KISA CHA BABA-ABDALLA KIPOFU
“EWE, Jemadari wa Uaminifu, mimi nilizaliwa Baghdadi, nami niliachwa yatima wakati nilipokuwa mtoto mdogo sana, maana wazazi wangu wote wawili walikufa. Basi nikarithi mali kidogo niliyoifanyia biashara kutwa kucha ili nipate kuiongeza, hata mwisho nikajiona nimepata ngamia themanini. Hawa niliwaajirisha kwa wafanyaji biashara waliokuwa wakisafirisafiri, ambao nilikuwa nikiandamana nao katika safari zao nyingi, na kila mara nilikuwa nikirudi na faida kubwa.
Hata siku moja mchana nilipokuwa nikirudi kutoka Basra, nimechukua bidhaa nilizokusudia kupeleka Bara Hindi, nikaja nikatua mahali pa pweke nilipopaona pana malisho mazuri kwa ngamia wangu, nami mwenyewe nikakaa chini ya mti kupumzika. Mara nikitazama nikamwona walii aendaye Basra kwa miguu amekaa kitako karibu yangu anapumzika, nikamwuliza anakotoka na wapi anakokwenda; mara pale tukasuhubiana. Na baada ya kuulizana habari kama desturi, tukatoa chakula tulichokuwa nacho tukala.
Tulipokuwa tukila, yule walii alitukia kutaja mahali palipofichwa mali ambapo hapakuwa mbali sana na pale tulipokaa, akanena, ‘Hata kama ngamia wako themanini wangepakiwa barabara hata wasiweze kuchukua zaidi, ile mali iliyofichwa huko ingeonekana nyingi vile vile kama haikupnguzwa.’
Kusika habari hii nikawa na furaha sana kwa tamaa, nikamtupia mikono yangu shingoni mwake kumkumbatia, nikinena: ‘Ewe walii mwema, nasadikisha kuwa mali ya dunia hii si kitu kwako, na kwa hivyo yakufalia nini kujua mali hiyo ilipo? Kwa wewe pekeo njiani kiasi waweza kuzichukua kiganja tele. Lakini niambie mimi zilipo, niende nikawapakie ngamia wangu themanini, na mmoja wao nitakupa wewe kuwa dalili ya shukrani zangu.’
Ama kwa kweli ile kiasi nilichokisia kumpa hakikuwa kikubwa sana, lakini kwangu mimi niliona kikubwa mno, maana kwa choyo na tamaa iliyoniingia moyoni, nikaona kuwa ngamia sabini na tisa watakaonibakia hawatakuwa sawa kama wakilinganishwa na yule mmoja.
Walii aliyaona waziwazi mawazo yaliyokuwa yakinipitia moyoni
Mwangu, lakini yeye hakunibainishia jinsi nia yangu ilivyo. Ila alijibu taratibu, ‘Ndugu yangu, wajua sana kama nijuavyo mimi, kuwa kufanya hivyo si haki. Maana hapo mahali nilionyeshwa mimi tu kusudi nizuie siri, na hiyo mali iwe yangu mwenyewe. Lakini maadam nimekuambia jinsi ilivyo yaonyesha kuwa nilikuwa na matumaini nawe, na hivyo nataraji kupata shukrani zako daima, kwa kukufanya wewe uwe na malı kama mimi.
Lakini, kabla sijakufunulia siri ya mali hizo, huna budi uape, kuwa baada ya kwisha kuwapakia hao ngamia wako kwa kadiri wanavyoweza kuchukua, na mimi utanipa nusu, kisha kila mmoja ashike njia yake. Nadhani hivi ni vizuri, kwani kama ukinipa ngamia arubaini, na mimi kwa upande wangu nitakuonyesha njia ya kununulia elfu wengine.’
Sikuweza kukanusha maneno yake, maana yale aliyoyasema yule walii ndiyo sawa hasa, lakini pamoja na hayo, lile wazo la kuwa yule walii atakuwa tajiri kama mimi lilikuwa halistahimiliki. Mradi nikaona hapana haja ya kubishana au kuililia hasara ya mali nyingi hiyo mpaka mwisho wa maisha yangu, ndipo nikakubali masharti yake.
Basi nikawakusanya ngamia wangu tukaenda pamoja na walii. Baada ya hatua kidogo, tukafika mahali palipokuwa kama bonde; lakini kijia cha kuingilia hapo kilikuwa chembamba mno hata ngamia wangu hawakuweza kupita wote pamoja ila mmoja mmoja. Lile bonde dogo au pale palipokuwa na nafasi wazi, palizibwa na milima miwili, na kwa kila upande kulikuwa na majabali yaliyosimama sawasawa wala hayapandiki.
Hata tulipokuwa hasa katikati ya milima hiyo, yule walii akasimama. Akaniambia, ‘Wakalishe chini ngamia wako hapa palipo na nafasi, ili tuweze kuwapakia kwa urahisi, kisha wewe na mimi tutakwenda huko kuliko na mali.’
Basi nikafanya kama nilivyoambiwa, na kisha nikamrudia walii, niliyemwona akijaribu kupekecha moto kwa vijiti vikavu.Hata moto ulipowaka, akatwaa konzi tele ya uvumba akatia motoni huku akinuizia maneno ambayo sikuyafahamu, na mara pale pale moshi mnene ukapanda juu hewani, naye akawa anautandua moshi pande mbili, ndipo halafu nikaona jabali lililosimama kama nguzo kati ya milima miwili, likafunguka taratibu, na jumba zuri kama nini likaonekana ndani yake.
Lakini, Ewe Jemadari wa Uaminifu, ile tamaa ya dhahabu ilinishuka sana hata nisiweze kujizuia kutazama mali jinsi ilivyo, ila nikaivamia chungu ya kwanza ya dhahabu iliyokuwa karibu nami, nikitia ndani ya kanda nililokuwa nalo. Na yule walii naye akaingia kazini vile vile, lakini mara nikaona kuwa yeye hakushughulika na dhahabu ila alishughulika kukusanya vito tu, basi na mimi nikaona ni afadhali nimwige afanyavyo. Mwisho wake wale ngamia tuliwapakia sana kadiri walivyoweza kuchukua, sasa ikawa hakuna jambo lililobakia ila kufunga ile hazina, twende zetu.
Lakini kabla hatujaifunga, yule walii akaenda kwenye dawati kubwa la dhahabu lililokuwa limenakshiwa vizuri, akalifungua na kutoa kisanduku kidogo cha mbao akakifutika kibindoni mwake; nilipomwuliza kina nini, akaniambia kuwa kina mafuta ya namna ya pekee. Halafu yake akapekecha tena moto, na kutwaa konzi ya uvumba akatia motoni na huku akinuizia maneno ambayo sikuyafahamu, na mara pale pale jabali likafungika, pakawa kama zamani.
Jambo la pili lilikuwa la kugawanya ngamia pamoja na mali yao, basi tulipokwisha gawanya kila mtu akawa anachunga mwenyewe wanyama wake, tukatoka bondeni. Hata tulipotokea njia kuu kwa mahali palipokuwa na njia panda tukaagana kwa kukumbatiana kwa mapenzi huku nikimpa shukrani zangu kwa ukarimu aliyonifanyia, kwa kunigawia mali nyingi kama ile. Nami nilimuaga kwa wema, kisha tukapeana migongo na kila mmoja akakimbilia ngamia wake, yeye akashika njia yake kuelekea Basra na mimi kuelekea Baghdadi.
Kusema kweli, mimi nilifika kwa shida kwenye ngamia wangu jinsi shetani mbaya alivyonikalia moyoni, hata nikasema binafsi, ‘Mtu aliye walii, mali kama ile aitakia nini? Yeye pekee ndiye aaminiwaye na hazina ile, na siku zote aweza kwenda kuchukua nyingi kwa kadiri aitakayo.’ Basi kuisha kusema hivi, mara nikasimamisha ngamia wangu kando ya njia, nikarudi mbio kumfuatia.
Nilikuwa hodari sana wa kupiga mbio, na hivyo sikukawia kukutana naye. Nilimwita, nikinena, ‘Ndugu yangu, wakati tulipokuwa tukiagana mara nilijiwa na mawazo ambayo labda ni mageni nawe, Na hasa kwa kazi yako, wewe u walii unayeishi maisha ya utulivu, wala hutamani kitu cho chote cha dunia hii ila kufanya mema tu. Na sasa naona umesahau kuwa wajitweka mwenyewe mzigo kwa kujikusanyia mali nyingi kama hiyo, na baada ya hivyo, kwa kusema kweli, hakuna mtu ambaye tangu kuzaliwa kwake hajapata kuzoeana na ngamia, akaweza kuchunga wanyama wakaidi kama hawa. Basi kama u mwenye akili, hutapendelea kujidhili nafsi yako kwa taabu za ngamia zaidi ya thelathini, nawe utaona mwenyewe kuwa taabu na mashaka yatakayokukuta kwa hao thelathini tu, yatosha.
Yule walii, ambaye alinifahamu sana, akajibu kwa upole maana hakupenda tubishane, ‘Hayo usemayo ni kweli, lakini mimi hapo kwanza sikufikiri hayo, na sasa ikiwa ni hivyo, chagua kumi uwapendao uchukue.’
