Svalbard: Eneo pekee Duniani unaloweza kuishi na kufanya kazi bila Visa

Forgotten

JF-Expert Member
Jul 20, 2018
3,346
10,220
Svalbard, eneo linalopatikana karibu na ncha ya kaskazini mwa dunia ni kisiwa cha barafu kinachojulikana kwa hali yake ya baridi kali sana nchini Norway.

Raia kutoka nchi yoyote Duniani anaweza kuishi na kufanya kazi Svalbard bila Visa maalumu. Ila, kwa raia kutoka mataifa ambayo hayapo Schengen area ni lazima aombe Visa itakayomruhusu kupita eneo la Schengen na kuingia Svalbard. Hii ni kwa sababu hakuna usafiri wa ndege ya moja kwa moja kutoka mataifa nje ya Schengen.

Svalbard ina wakazi zaidi ya 2500 hali inayopelekea eneo hilo kuwa na maisha ghali sana kwasababu ni eneo lililojitenga mbali kabisa na huduma za kijamii. Wakazi wa huko mara nyingine hupaswa kusubiri wiki nzima pale vyakula kadhaa vya aina fulani vinapoisha kwenye Supermarket mpaka pale ndege itakapopeleka vyakula kutoka Norway.

Eneo hilo zamani lilikuwa likitumika kwenye shughuli za migodi hivyo hata majengo mengi na nyumba za wakazi zinamilikiwa na makampuni na siyo watu binafsi jambo linalofanya upatikanaji wa makazi kwa wageni wapya wa kudumu kuwa mgumu.

Svalbard inatambulika kama nyumbani kwa kila mtu wa Dunia hii lakini kwa wageni ni lazima uthibitishe una kiwango cha fedha cha kutosha kuweza kujikimu kwa muda wote utakaoishi hapo au upate kazi maalumu ya kukuingizia kipato kwani serikali ya Svalbard haitoi fedha za kujikimu kwa wasiojiweza jambo ambalo linapelekea eneo hilo kuwa eneo pekee Duniani ambalo halina ombaomba, kitu kinachofanya pia eneo hilo kuwa eneo pekee Duniani ambalo lina kiwango kidogo zaidi cha uhalifu au hakuna kabisa.

Eneo la Svalbard ni eneo hatari kuishi, ukiachana na hali ya hewa ya baridi kali na barafu, kuna wanyama wakali aina ya Dubu (Polar Bear) hivyo wakazi wa eneo hilo hupaswa kubeba bunduki pale wanapotoka maeneo ya makazi ya watu. Pia, Dubu (Polar Bear) ni wengi kushinda watu katika eneo hilo. Inakadiriwa kuwa Svalbard ina Dudu zaidi ya 3000 ikiwa ni zaidi ya idadi ya watu.

Katika eneo hili wakazi wa hapo ni kawaida kutokufunga milango ya magari na nyumba zao ikiwa ni katika kuchukua tahadhari iwapo mtu akawa katika hatari ya kushambuliwa na Dubu aweze kupata hifadhi ya kujificha.

Svalbard inatambulika zaidi kwa utalii kwani wageni wengi hufika hapo kujionea vivutio na maajabu mbalimbali ya eneo hilo.

Mambo ya kushangaza kuhusu Svalbard: Eneo hilo kwa miezi 4 katika mwaka huwa ni giza nene kwa masaa yote 24 katika siku na mfululizo na miezi 5 mingine huwa ni mwanga wa jua kwa masaa yote 24 katika siku. Juzi wakazi wa Svalbard walitoka nje na kusheherekea kurejea kwa jua baada ya miezi kadhaa ya giza nene tokea mwezi October 2023.

Northern lights ni moja ya kivutio kikubwa katika eneo hilo, hakika ni moja kati ya maajabu mengi ya Dunia hii ya kuvutia. Watalii wengi hufika kuanzia September hadi March kushuhudia maajabu haya yaliyopo Svalbard, Norway.

Uchumi wa Svalbard umeshikiliwa na utalii hivyo shughuli nyingi zinahusiana na utalii: hoteli, safari za kitalii n.k.

Svalbard ina chuo kimoja tu ambacho kinapokea wanafunzi wa uhamisho tu kutoka vyuo vya nchini Norway.

Pia, Svalbard ndiyo eneo ilipo Svalbard Global Seed Vault, kuba maalumu ya kutunzia mbegu za mimea yote Duniani. Kuna zaidi ya sampuli 1,214,000 za mimea yote Duniani. Kuba hii ilianzishwa ili kulinda mimea yote Duniani isiweze kupotea kutokana na sababu zozote zile zitakazoikumba Dunia.

Haya ni machache katika yale mengi ya kushangaza kutoka Svalbard.

Forgotten 🇳🇴🐻‍❄
 
Back
Top Bottom