Anza kujisomea riwaya ya "Majeruhi wa Mapenzi"....

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,460
39,928
282656_10151010983876156_1914957068_n.jpg

Sasa kinapatikana kwenye Amazon.com na kwenye Kindle tafuta "Mwanakijiji"
Kitapatikana Tanzania wakati wowote kuanzia sasa....


1






KWA WIKI nzima Erica Tossi hakutoka chumbani kwake isipokuwa kama ilikuwa kwenda bafuni au kwenda jikoni kuchukua chochote alichojisikia kula – zaidi kikiwa ni matunda na maji. Alikuwa hana hamu sana ya kula wala hamu ya kumuona mtu mwingine yeyote pale nyumbani. Kwa siku tatu za kwanza hakula kitu chochote kabisa zaidi ya maji; na siku zilizofuatia alikula kidogo sana kwa ajili ya kuwa hai tu na si kwa ajili ya kufurahia chakula. Hakukuwa na mtu yeyote pale nyumbani aliyeweza kumfajiri kwa namna yoyote ile. Upweke na maumivu ya moyo aliyokuwa nayo hayakuweza kutulizwa kwa maneno yoyote ya faraja kutoka kwa mama yake wala kwa baba yake.
Uso wake ulikuwa umevimba kwa machozi, nywele zilikaa bila kuchanwa wala kutengenezwa kwa namna yoyote ile kwa karibu wiki nzima. Alikuwa kwa kila kipimo katika hali mbaya sana ya kihisia na kifikra. Erica alikuwa ameumizwa, alikuwa amegeuka kile ambacho kwa


miaka yake yote ya usichana alikuwa akikihofia kwani alishakiona kwa wengine - yaani majeruhi wa mapenzi.
Wazazi wake na ndugu zake walimsihi na kumbembeleza ayaache yote yale yaliyomsibu kwani yote ni "mapenzi ya Mungu" na kuwa kila jambo huwa linatokea kwa sababu yake. Erica hakutaka kumsikia yeyote kati yao japo aliwaheshimu sana. Mama na baba yake walijaribu siku ile ya kwanza kumbembeleza na kumliwaza bila mafanikio. Unyonge wa Erica kwa wiki ile nzima ulikuwa ni mzigo mkubwa kwa kila mtu ndani ya nyumba.
"Erica mwanangu haya yote ni masahibu ya maisha" katikati ya majonzi ya mwanae siku ile ya kwanza tu walipojua kilichotokea mama Tossi alimwambia bintiye kwa upole akiwa ameushika mkono wa kushoto wa bintiye akiupapasa kwa kumbembeleza.
Erica hakuwa na kitu cha kusema zaidi ya kuendelea kunung'unika, machozi yakimchuruzika. Mama alijaribu kumsemesha lakini kwa kadiri alivyokuwa akimsemesha ndivyo Erica alivyozidi kushikwa na uchungu. Mama ilibidi amuache kwa muda. Usiku ule Erica hakulala kabisa. Hata kelele za watu waliokuwa wamekuja kuondoa mahema pale nyumbani hakuzisikia. Alikuwa katika dimbwi la upweke, kwenye shimo la uchungu.
Husna - rafiki mpenzi wa Erica - alilala pale pale nyumbani huku akijaribu kumpa kampani Erica pale chumbani lakini Erica hata hivyo alimsihi atoke kwani kuwepo kwake mle kulikuwa kunamuongezea uchungu. Husna hata hivyo alijua wajibu wake kama rafiki. Hakutaka kumwacha Erica mpweke. Alijaribu kumletea chakula, maji na fanta.
Erica hakutaka chakula chochote isipokuwa maji tu. Husna aliondoka jioni ya siku ya pili akiwa mwenye huzuni na mnyonge kwenda kwake akiahidi kurudi kesho yake. Hata aliporudi hakuwa na mengi ya kusema zaidi ya kukaa na rafiki yake bila maneno yoyote na kukubali kutumwa huku na kule. Alimsaidia kumchukulia nguo na hata kwenda kumfulia nyingine. Kama ilikuwa ni ugonjwa basi Erica alikuwa hoi bin taabani. Husna hakuwa tayari kumuacha rafiki yake. Alijaribu kumtania ili kumchekesha bila mafanikio. Kila alipojaribu kudokeza kuhusu kile kilichotokea, Erica machozi yalianza kumtiririka. Husna aliamua kuiacha mada hiyo.
Jumamosi ilipofika ikiwa wiki nzima tangu tukio litokee siku ile ya send off, Erica ndio alizidiwa na majonzi na simanzi. Ilikuwa ni Jumamosi hiyo ndio ingekuwa siku yake kuu ya furaha; Jumamosi ile ilikuwa ndio iwe siku ya harusi yake kwa nyonda'ake, mahabuba wa moyo wake, yaani pete ya chanda chake. Lakini haikuwa hivyo. Ilikuwa ni Jumamosi ambayo alitamani ingefutwa katika historia ya siku za dunia. Ilikuwa ni Jumamosi ambayo aliisubiria ije na kupita iondoke na kusahauliwa katika kumbukumbu za vizazi.
Hata hivyo, haikuwa hivyo. Kwa kadri siku ilivyokwenda ndivyo unyonge ulivyozidi kumnyong'onyeza. Husna alijua ugumu wa siku hiyo hivyo hakutaka kumuacha rafiki yake. Erica alijaribu kumpigia kelele na kumtaka aondoke amwache peke yake; Husna hakutoka. "Leave me alone
Husna" wakati mmoja Erica alimkaripia Husna. "I'm not leaving you alone Erica, I won't leave you alone. I don't care if you scream hadi
mapafu yakupasuke!" Husna naye alimjibu. Machozi ya uchungu yaliwatiririka wote wawili taratibu kama mifereji ya maji kwenye mashavu yao; mmoja akiwa ameumizwa na mapenzi na mwingine ameumizwa na maumivu ya rafiki yake mpenzi. Husna alijua pasi ya shaka kuwa tukio lile lilikuwa linaupitisha urafiki wao kwenye tanuru ya moto. Hata hivyo, alikuwa na uhakika kuwa hakuwa tayari kumuacha rafiki yake siku ile.
Katikati ya wiki ile Erica alipomfokea Husna pasi ya sababu yeye Husna alikaa kimya lakini Jumamosi ile Husna hakuwa tayari kumuacha. Wazazi wa Erica walimuomba mapema Husna asimuache binti yao siku ile kwani ndio siku ngumu zaidi kuipitia. Wazazi na ndugu wengine walisikia majibizano ya Husna na Erica kule chumbani juu lakini hawakutaka kuingilia; waliombea tu mambo yaishe salama. Erica alijikuta amekubali uhalisia kuwa Husna hatoki mle ndani na ndani ya moyo wa moyo wake alishukuru rafiki yake hakumuacha peke na mpweke. Husna alikuwa ameshika kitabu cha simulizi la "Kamanda" kilichokuwa kimetoka wiki ile kutoka kwa mmoja wa watunzi maarufu wanaochipukia nchini. Husna alikuwa amekishika tu kukisoma kwa kweli alikuwa hakisomi. Erica naye alikuwa amejilaza kitandani pembeni ya Husna akiwa katika dimbwi la mawazo.
Kwa kadiri dakika zilivyopita ndivyo Erica alijikuta akipatwa na simanzi kuliko awali. Ndani yake alikuwa kama chupa iliyokuwa ikijaa taratibu na kila ilipofurika alimwaga machozi na kuanza tena kujaza
uchungu. Alianza kurudi kuanzia tukio lilivyotokea na kujaribu kujibu maswlai mbalimbali ya ilikuwaje afike alipofika na kwanini hakuweza kuepuka pale alipofikia. Moyoni alijilaumu na kujilaani kwani alipoanza kujumlisha vitu mbalimbali aliweza kuona dalili kuwa mchumba wake alikuwa na mambo mengine zaidi ya mapenzi kwake.
Alianza kufikiria kwanini ukweli uje kujitokeza siku ya kumuaga? Kwanini Sam asingeumbuliwa kabla ya siku ile muhimu, yaani siku moja tu kabla ya harusi yao ambayo ilikuwa inasubiriwa kwa hamu na familia zao, jamaa na marafiki? Kila alivyojaribu kutafuta jibu la kumridhisha alijikuta ananyong'onyea kwani hakukuwa na jibu rahisi ambalo lingemtuliza.
Alikuwa amelala kwenye kitanda chake kikubwa cha mbao nyeusi inayong'ara kilichokuwa kimewekwa godoro maridadi kutoka kampuni ya Quality Foam. Juu ya kitanda hicho kulikuwa na mito minne ya rangi nyeusi na nyeupe rangi zake zikipishana katika mtindo wa pembetatu sawa. Kitanda chenyewe kilifunikwa kwa mashuka meupe na juu yake kulikuwa na blanketi jepesi la rangi nyeupe lenye madodoa kama ya chui hivi. Kitanda kilikuwa kimewekwa upande wa katikati kabisa ya chumba huku kwenye kingo zake za kwenye upande wa kichwa zikiwa zimesimamiwa na vinara vya taa za umeme. Upande wa kulia wa kitanda mahali ambako kulikuwa na nafasi ya kutosha kulikuwa na kochi moja lililochirizwa mishono ya maua ya rangi nyeusi na nyeupe likiwa limeelekea upande wa miguu wa kitanda. Husna alikuwa amekaa kwenye



