Nyie watu wa ajabu kweli kweli
Kwamba ndio mmejua leo kuwa Chenge hafai?
Mlivyomchagua kuwa mwenyekiti wa Bunge kwa kura nyingi za wabunge wa CCM hamkujua?
Hebu msituchoshe na msitufanye wajinga kwa makosa yenu mnayofanya kila siku.
Waingereza walirudisha chenji ya Rada Bil 40 na ushee na SFO ikasema kabisa Chenge amehongwa...Mlifanya nini?
Msituchoshe wezi nyie CCM
Haya Ya Akina Chenge Tumeyapigia Kelele Imepita Miaka 16 Sasa...!
- Mfupa huu ukimshinda na Magufuli, basi, hicho Chama Tawala kitakuwa kweli kimeoza, na nchi itakuwa kweli imelaaniwa.
Ndugu zangu,
Hapo chini ni makala niliyoandika na kuchapwa na jarida Raia Mwema mwaka 2009.
"Sakata la rada: Chenge ametajwa,hatushtuki!
Na Maggid Mjengwa,
ZIMETUFIKIA habari za Makachero wa Uingereza kitengo cha Makosa
Makubwa ya Jinai ( SFO) kubaini maovu zaidi ya kifisadi anayotuhumiwa
kuyafanya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Miundo
Mbinu Bw. Andrew Chenge. Kwamba Chenge ameongopa chini ya kiapo juu ya
fedha,dola za Kimarekani miloni moja na nusu alizoweka kwenye akaunti
yake Kisiwani New Jersey.
Katika hali ya kawaida tulitarajia idara zinazohusika zishtuke. Na
mshtuko wake ndio utakaopelekea pia jamii kushtuka. Ni kashfa kubwa.
Ni aibu kwa nchi, kwa Serikali na kwa chama tawala,CCM. Maana, Chenge
amekuwa kiongozi mwandamizi Serikalini na hadi sasa anakalia kiti cha
ubunge.
Habari hizi zimetufikia wakati Bunge likiendelea na kikao chake mjini
Dodoma. Watanzania hatuwaombi wawakilishi wetu,bali tunawataka
wawaulize na kuwahoji wenye kuhusika na kutoa ufafanuzi juu ya kashfa
hii. Hili halihusu itikadi za vyama, lina maslahi mapana ya nchi yetu.
Kazi hii tusiache ifanywe na wabunge wa Uingereza.
Itakumbukwa huko nyuma wabunge wa Uingereza wakiongozwa na mbunge wa
kujitegemea mwanamama Clare Short, walipata kuichachafya serikali
iliyopita ya Bw. Tony Blair juu ya sakata la nchi yetu kuuziwa rada ya
bei juu na pia rushwa kutumika katika ununuzi huo.
Wakati huo Bi. Clare Short alikuwa Waziri mwandamizi wa Masuala ya
Maendeleo na Misaada katika Baraza la Mawaziri la Bw. Tony Blair.
Yeye na mwenzake aliyekuwa Waziri wa Fedha kansela Gordon Brown
walipinga ununuzi huo. Leo tunaona,kuwa Clare na Brown walikuwa
sahihi. Gordon Brown ndiye Waziri Mkuu wa sasa wa Uingereza. Huku
kwetu tulihoji na kudadisi tuliitwa kwa majina mengi; " wavivu wa
kufikiri", " wenye wivu wa kike" na mengineyo.
Nilipata kuandika, kuwa aibu hii kamwe haiwezi kuwa yua Uingereza tu,
ni aibu yetu pia. Ni aibu yetu kwa vile kuna baadhi ya Watanzania
wenzetu wenye kutuhumiwa kuhusika na uhalifu huu. Wakati mjadala wa
ununuzi wa rada hiyo ulipofukuta mwaka ule wa 2001, sio tu tulionekana
wajinga tuliokuwa tukihoji ununuzi ule bali hata wale waliokuwa nasi
katika kupigania kufutiwa ama kupunguzwa kwa madeni yetu tuliwageuka;
mfano mzuri ni Shirika la Oxfam. Tuliwaacha wakiduwaa , wakati wao
walisisitiza, kuwa Serikali ya Uingereza isitoe leseni kwa kampuni ya
BAE, kwa vile mkataba huo haukuwa na manufaa kwa Watanzania walio
wengi. Serikali yetu ilitangaza kuupokea uamuzi wa serikali ya
Uingereza "Kwa mikoni miwili".
Tangu awali, sakata hili la ununuzi wa rada liliamsha maswali mengi
yenye kuhitaji majibu, mwaka 2001 kupitia safu ya " Gumzo la Ijumaa"
kwenye gazeti la Majira nilipata kuuliza yafuatayo; Je, ni nani hasa
wahusika wakuu wa manunuzi ya rada hiyo? Ni akina nani waliopitisha
uamuzi wa manunuzi ya rada hiyo? Je, bunge letu lilipata kufikishiwa
muswaada wa manunuzi ya rada hiyo, kuujadili na kutoa mapendekezo yao
kwa niaba ya wananchi? Je, kulikuwepo na hali ya kushindanisha
makampuni ya utengenezaji wa rada hizo duniani? Hivi tukiwa tumezama
ndani ya lindi la umasikini, je, ni rada ya kisasa na ghali mno
ndiyo tuliyohitaji ? Je, kuna mianya ya rushwa ya kimataifa katika
manunuzi ya rada hii? Leo tunapata majibu ya baadhi ya maswali yale.
