Ambayo hujayasikia bado | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ambayo hujayasikia bado

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Bujibuji, Nov 18, 2009.

 1. Bujibuji

  Bujibuji JF-Expert Member

  #1
  Nov 18, 2009
  Joined: Feb 4, 2009
  Messages: 35,328
  Likes Received: 22,172
  Trophy Points: 280
  NI historia inayoturudisha nyuma hadi miaka milioni 20 iliyopita, ambapo mapango ya Amboni yaliyopo nje kidogo ya jiji la Tanga, yalipokuwa yamefunikwa na Bahari ya Hindi, kabla ya maji hayo kuhama katika eneo hilo na kuacha sura ya dunia yenye maumbile ya ajabu yaliyoumbwa na maji katika miamba iliyokuwa chini ya bahari.

  “Miaka milioni 20 iliyopita, eneo hili lote lilikuwa limefunikwa na maji lakini baadaye maji yalihama na kuacha sura hii inayoonekana leo katika mapango haya ya Amboni,” anasema Mhifadhi Mkuu wa mapango ya Amboni, Misana Bwire.

  Mapango ya Amboni yamebeba urithi ambao unaonyesha namna maji ya bahari yalivyoweza kufanya maajabu ya kuunda maumbile ya aina mbalimbali wakati maji ya bahari yalipokuwa juu ya miamba miaka milioni 20 iliyopita lakini bado sura ya maumbile hayo ikiendelea kuonekana kwa uhalisia hadi sasa.

  Bwire anasema pamoja na kuwapo kwa kumbukumbu nyingi za kihistoria ndani ya mapango hayo lakini bado Watanzania wengi hawajapata fursa ya kufika katika eneo la mapango hayo kujionea urithi uliopo ndani yake.

  “Idadi kubwa ya watu wanaofika katika maeneo haya ya mapango ni wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi na sekondari ambao kwa kweli wanaonyesha dhamira ya dhati ya kujua ni mambo gani yapo ndani ya mapango,” anasema Bwire.

  Mhifadhi huyo anasema hata hivyo bado kuna ulazima kwa Watanzania na raia wa kigeni wasio wanafunzi kufika katika mapango hayo ili kujionea kwa macho yao utajiri wa matukio ya kihistoria yaliyopo ndani ya mapango hayo ya Amboni.

  “Inawezekana bado elimu ya kutosha haijatolewa kwa wananchi lakini pia inawezekana bado hatujajitangaza kiasi cha kuwawezesha wananchi wengi kufika hapa ili kujionea maajabu yaliyopo ndani ya mapango haya ya Amboni,” anasema Bwire.

  Ni safari isiyozidi muda wa saa moja tangu unapoingia katika lango kuu la mapango haya ya Amboni, umbali ambao utakuwezesha kupita chini ya mapango hayo kwa staili tofauti zikiwamo za kutembea wima na wakati mwingine kutambaa kutokana na baadhi ya maeneo kutomuwezesha mtu kupata nafasi ya kusimama.

  “Ni vigumu mtu kuweza kuingia ndani ya mapango haya bila ya kuwa na mwenyeji anayemwongoza kwa kutumia tochi yenye kurunzi kali, kwani ndani yake kuna giza nene lakini pia kuna njia nyembamba na ambazo katika baadhi ya maeneo ni lazima mtu apite kwa kusota au kutambaa kama nyoka,” anasema Bwire. Kichwa cha Simba:

  Maajabu ya maumbile yaliyotokana na maji, yanaanza kuonekana katika lango kuu la kuingilia ndani ya mapango ambapo maji yameweza kutengeneza umbo la kichwa cha mnyama simba katika mwamba. Ni umbile halisi kabisa la kichwa cha simba dume, ambalo linaonyesha upande mmoja wa mnyama huyo.


  Mzimu wa Mabavu:

  Hili ni eneo ambalo maji yametengeneza eneo ambalo linatumiwa na watu mbalimbali kama eneo la kufanyia matambiko ili kuomba mambo yao kuwanyookea. Bwire anasema eneo hilo ni maarufu kwa jina la Mzimu wa Mabavu ambapo baada ya watu kufika eneo hilo huomba mizimu kuwasaidia waweze kufanikiwa katika mambo mbalimbali na kutoa ahadi ya sadaka.

  Bwire anasema maajabu yaliyopo katika eneo hilo ni kwamba mtu anapotoa ahadi ya kutoa sadaka ya kitu na akashindwa kurejea eneo hilo kutoa sadaka aliyoahidi, mambo huanza kumuendea kombo na kama alikuwa na mali zilizotokana na mzimu wa mabavu, mali hizo huanza kupukutika hadi pale mhusika atakapofika eneo hilo na kutoa sadaka aliyoahidi.

  Alama za kutukuza Uislamu: Haya ni maajabu mengine yaliyopo ndani ya mapango haya ya Amboni, hili ni eneo ambalo kuna michoro ya sura ya kitabu kitakatifu cha dini ya Kiislamu cha Kurani. Lakini pia pembeni ya kitabu hicho, maji yameweza kutengeneza michoro ya maneno ya Kiarabu. Eneo hili hutumiwa na waumini wa madhehebu ya Kiislamu kusali swala mbalimbali.

  Alama za kutukuza Ukristo: Lipo eneo pia ambapo maji yameweza kuchora sura ya jengo la Kanisa na pia sura ya Biblia ambayo imefunuliwa yakionekana maandishi madogo ambayo hata hivyo hayasomeki kama vile yanavyosomeka vizuri maneno ya Kiarabu.

  Katika hatua ya kushangaza zaidi katika eneo hili maji yameweza kuchora umbo katika mwamba ambalo ni sura halisi kabisa ya Bikira Maria ambaye amesimama kama vile zilivyo sanamu zake zinazowekwa katika Makanisa mbalimbali ya madhehebu ya Katoliki duniani. Hapa waumini mbalimbali wa dini ya Kikristo wanaoingia katika mapango haya ya Amboni hupatumia kutoa sala zao.

  Shimo la ajabu:

  Hili ni eneo ambalo lipo shimo refu ambalo hadi sasa wahifadhi wa mapango ya Amboni wanashindwa kueleza siri iliyopo ndani ya shimo hilo. Hata hivyo wahifadhi hao wanasema miaka mingi iliyopita raia mmoja wa Uingereza akiwa na mkewe na mbwa wao walitumbukia katika shimo hili na hadi leo hawajajulikana mahali walipo.


  Wanasema jambo la kushangaza mbwa aliyetumbukia na Waingereza hao alikuja kupatikana mwezi mmoja baadaye akirandaranda pembezoni mwa Mlima Kilimanjaro.Wanajenga dhana kwamba shimo hilo limeweza kufuata mwamba ulioanzia Amboni na kuishia jirani na Mlima Kilimanjaro.

  Kochi la ajabu: Hapa maji yameweza kufanya maajabu mengine kwa kutengeneza kochi aina ya sofa ambalo hutumiwa na watu wanaoingia ndani ya mapango hayo kupumzika au kupiga picha huku wakiwa wamekaa na kutulia kama vile wapo katika kochi zao za sofa majumbani.

  Kitanda cha ajabu: Katika eneo hili, maji yameweza kutengeneza kitanda cha ajabu. Inaaminika kuwa raia mmoja wa Kenya, Othare Otange aliyekimbia vita ya Mau Mau nchini humo alifika katika maeneo hayo ya Amboni mwaka 1952 na kukutana na mwenyeji wa eneo la Amboni, Paulo Hamisi na kumuomba kumpa hifadhi ili asijulikane.

  Wahifadhi hao wanasema baada ya makubaliano yao, Otange na mwenyeji wake Hamisi walianza kuishi ndani ya mapango ya Amboni na kulala katika kitanda hicho kuanzia mwaka 1952 hadi mwaka 1956, bila watu kugundua kama kuna watu walikuwa wakiishi ndani ya mapango hayo.

  Pikiniki:
  Hili ni eneo kubwa la wazi ambalo limebatizwa jina la pikiniki ambalo hutumiwa na watu wanaozungukia maeneo mbalimbali ya mapangoni kupumzika baada ya safari ndefu ya kuangalia maajabu yaliyopo ndani ya mapango hayo.

  Mlima Kilimanjaro:

  Hili ni eneo linalofuata baada ya kupita eneo la pikiniki, ambapo watalii hulazimika kupanda mwamba mrefu uliopachikwa jina la Mlima Kilimanjaro.

  Ingawa si mlima halisi lakini mwamba huu una mteremko mkali ambao humfanya mtu kupanda na kushuka kwa tabu kama vile anapopanda mlima halisi.

  Uwanja wa Ndege:
  Hili ni eneo la ajabu ambalo maji yameweza kutengeneza umbo la ndege na ngazi ambazo abiria huzitumia wanapotaka kuingia au kutoka ndani ya ndege. Katika eneo hili maji yameuchonga mwamba katika picha halisi ya ndege ambayo ipo kiwanjani mlango wa kuingilia abiria ukiwa wazi.

  Watalii wanapofika katika eneo hili ambako pia ndiko ulipo mlango wa kutokea nje ya mapango haya ya Amboni, hulazimika kupanda ngazi mfano wa vile abiria wanapopanda ngazi za ndege na baadaye huingia kwenye tundu ambalo linafanana na mlango wa kuingilia ndani ya ndege. Tofauti pekee hapa ni kwamba mtu anayepanda ndege halisi akifika mlangoni huingia ndani ya ndege lakini huyu anayepanda ngazi hizi katika mapango ya Amboni akifika katika tundu hilo lenye sura ya mlango huingia na kujikuta akitokeza sehemu ya nje ya mapango yenyewe.

  Njiwa wa ajabu:

  Maajabu mengine yanayowavutia watalii katika mapango haya ya Amboni ni njiwa wanaojifuga wenyewe ndani ya mapango. Tofauti na njiwa wa kawaida ambao wanapoona watu huruka na kukimbia, njiwa wa Amboni wao huwafuata watu hasa pale mtu anapoweka mtama katika viganja vyake vya mikono kwani njiwa hawa humfuata na kutua viganjani na kuanza kula mtama bila wasiwasi.

  Bwire anasema njiwa hawa wanaishi ndani ya mapango lakini katika maeneo ambayo hayafahamiki. Anasema wahifadhi wamejaribu kujenga mabanda ili waweze kuishi nje ya mapango lakini mpango huo umeshindikana kwani njiwa hao wamekuwa wakishindwa kuishi ndani ya mabanda hayo na kurejea mapangoni inapofika jioni na kutoka nje ya mapango kila asubuhi

  SOURCE: HABARI LEO
   
Loading...