kochi hilo. Mbele ya kochi hilo kulikuwa na zuria dogo la Kituruki ambalo lilikuwa limefunika sakafu ya mbao iliyonakshiwa vyema.
Zuria lenyewe lilikuwa la rangi nyeupe ya sufu huku huku limechirizwa picha ya tausi aliyechanua mkia wake. Kwenye ukingo mmoja wa zuria hilo kulikuwa na meza ndogo iliyokuwa na sanamu ya mnara wa Eiffel wa kule Paris, Ufaransa; mahali pekee nje ya Tanzania ambako Erica alikuwa amewahi kutembelea. Pembeni ya sanamu ile ndogo ya mnara wa Eiffel kulikuwa na kibakuli cha mapambo ambacho ndani yake kiliwekwa magamba ya konokono wa baharini na maua machache.
Erica alikuwa amelala kifudifudi. Siku ya nane ya machungu ilikuwa inaelekea ukingoni na kwa mara nyingine tena alikataa wito wa baba yake wa yeye na Husna kwenda kukaa na wenzao sebuleni. Na kwa hakika hata hakuchangamkia jaribio la mdogo wake wa mwisho wa kiume Ray ambaye naye kunyong'onyea kwake kulikuwa ni zaidi ya dadake kwani kati ya dada zake wanne, alikuwa karibu zaidi na Erica. Ray alikuwa mtoto wa mwisho wa baba na mama Tossi. Hivyo, tangu tukio lilipotokea wiki moja nyuma Ray alijaribu sana kumbembeleza dada yake aache kulia huku yeye mwenyewe akijikuta analia. Dada zake wengine walikuwa na kazi ya kuwabembeleza hao ndugu wawili hadi mle ndani ikawa ni kugombezana tu. Mwisho katika hali ya kumuumiza mdogo wake kabisa Erica alimpiga marufuku Ray kuja chumbani kwake. Ray alilia sana siku ile na kulalamikia kuwa dada yake "hampendi". Mwisho Mzee Tossi



aliamua kuingilia kati na kuwaambia kuwa wampe nafasi Erica augulie moyo wake, "akiwa tayari atarudi tu" alisema mzee Tossi.
Pamoja na hayo yote mawazo ya Erica hayakuwepo katika nyumba yao ile, wala kwa wazazi wake wala kwa mdogo wake Ray. Mawazo yake yote yalikuwa yamezunguka kwenye neno moja tu – fedheha.
Kwa muda mrefu pale mtaani kwao na hata kwa kwa familia yao kila mtu alikuwa anasubiri kuona Erica ataolewa na nani. Kati ya watoto wote wa kike wa mzee Tossi, ni huyo mtoto wake wa kwanza ambaye alikuwa anaangaliwa kwa macho ya wivu, matumaini na mfano. Wadogo zake wawili wa nyuma walikuwa ni mapepe na yule wa tatu alikuwa bado hajaonesha mwelekeo wake wa maisha kwani ndio alikuwa amevunja ungo tu. Erica alikuwa mtoto wa kwanza, wa pili Eliza, wa tatu Ela, wa nne Elineema. Toka utotoni na hata alipoanza kupevuka Erica alikuwa ni binti ambaye aliyachukulia maisha yake kwa umakini mkubwa na kujiweka kuwa mfano kwa wadogo zake.
Aliamini kabisa kuwa mtoto wa kwanza ni lazima awe ni kama mzazi kwa wadogo zake. Na wazazi wake walimpa hilo jukumu zaidi na kumuamini hata kufanya maamuzi kwa wadogo zake. Alikuwa mkali kwa wale waliomfuatia na alijaribu kuwalinda sana na ulaghai wa wanaume. Alianza mahusiano ya kimapenzi na wavulana akiwa shule ya sekondari lakini ilikuwa kwa siri sana akihofia kuleta kashfa kwa familia yake. Hakujiacha apagawe na mapenzi, mara zote alikuwa anahakikisha kuwa mvulana hampelekeshi ovyo na mambo yalipomzidia



hakuchelewa kujitoa kwenye uhusiano mbovu na kubaki mpweke. Katika mambo ya mapenzi alijiaminisha kuwa ana "control" ya moyo wake.
Kwa kadiri alivyozidi kukomaa ndivyo alivyozidi kuwa makini katika mambo ya mapenzi. Hakuwahi kumleta kijana yoyote pale nyumbani kwao na kumtambulisha kuwa ni rafiki yake wa kiume; marafiki walikuwepo lakini siyo wa kimapenzi. Wengine walikuwa ni marafiki wa familia ambao miaka nenda rudi walikuwa wanaombea siku moja Erica angewaangalia kwa jicho la mapenzi. Lakini yeye mwenyewe macho yake yalikuwa kwenye masomo muda wote alipokuwa shuleni. Hata alipoanza mahusiano ya mapenzi akiwa sekondari ilikuwa ni na kijana mmoja na yalikuwa mapenzi tu ya juu; alivunja ubikira akiwa kidato cha sita na kwa maamuzi yake mwenyewe.
Alipokuwa chuoni alikuwa na mpenzi wa kusoma naye na kutoka naye, hakutaka kuwa na mapenzi mazito sana. Vijana wengi walivutiwa naye sana na wasichana wengine walimuona kama dada yao. Wenyewe walikuwa wakimuita jina la utani la ‘mgumu' kwani alikuwa halainiki kirahisi na maneno matamu ya wanaume. Wakati ulipofika kuwa ameanza kutamani kuwa katika mahusiano ya kudumu familia nzima ilikuwa inasubiria. Hatima ya subira yao ilikuja kama miezi nane nyuma ambapo familia ya kijana Samsom Lugo ilipoleta posa. Ilikuwa ni mwaka mmoja tu baada ya kumaliza Chuo Kikuu.
Mahusiano yake na Sam yalianzia kazini ambapo walikutana kwa nasibu tu. Sam alikuwa amefika siku moja kwenye tawi la Benki la NMB Makao Makuu kuleta fedha za kigeni za mauzo akiwa na walinzi wa kampuni ya SECURITAS ya jijini Dar. Erica alikuwa ni miongoni mwa maafisa watano wa kampuni hiyo ambao walikuwa wamepewa jukumu la kusimamia akaunti za kigeni za makampuni kama kumi hivi, kampuni ya kina Sam ikiwa imeangukia mikononi mwa Erica.
"Naitwa Sam Lugo" Sam alinyosha mkono kujitambulisha rasmi kwa Erica.
"Ah nakufahamu Sam, naitwa Erica Tossi" Erica alisimama kutoka kwenye kiti chake cha rangi nyeusi inayong'ara na kunyosha mkono wake wa kulia kumsalimia. Kucha zake zilikuwa zimenakshiwa kwa rangi nyekundu kali. Ana macho na meno mazuri, Erica alijiambia moyoni. Sam alikuwa amevaa suruali ya kijivu na shati la mikono mirefu la bluu iliyopauka. Alikuwa amekata nywele zake chini kabisa na mashavu yake yakiwa yamepambwa kwa masharafu kama ya mvulana mdogo. Alikuwa na kile ambacho wanakiita ‘babyface'.
Walipomaliza mahesabu na kukabidhiana lundo la fedha na kupeana fomu zote zinazohitajika Sam alimuaga Erica pale ofisini. My God she is gorgeous, Sam alijisemea mawazoni alipopiga hatua ya mwisho tu kutoka kwenye mlango wa ofisi ya Erica. Alimuacha Erica NMB lakini hakumtoa mawazoni mwake. Wiki moja baadaye alirudi na mzigo mwingine na safari hii alikuwa amenuia kabisa kuomba mawasiliano na dada yule. Baada ya kumaliza mahesabu alikuwa tayari kutoka tena huku moyo ukimdunda.
"Samahani dada Erica" alisema na kugeuka nyuma alipokua kwenye kizingiti cha mlango wa ofisi ndogo ya Erica. "Bila ya samahani Sam, nini tena?" Erica aliacha alichokua anafanya na kuinua kichwa chake macho yakimkazia Sam, kifuani; hakutaka kuyaangalia yale macho. Moyo ulimuenda mbio na alijisikia kijoto cha ghafla. Hakuwa tayari kujionesha hivyo.
"Nina swali binafsi Erica naweza kukuuliza?"
"Aah uliza Sam"
"Una mtu unayetoka naye kimapenzi"
"Sam! That's too personal" alisema Erica huku akiangua kicheko cha kivivu. Kwa namna fulani ya kikorofi alipenda uthubutu wa Sam wa kuja moja kwa moja kama dume la ng'ombe lililokata kamba.
"I'm sorry, sikumaanisha kusound nakuhoji maisha yako. Kama hauko comfortable kujibu naelewa. Samahani tena" Sam alionesha unyenyekevu na macho yake yalibeba maumivu ya kukataliwa, aliuma midomo yake ya chini na kugeuka kuanza kuondoka. Madhara yalikuwa yamekwisha fanyika.
"Sam!" Erica alimuita. Sam aligeuka utadhani ameamriwa kutoa heshima kulia.
"Naam"
"Sikusema kwamba sitakujibu" alitulia kidogo, "Hapana sina mtu kwa sasa, niko single" alimjibu Sam kwa maneno yaliyopimwa. Erica aliyaangusha macho yake chini kwa aibu kidogo na kuyarudisha kwa Sam mara moja. Sam nusura aruke juu kwa furaha. Macho yake yalichezacheza kwa kushangilia.



