Watu sita akiwemo dereva wa gari wamepoteza maisha na wengine wanne kujeruhiwa vibaya baada ya magari mawili kugongana uso kwa uso katika ajali iliyotokea wilayani Monduli, Mkoani Arusha .
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoani hapa ,Justini Masejo tukio hilo lilitokea Jana majira ya Saa nne usiku katika kijiji cha Alikatani,wilayani humo.
Kamanda alisema kuwa ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Toyota Noar lenye namba T 186 DFY ambalo liligongana uso kwa uso na Lori aina ya Scania namba T 250 CA .
Alifafanua kwamba gari aina ya Scania lilikuwa likitokea Eneo la Makuyuni Kuelekea jijini Arusha huku gari aina ya Noar likitokea Arusha mjini na kuelekea Wilayani Karatu likiwa limebeba abiria.
Kamanda alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo bado haijajulikana Ila wapo katika hatua za uchunguzi wa tukio.
"Taarifa za awali zinaonesha kuwa dereva wa Lori ambaye anashikiliwa na Polisi alihama ghafla kutoka upande wake na kwenda upande wa pili na kukutana na gari aina ya Noar" alisema.
Alisema kuwa miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha maiti katika hospitali ya Mkoa Mount Meru na majeruhi wanapatiwa matibabu katika hospital ya jeshi iliyopo wilayani humo.
Kamanda Masejo alitoa rai kwa madereva wa magari kuwa makini wanapokuwa wakiendesha vyombo vya moto ikiwemo kuzingatia kanuni za usalama barabarani.