Suley2019
JF-Expert Member
- Oct 7, 2019
- 1,815
- 4,563
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Kaskazini imetangaza kibano kwa mafundi wa vifaa vya kielektroniki zikiwamo simu za mkononi kwamba wale wasiosajiliwa hawataruhusiwa kufanya kazi hiyo.
TCRA imesema kibano hicho kitaanza Julai, mwaka huu, na kwamba hakuna fundi ambaye atafanya kazi kama hajasomea wala kusajiliwa hivyo ni muhimu kujiunga kwenye kikundi ili kupatiwa elimu.
Mwanasheria wa TCRA, Kant Mosha, alisema hayo juzi katika mkutano wa mafundi wa vifaa vya kielektroniki uliofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Arusha.
Mushi aliwataka mafundi hao kuwa na usajili wa kikundi na hilo ndilo suluhisho.
Alisema mafundi simu ni kada ambayo ilikuwa imesahauliwa lakini kuanzia sasa, serikali imeamua kuwatambua, hivyo kuungana ni sehemu ya kufanikiwa kwa malengo yao.
Mwenyekiti wa Chama cha Mafundi Simu Kanda ya Ziwa, Maguwa Manyanda, aliwataka kutambua kwamba mafundi simu ni wa thamani kwa kuwa jamii inawategemea na wanachangia mapato ya serikali.
Kutokana na hali hiyo, alisema ni muhimu kuona umoja ndio suluhisho la changamoto zao.
Alisema mafunzo hayo yataondoa changamoto na kuwafanya kuwa huru katika shughuli zao za kila siku, hivyo umoja ni nguzo ya kuwafikisha kushirikiana na serikali katika masuala mbalimbali vikiwamo vyombo vya dola.
Manyanda alisema ili kila moja atende kazi zake ni muhimu akajiunga na umoja ili kuondoa changamoto zao ambazo zimekuwa
zikiwafanya kukumbana na misukosuko kutoka polisi.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Mafundi Simu Kanda ya Kaskazini, Nasri Mtengeti, alisema wamefurahi kupata elimu hiyo ya umoja ambayo itawasaidia kuondokana na changamoto mbalimbali.
Awali, akitoa mafunzo kwenye mkutano huo, Mratibu wa Vikundi hivyo kutoka TCRA, Mhandisi Kadaya Buluhye, aliwataka mafundi hao kufanya kazi kwenye umoja kwa lengo la kupata elimu na usajili.
Alisema Jeshi la Polisi linafanya kazi ya kulinda usalama na mali za raia, lakini umoja wao utasaidia kufanya kazi kwa karibu na jeshi hilo na kuondoa changamoto ambazo wamekuwa wakikumbana nazo kama mafundi.
IPP Media