Wakati ule Serikali ya Uingereza ililazimika kuahirisha
kutoa uamuzi wake wa kuuza au kutoiuzia Tanzania, rada yenye thamani
ya Dola za Kimarekani milioni 40 baada ya kubainika kwamba tayari
kiwanda cha BAE ambacho ndicho chenye tenda hiyo kilishatengeneza na
kuiweka tayari kwa kuisafirisha.
Ikaelezwa, kuwa rada hiyo ilitengenezwa baada ya maafisa
wa BAE kupewa uthibitisho na wizara ya ulinzi ya Uingereza kwamba
itapita na suala la leseni lingekuwa ni suala la kupitisha tu
(formality). Kwamba kusingekuwa na ugumu katika hilo.
Ikasemekana, kuwa hata Waziri Mkuu wa Uingereza, Bw. Tony
Blair akiungwa mkono na aliyekuwa waziri wake wa ulinzi Geoff Hoon
alishinikiza leseni itolewe kwa vile mkataba huo wa mauzo ungeokoa
ajira ya Waingereza 250 katika kisiwa cha Wight. Kwamba muhimu kwa
Uingereza ilikuwa ni ajira za watu wao kwa gharama za walalahoi wa
Tanzania!
Ndani na nje ya nchi yetu, tuliokuwa tukipinga manunuzi ya
rada hii ya gharama kubwa tulielewa umuhimu wa Tanzania kuwa na rada
bora ya kudhibiti safari za anga, lakini, tulichohoji ni umuhimu wa
kununua rada ya thamani kubwa ilhali kulikuwa na uwezekano wa
serikali kununua rada bora kwa thamani isiyozidi dola za Kimarekani
milioni kumi kwa wakati huo. Kumbe, leo tunafahamu, kuwa kung'ang'ania
kule kuinunua rada ile kulikuwa ni kwa maslahi ya baadhi ndani ya nchi
yetu! Kulikuwa na " Sete Pasenti! Ama kweli; Mvunja nchi ni mwananchi.
Muhimu lingine kulifahamu hapa ni ukweli, kuwa kiwanda kile cha BAE
kilichotuuzia rada ile, kimo katika rekodi ya kuhusishwa na kashfa ya
rushwa ya kimataifa. Vielelezo vya kuthibitisha kiwanda hiki na rushwa
vipo kupitia kumbukumbu za Shirika la Habari la Uingereza , BBC
hususan kwa kutafuta habari kuhusiana na kashfa ya mauzo ya silaha
nchini Afrika Kusini(
www.bbc.co.uk)
Kule Afrika ya Kusini, BAE inatuhumiwa kuhusika na kutoa rushwa
kwa mwanachama mashuhuri wa chama cha ANC Bw. Toni Yengeni akiwa kama
mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge la Afrika ya
Kusini. Ilidaiwa Toni Yengeni alifanikisha kiwanda cha BAE ambacho
ni mmoja wa wamiliki wa kampuni ya kutengeneza zana za kijeshi nchini
Sweden, SAAB kupata tenda ya mauzo ya silaha za angani. Kufuatia
kashfa hiyo, Bw. Toni Yengeni mwezi Oktoba mwaka 2001, alikamatwa na
kulazimika kujiuzulu nyazifa zake ndani ya ANC. Yengeni alihukumiwa
kifungo cha miaka minne jela.
Kwa taarifa hizo, tunaona wazi, kuwa hawa watu wa kiwanda cha
BAE wananuka rushwa katika kuendesha biashara zao. Kwanini basi
tusiwe na mashaka kuwa wametumia rushwa katika kufanikisha tenda ya
mauzo ya rada yao Tanzania kama sasa tunavyothibitishwa na Kitengo cha
Makosa Makubwa ya Jinai cha Uingereza?
Naam. Waingereza wamefanya uchunguzi wao,wamekuja na taarifa
ya kisayansi. Lakini, kama nchi, ingekuwa vema na sisi kama tukafanya
uchunguzi wetu kuwatafuta wengine zaidi waliohusika na uhalifu huo.
Maana,haiyumkini kiongozi mmoja tu mwandamizi akahusika peke yake na
wizi huo mkubwa. Tufanye hivyo kwa maslahi ya nchi yetu. Tufanye hivyo
ili kurudisha imani ya wananchi.
Na kama watapatikana wahusika zaidi, basi, kama walivyofanya Afrika
ya Kusini, nasi tuwafungulie mashtaka mahakamani. Ni kwa namna hii
tutarudisha heshima yetu kama nchi, na vile vile kutoa fundisho kwa
wengine."
Maggid Mjengwa.