Ali Hassan Mwinyi: Azimio la Arusha limepitwa na wakati, hali imebadilika

figganigga

JF-Expert Member
Oct 17, 2010
25,492
54,895
Heshima kwenu wakuu,

Kwanza naomba Serikali iruhusu hotuba za Mzee Mwinyi zisomwe na Vijana.

Naomba nirudi kwenye mada. Jana kwenye mdahalo wa Mwalimu Nyerere, nlimsikia Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akisema inatakiwa turudishe azimio la Arusha. Nikatamani asome hii hotuba ya rais mstaafu mwinyi halafu ndo tuendeleze mjadala.

HOTUBA YA MWENYEKITI WA CCM, RAIS ALI HASSAN MWINYI WAKATI AKIZUNGUMZA NA WAZEE WA CHAMA, VIONGOZI WA TAIFA, MASHIRIKA YA UMMA NA WATU BINAFSI JUU YA UFAFANUZI WA MAAMUZI YA HALMASHAURI KUU YA TAIFA KATIKA KIKAO CHAKE CHA ZANZIBAR: DIAMOND JUBILEE DAR ES SALAAM, TAREHE 25/2/1991

Ndugu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Mkoa wa Dar es Salaam,
Ndugu Katibu Mkuu,
Ndugu Mwenyekiti wa Wazee wa Dar es Salaam,
Ndugu Viongozi wa Chama na Serikali na
Ndugu zetu waalikwa,

Kabla ya yote, labda niseme kwamba kwa kuwa tumo katika mwezi wa pili tokea kuanza kwa mwaka mpya, nami sijapata nafasi ya kukutana nanyi wazee, na vyema nitumie nafasi hii kwanza kukutakieni heri ya mwaka mpya, na baraka zote za mwaka 1991. (Makofi). Ninakuombeeni uzima, nguvu, baraka na mafanikio.

Pili, tuna kawaida katika nchi yetu, kwamba kila linapotokea jambo muhimu katika Taifa, tunatafuta nafasi ya kukutana nanyi na kukuelezeni. Hivyo, leo napenda kuzungumza nanyi wazee wa dar es Salaam na, kupitia kwenu, iwe ninazungumza na Wazee wenzenu wa tanzania nzima. Kwa hiyo, hayo nitakayokuambieni nyinyi, ninawaambia pia Wazee wa Taifa letu wote kwa jumla.

Hivi karibuni Halmashauri Kuu ya Taifa ilifanya kikao chake cha kawaida Zanzibar, ambacho kilijadili mambo mbalimbali. Kikao hicho kilimalizika kwa kutoa maamuzi maalum. Maamuzi hayo yana uzito mkubwa. Inaelekea baadhi yetu, pamoja na vyombo vyetu vya Habari, hatukuyaelewa vizuri maamuzi hayo. Kwanza, nataka nivivue na lawama Vyombo vyetu vya Habari. Maana hatukuwa nao huko. Kwa hivyo walitangaza vile walivyoelewa. Kwa sababu hiyo nimeona ni vyema kuzungumza nanyi ili kusahihisha matangazo ya vyombo vyetu. Nimeona ni vyema kutumia nafasi hii kutoa ufafanuzi.

LAZIMA TWENDE NA WAKATI
Inaelekea kuna hofu kwamba Azimio la Arusha linageuzwa. Kwa hiyo, tokea mwanzao, kabla ya kusema lolote, nataka tuelewane kwamba siasa yetu bado ni ile ile ya Ujamaa na Kujitegemea. (Makofi). Haikugeuka wala hatutazamii kuigeuza. Kwa hali yoyote sisi Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi hatutaigeuza Siasa hii. (Makofi) . Kule Zanzibar tulizungumza mambo mengi, miongoni mwao, ni kutoa tafsiri ya baadhi ya vipengele vya Azimio ili vifanane na wakati tulionao.

Azimio la Arusha, kama tunavyojua, limetangazwa mwaka 1967. Hii leo tuko katika mwaka 1991. Imepita miaka mingi, zaidi ya 20 tokea kutangazwa kwa Azimio la Arusha. Na katika kipindi cha miaka 20 yametokea mabadiliko mengi duniani na pia katika hali ya maisha yetu. Hali yetu ya sasa, hasa ya kiuchumi, siyo ile ile ya mwaka 1967. Ndio maana mishahara ya wafanyakazi ingawa imeongezeka sana lakini bado haikidhi mahitaji yao - haiwatoshi hata wale wanaopokea mishahara mikubwa miongoni mwetu. Isitoshe, wakati wa Azimio idadi ya Watanzania ilikuwa ndogo. Sasa hivi idadi yetu imeongezeka zaidi ya mara mbili. Kwa sababu ya wingi wetu mahitaji yetu nayo yemeongezeka sana, wakati mapato yetu yamekuwa yakipungua wakati wote.

Kwa hivyo ni dhahiri kwamba jamii ya Tanzania lazima itie maanani mabadiliko haya na ijiandae kwenda na wakati. Kama hatukwenda na wakati, kazi yetu itakuwa ni kufukuzia wakati - jambo ambalo hatulimudu.

Tabia ya wakati ni kama ile ya bahari. Bahari inakupwa na kujaa mapaka ukiongoni mwa maji. Baadaye maji hukupwa polepole, mpaka kufika wakati ikawa maji yote yamekwishaondoka ufukoni. Samaki werevu huondoka nayo hayo maji, yaani yakijaa huja nayo, yakitoka kutoka nayo, vinginevyo hupwelewa. Samaki watakaozembea kufuta maji watajikuta wamechelewa wanatapatapa juu ya mchango wakati maji hayo hayapo. Hiyo ndiyo maana ya kupwelewa (Makofi).

