya Tano, Tanzania ilihitaji Rais na wasaidizi wake wawe wakali katika vita ya ukombozi wa kiuchumi na kijamii, wakijenga katika msingi na kazi ya uongozi uliowatangulia. Ndiyo maana akapatikana Rais Magufuli, Samia Suluhu Hassan na Kassim Majaliwa ambao wameletwa kwa wakati mwafaka na kwa kazi maalumu.

Swali: Umezungumzia suala la ukali, unamaanisha ni na kuna faida yoyote kwa kiongozi kuwa mkali?

Jibu: Ukali ninaouzungumzia mimi ni wa uthubutu na kufanya maamuzi. Rais Magufuli ni jasiri mwenye moyo wa kuthubutu na kujitoa kwa manufaa ya watu. Ni mkali kwa wachache wenye tabia sugu ya kukwamisha maendeleo ya watu na tamaa ya kupata utajiri kwa njia haramu.Kwa hiyo, jambo kubwa la kujivunia ni kumshukuru Mungu katika miaka hii minne ya Uongozi wa Rais Magufuli kwamba hajawasaliti Watanzania kwa mambo aliyoahidi na matazamio yao, kwani ameendeleza ukombozi wa Mtanzania kwa kasi na ukali zaidi unaotakiwa akiwa na mafunuo ya mbali.

Swali: Unaweza kutaja kwa mifano kuhusu alama aliyoweka kwa miaka minne?

Jibu: Naam, huyu bwana ametutoa katika meza ya majadiliano, sera, mikakati na maazimio na kutupeleka kwenye uwanja wa utekelezaji kama tunavyowaona mawaziri wake wakichapa kazi nzuri. Mfano mzuri ni Profesa Palamagamba Kabudi na wenzake, kwani wengi wamemwelewa kuwa hataki habari ya tuko mbioni, upembuzi yakinifu bado unafanyika, na kauli kama hizo ambazo zilizoelekea.Kingine ni kuwa ametuoa katika vikao visivyokuwa vya lazima na kutupeleka kwa watu kujibu hoja kwa vitendo kwani malezi ya awamu zilizotangulia yalitumiwa visivyo kwa kuitisha utitiri wa vikao, semina na kulipana posho nono na sherehe ili kuzungumzia mambo yenye majawabu yaliyo wazi.

Tena huyu anatufanya tutembee kifua mbele na kuzidi kujiamini, ndiyo maana sisi Wakristo tunaangalia katika Kitabu cha Ezra 10:4 ambacho kinasimulia jinsi Ezra alivyotumia muda mrefu madhabahuni akiomba na kuomboleza juu ya ugumu wa maisha, ugumu wa mioyo ya watu, nchi inavyoangamia, ndipo akatokea mtu wa Mungu kumwambia Ezra, “Inuka, ukatende, kazi hii inakuhusu wewe, na sisi tupo pamoja nawe” Ezra akaamka akavaa mavazi ya mapambano, ujenzi wa Yerusalemu ukaendelea kwa kasi na hiyo.

Swali: Uliwahi kuhudumu katika serikali ya awamu ya kwanza ambayo iliweka misingi ya taifa, je unadhani serikali hii inaifuata misingi hiyo?

Jibu: Ndiyo. Serikali ya awamu ya tano inafuata kwa karibu zaidi misingi iliyowekwa na Mwalimu Nyerere, na kielelezo kikubwa ni kule kurejea mara kwa mara kwa maamuzi makubwa yaliyofanywa na Chama tawala na Serikali yake kama Uhuru na Umoja, Muungano wa Jamhuri yetu, Azimio la Arusha, Elimu ya Kujitegemea na afya bora kwa wote. Mshikamano ndani na nje ya nchi yetu haya yote naona amefafanua katika miradi mikubwa inayofanyika kwani inalenga kupambana na maadui watatu - umasikini, ujinga na maradhi.

Swali: Rais anahimiza kubana matumizi lakini watu wanalia kuwa amesababisha maisha magumu, wewe unasemaje?

Jibu: Hakuna ukweli wowote katika madai hayo. Rais anataka kila mtu avune alichokipanda kwa jasho lake na ameziba mianya ya matumizi ya ubadhilifu na kifahari ili kuwekeza katika miradi inayomuinua masikini lakini kauli kama hizo zinaweza kutolewa na wachache waliozoea kuchuma kwa njia za mkato.

Swali: Umekuwa mdau mkubwa wa mazingira, ungetamani afanye nini kwenye mazingira ili unakipigania kifanikiwe?

Jibu: Anayofanya Rais Magufuli yanahusu pia ukombozi wa mazingira yetu. Anafahamu kuwa ukombozi wa mazingira unaanzia na ukombozi wa fikra, hivyo anapambana kuinua mioyo yetu iliyokata tamaa, ikajibatiza majina ya ‘haiwezekani’, anataka tuamini wito wa Baba wa Taifa kwa inawezekana kukomboa mazingira yetu tukitimiza wajibu wetu, na hapa naomba wasaidizi wake wasimame vizuri ili taifa letu lisiwe jangwa.

