Amani ipitayo mema na mabaya

Christiba

Member
May 27, 2020
24
32
AMANI ILIYO JUU ZAIDI YA MEMA NA MABAYA

Je kuna tofauti kati ya furaha na amani ya ndani?

Bila shaka jibu ni ndiyo, furaha ni matokeo ya hali chanya tunazozipitia katika maisha yetu ya kila siku, kwa upande mwengine AMANI ni undani ni zaidi ya furaha, AMANI haipatikani katikati ya mema na mabaya bali ndani zaidi ya mema na mabaya.

Je ni kweli haiwezekani kupitia hali chanya pekee pasipo kupitia hali hasi katika mzunguko wa maisha yetu?

Kama tabia zetu na mawazo yetu ni chanya kila siku hakika maisha yetu yatapitia kwenye hali chanya pekee, sivyo?

Hivi ni kweli unazifahamu zipi ni hali chanya(mafanikio) na zipi ni hali hasi(Tabu)? Je unajua kuna watu kwa kupita kwenye hali tunazoziita hali hasi(tabu) kama, huzuni, kutengwa, maumivu na kupoteza mambo muhimu kwenye maisha yao, zimewafanya kuja kuwa walimu na mashujaa wa kuigwa, je hii haitoshi kuona kuwa hakuna hali hasi(tabu) ila ni taswira na upinzani wa fikra zako katika kuikubali hali unayoipitia? Je haikufanyi ubadilike na kuachana na utu feki wa kifikra(Ego) ambao huzipinga baadhi ya hali na kutufanya kunasa kwenye huzuni na msongo wa mawazo milele. Hali yoyote unayohisi ni hasi unayoipitia amini inamatokeo chanya kwenye maisha yako usikubali fikra zikudanganye ukaishi bila AMANI, ni muda tu haujafika au ni wewe mwenyewe haujaruhusu kujitegua kwenye mtego wa fikra. Hata ajali na magonjwa yanaweza kukupa uelewa kuhusu kipi au nani ni wa kweli na yupi si wa kweli katika maisha yako, je funzo hili kwako halina thamani ya kuyathamini unayoyaita mabaya(matatizo).

Kama umeanza kupata picha kuwa hali zote unazozipitia ni chanya(zinafaida) hakika utakuwa bado umekwama kwenye gereza la fikra, bado utakuwa upo kwenye maisha ya utu feki. Ukitoka nje na ukiyachungulia mawazo na fikra zako utagundua hakuna hali chanya (mafanikio) wala hali hasi( matatizo) hakuna jema wala hakuna baya katika maisha yako bali hali ilivyo ndivyo hivyo ilivyo na kama ukitaka kuishi kikamilifu na kwa AMANI imekupasa kupokea hali yoyote kama ilivyo kwa wakati huo, hakikisha kwako hakuna jema wala baya hakika utaionja AMANI ya ndani. Maisha ya utu feki yametuletea hali ya ugunduzi wa mema na mabaya katika maisha yetu ambayo kiundani hali zote hizo ni feki na ni taswira tu ya maisha wala si maisha halisi, kama mafanikio yanaweza kukuletea huzuni, matatizo na magonjwa, na matatizo na magonjwa yanaweza kukuletea mafanikio je mafanikio ni kitu gani? Huoni ni taswira na mzunguko usioeleweka wa maisha feki? Mafanikio ya kweli ni Amani iliyo ndani yetu ambayo hupatikana nje ya gereza la mema na mabaya. Je umeshawahi kujiuliza kwanini maisha ya Adamu kabla ya kujua mema na mabaya yaliitwa paradiso? Je ushawahi kujiuliza kwanini Mungu alichukia kitendo cha kiumbe chake kujua mema na mabaya? Mungu hakutaka binadamu awe mtumwa wa fikra zake hakutaka tuishi kwenye maisha ya utu ambao sio sisi halisi.

Unaweza kujiuliza je mabaya kama ajali, ugonjwa, kutengwa, maumivu hata misiba yanaponitokea inanipasa niigize kuwa sio mabaya?