Hapa Afrika, kwa mfano, imeanzishwa mipango mbalimbali ya ushirikiano wa uchumi. Mipango hiyo ni pamoja na Ushirikiano wa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADCC) na Eneo la Soko Nafuu (PTA). Afrika pia imeazimia kuunda Jumuiya ya Uchumi. Nchi zinazoendelea nazo zimedhamiria kuzidisha ushirikiano miongoni mwao. Nchi yetu lazima ifanye mabadiliko ili iweze kushiriki kwa ukamilifu katika shughuli zote hizo zinazosaidia maendeleo yetu.

KILA ZAMA NA MWONGOZO WAKE
Ndugu Wazee, Msahafu wa Waislam unasema ‘LIKULLI AJALIN KITABU" Mwingereza mmoja kaitafsiri aya hiyo hivi: ' TO EVERY AGE ITS BOOK" yaani "Kila zama ina Kitabu (Mwongo) chake". Na sisi Wana-CCM tunakubali kuwa "kila Zama zinahitaji kuwa na Mwongozo wake". Azimio la Arusha ni Mwongozo wetu wa msingi. Ni dira inayoongoza mwelekeo wa jamii yetu. Lakini tafsiri zake zinabidi zirekebishwe kila inapohitajika ili zisipitwe na wakati. Miongozo ina tabia moja: inakuja ili kufafanua, kuelekeza au kukemea hali mbaya inayojitokeza.

Mojawapo ya malengo ya maamuzi ya Zanzibar ni kutoa tafsiri sahihi ili kupunguza kebehi inayofanywa dhini ya siasa yetu ya Ujamaa na Kujitegemea na pia kwenda na wakati.

Mwaka 1967 lilitangazwa Azimio la Arusha. Mwaka 1971 ulifuatiwa na tamko la Iringa la "Siasa ni Kilimo". Tamko hili lilikuwa ni mbinu na msisitizo wa Siasa yetu ya Kujitegemea. Zlilipanua tafsiri ya Azimio la Arusha. Katika mwaka 1981 ilionekana kuna haja ya kutolewa mwongozo mwingine kulingana na wakati ule ambao nao ni upanuzi wa tafsiri ya Azimio. Ulitangazwa ili kukidhi haja ya wakati ule.

Aidha, kabla ya hapo, katika mwaka 1974, Chama kilipitisha Agizo la Musoma kuhusu Elimu ya Kujitegemea ambalo madhumuni yake yalikuwa kutazama upya suala la uingizaji wanafunzi Chuo Kikuu na kupanua Elimu ya Msingi ili kutoa fursa kwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule kufanya hivyo.

Maandiko yote hayo hayakupingana na Azimio la Arusha ila yakiongeza mwangaza kwa mambo ambayo yalihitaji yafanane na wakati wake. Na lazima iwe hivyo, kwani bila ya kwenda na wakati tungechekesha.

Kwa mfano wakati wa Azimio la Arusha, mtakumbuka kuwa tafsiri ya neno Kiongozi ni pamoja na yule mwenye mshahra uliofikia shilingi 1,066/= kwa mwezi. Tungeng'ang'ania tafsiri hii tu, basi leo pasingekuwapo wafuasi. Wafanyakazi wote wangetafsirika kuwa ni viongozi wa CCM. Kwani ukiacha wakulima wafanyakazi wote sasa kwa tafasiri ya 1987 ni viongozi tena maradufu. Maana kima cha chini sasa ni Sh.2,500/=, ambazo ni zaidi ya mara mbili ya Sh.1,066/=. Ndiyo maana tukasema jamii yetu italazika Kufanya marekebisho kila inapokuwa lazima kufuatana na wakati. Tutafanya hivyo bila ya kuachana na misingi ya siasa yetu.

Kwa hivyo, tulichokifanya kule Zanzibar ni kupanua tafsiri za Azimio ili ilingane na wakati tulionao. Kufanya hivyo si kuua Azimio bali ni kuliimarisha.

CHIMBUKO LA AZIMIO LA ARUSHA
Historia ya Azimio la Arusha tunaijua sote. TANU ilipigania kwa maneno mpaka nchi ikapata UHURU wake. Tanganyika ilipopata Uhuru na tukaanza kujitawala ishara potofu zilianza kuchomoza. Baadhi ya Viongozi walianza kuutumia uongozi wao kama mradi wa kujineemesha. Kwa kutumia nyadhifa zao, wakikopa fedha benki na kuanza kujijengea mashamba - si ya miti - bali ya majumba; si nyumba za kuishi tu bali majumba mengi ya kupangisha.

Tabia hiyo ilizusha manung'uniko ya watu. Jamii ilianza kugawanyika makundi mawili; manaizi na makabwela. Kitendo hicho ndio chimbuko la kutangazwa kwa Azimio la Arusha. Azimio lilikuja kutoa mwongozo wa maadili ya wanachama na viongozi wa TANU. Kwa hivyo nia ya Azimio la Arusha, miongoni mwa mambo mengine, ilikuwa ni kuwazuia viongozi kutumia uongozi wao kujitajirisha. Hilo ndilo lililokuwa tatizo la hatari miongoni mwa matatizo wakati ule. Azimio lilikuja kuokoa jahazi - kukemea tabia potofu.