Shirika letu la Lead Foundation linamuunga mkono Rais Magufuli katika juhudi kukomboa kifikra na kujenga moyo wa kujiamini na kuthubutu ili kurudisha uoto wa asili wa taifa baada ya kuona wakulima na wafugaji wamekata tamaa kuikomboa ardhi ya mashamba na malisho yao, badala yake wanakimbilia kwenye misitu na milima iliyohifadhiwa kutafuta riziki kwa familia zao.

Njia pekee ya kunusuru mazingira ni kufuata kilimo misitu ambacho kinaruhusu mtu kulima huku akiwa na miti mingi shambani kwake pamoja na kutunza visiki hai ambavyo hukuza misitu kwa haraka kuliko miti ya kupandwa.

Tanzania ya viwanda lazima inahitaji mazingira yaliyokombolewa yatakayowawezesha wakulima na wafugaji kutoa mchango wao kikamilifu.

Swali: Kama utakutana na Rais Magufuli leo una lipi la kumshauri kwa maslahi ya nchi?

Jibu: Nina hamu kubwa ya kukutana na Rais, kwanza kumpongeza na kumshukuru kwa maajabu anayoyafanya, pili, kusema machache yaliyo moyoni mwangu hasa katika miaka hii minne ya utawala wake.

Swali: Yapi hayo yaliyo moyoni mwako?

Jibu: Nitamshauri vitu viwili, kwanza awaambukize viongozi na watendaji wa halmashauri za wilaya, kata na vijiji ukali alio ili nao wadhibiti uharibifu wa mazingira, na kutusaidia katika maendeleo ya kweli kikubwa tujiwekee misitu kwa faida ya vizazi vijavyo.

Anasema angemwambia Rais Magufuli awe tayari kuitika wito wa Mungu na Watanzania kuiongoza nchi kwa kipindi kingine cha miaka mitano kwa kuwa anaamini katika miaka 10 nchi itakuwa mahali pazuri.

Dk Chiwanga anasifia miradi mikubwa ambayo inajengwa na ambayo yalikuwa ni migumu kutekelezwa na kutoa elimu ya msingi bure kwa wote, kujenga mradi wa umeme wa Stigler’s Gorge, barabara za lami na ujenzi wa zahanati na vituo vya afya.
 

Attachments

  • pic+askofu.jpg
    pic+askofu.jpg
    19.2 KB · Views: 2
Askofu chimwaga tunashukuru Baba kwa kuendelea kumwombea Rais wetu mpendwa Magufuli

Nyie ndio nembo ya Amani

Viongozi waongeze ukali ili maendeleo yafanyike
 
Sina hakika kama wapo wataothubutu kukuvunjia heshima!.

Imekua ni ada yeyote ajaye na hoja za kukubaliana na Mhe. Dr. Magufuli katika maono yake, huishia kushushiwa hadhi, kuzodolewa na hata kutukanwa.

Umenena vyema Mzee wetu
 
Kwahiyo siruhusiwi kukomenti nimeandika jambo gani baya au kuna tusi lolote hapo mnafuta tu komenti zangu, nauliza wakati watu wanatekwa, wanauawa, wanafungwa kwenye viroba, wanapotea, demokrasia na haki za binadamu zinavunjwa askofu alikuwa wapi? Au ndio walioandaliwa kushawishi upinzani kurejea kwenye uchaguzi, kashindwa tu kuichomeka hiyo ajenda.
 
Alipata pia kuwa waziri wa elimu. Kipindi kile kila mtu alikuwa ccm. Alipata pia kuwa Mbunge na waziri wa elimu. Cheti changu cha form 4 kina sahihi yake; sikumbuki wakati huo alikuwa na wadhifa gani.
 
Mwacheni Askofu wetu apumzike jamani. Huyu alishajitoa kwenye active politics zamani! Huyu sio Kakobe.
 
Astaafu kwa amani. Katika umri huo hana tena connection na jamii. Ndiyo maana anaamini Jiwe ni mkali na siyo dikteta. Udikteta ni laana kwa nchi yoyote ya kidemokrasia.
 
du tunakokwenda kunazidi kuwa giza kuliko tulikotoka ,badala ya kumwambia our no 1 atuongoze kwa mujibu wa kikatiba yeye pamoja na uaskofu wake anaongelea ukali ,na huku akielewa kuwa ukali unaandamana na lugha za kikali,ukandamizaji ,kutokua huru kutoa maoni etc etc,duuu ninamshukuru mno baba yangu (RIP) aliyenilea kwa upendo sio ukali na mimi ninailea familia yangu kwa upendo sio ukali.
 
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom