"KUZUNGUKA huku na huko kwa CCM ni kutuiga sisi. Tumeanza muda mrefu baada tu ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 tumekuwa tukizunguka na kuwaleza wananchi mambo mbalimbali", ndivyo anavyosema Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa!
Anaongeza kwa kusema kuwa "Chadema ni mwalimu" na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kama mwanafunzi na ndiyo maana siku zote inafuata nyayo kwa mambo yanayofanywa na chama chake hicho. Alikuwa akizungumza na gazeti moja la kila siku nchini kufuatia ziara iliyofanywa na Katibu Mkuu wa CCM, Kanali Abdulrahman Kinana katika mikoa minne ya Mtwara, Rukwa, Geita na Arusha hivi karibuni.
Siku chache baadaye, Dk. Slaa naye alifanya ziara yake katika majimbo matatu ya Temeke, Kigamboni na Kinondoni jijini Dar es Salaam na kukumbana na hali ngumu kuliko wakati wote uliopita.
Tatizo hilo liliambatana na ‘kudoda' kwa harambee ya kuchangia kile kinachoitwa kuwa ni Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) iliyofanyika jijini Mwanza, na kukitia chama hicho hasara ya shilingi milioni tisa.
Wakati hayo yakiendelea, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM wa Idara ya Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye aliibua tuhuma kwa Dk. Slaa kuwa ingawa alikuwa mstari wa mbele akiwashambulia viongozi wenzake wilayani Temeke akidai ni mamluki wa CCM, yeye mwenyewe bado anamiliki kadi ya chama hicho kinachotawala na anailipia ada, jambo alilosema ni kweli kwamba anayo na ataendelea kuitunza kwa makini yake yote, mapenzi yake yote na uaminifu wake wote!
Alisema kadi hiyo ni mali yake, hivyo ataitunza katika maisha yake yote ili wajukuu zake pia waje waione na kuwaachia usia wa kuwa CCM ni chama alichokitumikia kwa moyo wake wote, akakihama kwa shinikizo litokanalo na uchu wa madaraka, lakini akaendelea kuwa mwanachama mwaminifu kwake hata kama alifanya hivyo kwa siri mpaka majuzi alipokuja kuumbuliwa na Nape na kukiri kuwa ni kweli.
Tayari hali hiyo imeibua mtafaruku katika chama chake ambapo kuna wanachama, viongozi na wafuasi wake hivi sasa hawana tena imani naye yoyote na kuanza kumtilia wasiwasi kwa kusema kwamba inawezekana pia ndiye anavujisha siri nyingi za Chadema kwa CCM.
Wanadai kwamba hata siasa zake za vurugu, uchochezi na uvunjaji wa sheria kwa makusudi unalenga kuifanya Chadema ichukiwe na wananchi. Anataka ionekane kwamba kuendesha harakati zinazolenga kuhamasisha pamoja na kukumbatia umwagaji wa damu, mkakati wa chini kwa chini unaofanyika kwa kivuli cha M4C ili wenye akili kidogo wasijue chochote.
Nashukuru kwamba hatimaye wananchi wameanza kukiogopa chama hicho na siasa zake za kiharakati zinazofanywa zaidi na Dk. Slaa. Wameanza kukitenga wakiwemo viongozi wake muhimu kama wenyeviti na makatibu wa wilaya pamoja na mikoa, madiwani na kadhalika.
Katika hesabu kwa mfano yumo aliyekuwa Katibu wa Chadema wa Mkoa wa Morogoro, Abel Luanda; aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema wa Wilaya ya Morogoro, Rajabu Ali, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema wa Wilaya ya Iramba, Mkumbo, waliokuwa madiwani wa Arusha ambao ni Rehema Mohammed (Viti Maalum), Frank Takachi (Kata ya Olasiti), Simba Salum (kata ya Kati) na viongozi wengine wengi.
Akihutubia mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, Rehema aliweka wazi kwamba Chadema imegeuzwa kuwa sawa na kampuni binafsi ya Dk. Slaa, hivyo anaweza kufanya lolote, wakati wowote na mahali popote ili mradi anakidhi matakwa yake mwenyewe kwa kutumia kisingizio chochote.
Amekuwa akitimua viongozi na kuweka wengine kadri anavyojisikia yeye kwa kuwatuhumu kuwa ni mamluki wa CCM, vinginevyo huwatwisha lawama kwamba wanakwenda kinyume cha Katiba ya Chadema ambayo hata hivyo kamwe haipo matawini, majimboni, wilayani na mikoani isipokuwa kwake mwenyewe jijini Dar es Salaam.
Ndiyo maana alikwenda akavuruga uteuzi wa mgombea nafasi ya Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza kwa kuwapelekea mgombea ambaye alimteua yeye jijini Dar es Salaam. Aligoma kumtambua diwani wa chama hicho chenyewe ambaye aligombea kwa njia zote halali, akashinda kura za maoni za ndani na kudai alishavuliwa uanachama na kung'ang'ania matakwa yake.
Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Ndago wilayani Iramba hivi karibuni, Mkumbo alisema ameamua kuacha uenyekiti wa wilaya wa Chadema na kuingia CCM ili apone moyo wake kuliko kuendelea kunyanyaswa kisiasa na viongozi wake wakuu.
Alisema hawezi kamwe kuendelea kuwa mwanachama na hata kiongozi wa Chadema katika ngazi yoyote "kwa sababu ni chama kilichojaa majungu, fitina na chuki nyingi".
Madai hayo yanafanana kwa kiwango kikubwa na yale yaliyotolewa na aliyekuwa Katibu wa Chadema wa Mkoa wa Morogoro, Abel Luanda aliyezungumza katika mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika kwenye Uwanja wa Mashujaa mjini humo, kwa niaba ya wanachama na viongozi wenzake na kubainisha:
"Ndani ya Chadema tuliingia kwa bahati mbaya tu. Ilikuwa ni kama uko barabarani unasubiri gari na linalotokea unapanda, lakini ukishakuwa ndani unagundua kuwa ni mkweche na kushuka ili usbiri jingine. Tumeshuka na tumepanda gari la kweli linaloitwa CCM.
"Nilishikilia chama mkoani na wilayani, nawahakikishia kwamba hakuna cha maana kinachoendelea kule. Ndani ya Chadema hakuna sera za kumkomboa mlalahoi, badala yake kuna udikteta tu unaofanywa na viongozi wa ngazi za juu".
Kuanza kusambaratika kwa kasi kiasi hicho kwa Chadema kulithibitika waziwazi wakati wa ziara ya siku tatu ya Dk. Slaa wilayani Temeke na Kinondoni jijini Dar es Salaam. Alikuwa akiwashutumu viongozi wenzake kuwa ni mamluki wa CCM eti kwa sababu tu mahudhurio aliyokuwa akiyakuta huko ni hafifu sana.
Mathalani, Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema wa Jimbo la Kinondoni walimsotesha ukumbini akiwasubiri tangu saa 4.00 asubuhi hadi saa 6.47 mchana aliposhindwa kuvumilia, akaona afungue kikao chake hicho na kuongea na hao wachache waliofika baada ya wao pia kubembelezwa sana kwa kupigiwa simu zao za mikononi.
Badala ya wajumbe 130 waliotakiwa kuhudhuria kikao hicho ili kujua nini wanaambiwa na bosi wao huyo, wale waliokuwa tayari wamefika hadi wakati huo walikuwa ni chini ya 50 tu huku wakionekana kutokuwa tayari kumsikiliza kwa muda mrefu isipokuwa vinginevyo.
"Chadema ni chama ambacho kinajiandaa kushika dola mwaka 2015, endapo hali hii ya wajumbe kutafutana kwa simu itaendelea ni hatari wakati wa kuunda Baraza la Mawaziri", alisema na kuendelea: "Haiwezekani Rais aje kutafuta Baraza la Mawaziri kwa njia hiyo. Bila kujipanga wakati huu (hakika hali) itakuwa ngumu huko mbele tunakokwenda".
Simshangai Dk. Slaa kuwa na roho ngumu kama ya paka kwa kuendelea kufikiria ndoto ya kushinda uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2015 huku chama chake kikisambaratika kila mahali. Kiongozi anayefikiri kwa akili timamu kichwani mwake hakika asingeweza kabisa kuzungumzia suala hilo isipokuwa vinginevyo.
Kama viongozi waliowekwa madarakani ili kukiongoza chama hicho na kuwa kiungo kati ya wanachama, wapiga kura na uongozi wa juu nao tayari wanaonyesha kuwa mioyo yao haipo nacho tena, nani ataendelea kukiunga mkono na ili iweje?
Nimekuwa nawaambia rafiki zangu kuwa tokea mfumo huu wa vyama vingi vya siasa nchini ulipoanza tena mwaka 1992 kama inavyosema Ibara ya 3(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakuna mpinzani hata mmoja aliyewahi kuwa ‘lulu' kwa wafuasi wake kama aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha NCCR – Mageuzi, Augustine Mrema.
Alikuwa kimbilio la wengi na kuungwa mkono kila mahali mijini na vijijini. Aliteka hisia za kina mama na vijana, matajiri na masikini, wasomi na watu waliosoma katika viwango vya kawaida na kadhalika.
Ndiyo maana gari lake akimaliza kuhutubia mikutano ya hadhara hasa mijini kama Dar es Salaam lilikuwa likisukumwa na mamia ya vijana, tena kwa hiari na matakwa yao wenyewe hata kwa zaidi ya saa nzima mpaka wanapokuja kusambaratishwa na polisi waliofanya hivyo ili kumlinda dhidi ya vibaka, wezi na waporaji wengine linapoanza giza.
Lakini baada ya kutamba kwa miaka minne mfululizo akiwa katika hali hiyo kuanzia mwaka 1995 – 1999, Mrema aligunduliwa kuwa ni ‘msanii', muongo, mzushi, mchochezi na mtu anayependa zaidi kusifiwa binafsi na kutumia kila aina ya ujanja wa kisiasa kuwadanganya wafuasi wake.
Hapo ndipo umaarufu wake wote uliposambaratika kama kishada kilichokwenda harijojo na kubaki na kikundi kidogo cha watu waliokuwa na maslahi naye wenyewe. Hao wanaendelea kumuunga mkono hadi leo na wengine kati yao wapo radhi na tayari hata kumfia utadhani kupe linavyong'ang'ania kwenye ngozi ya mnyama hususan ng'ombe, mbuzi ama kondoo bila kuiachia hata kama tayari ameshakufa!
Hivyo ndivyo wanavyofanya wafuasi wa Chadema wakiwemo baadhi ya wasomi, ngumbaru na kadhalika. Wengine wamejitokeza mstari wa mbele kuthibitisha umahiri wao wa kuitetea kwa uongo, uzushi na majungu.
Wanafanya hivyo kwa kuelewa matumaini ‘hewa' wanayolishwa na viongozi mbalimbali wa Chadema hususan Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa ambaye amethibitisha kuwa ana uwezo mkubwa wa ghiliba, uzushi na kufanya kila aina ya siasa za ‘kisanii' na ‘chafu'.
Amejitokeza kuwa mstari wa mbele kusingizia chochote, wakati wowote na mahali popote ili mradi anakidhi matakwa yake ya kutafuta umaarufu kwa njia zote anazozijua mwenyewe, mtu ambaye siku zote amekuwa akiishi kwa kutegemea majungu, umbeya na uzandiki kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), serikali na viongozi wake wakuu.
Amekuwa tanuru la kupikia uongo, uzushi, fitina na kutengenezea kila aina ya hasira na chuki kwa wananchi, lakini anafanya hivyo siyo kwa ajili ya maslahi ya nchi yake, watu wake wala chama chake ila yake mwenyewe kwa ajili ya tumbo lake na matamanio yake mengine.
Tayari hali imekuwa kinyume baada ya miaka miwili tu ya wanachama, viongozi na wafuasi wa Chadema kukiamini chama hicho kwa mkumbo na kudanganywa na hivyo wengi wao wameanza kukiasi.
Mbali na viongozi waandamizi waliokihama katika mikoa ya Arusha, Singida na Morogoro, mgogoro mzito unaofukuta katika Makao Makuu ya Chadema jijini Dar es Salaam kati ya Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe dhidi ya Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), Zitto Kabwe ni miongoni mwa majanga yanayofukuta chini kwa chini.
Kana kwamba haitoshi, mgogoro mwingine uliopo ni kati ya Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana (Bavicha), John Heche dhidi ya Afisa wa Kurugenzi ya Sera na Utafiti, Mwita Waitara na Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Juliana Sonza.
Tayari pia mgogoro huo umeanza kuenea nchi nzima ambapo kwa mfano, Katibu wa Chadema wa Mkoa wa Mbeya, Eddo Mwamalala, uongozi wa Bavicha wa Mkoa wa Mwanza mbali na sehemu nyingine, wanamtaka Dk. Slaa ajiuzulu kwa madai kuwa anakivuruga chama hicho.
Ndiyo maana sasa amechanganyikiwa kiasi cha kupayuka bila mpangilio wowote mdomoni ikiwemo kudai eti CCM inapofanya ziara zake inakuwa inaiiga Chadema, jambo ambalo hata mwendawazimu wa akili hawezi kulitangaza.
Haiwezekani kwa namna zote kuwa viongozi wa CCM ambayo ilianzishwa mwaka 1977 wawe hawajafanya kabisa ziara hadi walipoiga Chadema wiki tatu zilizopita!
Ndiyo maana Dk. Slaa sasa amechanganyikiwa baada ya kuanza kususiwa mikutanoni na viongozi wake, wanachama wake na wafuasi wake huku wengine wakisema wamechoshwa na udikteta, kuburuzwa kusikoisha na siasa za kitapeli anazofanya yeye na viongozi wengine wa kitaifa.
Katika hali hiyo na hata vinginevyo ndiyo maana wameanza kukikimbia chama hicho huku wakisema waziwazi kuwa kinasambaratika, na kwamba miaka miwili iliyotumika kwa kuwajaza fitina, uzushi, uongo na kila aina ya ghiliba tokea kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 imetosha, na sasa ‘arobaini' ya Chadema hatimaye imewadia!