ATATIZO LA SASA NI UCHUMI TEGEMEZI
Mtu anaweza kuuliza je sasa kuna tatizo gani? Tatizo letu katika miaka ya tisini na kuendelea ni lile la uchumi tegemezi. Tatizo letu sasa ni kwamba uchumi wetu ni duni mno. Wakati idadi yetu inaongezeka, mapato ya Taifa, hasa ya fedha za kigeni, hayaongezeki. Wakati wa Uhuru idadi yetu ilikuwa ni watu milioni tisa. Lakini leo, tuko milioni tisa na tisa tena na nusu ya tisa. Lakini mapato yetu ya pesa za kigeni yapo pale pale, $ milioni 400. Wakati Azimio la Arusha lilitutaka tujitegemee, hali halisi ni kuwa tumekuwa wategemezi wakubwa. Maana Taifa letu hizi sasa, kwa pato lake lenyewe la fedha za ndani, linaweza kujitegemea kwa kipindi cha miezi saba tu katika mwaka. Tunategemea watu wengine, kwa njia ya ruzuku na mikopo, kumalizia miezi mitano inayosalia katika mwaka. Hii ni hatari. Lazima tunendelee kubuni mbinu za kuondokana na hali hiyo.

MBINU ZA KUJITEGEMEA
Ilani ya Uchaguzi inasema hivi:

"Makusudi ya Chama katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni kwa Taifa kukusanya nguvu zote za wananchi kwa kusaidiana na Serikali zao (Mbili), na kuzitumia katika kila eneo la maendeleo ili kutoa msukumo mpya wa utekelezaji wa siasa ya Ujamaa na Kujitegmea".

Hivyo, Chama na Serikali zake zinawajibika kuwarahisishia wananchi wao kujitegemea kwa chakula, kujitegemea kwa mavazi na kujitegemea kwa malazi. Ili kutimiza lengo hilo Taifa lazima liwawezeshe wananchi wake kuzalisha mazao ya biashara na chakula kwa wingi. Pia ni wajibu wa Chama na Serikali kuandaa mbinu za kuwasaidia wananchi kujijengea nyumba zao za kuishi ili ziwasitiri wanapostaafu au kuwa wazee.

Je wananchi wakituuliza: hivi ni mbinu gani mlizofanya kumshirikisha kila mmoja wetu kutumia nguvu zake zote katika kuzalisha kama Ilani inavyosema? Tungejibu nini? Lakini sasa kila mwananchi, pamoja na mwana CCM, hataweza kutoa kisingizio kwa kusema:-

"Mimi sikuweza kutumia nguvu zangu zote katika kufanya kazi ya kuzalisha kwa sababu nimezuiwa na Azimio la Arusha."

MWANACHAMA KUCHANGIA UCHUMI KIKAMILIFU
Azimio la Arusha lipo. Narudia tena kusema kuwa wanaohusika na tafsiri hii ni wanachama. Sisemi Viongozi, bali wanachama wa CCM. Tunataka kumpa Mwanchama wa CCM, kama mwanachama mwingine yeyote, uhuru zaidi wa kuzalisha ili kuchangia kadiri ya uwezo wake katika pato lake yeye mwenyewe na pato la Taifa Kwa jumla.

Ili tujitoe, kitaifa, kwenye shimo la utegemezi tulimo hivi sasa, mbinu bora ni kutoa uhuru kwa kila mwananchi wa kila Kaya, wa kila Kata, wa kila Tarafa, wa kila Wilaya na wa kila Mkoa kutumia nguvu zake zote katika kuzalisha. Matokeo ya hatua hii ni kumwezesha kila mtu katika Kaya, Kata, Tarafa, Wilaya na Mkoa kujigemea. Tukifika hapo ndipo Taifa litapokuwa limeondokana na hali ya sasa ya uchumi tegemezi.

KUPANGISHA NYUMBA
Jambo la kupangisha nyumba nalitaja tu, kwani si lazima kwa sababu si jipya; hata hivyo ni vyema nalo litajwe. Mwenyekiti Mstaafu alilisemea jambo hili mahali pengi sana, tena alianza zamani kulisemea, sijui. Kwa mfano, hivi karibuni alilitaja tena katika hotuba yake ya kuadhimisha miaka ishirini ya Azimio aliposema hivi:

"Nasharti hayo yanamkataza kiongozi wetu kuishi kikabaila kwa mbinu za kupangisha majumba.

Lakini sharti hili halimkatazi mtu mwenye vyumba vya ziada katika nyumba yake anamoishi kuvipangisha kwa watu wengine kwa kodi nafuu, Hili ni jambo la kawaida kabisa katika nyumba zetu za "Waswahili"' na upangishaji huu mimi nimekuwa nikiutetea tangu zamani. Utaratibu huu unawasaidia sana watu wenye mapato madogo, wanafunzi, au wafanyakazi ambao bado hawajaoa au kuolewa kupata vyumba vya kupanga kwa kodi nafuu.

Ni kweli kwamba huko nyuma tumekuwa wakali mno katika kutafsiri msharti haya.

Azimio la Arusha linachokataa ni unyonyaji. Hivyo maskini ya Mungu mwenye kijumba chake cha mbavu za mbwa akimwona maskini mwenziwe anapata taabu, hana pakukaa, asimpangishe? Je akimpangisha atakuwa anamnyonya? Au anamstiri? Kwa hiyo tangu zamani kustiriana ni ruhusa (Makofi).