"Nilikuwa naombea iwe hivyo, naweza kukutoa out weekend hii kama hutajali?" Sam alipeleka ombi lake.
"Sam, sidhani kama itakua idea nzuri ila nafurahi wewe kuwa na interests nami" alisema.
"Kwanini haitakuwa wazo zuri Erica" Sam aliuliza. Alikuwa amepata ujasiri wake uliokuwa chupu chupu kupotea.
"Wewe ni mteja wangu, so kutoka pamoja haitakuwa idea nzuri kikazi kutakuwa na mgongano mkubwa wa kimaslahi" alisema Erica kwa staha na heshima kubwa.
"Kwa hiyo kama nisingekuwa mteja wako ungekubali nikutoe?"
"Ndio Sam"
Wiki moja baadaye Erica aliitwa na bosi wake na kuambiwa kuwa akaunti ya Lugo Investments and Holdings ilikuwa imehamishwa kwenda kwa meneja mwingine wa akaunti za kigeni pale NMB. Kesho yake Sam alipokuja hakuingia kabisa ofisini kwa Erica. Erica hakutaka kujipendekeza; alimuona Sam akienda kwenye ofisi ya yule meneja wa akaunti yake lakini alijifanya kama hakumuona. Hata hivyo moyoni aliombea kweli Sam amuombe tena kumtoa out kwani mazingira yalikuwa yamebadilika. Alimuona Sam kupitia dirisha la kioo akiwa amesimama kuaga akiwa amemalizana biashara na yule meneja mwingine. Sam alianza kuondoka bila kuonesha ishara yoyote kuwa bado alikuwa ana nia naye. Alikuwa anapita nje ya ofisi yake, Erica aliteremsha macho yake kwenye kazi iliyokuwa mezani hakutaka kumwangalia.



"So nije kukuchukua saa ngapi?" Sam alisema na kumgutusha Erica. Alikuwa amesimama mlangoni mwa ofisi ya Erica akichungulia ndani.
"Sam. You did it! You evil you!!" Erica alisema kwa kucheka huku akisimama na kumnyoshea kidole.
"Nilikuambia naitwa Sam Lugo, remember?" akiwa mwenye kujiamini Sam alimuuliza kwa kujigamba kidogo.
"Kaka sikuwezi; una majigambo si utani; mmh! nakumbuka, Jumamosi saa moja jioni"
"Asante Erica, hautajuta" Sam alisema na kumpungia mkono huku akiondoka. Tayari alikuwa na namba za mawasiliano na Erica kwenye kadi yake ya biashara ambayo alikabidhiwa. Kukutana kwao hakukuwa kwa bahati mbaya kama Erica alivyodhania; nyuma ya yote hayo alikuwa mzee Lugo mwenyewe ambaye alikuwa ndiye mwenye kuleta biashara zake pale NMB hadi alipomuona Erica na baada ya miezi kadhaa ya kufanya biashara naye alimtambua kama binti ambaye kwa kweli angemfaa kabisa mwanae na hivyo hata uamuzi wa kuanza kumpa Sam mojawapo ya majukumu yake ilikuwa ni katika kumlengesha tu kwa binti yule.
Walipotoka mara ya kwanza ilikuwa ni mwanzo wa mapenzi motomoto; Erica hata hivyo hakumtambulishakwa wazazi wake hadi pale ilipoletwa posa rasmi. Erica alikuwa anamfikiria Sama masaa ishirini na nne. Na kijana wa watu alikuwa akimpeleka mbio mbio kweli. Alijikuta anazama kwenye mapenzi kwa namnba ambayo hakuwahi kabla yake. Pale nyumbani walihisi kuwa amempata mtu kwani alikuwa ameanza tena kuondoka na kuchelewa kurudi au kudai yuko kwa rafiki zake mwishoni mwa juma.
Ray mdogo wake Erica ndiyo alikuwa mtu ambaye pole pole alianza kuingizwa kwenye uhusiano huo kwani wakati wanaanza mahusiano Erica alikuwa na mazoea ya kwenda na Ray alipokuwa kwenye miadi na Sam hadi mambo yalipoanza kupamba moto. Ni Ray aliyewatonya nyumbani juu ya mtu aitwaye Sam. Walikuwa hawajamuona hata hivyo wala kujua jina la ubini wake. Licha ya kumtaka amlete kumtambulisha Erica aliwakatalia hadi atakapokuwa tayari yeye. Hakuwahi kulala kwa Sam. Mambo yao mengine yote walihakikisha yanaisha kabla ya kwenda kulala. Erica hakutaka kuwa mfano mbaya kwa wadogo zake.
Ndivyo mapenzi yao yalivyoanza na kuwakolea. Usiku ule akiwa amejikunyata kitandani akifikiria yote yaliyomsibu na jinsi alivyojaribu kuwa mfano mzuri kwa wadogo zake alijiona duni na kudharaulika. Aliona aibu hata mbele ya wadogo zake. Wadogo zake wale wakike wawili mwanzoni walionesha kumcheka kimoyomoyo lakini siku zilivyopita walianza kweli kumuonea huruma dada yao. Kwa jinsi alivyokuwa akiwafuatilia maisha yao waliona kama amestahili kilichompata. Lakini damu nzito kuliko maji; uchungu wake ukaanza kuwa uchungu wao. Na wao wakapoteza furaha.
Erica alikuwa hana hamu ya maisha kwani kila alivyomfikiria Sam na lile tukio la wiki moja nyuma aliamini kabisa msemo wa wazee kuwa "hujafa hujaumbika" Alikuwa amelala kifudifudi huku amevuta shuka moja tu jepesi na chini ya shuka hilo alikuwa amebakia na kanga mbili na sidiria na nguo ya ndani tu; kanga moja ilimfunga kifuani na nyingine kiunoni. Nywele zilikuwa bado zinaonesha jinsi zilivyokuwa zimetengenezwa siku ile ya sendoff lakini kwa kujigaragaza pale kitandani na jinsi alivyokuwa anazishika shika bila kujali zilikuwa zimefumuka fumuka na kumfanya aonekane kama msichana asiyefundishwa kuwa nywele za mwanamke zinaonesha hali yake ya kihisia. Hata Husna alipombembeleza azichane au amsuke japo mabutu Erica hakutaka kabisa. Hali ya nywele zake ilikuwa ndivyo ilivyo hali ya moyo wake.
Msongo wa mawazo ulimzidia na alijikuta mwili unamtetemeka kama mtu aliyezidiwa na homa ya Malaria. Hakutaka kwenda na kufikiria kilichotokea na kurudi nyuma hadi usiku ule wa sendoff. Lakini kama punda aliyelazimishwa kubeba mzigo asiotaka na kwenda asikochagua Erica alianza kutembea taratibu katika mawazo yake kwenye barabara ya majonzi; kwenye njia ya kumbukumbu zisizokoma. Alijigeuza chali kuangalia dari na kuyafumbua macho yake, mikono yake aliikunja juu ya kifua chake huku vidole vyake akiwa amevikutanisha. Chozi lilimtiririka kwenye jicho la kulia na kutengeneza njia hadi kwenye sikio lake la kulia, hakutikisika wala kujaribu kujipangusa.



2
WIKI MOJA KABLA







USIKU WA kumuaga Erica ulikuwa umeenda vizuri kabisa na kwa kiasi kikubwa ulikuwa unaelekea kuweka historia ya mafanikio. Hakuna aliyekuja ambaye hakula na kusaza na hakuna aliyetaka kunywa ambaye hakunywa hadi kupaliwa. Maandalizi yote yalifanywa vizuri sana na mchanganyiko wa mila na desturi za kabila lake pamoja na vikolombwezo vya kisasa vilifanya sherehe nzima kuwa na utamu wa aina yake. Ukumbi ulipambwa vizuri kwa rangi nyekundu za kumeremeta zikisindikizwa na kijani na nyeupe huku mitungi mikubwa mirefu ya maua ikitengeneza njia kuanzia mlangoni hadi karibu na meza kuu. Mitungi ilikuwa na maua pamoja na miche mikubwa ya miwese ambayo ilifanya ukumbi uwe wa aina yake.



Taa za rangi mbalimbali zilikuwa zimetanda kwenye dari la hema kubwa lililokuwa kwenye viwanja vya familia ya mzee Tossi. Hawakutaka kukodi ukumbi mahali popote kwani walisema kama wanamuaga binti yao basi watamuagia "kwake". Hivyo pale nyumbani palikuwa pamechangamka kwa shughuli mbalimbali za maandalizi ya send off hiyo. Chini palikuwa pametandazwa sakafu maalum ya kuunganisha vipande vipande ya vigae vya plastiki. Upande wa kulia wa hema lile kubwa kulikuwa na meza zilizokuwa zimewekwa mabakuli makubwa ya vyakula mbalimbali yaliyokuwa yamefunikwa huku pembeni yake kukiwa na miko mikubwa ya kupakulia vyakula hivyo.
Meza kuu yenyewe ilikuwa imepambwa kwa rangi nyeupe na nyekundu angavu pamoja na msururu wa maua ya kila aina. Pembeni yake kulikuwa na sehemu iliyotengenezwa kama jukwaa duka ambalo lilikuwa limeinuliwa juu kidogo na mtu angeweza kupafikia kwa kupanda ngazi ndogo mbili kila upande. Juu yake kulikuwa na viti vikubwa viwili ambavyo vilikuwa na rangi nyeupe inayong'ara huku mbele yake kukiwa na meza nzuri ndogo ya rangi nyeusi iliyong'ara vizuri sana.
Juu ya meza hiyo kulikuwa na maua ya rangi mbalimbali yakifunuliwa vizuri zaidi na dazeni mbili za mawaridi ya rangi nyekundu na nyeupe. Kwenye ukuta nyuma ya viti hivyo kulikuwa na kitambaa kikubwa cheupe kilichopambwa kwa taa nyeupe zilizotengeneza umbo la moyo katika mistari midogomidogo iliyotengeneza maumbo ya moyo mkubwa ndani yake maumbo mengine ya moyo hadi mdogo kabisa; mshale wa taa nyekundu ulipita katikati ya moyo ule mdogo wa katikati kwa taa za rangi nyekundu zilizokuwa zinawaka mithili ya mkuki ukiuchoma moyo huo. Ukumbi wa hema lile ulifurika kupita kiasi kwa ndugu, jamaa na marafiki waliokuja kumuona Erica akiagwa.
Utamu wa send off ile ulikatishwa kabla sherehe haijanoga sana majira ya saa tano za usiku. Erica alikuwa ametoka kucheza muziki kidogo na kundi la marafiki zake wa kike waliokuwa wamekuja kumuunga mkono. Mabinti wote walikuwa wamevaa sare za rangi ya bluu bahari iliyosindikizwa na rangi nyeupe angavu. Walikuwa na sare nyingine kwa ajili ya harusi. Wakati huo hotuba mbalimbali za wanafamilia zilikuwa zimekwishatolewa kuwatakia maharusi maisha ya baraka. Zawadi pia zilikuwa zimetolewa kwa bi harusi na kilichokuwa kimebakia ilikuwa ni muziki tu. Shughuli zilikuwa ziendelee hadi majogoo.
"Sam yuko wapi?" Erica alimuuliza rafiki yake kipenzi Husna aliyekuwa naye pembeni.
"Alikuwa anacheza kule" Husna alimuelekeza kwa kichwa tu mahali ambapo dakika chache nyuma yake Sam naye alikuwa na kundi la vijana wenzake wakicheza muziki. Yote hiyo ilikuwa baada ya chakula na hotuba za familia. Walipoangalia tena kundi la vijana walikuwa bado wanacheza isipokuwa Sam.
"Unajua wanatakiwa kwenda kupumzika wawaache wengine waburudike" Mama Tosi alimwambia Husna.
"Ah mama waache wacheze jamani si unajua tena baada ya hapa ndio keshakuwa mke wa fulani" wakacheka wote. Erica na Matron walirudi kuelekea kwenye kiti cha meza kuu wakati Husna akielekea kwenye kundi la wale vijana kumuuliza Kevin, mpambe wa harusi wa Sam alikoenda bwana harusi. Kevin alimwambia Husna kuwa Sam alitoka nje mara moja akiaga kuwa anaenda msalani. Akaangalia saa yake na kutikisa kichwa kidogo. "duh naona imepita karibu dakika kumi na tano ngoja niende kuangalia" Kevin alisema kwa kushangaa kidogo huku miguu yake ikiwa katika hatua za kuelekea nje.
Husna alirudi na kuketi upande wa kushoto wa Erica kwenye ile meza kuu. Matron alikuwa ameketi upande wa kulia. Alimnong'oneza Erica na Matron kuwa Sam alionekana akitoka nje kana kwamba kuna mtu amemuita; akawaambia kuwa Kevin ameenda kumuangalia. Waliendelea kunywa soda na vitafunio vilivyokuwa bado viko mbele yao. Kwa mara karibu ya nne usiku ule mziki wa Carolina ulichezwa tena na kuwapagawisha watu chini ya hema lile. Vikundi vya vijana walikuwa wakicheza kwa kupokezana huku wengine wakioneshana umahiri wao kwa kucheza katikati huku wakiwa makofi na vigelegele na vijana wengine ambao nao walikuwa wanasubiri zamu zao kujimwaga katikati.

TAARIFA ZA kutoweka kwa Sam na Fiona hazikuchelewa kufika mle ndani ambako bado kina mama na familia walikuwa wanapiga soga na kuendelea kuburudika na muziki. Tetesi zilianza kama utani hivi na hazikuchelewa kumfikia Ray ambaye mara moja alikimbia ndani kumuuliza mama yake.
"Mama mama!" aliingia na hata bila kujali mama na shangazi zake wanazungumzia nini aliwashtua kwa sauti yake.
"Nini baba, nini?" mama Erica alishtuka na wengine wote waka kimywa macho yao yakimuangalia Ray aliyekuwa na shauku.
"Mmesikia ati Sam na Fiona wameondoka pamoja na hakuna anayejua walikoenda?" ilikuwa ni habari mpya.
"Una maana gani wameondoka pamoja?" aliuliza shangazi yao mkubwa aliyekuwa amesimama karibu na friji kubwa jeupe.
"Wameondoka" Ilikuwa sauti ya Elineema ambaye naye aliingia humo ndani na kukuta hilo gumzo. Mama Erica na shangazi Tossi walijua kuna tatizo. Kabla hawajaamua la kufanya mzee Tossi mwenyewe alikuja jikoni. Hakusema neno lolote zaidi ya kumuashiria mkewe amfuate na pia akamuita dada yake. Mjomba mkubwa aliyekuwa ametoka kijijini kwa ajili ya shughuli hizo naye akaitwa. Haikuwachukua muda kuweza kujua nini kilikuwa kimetokea. Mambo ya kwanza kuamuliwa kwa haraka ni kwenda kumtoa Erica kiaina kule ukumbini na shangazi alienda na kufanya hivyo; wengine waliokuwa wanacheza muziki bado walikuwa hawajasikia kinachoendelea na walidhani labda Erica ametoka kwenda kujisaidia. Shangazi hakumwambia lolote lakini macho ya watu na hali ya nyuso zao ilimhakikishia kuwa jambo fulani haliko sahihi.
"Mama nini?" aliuliza kwa shauku alipoingia ndani na kulakiwa na wazazi wake.
"Mwanangu, mwanangu" mama Erica alianza kusema.
"Dad is Sam Ok?" alimuuliza baba yake aliyekuwa amesimama pembeni ya mke wake.




"Oh Sam is ok my dear princess" Mzee Tossi alisema huku akinyosha mkono wake kumpokea binti yake. Wazazi wake walimchukua chemba na kumdokeza kilichotokea. Waliokuwa pembeni waliweza kusikia kelele aliyopiga Erica kwa nguvu kama mtu aliyekuwa na maumivu makali. Erica aliangusha kilio kilichokuwa na maneno ya kuuliza ‘why why' huku akikataa kuamini. Lakini baada ya muda hakukuwa na utata wala wasiwasi, Sam na Fiona waliondoka pale na familia ya Fiona nayo iliyokuwepo pale nao waliondoka kimya kimya wakifuatiwa na jamaa na ndugu za Sam.
Haikuchukua muda sherehe nzima ikaharibika na muziki ukidoda na pakageuka kama mahali ambapo kuna ugonjwa au wamepewa taarifa za msiba katikati ya sherehe. Palipooza kupita kiasi. Erica aliingia chumbani kwake machozi yakimtiririka; Husna alihakikisha yuko pembeni yake na mabinti wale wawili walijikuta wanalia kwa pamoja huku Husna akijitahidi kwa kila hali kumbembeleza rafiki yake. Erica hakuamini kilichomkuta na alitamani ardhi ipasuke na immeze na historia imsahau. Swali pekee alilojiuliza muda wote na alimuuliza rafiki yake usiku ule ni amekosea nini kwa Mungu? Hakukuwa na jibu la kutosheleza.



3








KWA WIKI nzima Sam na Fiona walikuwa wamejificha kwenye hoteli ya Njuweni eneo la Kibaha Maili Moja umbali wa kutupa jiwe tu toka kituo cha mabasi cha Kibaha. Walikuwa wanasubiria tiketi zao ziwe tayari. Walijua wasingeweza kukaa Tanzania kwa wakati huo hasa baada ya kasheshe walilokuwa wamelianzisha. Usiku ule wa Send off Fiona aliamua kumwambia Sam kuwa mchezo wao wa mafichoni ulikuwa na matokeo. Fiona alikuwa mja mzito. Mwanzoni Sam alidhani ni utani tu kwa sababu ya wivu wa Fiona. Hivyo, wakati watu wanacheza mziki Fiona alimfuata na kumwambia kuna kitu anataka kumwambia; walitoka na walikuwa wamesimama pembeni ya hema na Fiona ilibidi amwambie ukweli.



"Sam, sijui nifanye nini sikutaka kukuambia" Fiona alianza. "Kuniambia nini Fiona, tulikubaliana hakuna kitu kitabadilika hata nikimuoa Erica" Sam alisema kwa sauti ya kumtia moyo.
"Najua hilo Sam lakini nina jingine linanisumbua"
"Nini Fiona"
"Sam, nina mimba yako" Fiona alisema kwa uhakika huku akionesha macho ya kufuraha na uso wa mashaka.
"Oh My God! Are you serious?" Sam aliuliza katika hali ya kutokuamini na kushtukizwa. Sam alijihisi kuchanganyikiwa. Alianza kutembea tembea huku akisema "dah dah" asijue la kufanya. Fiona alikuwa anabubujikwa na machozi. Sam alimuangalia Fiona na alimfikiria Erica aliyekuwa ndani kwenye hema akifurahia na watu wengine siku ile muhimu. Ilikuwa ni bahati nasibu ya maisha yake na aliamua kuicheza.
Watu waliokuwa pembeni hawakusikia ila walimuona Sam ameshika kichwa kwa dakika chache.
"Niko Serious Sam, nilipata majibu jana na nilidhani ningeweza kunyamazia tu hadi harusi lakini nilijua kabisa kuwa sitaki kushare mapenzi yangu kwako na Erica" alisema Fiona.
"Fiona, tayari tumeshafanya mambo mabaya na hili sasa tutafanyaje? Una uhakika ni ya kwangu?" Sam aliuliza swali ambalo labda hakuwa amelifikiria lilimaanisha nini. Lakini kabla akili hazijakaa sawa alizibuliwa na kibao cha haraka, chepesi lakini kilichodhamiriwa na Fiona. Aliona nyota kadhaa kichwani na kuusikia uchungu hadi kwenye ulimi.



"Una maana gani ni ya kwako?" Fiona alitahamaki. Hisia zikamzidia. "Yaani kweli Sam unafikiria kuwa nilikuwa na mtu mwingine?" bila kujua Fiona alianza kulia kwa kwikwi nyepesi nyepesi. Sam hakutaka watu waone hilo alimvuta mkono Fiona na kuelekea naye kwenye eneo ambalo magari ya wageni yalikuwa yameegeshwa.
"Hapana baby sina maana hiyo, nimechanganyikiwa tu" Sam naye alimbembeleza akiwa amemvuta karibu yake. Chini ya giza kidogo upande ule hakuna aliyewaona.
"Sam huwezi kumuoa Erica, please don't marry her" alisema Fiona. Sam alijua hata kabla ya kuambiwa kuwa mambo hapa yamebadilika. Ni kweli alimpenda Erica lakini dakika ile na saa ile alijua kabisa kuwa mapenzi yake hasa yalikuwa kwa Fiona. Erica alikuwa kwa kila namna mwanammke mzuri lakini Fiona alikuwa na vitu vingine ambavyo Sam peke yake alivijua na vilimvutia. Fiona alikuwa msichana mtundu kweli kwa kila kipimo. Kinyume na alivyoanza na Erica, Sam alianzana na Fiona kama utani wa "mashemeji" hivi. Erica aliwatambulisha marafiki zake Fiona na Husna kwa Sam na wote walimuita Sam shemeji. Fiona hakuwahi kuonesha kuwa alikuwa ana hisia za aina yoyote kwa Sam hadi siku moja walipokutana kwa bahati mbaya katikati ya jiji. Sam aliamua kumpa ofa ya lunch shem wake.

MAZUNGUMZO YAO yalikuwa hayana hatia yoyote hadi sekunde ile kijiko cha Sam kwa bahati mbaya kiliteleza mkononi na kuanguka kwenye mapaja ya Fiona aliyekuwa amevaa sketi fupi iliyokuwa juu kidogo tu ya magoti yake. Sam bila kufikiria alinyosha mkono wake na kujaribu kukichukua kijiko hicho na alipofanya hivyo kwa bahati mbaya akagusa ngozi ya Fiona. Ngozi ilikuwa kama kuku aliyebanikwa vizuri.
"Ah shemeji!" Fiona alisema kwa utani akijilegeza.
"Ah samahani Shemeji" Sam aliacha kukichukua kijiko na kurudisha mkono wake. Lakini madhara yalikuwa yameshafanyika. Ilikuwa ni kama amegusa nyaya za umeme kwani mwili wake uliitikia kwa ghafla. Mawazo ya kila namna chafu yaliporomoka kichwani mwake kama maporomoko ya maji machafu.
"Shemeji, unaweza kugusa bwana, kwani utachukua?" Fiona
"Fiona acha hizo bwana, unataka Erica aniue eh, we kweli hunipendi" Sam alisema huku akijaribu kukunja uso wake kuonesha msisitizo. Moyo hata hivyo ulikuwa ukimdunda.
"Kwani ukinigusa utaweka matangazo?" Erica alimchombeza. Mazungumzo yao yalikosa breki.
"Hapana Shem, wacha niendelee we malizia kula tutaonana nataka nimuwahi Erica akitoka kazini" Sam aliamua kutegeua kitendawili hicho. Fiona nusura acheke alijua kabisa Sam ametegeka hasa alipomuona mkono wake wa kushoto ukiwa mfukoni wakati anainuka. Fiona alisemama na kumpa hug shemeji yake. Alipokuwa katika usawa wa sikio lake, Fiona alinong'ona "Sam, Shemeji nyama ya hamu!" na kabla Sam hajajinasua Fiona aling'ata sikio la Sam kiuchokozi. Alipoliachilia Sam nusura apige kelele "mamaweeee!"
Ndio ulikuwa mwanzo. Kila walipokuwa pamoja wanne, Fiona alijifanya hajali sana na aliendelea kawaida ya kumgusa gusa na kumsukuma Sam. Husna aliwahi kumuasa Fiona aache hivyo lakini Fiona alimwambia tu kuwa anamtania tu wala hana nia yoyote mbaya kwani yeye naye alikuwa na boyfriend wake. Husna alipolalamikia hilo kwa Erica, Erica alimtuliza kuwa Fiona ni Fiona wote walimjua alivyokuwa anapenda utani. Utani ulikuwa utani lakini Fiona kumbe moyoni alikuwa anaugua; alikuwa ameguswa na kufadhaika. Moyoni alikuwa analia machozi kila akimfikiria Sam. Alijaribu kujizuia sana lakini kila usiku alipoenda kulala au hata alipokuwa na huyo boyfriend wake mawazo yake yalikuwa kwa Sam. Jinsi gani angejisikia kama angepewa tunda japo mara moja tu na Sam. Mwili wake ulikuwa unalalamika kwa tamaa na alikuwa hadi anajichukia jinsi alivyokuwa akijisikia mbele ya Sam.
Alijitahidi kujikaza sana lakini kwa kadiri alivyojikatalia ndivyo alivyokuwa anazidisha moto wa tamaa ndani yake. Alikuwa na uhakika kuwa Sam naye alikuwa anamtamani lakini alikuwa mzuri katika kuficha hamu zake. Na Sam alijitahidi kwa kila namna kuondolea hamu zake kwa Erica, lakini wakati mwingine akiwa na Erica katika mapenzi mawazo yake yalikuwa kwa Fiona; jinsi ingekuwa, je alikuwa ni mtundu kiasi gani, je ni kweli shemeji nyama ya hamu tena tamu? Udadisi wake huo ulikuja kumuingiza kwenye mstari wa Fiona.
"Sam, unakuja au hauji?" Fiona alimuuliza Sam kwenye simu siku moja.
"Kuja wapi tena?" Alimuuliza.
"Tuko tunakusubiria hapa kwangu kwa ajili ya mambo yenu ya harusi" Fiona alisema. Ni kweli wamekuwa wakikutana wakati mwingine kwa kina Husna na wakati mwingine kwa Fiona pale Ada Estate. Walikutana hivyo pale ambapo timu hiyo ya watu wanne ilipokuwa inataka kukaa kama marafiki na kuangalia maandalizi ya hasuri yanavyokwenda na kupeana mashauri. Vikao vya wazee familia vilikuwa vinaendelea na hivi vya kwao ambavyo havikuwa rasmi vilikuwa vinaitwa wakati wowote kuna jambo la kujadiliana.
"Ah basi ngoja nipitie huko wala siko mbali sana, nipeni kama nusu saa hivi" Sam alisema. Hakufikiria chochote na alibadili mipango yake jioni ile na kuanza kuelekea kule Ada Estate. Baada ya kufika pale hakuchukua hata muda kuangalia kama magari ya Husna na Erica yapo pale alielekea moja kwa moja kwenye ghorofa la Fiona. Fiona alifungua mlango na kumkaribisha ndani.
"Ah Fiona wengine wako wapi?" Sam aliuliza baada ya kujikuta yuko peke yake. Mara moja kengele zote za tahadhari zikaanza kupiga kichwani mwake.
"Wanakuja tulia hapo, unataka kitu chochote cha kunywa" Fiona alimuuliza.
"Yeah labda maji ya kunywa"
Fiona alielekea jikoni na kurudi na glasi ya maji baridi.
"Shem wacha nijimwagie maji mara moja kabla hawajafika hawa maana vumbi la Dar hili bwana" Fiona alisema.
"Hamna neno"
"Unaweza kuangalia TV, remote iko hapo juu ya meza" Fiona alisema huku akielekea chumbani kubadilisha. Wakati Sam alikuwa akiangalia TBC1 alimuona tu kwa jicho la pembeni Fiona akiwa na kanga yake akipita kuelekea bafuni. Alikuwa na uhakika kuwa macho yake yalimuona akiwa amevaa kanga moja tu. Maporomoko mengine ya maji yalianza kumjia. Alitaka kupiga simu kuuliza kina Husna na Erica watafika saa ngapi lakini shetani gani alimpitia na kumkataza. Kama dakika ishirini hivi maji yalikatika bafuni. Sam alijifanya yuko anaangalia TV lakini macho yake yakimtegea shemeji yake atoke bafuni.
Fiona alitoka bafuni akiwa na kanga ile moja kajifunga kuanzia kifuani. Miguu yake ilikuwa wazi na kumkumbusha Sam siku ile kijiko kilipodondoka mapajani mwa Fiona.
"Shem unaangalia nini?" Fiona aliuliza akiwa karibu kabisa na mlango wa chumbani.
"Aah TBC1 tu" Sam alijibu akiogopa kuinua macho yake kumwangalia. Moyo ulikuwa unamdunda kwa kasi, huku pumzi ikianza kumuenda kasi. Damu ilianza kujaa kwenye viungo vya mwili ambacho vilikuwa vinaonesha pasipo damu hiyo vingekufa.
"Kuna nini kwenye TBC1?" Fiona aliuliza. Taratibu alianza kuja alikokuwa ameketi Sam na kujaribu kuangalia iliko TV. Alisimama karibu zaidi na TV kuliko na Sam.
"Yaani unaangalia vikatuni Shemeji!" Fiona alicheka.
"Ah si unajua tena" bado hakutaka kumuangalia.
"Shem!" Fiona alimuita.
"Nini Fiona?" Aliyainua macho yake kumuangalia. Fiona alikuwa amedondosha kanga yake chini. Alikuwa kama alivyokuja duniani. Kabla Sam hajafanya lolote Fiona akaanza kumsogelea. Sam alijua kabisa kuwa uzalendo ungemshinda aliinuka kwa haraka na kwenda kuichukua ile kanga ili aje kumhifadhi Fiona. Aliiwahi kuichukua kanga na alipoileta kumfunika Fiona alikuwa amefanya kosa.
"Shemeji jamani"
"Sam!"
Ndio ulikuwa mwanzo wao. Walianza kuibiana muda na kupeana mapenzi kama vile hawataki. Yalikuwa kama mahaba ya bahati mbaya imetokea. Wiki zilivyopita na miezi ilivyopita ndivyo walivyojua kuwa ilikuwa ni zaidi ya mapenzi ya kimwili; wawili hao walikuwa wamewasha moto wa mapendo kati yao, mapendo ambayo hawakuwa kuyapata kwa mtu mwingine. Aidha kwa sababu yalikuwa ni ya siri au ni kwa sababu yalikuwa ni ya mashemeji; lakini kwao yalikuwa ni matamu sana.
* * *
Hivyo, walipokuwa bado wako pale nje na walivyoambiana habari za ujauzito walijua kabisa kuwa hakuna jinsi isipokuwa itawapasa wawe pamoja. Sam hakutaka mtoto wake aje kulelewa na mtu mwingine. Alijua ameshafanya kosa moja la kumsaliti Erica na kilichobakia ni kulikamilisha tu kosa lenyewe.
"Hatuwezi kukaa hapa Fiona, we have to leave" lilikuwa wazo la Sam
"Tutaenda wapi na sherehe hii?"
"Gari lako liko wapi?" Sam alimuuliza Fiona
"Liko upande ule kule" alielekeza kwa kidole cha mkono wake wa kulia.
"Unazo funguo za gari lako?"
"Hapana ziko ndani" Fiona alijibu.
"Nenda kachukue utanikuta kwenye gari lako na chukua chochote unachoweza maana sijui tunaenda wapi na tutafanya nini" Sam alimuagiza.
Fiona aliondoka taratibu na kujirudisha kwenye sherehe kama kawaida yake hakuna aliyekuwa amegundua alikuwa ametoweka. Alipanda juu hadi kulikokuwa na vitu vyake. Alichukua pochi yake, alienda kwenye chumba cha Erica na kwa vile alikijua vizuri alijua mahali ambako alikuwa anaweka fedha zake za ziada. Kwenye kiboksi kidogo cha viatu kilichokuwa juu ya kabati, kulikuwa na dola mia nne hivi. Alizichukua zote. Alipotoka mle ndani ilikuwa kama utani utani tu; aliacha vitu vingine vyote ndani hivyo alipotoka nje hakuna aliyehisi kuwa anaondoka kwenda mbali. Alimkuta Sam anamsubiri akiwa amejificha nyuma ya gari lake. Fiona alimfungulia mlango wa nyuma ambako Sam alijibanza kwa kujificha. Gari lilipotoka kwenye lango kuu la nyumba ile Fiona aliaga tu kuwa anatoka mara moja na atarudi, walinzi walikuwa wamemzoea pale nyumbani na walimuaga "Dada Fio"
Maili chache baadaye, Fiona alisimamisha gari, Sam alihamia kiti cha dereva, walishika barabara ya Morogoro. Karibu saa saba na nusu za usiku walijiandikisha kwenye hoteli ya Njuweni. Sam alijua kimbunga kitakachofuatia kitakuwaje. Hawakulala usiku ule bali walibembelezana na kutiana moyo, karibu alfajiri asubuhi baada ya mikakati mingi walijikuta wanakumbatiana na kuanguka kitandani.



4







ERICA ALIKUWA amechoka. Usiku ule wa Jumamosi zikiwa zimepita siku saba kamili za kulaani na kujilaumu alijikuta amejawa chuki ya kweli. Husna alikuwa amejirusha naye kitandani akiwa amelala chali pembeni ya Erica. Husna hakusema kitu kwa muda mrefu akimuacha rafiki yake azame katika dimbwi hilo la mawazo.
"Husna"
"Bee"
"Unajua wanaume ni wanyama sana" Erica alisema siyo kama swali au wazo tu ilikuwa kauli ambayo imetolewa kama na mwanasayansi aliyefanya utafiti wa kutosha na hatimaye kufikia hitimisho hilo baada ya kupima na kuchambua ushahidi wote wa kisayansi ulioko mbele yao.
"Hapana Erica sema Sam mnyama"
"Husna" Erica alirudia kuita kama alivyomuita mara ya kwanza rafiki yake huyo.


"Bee Erica"
"Unajua sisi wanawake tunaweza kutendana sana" alisema tena.
"Mmmhu" katika hilo Husna hakuwa na ubishi. Alijua Erica alikuwa anamaanisha nini. Kwa wiki nzima Erica hakutaka kuzungumzia kwa mtu yeyote mambo ya Sam na Fiona. Mazungumzo yote aliyoyafanya aliyafanya katika kichwa chake. Usiku huo hata hivyo alijaribu kujifungua na kuzungumza na shosti wake.
"Shosti pole mpenzi" Husna alimuambia rafiki yake huku akimuangalia kwa jicho la pembeni, kichwa chake kikiwa katika usawa wa kichwa cha Erica pale kitandani. Kwa mara ya kwanza alifanikiwa kumpa pole ambayo alijua ingeweza kumfikia rafiki yake.
"Asante shosti, yamenikuta mwenzako" alisema Erica kwa sauti ya unyonge ambayo ilikuwa kama sauti nyembamba ya mamake.
"Mwenzangu, hujafa hujaumbuka" Husna alisema. Ulipita ukimya kati yao na kwa mara ya kwanza, Husna aliyaachilia machozi na yeye yamtiririke. Kwa karibu nusu saa walilala hivyo chali wakiacha machozi yatiririke. Husna alikumbuka maisha ya marafiki wote watatu yalivyokuwa; pamoja na kuwa na ukaribu wa namna hiyo watatu hao walionekana kila sehemu zenye shughuli au tafrija yenye maana. Kama ilikuwa ni kwenda kuangalia bendi ya muziki walienda kama ilikuwa ni kwenye taarabu walienda kwenye taarabu na hawakukosa kwenda kwenye matamasha ya muziri au burudani. Kwao haikuwa kutafuta wanaume au kujionesha ilikuwa tu kwenda kustarehe na kufurahia maisha. Lakini ule umoja wao Husna alitambua haupo tena. Husna alipitiwa na usingizi hivyo hivyo. Erica aliinuka na kuchukua shuka na kumfunika rafiki yake. Yeye mwenyewe alitoka na kuelekea bafuni kwenda kuoga. Alijaza sinki maji ya moto kiasi na kuweka sabuni ya mapovu. Aliingia ndani ya maji yale ya moto kiasi na huku akiwa ameshika dodoki lake vizuri alianza kujiosha mwili wake kama mtu ambaye alikuwa anajaribu kujitoa uchafu wa kila namna. Bafu lake lilikuwa zuri na la kisasa likiwa limepambwa vizuri. Machozi yalikuwa yakimtiririka lakini safari hii yalikuwa ni machozi ya kukubali ukweli, kuachilia kile kilichokuwa kimemshika au yeye amekishika moyoni.
Wakati akiendelea kuoga alianza kutafakari kile alichokuwa akikisikia moyoni. Kwanza alikuwa na hasira na uchungu kupita kiasi dhidi ya Fiona. Wao watatu Fiona, Husna, na yeye walikuwa ni marafiki tangu wakiwa wadogo sana. Walikutanishwa kwa mara ya kwanza shule ya Tanganyika International ambako urafiki wao ulianzia na wazazi wao walikutana kwa sababu yao. Walikuwa ni kama dada watatu; hawajawahi kuachana hata walipoenda chuo walienda pamoja. Lakini zaidi ni kuwa waliheshimiana sana na lilipokuja suala la mahusiano, walipeana maonyo na kusaidiana. Lakini hakuna aliyewahi hata mara moja kujaribu kuchukua bwana wa mwingine. Hivyo kitendo cha Fiona kumkubali Sam kilikuwa ni usaliti tosha.
Erica alijaribu kujiuliza maswali lukuki ilikuwaje Fiona akaingia mtego wa Sam, je ilikuwa ni fedha? La hasha kwani familia ya kina Fiona walikuwa na uwezo mkubwa tu na Fiona mwenyewe alikuwa na ajira nzuri tu akiwa afisa katika ubalozi mmoja wa kimagharibi jijini Dar. Alijiuliza je ilitokea kwa bahati mbaya au vipi? Hakukuwa na majibu zaidi ya kuanza kufikia hitimisho tu kuwa Sam alikuwa amemdanganya. Sam alikuwa amemdanganya kuwa anampenda lakini hakuwa anampenda kiukweli. Alijilaumu kwa kumuamini Sam na siyo kumuamini tu bali kuwa tayari kujitoa awe wake wa milele. Erica alijihisi donge likimkaba kooni.
Halikuwa donge la uchungu kama ule aliojisikia pale alipotambua kuwa amesalitiwa na Sam. Na halikuwa donge la hasira kama aliyojisikia alipotambua kuwa aliyemsaliti alikuwa ni rafiki yake wa damu. Alivyojisikiwa ilikuwa ni donge tofauti kabisa lililoambatana na hisia ya ubaridi na ganzi katika mwili wake wa kike. Hata katika maji yale ya moto ambayo alikuwa amejichovya na kutulia akijisikilizia, yakimlainisha na kumtuliza hisia zake ubaridi huo kama wa kupitiwa na pepo mchafu aliuhisi hadi kwenye mifupa na nyonga yake. Ulikuwa ni ubaridi uliopita kuanzia kwenye utosi wa nywele zake na ukapuliza maungo yake na kupenya vinyweleo vya ngozi yake na kusafiri katika mishipa ya damu yake hadi kuelekea moyoni na kuufanya moyo wake uwe kama wenye kupulizwa na upepo wa ubaridi wa alfajiri wa kule Mafinga, Iringa. Alifumbua macho yake akiwa bado ameketi kwenye sinki lile la maji bafuni huku kioo cha pembeni mbele ya sinki la kunawia mikono kikiwa kimefunikwa kabisa na mvuke.
Katika ubaridi huo wa moyo wake aliinuka na kusimama kwenye sinki huku akiyaachilia maji yaliyokuwa yamemtuwama yaanze kutiririka na kuondoka kwenye sinki hilo siyo na uchafu wa mwili tu, bali na hata chochote ambacho moyo wake ulikuwa unajisikia kuhusu mapenzi. Maji machafu yalipotoka kabisa alianza kuosha nywele zake kwa kutumia shampoo yake aipendayo ya Just Natural ambayo imetengenezwa kwa kutumia kemikali za asili badala ya zile za viwandani. Alipomaliza kuziosha nywele zake kwa shampoo hiyo alituliza kwa kuweka conditioner ambayo nayo iliendana na falsafa yake ya kutokutumia kemikali kali kwenye mwili wake. Baada ya kuzisuuza mara mbili nywele zake alijisuuza yeye mwenyewe pale bafuni kwa kuyaachilia maji ya vuguvugu yadondoke kwenye mwili wake kama mvua. Alijisikia upya na usafi wa ajabu
Alipoinua miguu yake na kutoka kwenye sinki lile kubwa la mviringo Erica alijisikia mwenye ujasiri wa ajabu. Alipokielekea kioo chake kikubwa pale bafuni alijihisi kama Halle Berry alivyokuwa akitoka baharini akiangaliwa na Pierce Brosnan katika ile filamu ya James Bond 007 Die Another Day. Erica mwenyewe alipenda zaidi toleo la Ursula Andress katika filamu nyingine ya Bond ya Dr. No hasa kwa vile Ursula alikuwa na nywele ndefu kidogo kama za kwake. Aliposimama mbele ya kioo kile kilichofunikwa na ukungu wa mvuke kutoka bafuni, hakuweza kuona kitu chochote. Na hivyo ndivyo alivyojihisi moyoni. Hakuwa kitu chochote mbele ya yeyote. Alitumia mkono wake kupangusa ukungu ule lakini sekunde chache hazikupita kabla ukungu haujatanda tena. Alichukua taulo kavu la rangi ya pinki na kulizungusha kichwani.
Ule ubaridi uliokuwa umeingia moyoni ulizidi taratibu kugandisha moyo wake kama maji yanavyogeuzwa kuwa barafu taratibu. Kwa kutumia kidole chake chake cha kuonesha cha mkono wa kulia alijikuta anaandika kwa Kiingereza kwenye kioo kile "HATE" akimaanisha chuki. Aliangalia kwa sekunde chache maneno hayo yakifunikwa taratibu na masalio ya mvuke japo hayakuweza kufutika kabisa. Aliuma mdomo wake wa chini kwa meno yake wakati akichukua taulo dogo na kuanza kufuta kioo kizima. Kiliposafishika alisimama mbele yake kama mshitakiwa katika kizimba cha mahakama ya bafuni; shahidi pekee kioo.
Alijiangalia mbele ya kioo kile akiwa ameweka taulo tu kichwani ambalo alilichukua wakati anatoka kwenye bafu. Alisimama mbele ya kioo kile kama sanamu nzuri ya Malkia Nefititi wa Misri ya kale akiwa kama alivyokuja duniani. Umbo lake likifichua kila kitu ambacho kilifichwa na mavazi yake anapokuwa nje. Alijiangalia na kujiuliza alikuwa na kasoro gani. Alijigeuza nyuma taratibu na kujiangalia umbile lake kwa nyuma bila kuona kasoro yoyote zaidi ya uzuri wa asili aliojaliwa na Mwenyezi Mungu uliofichua umbile lake zuri la kike ambalo lilikuwa ni la kumtamanisha mwanaume yeyote ambaye hakuhusiana naye kinasaba. Katika mwili wake alikuwa na baka dogo jeusi upande wa kulia ambapo lilikuwa limefifia ikiwa ni alama yake ya kuzaliwa. Nje ya hicho hakuwa na kitu kingine chochote. Aliporejea kujiangalia tena mbele alitambua kuwa alikuwa ni binti mzuri kwa sura na umbo, jambo ambalo nusura alitilie shaka baada ya kuachwa na Sam. Alijitengeneza nywele zake na kujipaka lotion isiyokuwa na harufu kali ambayo nayo ilikuwa ni organic. Baada ya hapo alivaa nguo zake za kulalia na kutoka zake bafuni akiwa na uso uliokuwa mwepesi na mwili uliochangamka.