Basi nikachagua ngamia kumi walio wazuri nikaenda nao, ili nikawachanganye pamoja na wale niliowaacha nyuma kule njiani. Sasa nikawa najisifu kimoyomoyo: ‘Nimepata niliyoyataka, lakini yule walii alikuwa rahisi sana kushika maneno. Kwa nini nisimtake kumi zaidi. Mara nikageuka nyuma kumtazama. Kumwona hajafika mbali sana, nikarudi kumfuatia.
Hata nilipoona namkaribia nikamwita, ‘Ndugu yangu -e-e! Mara naye akageuka, akasimama kuningojea. Nikamwambia, ‘Sipendi kuachana nawe kabla sijakuambia jambo moja ambalo naona hulifahamu vema. Kuchunga ngamia kunahitaji maarita makubwa, hasa kwa mtu ye yote anayekusudia kufuga kundi la ngamia thelathini. Na kwa faida yako mwenyewe, nina yakini kuwa utapendezewa mno, iwapo utaniamini na ngamia kumi wengine, maana kwa ustadi wangu nilionao kama nikiwa na ngamia wawili au mia mbili, kwangu mamoja.’
Basi ikawa vile vile kama zamani, yule walii hakufanya matata nami nikachukua ngamia kumi wengine nikaenda nao kwa furaha, nikamwachia ishirini tu, wawe sehemu yake. Sasa nikawa nimepata ngamia sitini, na hivyo mtu ye yote aweza kufikiri kuwa nimeridhika.
Lakini, ewe Jemadari wa Uaminifu, kuna methali inenayo: Zaidi mtu apatavyo, ndivyo zaidi atamanivyo; basi na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwangu. Sikuweza kuridhika kabisa kuona ngamia mmoja akibakia kwa walii, ndipo nikamrudia kuzidi kumwomba na kumshika miguu, na kumwahidi shukrani za milele, mpaka wale ngamia ishirini wa mwisho aliokuwa nao wakaingia mikononi mwangu.
Walii akasema, ‘Ndugu yangu, wachukue wakakufae. Lakiní kumbuka kwamba mara moja mali huweza kuruka; mfano kama vile isemwavyo: Mtaka yote kwa pupa hukosa yote.’
Macho yangu yalifumba nikawa kipofu kwa dhahabu, na masikio yaliniziba nikawa kiziwi hata sikusikiliza kamwe shauri lake la maarifa, ila nikawa nikitazama tazama huku na huku kufikiri nimtake kitu gani kingine.
Mara kwa ghafla nikakikumbuka kile kisanduku kidogo cha mafuta alichokifutika kibindoni mwake, ambacho nilikidhania kuwa kina mali ya thamani zaidi ya ile nyingine yote. Basi nikamshika miguu mara ya mwisho, na kumwuliza, ‘Wenda kifanyaje kile kisanduku kidogo cha mafuta? Ama naona vigumu kukichukua wewe; labda na hicho nacho utapenda kuniachia mimi vile vile. Hasa, kwa kusema kweli, walii aliyeacha mambo ya dunia hana haja na mafuta!’
Aa, laiti kama angenikatalia haja yangu! Nhu, lakini alijua mambo. Ehe kama angalikataa? Ningalikichukua kwa nguvu, maana hivyo ndivyo nilivyokuwa nimeazimia. Lakini hakukataa, pale pale akakitoa akanipa kwa kusema nami kwa wema, akinena, ‘Chukua rafiki yangu, na kama kuna kitu kingine niwezacho kukutendea, lazima uniambie.
Basi kile kisanduku kilipokwisha kuwa mikononi mwangu nikakifunua kifuniko. Kisha nikamwambia, ‘Maadam wewe u mtu mwema namna hii, tafadhali nakuomba uniambie faida ya mafuta haya.
Walii akanena, ‘Ni mafuta ya ajabu sana sana. Kama ukitwaa kidogo na kujipaka katika jicho lako la kushoto, saa ile ile utaona hazina zote zilizofichwa chini ya ardhi. Lakini tahadhari usije ukaligusa na mafuta jicho lako la kulia, au kuona kwako kutapotea milele.
Maneno yake yalinitia tamaa kubwa, nikamwambia, ‘Twaa unijaribie nakusihi, kwani wewe utajua vema zaidi kuliko mimi, namna ya kupaka kwake.’ Ama moyo wangu ulifanya hamu sana kujaribu uzuri wake, na hivyo nikatoa kisanduku cha mafuta nikampa.
Walii alipokwisha kipokea kile kisanduku akaniambia nifumbue jicho langu la kushoto, naye akalipaka mafuta taratibu. Hata nilipolifumbua tena nikaona mali za kila namna zisizo hesabu zimetandazika, kama zilizo mbele yangu. Lakini wakati huo wote lile jicho langu la kulia nilikuwa nimelifumba, nalo sasa lilikuwa limechoka sana kwa kufumbwa. Basi ndipo nilipomsihi huyo walii kulipaka mafuta na jicho lile pia.