Hatukuishia hapo kule Zanzibar, tulikwenda zaidi, tulisema pia kwamba wapo viongozi miongoni mwetu ambao baadhi yao wamefanya kazi za Chama au za Serikali kwa miaka 30 au zaidi. Lakini hawana nyumba; ukifika wakati wao wa kustaafu viongozi hao huwa wanababaika kwa kutojua wataishi wapi. Ndipo wanapoanza kutafuta mbinu - ndiyo maana siku hizi utakuta misururu mirefu katika Ofisi ya Vyeti vya kuzaliwa. Watu wanakwenda kubadilisha tarehe zao za kuzaliwa, kujifanya bado wangali vijana ili wachelewe kustaafu. (Makofi).

Sisi tunaamini kwamba baada ya kipindi kirefu cha utumishi, mtu aweze kuwa na nyumba ili, hata akiwa kipofu angalau aweze kupapasa kuta zake na kusema: Hii ni nyumba yangu niliyoipata kwa jasho langu la kazi ya miaka 30. Tunataka awe na kitu. Lakini, Ndugu Wazee, bahati nzuri wanachama wa CCM, kama wananchi wengine, wanaruhusiwa kukopa. Wanaweza kukopa kwenye benki zetu wakajenga nyumba za kukaa. Sasa jamani tukisema kwamba hata mtu aliyekopa asiipangishe nyumba hiyo atalipia nini huo mkopo?

Vinginevyo tutakuwa tunamfanyia mzaha mtu huyo. Maana atachukua mkopo, ajenge nyumba, kisha ashindwe kulipa huo mkopo. Waliomkopesha wataikama hiyo nyumba na kuiuza ili kurudisha fedha yao. Katika hali hiyo mwana-CCM gani atakayekuwa na nyumba iwapo mwisho wake ni kuchukuliwa na kile chombo kilichomkopesha? Kwa hivyo nasema mtu kama huyu ana dharura; ana dharura ya deni. Amejenga nyumba kwa nia ya kukaa mwenyewe lakini ana deni la mkopo. Kama anaweza kukaa nyumbani mwake, akae. Lakini pia awe na ruhusa ya kupangisha nyumba yake, akitaka, ili imsaidie kulipa mkopo. Anapostaafu awe anayo nyumba ya kumstiri uzeeni. Kitendo hicho kisimpotezee uanachama wake wa CCM.

Kwa hivyo Ndugu Wanachama, huko ndiko kwenda na wakati, vinginevyo tutapwelewa. Mtu kama huyu aruhusiwe kupangisha nyumba yake, iwe nusu ya nyumba, ama robo ya nyumba au yote: (makofi).

BIASHARA YA KUPANGISHA MAJUMBA BADO NI MWIKO
Lakini kikao cha Zanzibar hakikutengua miiko ya kiongozi wala ya mwanachama wa CCM. Bado ni mwiko kwao kuwa na biashara ya kupangisha majumba. Kwa mfano, kama kuna mwanachama anayeomba mkopo, akipata anajenga nyumba, halafu anaikodisha, akipata fedha za kodi anajenga nyingine mpya, ambayo nayo anaikodisha na kuendelea kujenga nyingine. Huyo ni mfanyabiashara. Kazi yake ni kujenga na kupangisha majumba. Kikao cha Zanzibar hakikusudii mwanachama wa aina hii. Huyu siye (Makofi).

Vile vile, Mwanachama wa CCM, hata akiwa kiongozi katika mazingira maalum, aruhusiwe kukodisha nyumba yake, ikiwa haihitaji kuikaa wakati ule. Inawezekana haihitaji kuishi katika nyumba yake kwa kuwa kapata uhamisho. Mfano, mtu kahamishiwa Iringa kwa kazi wakati nyumba yake iko Dar es Salaam. Je ikae bure watu waitumie bure tu kweli? (Makofi).

Ni mwanachama wa aina hii ndiyo tulisema huko Zanzibar kuwa aruhusiwe kupangisha nusu ya nyumba ama robo ya nyumba au yote, maadam mtu huyo anapo pengine pa kukaa. Lakini tunasisitiza kuwa bado si ruhusa kwa mwana CCM wala kiongozi wa CCM kuendesha biashara ya kupangisha majumba.

HISA KATIKA MAKAMPUNI YA UMMA, KUPUNGUZA UKWASI!
La pili lililoamuliwa huko Zanzibar ni kuwaruhusu wanachama wa CCM, kwa kufuatana na hali ya wakati ulivyo, sasa aruhusiwe kuwa na hisa katika kampuni ya Umma. Hii leo tunayo Mashirika ya Umma zaidi ya 400, lakini mengine yao hayana fedha za kuendeshea kazi zao.

Mfano kuna mwananchi mmoja alikwenda kwenye kiwanda cha Umma kutaka huduma ya kusafishiwa ngozi zake. Alipofika hapo alikuta "pamelala paka" Yaani palikuwa kimya, hapakuwa na kazi yoyote inayofanyika. Kumbe kile kiwanda kilikuwa kimefungwa kwa kukosekana fedha za kukiendeshea ........... umeme ulikatwa na wafanyakazi walipewa likizo.

Meneja alimfahamisha huyo mteja kuwa kiwanda kimefungwa kwa sababu ya deni la maji na umeme pamoja na pesa za mishahara ya wafanyakazi. Huyo mteja alikubali kulipa arubuni (advance ) ya milioni saba ili kukikwamua kiwanda. Wiki ya pili yake kiwanda kilianza kufanya kazi zake za kuzalisha kama kawaida.

Kisa cha kiwanda hicho kusimama kazi ni kukosa fedha za kuendeshea. Kiswahili cha siku hizi huitwa ukwasi. Kwa hiyo kazi ilisimama.

Katika hali kama hii, tumeona ni vyema kuwaruhusu wananchi wote pamoja na wakulima, na wafanyakazi wa shirika lenyewe wakiwemo wanachama wa CCM kununua hisa chache kwa kila atakaetaka

UBIA WA UMMA NA DOLA KATIKA SHIRIKA
Narudia, watakaoruhusiwa kununua hisa ni wananchi wowote watakaopenda pamoja na wakulima wa pamba, korosho, kahawa, tumbaku na wafanyakazi wa hilo shirika lenyewe. Kwa njia hiyo, Shirika hilo sasa litapata sura mpya, litakuwa ni la ubia kati ya Serikali, wafanyakazi na wananchi. Fedha tunazozizungumzia hivi sasa, za kulipia taa na mahitaji mengine zingetokana na ununuzi wa hisa ili uzalishaji uendelee. Katika hali kama hiyo kiwanda kitakuwa ni mali ya umma kweli. Maana kuna tofauti ya Shirika la Dola na Shirika la Umma kwa maana ya wananchi wenyewe.

Endapo shirika la umma litataka kuwashirikisha wananchi na wafanyakazi wake kwa kulichangia ili kuondoa tatizo la Ukwasi, jambo hilo liwe ni halali, na Mwana CCM naye aruhusiwe kuwa miongoni mwao. (Makofi)..Kilichofanywa na maamuzi ya Zanzibar ni kumruhusu mwanachama wa CCM naye kushiriki kikamilifu katika sera ya Taifa ya uwekezaji wa rasilimali nchini.

Katika sera ya uwekezaji rasilimali tunaruhusu ubia katika uchumi wetu. Ubia huo unaweza kuwa baina ya watu wa ndani ya nchi peke yao, au kati ya wawekezaji wa nje na wa ndani. Baada ya kuikubali misingi hiyo hatuoni kwa nini tusianzie kwa kuwaruhusu wananchi, wakulima na wafanyakazi kuwa na hisa katika Mashirika wanayofanyia kazi (Makofi).

WAFANYAKAZI KUSIMAIA UWAJIBIKAJI
Nia nyingine ya kufanya hivyo inatokana na kutambua kuwa wafanyakazi wenye hisa katika kiwanda watakuwa wasimamizi wakereketwa wa uwajibikaji katika viwanda hivyo. Watakereketwa zaidi pakiwa na ubadhirifu au kutowajibika.

Hivi leo baadhi ya mashirika ya Umma ni mashirika ya umma kwa jina tu. Watu wanayaibia wakidai wanachukua chao. Pengine wanashindana kufanya hivyo ili wasipunjwe. Baadhi ya mashirika ya Umma yanahujumiwa kana kwamba hayana wenyewe. Baada ya maamuzi ya Zanzibar kuanza kutekelezwa, Mashirika hayo yatakuwa na wenyewe.

MWONGOZO WA 1981 KUHUSU UWAJIBIKAJI
Maamuzi ya Zanzibar si mapya. Mwongozo wa chama wa 1981 umetoa ilani juu ya kupungua kwa uwajibikaji katika Mashirika ya Umma, jambo ambalo hivi sasa tunalitafutia ufumbuzi. Mwongozo wa 1981 unasema hivi:

"Imezuka tabia ya aibu nchini ambayo imekuwa ikiongezeka ya vitendo vya kuharibu na kuvitumia vibaya vyombo muhimu vya kazi na mali ya umma kwa jumla. Magari, matrekta, zana nyingine muhimu z chama, serikali, mashirika ya umma mara nyingi hayadumu muda mrefu kama ambavyo ingetazamiwa kutokana na matumzi mabaya."

Lakini ikiwa watu pale pale wenyewe wana hisa katika kampuni au shirika - mfano - TANESCO kuwa Mkurugenzi katika kampuni ya Kibepari. Napenda suala hili lieleweke vizuri ili kujibu fikra zilizojengeka kuwa uamuzi huo umevunja Azimio la Arusha.

Kwanza inafaa tufafanue maana ya Mkurugenzi. Tafsiri ya Mkurugenzi inayojulikana sana ni ile ya mjumbe wa bodi ya wenye hisa katika Kampuni fulan. Kwa hiyo wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi katika Kampuni ya Kibepari huwa ni miongoni mwa wale wenye hisa zao katika kampuni inayohusika Watu hao huchanguliwa na wenzao wenye hisa kama wa kuongoza shughuli za Kampuni yao kwa faida ya pamoja. Mkurugenzi wa aina hii hawezi kuwa mwanachama wa CCM.

Lakini kuna Mkurugenzi wa aina nyingine ambaye ni tofauti kabisa na Mkurugenzi mwenye mali. Mkurugenzi huyu ni yule ambaye ameajiriwa tu na wenye mali yao, kutokana na sifa zake za utaalam, kuendesha kampeni. Mtu huyu huwa ni mwajiri tu, anayefanya kazi. Huyu ni mtumishi tu kama watumishi wengine, hana chake katika kampuni inayohusika. Anachotegemea ni mshahara wake na marupurupu mengine kama yapo. Huyu ndiye Mkurugenzi anayeruhusiwa kuwa mwanachama wa CCM.

Azimio la Arusha bado lilo pale pale kwa wale wakurugenzi wa aina ya kwanza. Wao Azimio linawabana, hawawezi kuwa wanachama wa CCM. Lakini huyu wa aina ya pili aliyeajiriwa tu, akija kuomba uwanachama tunamkubali. Azimio la Arusha kamwe halijamkataa mfanyakazi mwenziwao kwa "koa" la kutumikia Kampuni ya Kibepari, hivyo ndivyo tulivyoamua Zanzibar

MWANA - CCM KUWA NA HISA KATIKA KAMPUNI YA KIBEPARI

Jambo jingine ambalo halikueleweka vizuri na linahitaji ufafanuzi ni lile la kumruhusu mwanachama wa CCM kuwa na hisa katika kampuni ya Kibepari. Hili nalo tumeliruhusu huko Zanzibar, lakini sharti iwe katika mazingira maalum.

Ni vyema kukumbushana kuwa yapo makampuni ya kibepari ambayo tumekuwa nayo hata kabla ya Azimio la Arusha. Kampuni hizo zimekuwa zikidhi kiasi fulani cha ajira ya Watanzania, pamoja na Wanachama wa CCM.

Ni jambo hili lieleweke vizuri, nitatoa mfano tu wa Kampuni ya mtu binafsi. Mwenye Kampuni ya binafsi anaweza kabisa akaamua kwa hiari yake kuuza baadhi ya hisa kwa wafanyakazi wake ili kuwapa motisha ya kazi Tajiri yeyote akiamua kufanya hivyo, Chama na Serikali vitamwona kuwa amechukua hatua ya kimaendeleo. Kitendo chake hicho ni halali. Kwa sababu itakuwa ameuzimua ubepari kwa kuifanya kampuni yake ni ya ubia kati yake na wananchi aliowaajiri. Kwa kweli kampuni hiyo itakuwa kama chama cha ushirika.

Katika hali hiyo, hata Mwanachama wa CCM anaruhusiwa kupokea/kununua hisa alingane na wafanyakazi wenzie.

Ni mazingira maalum ya namna hii tu ndiyo yanayoruhusu Mwanachama wa CCM, kama mfanyakazi mwingine, kuchukua hisa katika Kampuni anayofanyia kazi. Atakapostaafu ataweza kuendelea kupokea faida ya hisa yake au kuiuza.

MISHAHARA MIWILI KWA MWANA-CCM
Kuhusu mishahara miwili, Azimio la Arusha linasema hivi:

"Kwamba kila mtu anayo haki ya kupata malipo ya haki kutokana na kazi yake".

Kufuatana na ukweli huo, anayefanya kazi mbili za halali anastahiki kupata malipo ya kazi ya pili. Tuchukue mfano wa Profesa ambaye mchana kutwa anasomesha Chuo Kikuu. Baada ya saa za kazi anaweza kuamua kufanya azi ya akili, kwa mfano kutoa ushauri au kuandika mradi kwa aliyemwomba huduma hiyo.

Mwanachama huyo atastahiki kupata malipo ya kazi hiyo. Hili si geni, katika sherehe za kuadhimisha miaka 20 ya Azimio la Arusha, baba wa taifa alisema hivi:

"Lile sharti la kutopokea mishahara miwili kwa kweli ni sharti la tahadhari tu. Ni vigumu sana kufanya kazi mbili za kuajiriwa na zote mbili ukazifanya vizuri. Huwezi kuwatumikia mabwana wawili! Lakini sharti hili halimkatazi kiongozi wetu kujiongezea pato kwa kutumia muda wake wa kupumzika kwa kufanya shughuli nyingine: kama kulima au kufuga, ikiwa yeye si mkulima au mfugaji, kuandika, kufanya kazi ya useremala, au kufanya shughuli nyingine yoyote kwa mikono yake au kwa ajili zake".

Jambo la msingi ni kwamba lazima twende na wakati. Mwaka 1987 lilipotungwa Azimio la Arusha ilikuwa hakuna haja ya kuwa na mishahra au malipo ya kazi zaidi ya moja kwa sababu wakati ule mshahara mmoja ulikuwa unatosha kukidhi mahitaji yote muhimu. Kwa mfano, mimi, mwenyewe, mshahara wangu wakati ule ulikuwa shilingi 2,200/= kwa mwezi. Mshahara huo, hasa kwa Zanzibar, ulikuwa ukinitosha kukidhi mahitaji yangu yote ya lazima.

Wazee wangu watakumbuka kwamba wakai ule kule kitunguu, pilipili na bizari -yote hivyo kwa senti tano tu. Ilikuwa inawezekana pia kununua samaki mkubwa kiasi kwa senti ishirini mpaka 50 tu; au kununua kuni za kuweza kupikia mlo mzima kwa senti kumi tu.
Siku hizo iliwezekana mnunuzi kujaziwa mafuta ya kupikia au samli kikombe kizima kwa senti ishirini hasitini tu. Halikadhalika kwa senti ishirini tu mtu aliweza kununua matunda, kama vile fungu la ndizi mbivu au machungwa au papai. Kwa ufupi, kwa mahitaji ya siku nzima, tangu asubuhi hadi jioni, iliwezekana mtu kutumia pesa kidogo sana.

Katika hali hiyo, kulikuwa hakuna ulazima wa kufanya kazi ya pili. Afanyae kazi zaidi ya moja huonekana ni mlafi au ana tamaa. Kwa mshahara huo huo niliweza kudunduliza pesa na mwishowe kununua gari mpya kabisa. Gari hilo lilinigharimu pesa nyingi kwa wakati huo - shilingi 13,000/=!! Wakati huo bei ya mafuta nayo ilikuwa shilingi tatu tu kwa galoni zima. Katika mazingira ya aina hii mshahara mmoja ulimudu kukidhi mahitaji ya wafanyakazi wengi ukiacha walevi.

HALI IMEBADILIKA

Lakini leo mambo yamebadilika. Gharama ya maisha imepanda san. Serikali yenyewe imeungama waziwazi kuwa haina uwezo wa kumlipa mfanyakazi wake mshahara unaomwezesha kumudu gharama za maisha. Kutokana na hali hiyo, wafanyakazi wengi, wanashindwa kukidhai mahitaji yao muhimu. Ndio maana Chama na Serikali yake vimekuwa vikiwahimiza wafanyakazi kufanya shughuli nyingine za halali, baada ya saa za kazi, ili kujiongezea mapato. Mfano wa kazi hizo ni kama vile: kutibu, kuandika vitabu, kuandikamradi, kutoa ushauri wa kitaalamu, kufundisha, overtime, useremala, ufundi bomba, ufundi umeme, ufundi cherahani, kilimo, ufugaji, kuziba mipira ya magari, kuteka maji ya kuuza, kupiga matofali, kutengeneza baiskeli na kadhalika.

KOFIA MBILI MSHAHARA MMOJA
Lakini lazima tuelewane kuwa hii mishahara miwili tunayozungumzia haimhusu kiongozi mwenye kofia mbili. Kwa mfano, Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya, ambao vile vile ni Katibu wa Chama wa Mkoa au Wilaya, hawaruhusiwi kupokea mishahara miwili. Hawa watalipwa mshahara mmoja tu, maana hii kazi ya pili ni sehemu tu ya ile ya kwanza. Lakini wanaruhudiwa kufanya kazi za ziada kama vile kilimo, ufugaji na kadhalika, baada ya saa za kazi, kama walivyoruhusiwa wafanyakazi wengine. Hapa nitapenda kusisitiza kuwa wale watu wanaoeneza maneno ya kejeli kuwa ati Maamuzi ya Zanzibar ni mbinu tu za "wakubwa" kujifufanisha wenyewe, ijulikane kuwa si kweli. Kazi zilizoorodheshwa hapa si za wakubwa bali ni kazi zinazoweza kufanywa na kila mtu kufuatana na ujuzi alionao na mazingira ya mahali anapofanyika kazi.

MWANA-CCM MKULIMA NA MFUGAJI
Watanzania wengi ni wakulima, wakulima ndio wengi zaidi. Mkulima kwa maana pana ni pamoja na mfugaji. Katika siku za nyuma, baadhi ya wanachama waliwahi kutiwa msukosuko kwa kuwa na mashamba makubwa au kufuga kuku 500. Lakini baadaye Chama kilijisahihisha kama inavyosema Programu ya Chama:

"Chama Cha Mapinduzi ni Chama kinachokua (haikudumaa). Kinakaa katika nadharia na falsafa yake, (ili kwenda na wakati)".

Hii ndio ilivyokifanya Chama kijisahihishe kila kinapokosea.

Kwa hiyo kama siku moja tulimtia mwenzetu msukosuko kwa kuwa na shamba kubwa, mbuzi 18 au kuku 500, sasa Chama kimekua katika falsafa yake. Falsafa ya sasa inatia maanani hali halisi ya wakati wa sasa. Ndio maana kule Zanzibar tukaruhusu kiongozi awe na shamba lisilozidi hekta 20, hasa kama shamba hilo limo katika eneo la kijiji.

class=Section2>
Kuhusu ufugaji, kuna baadhi ya wenzetu katika makabila ya Tanzania ambao kwao ni utamaduni wao kuwa na ng'ombe wengi. Mfano mzuri ni wenzetu wa makabila ya wamasai, Wasukuma na Wagogo. Je, mwenye utamaduni wa kumiliki ng'ombe wengi akataliwe katika Chama kwa sababu ya kumiliki ng'ombe wengi? Tunasema hapana. Akiomba uanachama wa CCM akubaliwe. Chama Cha Mapinduzi hakimkatai tajiri aliyepata utajiri wake kwa njia ya halali na kulipa kodi ya Serikali analipa. Anayekataliwa na CCM ni yule aliyepata utajiri kwa wizi, kwa rushwa, dhuluma na kwa kwa njia nyingine za haramu.

Huko Zanzibar tulifikria labda tuweke kiwango maalum cha mifugo, kama vile iwe mwisho ng'ombe 200 peke yake. Lakini tulijiuliza kama ng'ombe mmoja akizaa na jumla kufikai 201, je huyo ndama amnyonge shingo?

Hiyo ndio hali halisi iliyotufanya tukubaliane kuwa mfugaji yeyote anaetaka kuwa mwanachama bila ya kujali idadi ya mifugo yake. Mwenye mshahara mkubwa, vile cvile hata wa malaki, maadam ni mshahara wa kazi halali, naye pia aruhusiwe kuwa mwanachama wa CCM.

MAFUNZO YA MIEZI MITATU
Ili kukiimarisha zaidi Chama, tumewaruhusu wananchi kuwa wanachama wa CCM bila ya kuhdhuria yale mafunzo ya miezi mitatu.

BIASHARA NDOGO NDOGO
Huko Unguja hatukuishia hapo. Tuliamua kuwa Mwanachama wa CCM wa kawaida naye pia aruhusiwe kuwa na biashara ndogo ndogo ili kumwongezea kipato. Biashara hizo, ambazo sharti zifanywe baada ya saa za kazi, ni pamoja na uvuvi, kuwa na gari ndogo au pick-up ya kukodisha kwa kuchukulia abiria au mizigo, kushona, kusindika matunda, mafuta na mashine ya kukoboa au kusaga unga.

Mwanachama mwenye mashine ya kusaga unga hanyonyi bali anatoa huduma kwa jirani zake kijijini. Chama na Serikali vimo mbioni kuhimiza na kutafuta teknolojia ya kumrahisishia kazi Mtanzania, hasa wanawake. Ni vyema kukaribisha teknolojia ya kuwasaidia wanawake waondokane na kufanya kazi ngumu ngumu zinazoweza kuwapotezea wakati na kuathiri afya zao, kama vile kutwanga au kusaga nafaka, kubeba mizigo ya kuni, maji na mtoto mgongoni. Si vyema kwa jamii yetu kuingia katika karne ya ishirini na moja katika hali hiyo. Ndio maana kule Zanzibar tulamua kuruhusu biashara ndogo ndogo kuendeshwa na mwanachama wa CCM kwa manufaa yao na ya jamii.

Ndugu Wazee, haya kwa muhtasari ndio yaliyoamuliwa Zanzibar. Haya kamwe hayabomoi Azimio la Arusha, badala yake yanaliimarisha. Azimio la Arusha ni msingi wa siasa yatu ya ujamaa na Kujitegemea. Ili tuweze kujitegemea lazima tuandae mbinu na mikakati ya kuzalisha maji, huduma na chakula. Hili ndio lengo la maamuzi ya Zanzibar.

Mshairi mmoja amesema:-

"Kutaraji uongofu bila kupitia njia zake ni kama kulitaka
jahazi kutembea nchi kavu"

Ndugu Wazee Ahsanteni sana. (Makofi).
 
huyu bashiru ni aina ile ya wasomi wa hovyo.wanaangalia tumbo badala ya uwezo ulio ndani yake.
 
Sasa pamoja na kurekebisha kote huko mbna sisi ni maskini sana.

Ila aliyesababisha yote haya ni Nyerere na falsafa zake za kufikirika. Ujamaa na umasikini haviachani. Hua najiuliza kwamba jiwe anasema tunaenda kuwa donor country na kutoa misaada sasa swali je ataweza kama Kikwete alishindwa na sera yake ya Maisha bora kwa kila mtanzania mpaka kuwa donor country. Viwanda havionekani tunadanganywa na karakana ya kutengeneza chaki anyway wacha twende tuu Mungu saidia.

Jiwe anadhani kuendesha nchi ni rahisi kama anavyowaendesha watoto wake pole sana maana unaweza kuwaambia leo tunakula makande na wakatii
 
Hii hotuba ni Master piece, ni Classic kwa kweli.
Azimio la Zanzibar lilikuwa ni mkasi wa kukatilia mbali baadhi ya sera zisizo na kichwa wala miguu za Azimio la Arusha!.

Ukiisoma hotuba hii imejaa logic na umakini na leadership ya hali ya juu

Asante sana Mzee Mwinyi kwa uamuzi wa Ujasiri wa kuvunjilia mbali baadhi ya itikadi za azimio la Arusha!, Zilikuwa ni itikadi za kimasikini haswaa!

Bashiru anaishi katika nadharia, Bila azimio la Zanzibar sasa hivi tungekuwa hohehahe zaidi ya tulivyo
 
Azimio la Arusha limegawanyika sehemu kuu mbili
1. Uchumi
2.Maadili ya uongozi
Hukutakiwa kukariri hotuba yote, bali ulitakiwa uchambue kati ya hivyo vitu viwili nini kilifeli na kwanini
 
Kama kweli hilo Azimio lilobana hivyp bora tu lilifutiliwa mbali.
Tungekuwa maskini wa kufa.
Asante Mwinyi
Azimio la Arusha limegawanyika sehemu kuu mbili
1. Uchumi
2.Maadili ya uongozi
Hukutakiwa kukariri hotuba yote, bali ulitakiwa uchambue kati ya hivyo vitu viwili nini kilifeli na kwanini
 
Hii hotuba ni Master piece, ni Classic kwa kweli.
Azimio la Zanzibar lilikuwa ni mkasi wa kukatilia mbali baadhi ya sera zisizo na kichwa wala miguu za Azimio la Arusha!.

Ukiisoma hotuba hii imejaa logic na umakini na leadership ya hali ya juu

Asante sana Mzee Mwinyi kwa uamuzi wa Ujasiri wa kuvunjilia mbali baadhi ya itikadi za azimio la Arusha!, Zilikuwa ni itikadi za kimasikini haswaa!

Bashiru anaishi katika nadharia, Bila azimio la Zanzibar sasa hivi tungekuwa hohehahe zaidi ya tulivyo
Kama ilivyoada Azimio la Arusha limekuwa likipitiwa na kurekebishwa ili liende na wakati huo au kutatua tatizo mahususi. Ndicho atakachofanya Dr Bashiru. Baada ya marekebisho ya Zanzibar ni wazi kuna mengi mazuri pia zipo dosari ndogo zimejitokeza. Hivyo ni vyema muongozo ukatoka
 
Nchi hii kwangu mimi huyu ndiyo aliipandisha Tz kiuchumi.
 
Uyu mzee alikua kichwa Sana

"Ili tujitoe, kitaifa, kwenye shimo la utegemezi tulimo hivi sasa, mbinu bora ni kutoa uhuru kwa kila mwananchi wa kila Kaya, wa kila Kata, wa kila Tarafa, wa kila Wilaya na wa kila Mkoa kutumia nguvu zake zote katika kuzalisha. Matokeo ya hatua hii ni kumwezesha kila mtu katika Kaya, Kata, Tarafa, Wilaya na Mkoa kujigemea. Tukifika hapo ndipo Taifa litapokuwa limeondokana na hali ya sasa ya uchumi tegemezi"

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Hakika alilibadilisha taifa pakubwa sana.Maana wakusanya kodi karibu wote ukianza na Mkapa,walipata kiki kwa kupitia mgongo wa mzee Mwinyi.
 
Similar Discussions

Back
Top Bottom