Hapana haya sio maigizo ila nikuruhusu hali iwe kama ilivyo, kwa kupingana na hali unayoipitia kunakufanya uwe mtumwa wa fikra na maumivu, kunakufanya usiipate paradiso iliyo ndani yako( Amani ya ndani). Kwa karuhusu hali unayoipitia kuwa ya kawaida kunakufanya uishinde fikra yako ambayo kwa kuupinga utu wako halisi fikra utengeneza hali chanya na hali hasi. Kuchukulia hali unayoipitia kama ilivyo ni kujiokoa na hatia inayokuhukumu, pia ni kitendo kizuri cha msamaha sio tu kwa watu wengine bali kujisamehe wewe mwenyewe. Kujisamehe katika kila tukio na hali inayokutokea kwa wakati huo(uliopo) wakati huu wa sasa hukufanya kuyapokea mambo na hali kama zilivyo bila kuzipa maana kuwa ni mbaya au njema(kuzihukumu) ambayo ni chanzo cha ukosefu wa Amani ya ndani. Kumbuka hatuongelei kuhusu furaha zinazokuja na kupotea hapa bali Amani idumuyo ndani yetu milele, kwa mfano; ukimpoteza mtu wako wa karibu sana hauwezi kuwa na furaha bali kwa kuchukulia hali kama ilivyo bila kuhukumu utakuwa na Amani.

Unaweza kujiuliza utalikubalije jambo kama lilivyo ikiwa lipo ndani ya uwezo wako kulibadilisha?

Kama swali hili linapita kwenye akili yako basi jibu ni kufanya hicho unachokiweza wakati huo ukiwa umeikubali hali unayoipitia kama ilivyo. Fikra au utu feki(Ego) ni pinzani na hakimu wa hali unazozipitia hivyo huleta msononeko na maumivu ili kuishinda fikra ni kukubali kile unachokipitia. Mara utakapoichukulia hali unayopitia kama ilivyo utakuwa umetoka ndani ya utu wa kifikra ambao wengi wetu tunaishi humo, utahisi uhuru fulani ndani yako ambao utakuonganisha na uhalisia wa utu wako na huko ndipo Amani huzaliwa. Kwa kutoka na kuzichungulia fikra zako utakuza uelewa wako kuhusu kujitambua wewe ni nani na hakika Amani itatawala maisha yako, kwa mfano sentensi hizi za Yesu, "akupigae shavu la kushoto mgeuzie na la kulia" na "akunyang'anyae koti mpe na kanzu" katika utu wa fikra hili jambo haliwezekani ila kusudi la Yesu hapa lilikuwa mtu kuishinda fikra na kufikiri zaidi kuliko kiwango chako cha fikra au ubinadamu wako feki (Ego) hali inayozaa msamaha na kutokupinga hali iliyokukuta na hizi ndizo funguo za Amani ya ndani.

Watu wengi hupata maangaiko na mateso kabla ya kuushinda upinzani wa kukubali hali wanazozipitia (kusamehe), ila jambo la kushangaza wakishakubali na kuzichukulia hali hizo kama zilivyo, Amani na nguvu mpya ya uelewa huchomoza ndani mwao na hapa huanza kugundua kuwa hali ambazo zilipokelewa kama mbaya kwao, maangaiko na mateso vinamatokeo katika kujitambua wao ni kina nani mbali na utu wa maumbo na majina yao. Kwahiyo vinavyochukuliwa kama mabaya kwenye maisha yetu ya kifikra(Ego) ni sehemu ya mema ya ndani kabisa ambayo hayana upinzani kutokea.

Haya huenda yakawa mageni machoni mwako ila utayapata kwa njia kuu moja ya msamaha, kusamehe na kujisamehe mwenyewe, kwa kusahau yaliopita na kuyaishi yaliyopo kama yalivyo. Amani haitafutwi nje yako Amani ipo ndani yako mbali na fikra zako ambazo uhukumu katika misingi ya mema na mabaya, Amani ya ndani ni zaidi sana kuliko mema ya nje ambayo hugeuka kuwa mabaya kwa sekunde.

Tujitafute leo!!!.
 
Back
Top Bottom