"Hey Shosti!" Ilikuwa sauti ya Husna iliyomrudisha katika ulimwengu wa walio hai.
"Hi Shosti" alimjibu kwa furaha na kumkuta Husna hakujiandaa kwa uchangamfu huo wa Erica.
"Unajisikiaje besti" alimuuliza akiinuka kitandani na kuhamia kwenye kochi alilokuwa ameketi awali.
"Niko pouwa ila nna njaa!" alisema na kumfanya rafiki yake aangushe kicheko.
"Unataka nikutengenezee kitu?" Husna alikuwa tayari kukimbilia jikoni kwani aligundua rafiki yake amerudi duniani.
"Wameshalala huko chini?" alimuuliza
"Yeah kitambo, saa saba hii na kesho watu kanisani"
"Oh yeah twende basi jikoni tukatengeneze chochote"
Husna alifurahi kumuona rafiki yake amechangamka tena na sauti yake ikiwa ya kawaida kwa kiasi kikubwa. Ilikuwa kama Erica mpya ametokea. Erica aliingia kwenye kabati lake na kuchukua kanga na kujifunga kiunoni. Hakuwa amevaa sidiria zaidi ya gauni lake lile la kulalia la rangi ya bluu bahari. Rafiki yake alikubaliana naye na pamoja wakizungumza kwa sauti ya chini walielekea jikoni. Walikuta kuna kiporo cha wali na nyama ya kuku pamoja na mchicha wa karanga vikiwa kwenye friji. Walivichukua na kuvipasha moto kwenye microwave kubwa pale jikoni. Vilipokuwa tayari walikaa jikoni na kuanza kupiga stori za mambo mengine yote isipokuwa suala la Sam na Fiona. Walicheka kimbeya hadi



kumwamsha Ray ambaye alikuja jikoni akiwa anajifukuta macho yake kushangaa kulikuwa na nini.
"Hi Little brother" Erica alimuita mdogo wake ambaye alimuangalia kwa kumshuku.
"Da'Erica mbona mnakula usiku" aliuliza huku macho yake yakizoea mwanga wa pale jikoni.
"Una njaa baba?" Husna alimuuliza Ray
"Kidogo dada"
Husna aliamua kumpashia Ray chakula kidogo kutuliza tumbo lake. Alipokula walimfukuza arudi kulala huku Erica akimuahidi kesho yake angempeleka Mlimani City kuangalia kama kuna video games mpya zozote. Ray alienda kulala akiwa na furaha moyoni kupita kiasi, kumpata dada yake tena lakini zaidi kuongeza maktaba yake ya video games. Erica na Husna walizungumza kwa karibu masaa mawili ilipofika saa tisa na nusu hivi waliamua kwenda kulala. Walipanda kitandani kulala huku wakiendelea kupiga soga na kukumbushana mambo mbalimbali. Husna alijitahidi sana kukwepa kumwingiza Fiona katika mazungumzo yao. Muda si mrefu Erica alijua Husna alikuwa ameanza kusinzia na hakuendelea kumzungumzisha sana kwani yeye mwenyewe usingizi ulikuwa umeanza kumchukua taratibu.
Kwa kadiri usingizi ulivyokuwa unambeba taratibu aliweza kuhisi kuwa lile baridi ambalo lilikuwa linaunyemelea moyo wake kama simba akimnyatia swala asiye na hili wala lile pembezoni ya kijito cha maji lilikuwa limeanza kuugandisha kabisa moyo wake na kuufanya uwe wa barafu; barafu ambayo ilikuwa inaganda taratibu na kuanza kutoa mvuke hafifu.
Wanaume ni wakatili sana -alianza kuwaza huku macho yake yakifumba na kufumbuka taratibu kama mwanasesere anapoinuliwa nan a kulazwa- hivi Sam alifikiria kuwa anaweza kunitendea hivi na kuendelea kula maisha ya furaha? Hivi wanaume wanafikiria mwanamke kaumbwa akiwa na moyo wa karatasi ambao unaweza kuukunja na kuukunjua kama utakavyo? Kwanini wanaume wanafanya hivi; kwanini Sam ameniadhibu moyo wangu kiasi hiki hivi? Anafikiria wanawake nao wakiamua kuwatenda wanaume haiwezekani? Hivi nikiamua kulipiza kisasi kwa wanaume kweli watajua? Au wanafikiria sisi wanawake tumeumbwa kusamehe tu kila tunapoumizwa? Hivi na mimi nikiamua kumuumiza mwanaume hivi atajisikiaje? Kwani wanaume nao wana mioyo? Kama wana mioyo tutaona basi kama wanaweza kusimama mbele ya kisasi changu, kisasi kitakachowafanya nao wajue uchungu wa kuwa majeruhi wa mapenzi
Alitabasamu kidogo wakati usingizi ukimchukua taratibu na kumpeleka kwenye bustani ya maua ya rangi za zambarau, njano, nyekundu na samawati na rangi nyingine ambazo hakuweza kuzijua mara moja. Bustani hiyo na ndege wa rangi mbalimbali miongoni mwao wakiwemo tetere, tausi na chiriku. Bustani ilikuwa imepambwa kwa vijito vya maji yakitiririka na kutoa sauti ya utulivu na amani. Miti midogomidogo ilipamba bustani hiyo ambayo ukubwa wake ulionekana kama hauna kikomo. Katika bustani hiyo Erica alijikuta ameketi kwenye kiti kikubwa cha enzi cha rangi nyekundu; alizungukwa na wanaume waliokuwa wamevaa kama watumishi wakimtumikia kwa heshima kubwa. Sura zao zilikuwa zimejaa hatia, uchungu, na unyonge huku wengine wakionekana kutokwa na machozi wazi mbele ya Erica. Erica alijiona kuwa ni malkia katika kasri lake la maumivu. Alitabasamu alipoona wanaume wanavyopita mbele yake na kumtetemekea. Alicheka kwa dharau huku akiyarembua macho yake.
Moyo wake uliowahi kuwaka katika mapenzi uligeuka kuwa barafu iliyoganda kwa kisasi, uchungu na maumivu ya moyo. Hakuwa tena na nafasi katika moyo huo isipokuwa kisasi kitakachoacha historia katika medani ya mapenzi na kuwa somo kwa wale wote wanaochezea mioyo ya wengine. Moyo wake ulikuwa umegeuka na kuwa barafu ambalo lilitoa mvuke wa ubaridi na kupooza viungi vingine vya karibu yake. Moto wa mapenzi haukuruhusiwa kuja karibu na hisia zozote za kupenda zilipokutana na moyo wa Erica na zenyewe ziligeuzwa na kuwa barafu.
Bustani yake ilikuwa inapendeza. Kulikuwa na nyuki wakirukaruka kutafuta asali na vipepeo wenye rangi mbalimbali. Erica alijikuta anatoa laana kwa vizavi vyote vya wanaume duniani isipokuwa baba yake na Ray mdogo wake. Alijua cha kufanya na alidhamiria kukifanya.
Watanikoma. Alijisemea moyoni.
 
Kwa yeyote yule anaetaka kununua hiki kitabu ..

Mimi nimepokea changu saa nne asubuhi Jmosi sijakiweka chini mpaka saa sita na dakika 38 (midnight)..

Waooo.
What a book. I have to admit "BEST SWAHILI BOOK I HAVE READ THIS YEAR"...

Kinakupa huzini, furaha, shangazwa, maswali
utaapigwa na butwaa.

I just love it, enjoyed Evey single minute.
Seriously is a five star book .. :)

Excellent work Mzee Mwanakijiji..
Keep up great job..

Looking forward for the next one :)
 
Last edited by a moderator:
Kwa yeyote yule anaetaka kununua hiki kitabu ..

Mimi nimepokea changu saa nne asubuhi Jmosi sijakiweka chini mpaka saa sita na dakika 38 (midnight)..

Waooo.
What a book. I have to admit "BEST SWAHILI BOOK I HAVE READ THIS YEAR"...

Kinakupa huzini, furaha, shangazwa, maswali
utaapigwa na butwaa.

I just love it, enjoyed Evey single minute.
Seriously is a five star book .. :)

Excellent work Mzee Mwanakijiji..
Keep up great job..

Looking forward for the next one :)

Thanks nilikuwa nasubiria kwa hamu kweli kusikia
 
Naamini Roho za kina Musiba, Mtobwa na Shabban Robert zimepata pumziko nafsini mwa Mzee Mwanakijiji.
Lazima niinunue hii riwaya

Asante BujiBuji.. I really want to change the writing and reading culture... lets see what happens..
 
Wengine wameshindwa kusoma kwenye ukurasa huo wa "Majeruhi"; so we made it easy for you to taste... the unfolding drama
 
Kitabu kizuri sana japo nimesoma yale tu yaliyoandikwa hapa, na nitamanio langu nikipate ili nifaidi uhondo uliomo ndani.
 

Similar Discussions

1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom