Alfu lela ulela, kitabu cha nne

Lycaon pictus

JF-Expert Member
Jan 31, 2021
7,206
12,702
Nitaweka hapa hadithi zote, kutoka vitabu vyote(vinne ) vya Alfu lela ulela. Fuatana nami kwenye safari hii ndefu. Pia vyote unaweza kuvisoma bure ndani ya maktaba app.

Tuanze na kitabu cha nne.

New Doc 2022-01-11 064029(2)_46.jpg


MAZUNGUMZO YA ALFU LELA ULELA

AU


SIKU ELFU NA MOJA



KIMEFASIRIWA KWA KISWAHILI NA

EDWIN W. BRENN







KITABU CHA NNE


YALIYOMO

Utangulizi

Kisa cha Baba-Abdalla kipofu

Kisa cha Sidi-Nouman

Kisa cha Ali Kogia, Mfanyi biashara wa Baghdadi

Farasi wa uchawi

Kisa cha ndugu wawili wanawake waliomwonea kijicho dada yao mdogo


UTANGULIZI





HADITHI zinazohadithiwa, zimekuwa kama zile zinazotolewa na wazee wanawake wa nchi mbali mbali wakiwahadithia wajukuu zao. Hapana mtu anayejua ni za tangu lini, au ni nani aliyezitoa kwanza. Labda watoto wa Ham, na Shem, na Japhet (Jaffari) walizisikia katika Safina, siku za Gharika!

Watu wa nchi zingine huzihadithia kwa njia mbali mbali lakini

hadithi ni zile zile moja, hata kwa watoto wadogo wa Kizulu walio Cape, au kwa watoto wadogo wa Kieskimo walio pwani ya kaskazini mwa nchi ya Amerika. Kubadilika huku kumetokea kwa ajili ya tabia na desturi za nchi, kama vile kuvaa au kutovaa nguo.

Katika hiadithi hizi mna wafalme wengi na malkia wengi, kwa sababu hapo zamani kulikuwa na wafalme wengi katika nchi, na yule mtu ambaye sasa ana heshima kwa watu, hapo zamani za kale alikuwa namna ya mfalme. Hadithi hizi za kale haziwezi kusahauliwa kabisa kwa maana ziliandikwa kwa miaka mbali mbali, lakini nyingi ni za karne hii ya sassa ambazo ziliandikwa kwa lugha za kila namna.

Hadithi hizi za "Alfu-lela-ulela," ambazo zingine, ingawa si zote, zimo katika kitabu hiki, ni hadithi za Mashariki. Wahindi na Waarabu na Waajemi, huzitoa kwa namna zao wenyewe, Lakini si kwa watoto, ila kwa watu wazima. Ni kweli kuwa hapo zamani kulikuwa hakuna vitabu vya hadithi, wala vitabu vilivyopigwa chapa, lakini kulikuwa na watu maalum ambao kazi zao zilikuwa ni kuwafurahisha wanawake na wanaume kwa kuwatolea hadithi, nao walikuwa wakiwatolea hadithi kwa kuwasifia vema Waislamu wanaokaa Baghdadi au Bara ya Hindi. Na mara kwa mara hudhaniwa kuwa mambo hayo yote yalitokea zamani za enzi ya Khalifa Mkuu, au Mtawala wa Uaminifu, Harun Rashid, aliyekaa Baghdadi tangu mwaka 786 hata 808, na huyo waziri wake aliyekuwa akia- ndamana naye vile vile alikuwa mtu wa kweli, katika ukoo mkubwa wa Mabamiside. Naye aliuawa na Khalifa kwa ukatili sana, wala hapana mtu ajuaye sababu yake. Katika kulikumbuka deni la mapenzi niliokopeshwa ambalo siwczi kulilipa nafurahi kumsheheneza shukurani za kweli Bwana A. A. M. Isherwood, O.B.E., M.A., Deputy Director of Education Bwana F. Johnson, Esq., Chairman of Publication Committee na mabwana wengine wote walio wanachama wa Publication Committee, na mwenyewe Bwana S. Rivers-Smith, C.B.E, M.A., The Hon'ble the Director of Education, kwa jinsi walivyokuwa radhi kunisaidia kwa mapenzi, katika kukisifia kitabu hiki changu hata kikapatikana kupigwa chapa.

Na hivi natumaini kwamba wasomaji wote watakaokipenda

kitabu hiki, wataungana nami katika kulishuhudia deni langu.



E. W. BRENN​

DAR ES SALAAM,

1st January, 1928.
 
KISA CHA BABA-ABDALLA KIPOFU​





“EWE, Jemadari wa Uaminifu, mimi nilizaliwa Baghdadi, nami niliachwa yatima wakati nilipokuwa mtoto mdogo sana, maana wazazi wangu wote wawili walikufa. Basi nikarithi mali kidogo niliyoifanyia biashara kutwa kucha ili nipate kuiongeza, hata mwisho nikajiona nimepata ngamia themanini. Hawa niliwaajirisha kwa wafanyaji biashara waliokuwa wakisafirisafiri, ambao nilikuwa nikiandamana nao katika safari zao nyingi, na kila mara nilikuwa nikirudi na faida kubwa.

Hata siku moja mchana nilipokuwa nikirudi kutoka Basra, nimechukua bidhaa nilizokusudia kupeleka Bara Hindi, nikaja nikatua mahali pa pweke nilipopaona pana malisho mazuri kwa ngamia wangu, nami mwenyewe nikakaa chini ya mti kupumzika. Mara nikitazama nikamwona walii aendaye Basra kwa miguu amekaa kitako karibu yangu anapumzika, nikamwuliza anakotoka na wapi anakokwenda; mara pale tukasuhubiana. Na baada ya kuulizana habari kama desturi, tukatoa chakula tulichokuwa nacho tukala.

Tulipokuwa tukila, yule walii alitukia kutaja mahali palipofichwa mali ambapo hapakuwa mbali sana na pale tulipokaa, akanena, ‘Hata kama ngamia wako themanini wangepakiwa barabara hata wasiweze kuchukua zaidi, ile mali iliyofichwa huko ingeonekana nyingi vile vile kama haikupnguzwa.’

Kusika habari hii nikawa na furaha sana kwa tamaa, nikamtupia mikono yangu shingoni mwake kumkumbatia, nikinena: ‘Ewe walii mwema, nasadikisha kuwa mali ya dunia hii si kitu kwako, na kwa hivyo yakufalia nini kujua mali hiyo ilipo? Kwa wewe pekeo njiani kiasi waweza kuzichukua kiganja tele. Lakini niambie mimi zilipo, niende nikawapakie ngamia wangu themanini, na mmoja wao nitakupa wewe kuwa dalili ya shukrani zangu.’

Ama kwa kweli ile kiasi nilichokisia kumpa hakikuwa kikubwa sana, lakini kwangu mimi niliona kikubwa mno, maana kwa choyo na tamaa iliyoniingia moyoni, nikaona kuwa ngamia sabini na tisa watakaonibakia hawatakuwa sawa kama wakilinganishwa na yule mmoja.

Walii aliyaona waziwazi mawazo yaliyokuwa yakinipitia moyoni

Mwangu, lakini yeye hakunibainishia jinsi nia yangu ilivyo. Ila alijibu taratibu, ‘Ndugu yangu, wajua sana kama nijuavyo mimi, kuwa kufanya hivyo si haki. Maana hapo mahali nilionyeshwa mimi tu kusudi nizuie siri, na hiyo mali iwe yangu mwenyewe. Lakini maadam nimekuambia jinsi ilivyo yaonyesha kuwa nilikuwa na matumaini nawe, na hivyo nataraji kupata shukrani zako daima, kwa kukufanya wewe uwe na malı kama mimi.

Lakini, kabla sijakufunulia siri ya mali hizo, huna budi uape, kuwa baada ya kwisha kuwapakia hao ngamia wako kwa kadiri wanavyoweza kuchukua, na mimi utanipa nusu, kisha kila mmoja ashike njia yake. Nadhani hivi ni vizuri, kwani kama ukinipa ngamia arubaini, na mimi kwa upande wangu nitakuonyesha njia ya kununulia elfu wengine.’

Sikuweza kukanusha maneno yake, maana yale aliyoyasema yule walii ndiyo sawa hasa, lakini pamoja na hayo, lile wazo la kuwa yule walii atakuwa tajiri kama mimi lilikuwa halistahimiliki. Mradi nikaona hapana haja ya kubishana au kuililia hasara ya mali nyingi hiyo mpaka mwisho wa maisha yangu, ndipo nikakubali masharti yake.

Basi nikawakusanya ngamia wangu tukaenda pamoja na walii. Baada ya hatua kidogo, tukafika mahali palipokuwa kama bonde; lakini kijia cha kuingilia hapo kilikuwa chembamba mno hata ngamia wangu hawakuweza kupita wote pamoja ila mmoja mmoja. Lile bonde dogo au pale palipokuwa na nafasi wazi, palizibwa na milima miwili, na kwa kila upande kulikuwa na majabali yaliyosimama sawasawa wala hayapandiki.

Hata tulipokuwa hasa katikati ya milima hiyo, yule walii akasimama. Akaniambia, ‘Wakalishe chini ngamia wako hapa palipo na nafasi, ili tuweze kuwapakia kwa urahisi, kisha wewe na mimi tutakwenda huko kuliko na mali.’

Basi nikafanya kama nilivyoambiwa, na kisha nikamrudia walii, niliyemwona akijaribu kupekecha moto kwa vijiti vikavu.Hata moto ulipowaka, akatwaa konzi tele ya uvumba akatia motoni huku akinuizia maneno ambayo sikuyafahamu, na mara pale pale moshi mnene ukapanda juu hewani, naye akawa anautandua moshi pande mbili, ndipo halafu nikaona jabali lililosimama kama nguzo kati ya milima miwili, likafunguka taratibu, na jumba zuri kama nini likaonekana ndani yake.

Lakini, Ewe Jemadari wa Uaminifu, ile tamaa ya dhahabu ilinishuka sana hata nisiweze kujizuia kutazama mali jinsi ilivyo, ila nikaivamia chungu ya kwanza ya dhahabu iliyokuwa karibu nami, nikitia ndani ya kanda nililokuwa nalo. Na yule walii naye akaingia kazini vile vile, lakini mara nikaona kuwa yeye hakushughulika na dhahabu ila alishughulika kukusanya vito tu, basi na mimi nikaona ni afadhali nimwige afanyavyo. Mwisho wake wale ngamia tuliwapakia sana kadiri walivyoweza kuchukua, sasa ikawa hakuna jambo lililobakia ila kufunga ile hazina, twende zetu.

Lakini kabla hatujaifunga, yule walii akaenda kwenye dawati kubwa la dhahabu lililokuwa limenakshiwa vizuri, akalifungua na kutoa kisanduku kidogo cha mbao akakifutika kibindoni mwake; nilipomwuliza kina nini, akaniambia kuwa kina mafuta ya namna ya pekee. Halafu yake akapekecha tena moto, na kutwaa konzi ya uvumba akatia motoni na huku akinuizia maneno ambayo sikuyafahamu, na mara pale pale jabali likafungika, pakawa kama zamani.

Jambo la pili lilikuwa la kugawanya ngamia pamoja na mali yao, basi tulipokwisha gawanya kila mtu akawa anachunga mwenyewe wanyama wake, tukatoka bondeni. Hata tulipotokea njia kuu kwa mahali palipokuwa na njia panda tukaagana kwa kukumbatiana kwa mapenzi huku nikimpa shukrani zangu kwa ukarimu aliyonifanyia, kwa kunigawia mali nyingi kama ile. Nami nilimuaga kwa wema, kisha tukapeana migongo na kila mmoja akakimbilia ngamia wake, yeye akashika njia yake kuelekea Basra na mimi kuelekea Baghdadi.

Kusema kweli, mimi nilifika kwa shida kwenye ngamia wangu jinsi shetani mbaya alivyonikalia moyoni, hata nikasema binafsi, ‘Mtu aliye walii, mali kama ile aitakia nini? Yeye pekee ndiye aaminiwaye na hazina ile, na siku zote aweza kwenda kuchukua nyingi kwa kadiri aitakayo.’ Basi kuisha kusema hivi, mara nikasimamisha ngamia wangu kando ya njia, nikarudi mbio kumfuatia.

Nilikuwa hodari sana wa kupiga mbio, na hivyo sikukawia kukutana naye. Nilimwita, nikinena, ‘Ndugu yangu, wakati tulipokuwa tukiagana mara nilijiwa na mawazo ambayo labda ni mageni nawe, Na hasa kwa kazi yako, wewe u walii unayeishi maisha ya utulivu, wala hutamani kitu cho chote cha dunia hii ila kufanya mema tu. Na sasa naona umesahau kuwa wajitweka mwenyewe mzigo kwa kujikusanyia mali nyingi kama hiyo, na baada ya hivyo, kwa kusema kweli, hakuna mtu ambaye tangu kuzaliwa kwake hajapata kuzoeana na ngamia, akaweza kuchunga wanyama wakaidi kama hawa. Basi kama u mwenye akili, hutapendelea kujidhili nafsi yako kwa taabu za ngamia zaidi ya thelathini, nawe utaona mwenyewe kuwa taabu na mashaka yatakayokukuta kwa hao thelathini tu, yatosha.

Yule walii, ambaye alinifahamu sana, akajibu kwa upole maana hakupenda tubishane, ‘Hayo usemayo ni kweli, lakini mimi hapo kwanza sikufikiri hayo, na sasa ikiwa ni hivyo, chagua kumi uwapendao uchukue.’

Basi nikachagua ngamia kumi walio wazuri nikaenda nao, ili nikawachanganye pamoja na wale niliowaacha nyuma kule njiani. Sasa nikawa najisifu kimoyomoyo: ‘Nimepata niliyoyataka, lakini yule walii alikuwa rahisi sana kushika maneno. Kwa nini nisimtake kumi zaidi. Mara nikageuka nyuma kumtazama. Kumwona hajafika mbali sana, nikarudi kumfuatia.

Hata nilipoona namkaribia nikamwita, ‘Ndugu yangu -e-e! Mara naye akageuka, akasimama kuningojea. Nikamwambia, ‘Sipendi kuachana nawe kabla sijakuambia jambo moja ambalo naona hulifahamu vema. Kuchunga ngamia kunahitaji maarita makubwa, hasa kwa mtu ye yote anayekusudia kufuga kundi la ngamia thelathini. Na kwa faida yako mwenyewe, nina yakini kuwa utapendezewa mno, iwapo utaniamini na ngamia kumi wengine, maana kwa ustadi wangu nilionao kama nikiwa na ngamia wawili au mia mbili, kwangu mamoja.’

Basi ikawa vile vile kama zamani, yule walii hakufanya matata nami nikachukua ngamia kumi wengine nikaenda nao kwa furaha, nikamwachia ishirini tu, wawe sehemu yake. Sasa nikawa nimepata ngamia sitini, na hivyo mtu ye yote aweza kufikiri kuwa nimeridhika.

Lakini, ewe Jemadari wa Uaminifu, kuna methali inenayo: Zaidi mtu apatavyo, ndivyo zaidi atamanivyo; basi na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwangu. Sikuweza kuridhika kabisa kuona ngamia mmoja akibakia kwa walii, ndipo nikamrudia kuzidi kumwomba na kumshika miguu, na kumwahidi shukrani za milele, mpaka wale ngamia ishirini wa mwisho aliokuwa nao wakaingia mikononi mwangu.

Walii akasema, ‘Ndugu yangu, wachukue wakakufae. Lakiní kumbuka kwamba mara moja mali huweza kuruka; mfano kama vile isemwavyo: Mtaka yote kwa pupa hukosa yote.’

Macho yangu yalifumba nikawa kipofu kwa dhahabu, na masikio yaliniziba nikawa kiziwi hata sikusikiliza kamwe shauri lake la maarifa, ila nikawa nikitazama tazama huku na huku kufikiri nimtake kitu gani kingine.

Mara kwa ghafla nikakikumbuka kile kisanduku kidogo cha mafuta alichokifutika kibindoni mwake, ambacho nilikidhania kuwa kina mali ya thamani zaidi ya ile nyingine yote. Basi nikamshika miguu mara ya mwisho, na kumwuliza, ‘Wenda kifanyaje kile kisanduku kidogo cha mafuta? Ama naona vigumu kukichukua wewe; labda na hicho nacho utapenda kuniachia mimi vile vile. Hasa, kwa kusema kweli, walii aliyeacha mambo ya dunia hana haja na mafuta!’

Aa, laiti kama angenikatalia haja yangu! Nhu, lakini alijua mambo. Ehe kama angalikataa? Ningalikichukua kwa nguvu, maana hivyo ndivyo nilivyokuwa nimeazimia. Lakini hakukataa, pale pale akakitoa akanipa kwa kusema nami kwa wema, akinena, ‘Chukua rafiki yangu, na kama kuna kitu kingine niwezacho kukutendea, lazima uniambie.

Basi kile kisanduku kilipokwisha kuwa mikononi mwangu nikakifunua kifuniko. Kisha nikamwambia, ‘Maadam wewe u mtu mwema namna hii, tafadhali nakuomba uniambie faida ya mafuta haya.

Walii akanena, ‘Ni mafuta ya ajabu sana sana. Kama ukitwaa kidogo na kujipaka katika jicho lako la kushoto, saa ile ile utaona hazina zote zilizofichwa chini ya ardhi. Lakini tahadhari usije ukaligusa na mafuta jicho lako la kulia, au kuona kwako kutapotea milele.

Maneno yake yalinitia tamaa kubwa, nikamwambia, ‘Twaa unijaribie nakusihi, kwani wewe utajua vema zaidi kuliko mimi, namna ya kupaka kwake.’ Ama moyo wangu ulifanya hamu sana kujaribu uzuri wake, na hivyo nikatoa kisanduku cha mafuta nikampa.

Walii alipokwisha kipokea kile kisanduku akaniambia nifumbue jicho langu la kushoto, naye akalipaka mafuta taratibu. Hata nilipolifumbua tena nikaona mali za kila namna zisizo hesabu zimetandazika, kama zilizo mbele yangu. Lakini wakati huo wote lile jicho langu la kulia nilikuwa nimelifumba, nalo sasa lilikuwa limechoka sana kwa kufumbwa. Basi ndipo nilipomsihi huyo walii kulipaka mafuta na jicho lile pia.
 
Walii akanijibu akinena, ‘Ikiwa wanishurutisha kulipaka, nitalipaka, lakini kumbuka yale maneno niliyokuambia sasa hivi kama mafuta yakigusa jicho lako la kulia, utakuwa kipofu papa hapa.’

Mama we! Ijapokuwa mara nyingi nimesadikisha maneno yake, lakini sasa niliona waziwazi kuwa ananificha thamani na faida ya mafuta yale. Mradi nikazidi kujifanya kiziwi kwa yote aliyokuwa akiniambia.

Nikamjibu huku nikicheka, ‘Ndugu yangu, ama sasa naona wanifanyia dhihaka. Haiwezekani kabisa kwa mafuta yaya haya mamoja kuwa na vioja namna mbali mbali.’

Walii akajibu, ‘Ni kweli kuwa yote ni mamoja, lakini itakuwa vizuri kwako kama utasadiki maneno yangu.’

Lakini sikusadiki, kwani choyo na tamaa ya mali ilinishika, nikafikiri hivi: Ikiwa jicho moja laweza kunionyesha mali, hili la pili nalo pengine huenda likanifundisha namna ya kuyachukua.

Basi nikazidi kumshikilia walii anipake jicho langu la kulia, lakini yeye alikataa kata kata. Akasema, ‘Baada ya mimi kukuvika faida ya mali kana ile, siwezi kabisa kukutendea uovu kama huo. Fikiri kwanza, mtu kuwa kipofu ni nini, wala usinilazimishe kukufanyia jambo ambalo utajuta maisha yako.’

Nikamjibu kwa hasira, ‘Ewe ndugu yangu, ni kazi bure kusema nami sana, na hivi tafadhali nakusihi usiseme nami zaidi, ila fanya hivi nikuambiavyo. Najua kwa ukarimu wako mwingi umenitekelezea yote ninayoyataka, basi tafadhali usiyaharibu mawazo yangu niliyonayo kwako kwa jambo dogo kama hilo. Wacha yote yatakayokuwa yawe juu yangu mwenyewe, wala mimi sitakulaumu wewe kamwe!’

Walii akajibu kwa huzuni, ‘Maadam wajisalimisha na hayo sina haja ya kusema nawe tena, ndipo akatwaa mafuta na kunipaka kidogo katika jicho langu la kulia, ambalo nilikuwa nimelifumba. Hata nilipojaribu kulifumbua ikawa ni mawingu manene manene ya giza yanapita mbele yangu, na saa ile ile nikawa kipofu kama hivi unionavyo sasa! Nikapiga kelele nikalia, ‘Ole wangu masikini! Aa, kumbe kweli! Taamaa yangu ya dhahabu imenitupa ndani ya shimo gani

Hili lisilo na mwisho! Kwanza macho yangu yalikuwa yamefumba lakini sasa yamefumbuka kweli. Najua kwamba mashaka haya yote yasingalinipata ila sababu ni mimi mwenyewe! Lakini basi ewe ndugu yangu mwema, uliye mpole na mapenzi, unayejua siri kubwa kama hizi za kumfundisha mtu, huna hata kitu cha kunipa ambacho kitaweza kunirudishia kuona kwangu?

Walii akajibu, ‘Ewe mkiwa, si kosa langu mimi hata ukafikiliwa na hayo yaliyokupata, ila huko ni kuadhibiwa unakoadhibiwa kwani upofu wa moyo wako ndio uliosababisha upofu wa macho yako. Na hizo siri usemazo, ndiyo ninazo, kwani kwa muda huu mfupi tuliopata kujuana mimi nawe, umeziona. Lakini zile zinazoweza kukurudishia kuona kwako, sinazo. Umejidhihirisha mwenyewe kuwa mali uliyopewa haikuwa fani yako; na sasa imeingia mikononi mwangu, kisha nayo itawanufaisha wengine wasio na choyo na wenye shukrani kuliko wewe.’

Basi walii hakusema tena ila aliniacha pale pale njiani nimesimama sina la kusema kwa haya, naye akawakusanya wale ngamia themanini, na kushika njia yake kwenda Basra. Ilikuwa ni kazi bure kumsihi kwangu asiniache pale njiani, ila anichukue anipeleke karibu na njia ipitayo misafara. Mradi alijifanya kiziwi kwa maombi yangu na kilio changu, na kama kwa siku ya pili yake hawangalipita wafanyaji biashara walionihurumia na kunichukua kunirudisha Basra, ningalikufa upesi kwa njaa na taabu.

Nilikuwa tajiri, sasa nimekuwa masikini kwa dakika moja, na tangu hapo hata sasa naponea sadaka ninazopewa na watu. Basi kwa ajili ya kuulipa uovu wa tamaa ya mali, napendezewa kwamba kila mpita njia, anipige. ‘Basi hiki ndicho kisa changu ewe Jemadari wa Uaminifu.’

Basi yule kipofu alipokwisha kuhadithia kisa chake, Khalifa alimwambia, ‘Baba-Abdalla, kweli makosa yako ni makubwa sana, lakini na taabu inayokupata nayo si ndogo. Lakini sasa tubia kwa siri, nami nitaangalia upewe kila siku fedha za kukutosha kwa haja zako zote.’

Kwa maneno haya, Baba-Abdalla akajitupa miguuni pa Khalifa, na kumwombea dua awe na fahari na furaha milele.
 
KISA CHA SID-NOUMAN​





KHALIFA Harun-Rashid alipendezewa sana na hadithi ya kipofu na walii, hata ilipokwisha akamgeukia yule kijana mwanamume aliyekuwa akimwadhibisha farasi wake, na kumwuliza jina lake. Kijana akasema kuwa jina lake linaitwa Sidi-Nouman. Khalifa akamwambia, ‘Sidi-Nouman, ama katika umri wangu wote nimepata kuona farasi wengi walioumia, na hata mimi mwenyewe nimewaumiza wengi, lakini sijapata kuona farasi ye yote aliyeumizwa kwa ukali kama yule wako wa jana. Kila mtu aliyekuwako kuangalia alikuwa akiona uchungu, na kukulaumu sana. Na mimi mwenyewe nilikasirika mno hata nilikuwa karibu kujitambulisha ili upate kunijua ni nani, tena nikukomeshe papo hapo. Na hasa nikikutazama sana sikuoni kuwa una sura za ukatili, basi kwa hivi nitafurahi sana kama ukinisadikisha kuwa hukufanya yale bila kuwa na sababu.

Tena, maadam nimeambiwa kuwa ile si mara ya kwanza, na kweli kila siku waonekana ukimpiga farasi wako na kumchosha kwa vyuma mbavuni mwake, nataka kujua shina la mambo haya. Ila niambie kweli, usinifiche.

Sidi-Nouman kusikia maneno haya alisawijika, akawa na wasiwasi: mradi akajiona hana hila. Ndipo akajitupa kifudifudi mbele ya kiti cha Khalifa huku akijaribu kusema, lakini maneno yalimkwama kooni, akanyamaza. Khalifa kuona vile akatafuta njia ya kumwondoshea wasiwasi. Akamwambia, ‘Sidi-Nouman, usinichukulie mimi Khalifa, ila nichukulie rafiki yako anayependa kusikiliza habari zako. Na kama una neno unaloogopa kusema kwa kudhani kuwa litanikasirisha, vile vile sema usiogope, nami natangulia kukusamehe kabla, basi sema waziwazi kama vile unavyosema na mtu anayekupenda, wala usiogope kitu.’

Kwa hivi alivyosemezwa na Khalifa, mwisho wake Sidi-Nouman akaanza kuhadithia habari zake, akanena, ‘Ewe Jemadari wa Uaminifu, naona sifa kuwa mbele yako, na nitafanya kadiri niwezavyo kukukidhia haja yako. Ingawa mimi sijakamilika, lakini asili ya ukatili sina wala sipendi kabisa kuvunja sharia. Nakubali kuwa kitendo nilichomtendea farasi wangu si kizuri, tena kimemwadhibu bure bila ya sababu, na hivyo natumai kwamba sitahukumiwa kwa udhalimu, ila kwa kusikitikiwa sana.

Ewe Jemadari wa Uaminifu, sitajisumbua kwa kuhadithia habari za kuzaliwa kwangu, maana naona hazistahili ujue. Ila wazazi wangu walikuwa watu hodari sana kwa kazi, hata walipo kufa nikarithi fedha za kutosha kuishi maridhawa, ijapokuwa sikujulikana.

Kwa hivi nikawa na mali kidogo, lakini kitu nilichokuwa nikikitaka sana ilikuwa ni mke atakayeweza kunizidishia furaha yangu, lakini baraka hii sikujaliwa kuipata. Maana katika siku ile ile ya harusi, mke wangu alizijaribu subira zangu kwa kila njia iliyokuwa ni vigumu sana kuvumilia.

Kwa desturi ya nchi yetu ilitulazimu kuoa bila mtu kujua tabia za mke atakayekaa naye. Na kwa kadiri ya siku mkewe anazomchukiza, au kumkashifu, au hata kwamba ana ila yo yote, mtu alikuwa hana haki ya kunung’unika.

Siku ya kwanza niliyopata kumwona mke wangu amevua ushungi, ni pale alipoletwa nyumbani kwangu kwa desturi ya ndoa, nami nilifurahi sana kuona sikudanganywa katika zile siku zilizokuwa nikisifiwa uzuri wake. Basi nikaanza kwa moyo mkuu maisha ya kuwa na mke pamoja na matumaini ya furaha kamili.

Siku ya pili yake tukapakuliwa chakula kingi, na kwa vile ambavyo mke wangu hakutokea upesi mezani kuja kula, nikamtuma mtumishi kwenda kumwita. Lakini vile vile hakuja, na mimi nikamngojea kitambo kwa wasiwasi. Mwishowe akaja, ndipo tukakaa mezani na sahani za wali zikawekwa mbele yetu.

Mimi nikala wangu kwa kijiko kama ilivyo desturi yangu lakini nilistaajabu sana kumwona mke wangu badala ya kula kwa kijiko, akatoa kijaluba kidogo mfukoni mwake, akakifunua akatoa sindano moja ndefu, na hiyo sindano akawa anachomea punje za wali moja moja akila.

Nikamwuliza kwa kustaajabu, ‘Amina! Hii ndiyo namna unavyokula wali huko kwenu? Wafanya hivi kwa kuwa huna hamu ya chakula, au ulipenda kuhesabu punje za wali kusudi usipate kula zaidi ya hesabu fulani? Ikiwa wafanya kusudi ya kupunguza gharama, na kwa kutaka kunifundisha mimi ili nisiwe mharibifu, huna haja ya kuyafanya hayo, hatuingii hasara kamwe kwa njia hiyo, kwani mali yetu ni nyingi ya kutosheleza haja zetu, na kwa hivyo, mpenzi Amina, usitafute njia ya kujihini nafsi yako. Kula sana kama upendavyo, kama hivi ninavyokula mimi!

Kwa macho yangu ya mapenzi, nilitaraji kujibiwa majibu mema; lakini Amina hakusema kitu kabisa, ila aliendelea kudondoa punje za wali vile vile kama kwanza, tena kwa maringo mno. Kisha, badala ya kujaribu kula chakula cha sahani zingine, alikuwa mara kwa mara akiokota chembe za makombo ya mikate akila, ambayo yalikuwa hayafai hata kupewa paka.

Nikaona uchungu sana kwa ukaidi wake, lakini kwa kule kumwia radhi kwangu kama nilivyoweza, nikafikiri kuwa labda hakuzoea kula pamoja na wanaume, au pengine katika adabu alizofundishwa na jamaa zake ni kutokula mbele ya mumewe. Lakini kama ni hivyo angalikuwa amekataa kitambo kuja mbele yangu, na kama angalitaka kula pekee angalikwenda chumbani kwake mwenyewe. Mradi sikujali sana habari hii, hata nilipokwisha kula nikatoka chumbani kimya kimya hali nimekasirika sana kwa tabia yake ya ajabu.

Mtindo ule ule ukafanyika tena wakati wa kula chakula cha jioni, na siku ya pili yake, na kwa kila tunapokula pamoja. Na ilivyo yajulikana kuwa hakuna mwanamke awezaye kuishi kwa makombo ya mikate miwili au mitatu na punje kidogo za wali, nikataka kupeleleza namna anavyopata chakula, na wapi anakokipata. Basi nikawa sijishughulishi tena kwa jambo lo lote analofanya, kwa kutumai kwamba kidogo kidogo atanizoea na kuwa rafiki kwangu zaidi, Lakini ah! Masikini, haikupata kitambo nikaona tamaa yangu yote ni bure.

Siku moja usiku nilikuwa nimejinyosha kitandani na macho yangu nimeyafumba, na nilionekana kama niliyelala fo-fo-fo, ndipo Amina alipoondoka taratibu na kuvaa nguo zake pole pole bila kishindo hata kidogo. Sikuweza kukisia wapi alikusudia kwenda, lakini kwa kuwa wasiwasi wangu ulikuwa mwingi nikakusudia kumfuata. Hata alipokwisha vaa akatoka chumbani kwa kunyatanyata.

Basi mara alipofungua pazia na kutoka nami nikaondoka nikatwaa shuka yangu nikajitupia mabegani, nikavaa na viatu vyangu. Nikaenda kuchungulia dirisha la nyuma lenye wavu ambalo lilikuwa wazi, nikamwona yu katika kushughulika kupita mlango wa mbele, ambao kisha aliuacha wazi.

Siku hiyo ilikuwa na mbaamwezi, na hivyo ilikuwa ni rahisi kwangu kumwona akienda mpaka akaingia makaburini ambayo hayakuwa mbali na pale nyumbani. Basi nikatoka nikaenda kunyatanyata nikajificha kwenye kivuli cha ukuta nilipomwona mke wangu amefuatana na kundi la wachawi mmoja wa wale wachawi ni yule, kama unavyojua Seyid yangu anayezungukazunguka nchini na kufanya makao yake katika magofu ya nyumba, na kuwarukia yeye na wenzake ghafla wasafiri wasiotahadhari, wakawala nyama zao. Na kama wasipopata mtu huenda makaburini wakafukua maiti, wakala nyama zao.

Basi katika kumwona vile mke wangu amefuatana na lile kundi la wanawake wanaotisha, nikawa kama bubu kwa hofu. Wakaja wakapita karibu yangu bila kuniona, wakaanza kumfukua maiti aliyezikwa siku ile: kisha wakakaa kitako ukingoni mwa kaburi kula karamu yao ya kutisha, huku wakizungumza taratibu na kucheka wakati wote, na ingawa sikuwa mbali nao, lakini sikusikia waliyokuwa wakisema. Hata walipokwisha kula karamu yao, ile iliyobaki wakairudisha kaburini, na kufukia mchanga juu yake. Wakati ule wote mimi nilikuwa nimetulia kimya kuwatazama wala sikuwastusha hata kidogo. Nilirudi nyumbani kwangu upesi na kuacha ule mlango wazi vile vile kama nilivyoukuta. Halafu nikapanda kitandani, nikajifanya kama niliyelala fo-fo-fo.

Baadaye kidogo Amina akaingia chumbani kimya kimya kama vile alivyotoka. Akavua nguo zake akapanda kitandani kulala.

Baada ya kuona vile sikuweza kulala tena kwa mawazo, hata mwadhini alipoanza kuadhini kuwaita watu kwenda kusali, nikaondoka nikavaa nguo zangu kwenda msikitini. Lakini hata kule kusali nako hakukuweza kuniburudisha moyo wangu, wala sikuweza kumwangalia mke wangu kwa huzuni. Nilifikiri namna ya kufanya kwa yale mambo yake. Kwa hivyo asubuhi ile nikawa nazungukazunguka kutoka bustani hii kwenda bustani hii, huku nikigeuzageuza mashauri mbali mbali ya kumlazimisha mke wangu aache desturi zake zinazotisha. Nikafikiri kutumia nguvu ili kumfanya awache, lakini nikaona vigumu kutokuwa na huruma naye. Basi nikaona afadhali niwe mpole, kwani nilijua kwamba njia za upole mwisho wake huleta bahati ya kushinda, basi kwa hivi nikaburudika kidogo, nikawa narudi kualekea nyumbani, ambako nilifika wakati wa chakula.

Mara nilipofika, Amina akaamrisha chakula kiandaliwe, nasi tukakaa mezani kula pamoja, lakini yeye aliendelea na ile ile desturi yake ya kudondoadondoa punje kidogo za wali, na mimi nikakusudia kumwambia mara moja yale yaliyokuwa yakinielemea moyoni mwangu.
 
Nikasema naye taratibu kama nilivyoweza, Amina, naona ajabu kuwa tangu siku ya harusi yetu huli kitu cho chote ila punje kidogo tu za wali. Mume mwengine angekukasirikia. Lakini mimi nimekuwa na subira nawe, tena nimejaribu mara nyingi kuishawishi roho yako itamani chakula, kwa kupikiwa vyakula vya tunu, lakini hayo yote hayakufaa kitu. Na hata sasa, Amina, juu ya vyakula hivyo vyote, naona kule kuna vinginevyo vilivyo vitamu zaidi kwa kusarif iwa vizuri zaidi kama nyama ya maiti.

Kabla sijamaliza kusema maneno haya, mara Amina akafahamu kuwa nilimfuata makaburini, akashikwa na hamaki kupita kiasi na uso wake ukabadilika kwa hasira, macho yake yakawa kama yatakayomtokea utosini, na povu likimtoka kinywani kwa ghadhabu.

Nikamtazama kwa hofu na kuwaza itakuwaje baadaye. Ndipo akashika gudulia la maji lililokuwa karibu yake, akatumbukiza mkono wake ndani yake huku akinuia maneno ambayo sikuyafahamu. Kisha akaninyunyizia usoni mwangu, na kupiga ukelele kama mwenye wazimu, akinena, ‘Ewe baa, pokea tuzo la upelelezi wako, ugeuke mbwa.’

Basi baada ya maneno kumtoka tu kinywani mwake na bila ya kujijua kuwa kuna mabadiliko yanayonipitia mwilini mwangu, kwa ghafla nikajiona si mtu tena.

Nikastuka sana na kustaajabu, maana sikudhania kuwa Amina alikuwa mchawi, wala na mimi sikufikiri kukimbia, ila nilikaa pale pale kama niliyeota mizizi, ndipo Amina akashika gongo akaanza kunipiga. Ama kwa hakika mapigo aliyonipiga yalikuwa makubwa mno, na nastaajabu kwa kuwa mapigo yake hayakunia mara moja. Lakini yaliniharakisha kumwondokea na mara Amina akanifuatia mguu kwa mguu huku akinifukuza kama, mwenye wazimu, na kunitupia gongo ambalo sikuwa mwepesi sana kuliepa, likanipata.

Mwisho wake akachoka kunifukuza, au pengine alikua amebuni hila mpya ambayo ingenitia maumivu na mauti ya upesi. Basi akafungua mlango utokeao barabarani, kusudi apate kunibana nao wakati nikipita.

Ingawa nilikuwa mbwa, lakini nilifahamu makusudio yake nami nikajiona ni katika hatari kuu, basi nikajichunga mwendo wangu barabara hata nikapata nafasi ya kuruka nikatoka nje, lakini ncha ya mkia wangu ilipata kubanwa na mlango, wakati alipo usukuma kwa nguvu kuufunga.

Mradi niliokoka, ila mkia wangu uiumia sana, nami nikalia sana na kugumia kwa nguvu njia nzima, hata mbwa wenzangu wakaja kunipiga, na hivyo mambo yalızidi kuwa mabaya. Basi kwa kutaka kujiepusha nao, nikakimbilia katika duka la mpishi mmoja, kulikokuwa kukiuzwa ndimi za ng’ombe na vichwa vya kondoo.

Kwanza yule mwenye duka alinifanyia hisani kubwa, maana aliwafukuza wale mbwa wenzangu walionipiga, ndipo nami nikapata nafasi ya kujikokota pembeni kwenye giza nikakaa. Basi ingawa nilikuwa salama kwa muda ule, lakini sikujaliwa kukaa sana katika ulinzi wake, maana yeye alikuwa ni mmoja wa wale wanaosema kuwa mbwa ni haramu, na maji yote yailiyoko duniani ni shida kumtoharisha mtu kama akigusana nao. Na baada ya adui zangu walipokwisha kwenda zao kutafuta mawindo mengine, yule mwenye duka alijaribu kunitoa kwa nguvu kule pembeni ili niende barabarani, lakini nilikataa kutoka, maana nilihitajia usiku ule nilale pale salama, baada ya kule kuumizwa nilikoumizwa na Amina.

Seyid yangu, sipendi kukuchokesha kwa kukueleza sana mashaka na huzuni zilizoandamana na mabadiliko ya umbo langu, lakini na ikupendeze kusikia kwamba asubuhi yake yule mwenyeji wangu aliamka mapema kwenda kununua vitu vya biashara yake, hata aliporudi nikamwona amechukua mzigo kichwani uliojaa vichwa vya kondoo na ndimi za ng’ombe, kuwa ndiyo biashara yake ya kutwa. Harufu ya nyama iliwavuta mbwa wengi wenye njaa wanaokaa karibu, wakaja wakakusanyikia mlangoni kuomba vipande vidogo vidogo vya nyama. Na mimi nikatoka kule pembeni kwangu nilikolala, nikaenda nikasimama pamoja nao.

Ijapokuwa aliwakataa mbwa kwa kuwa ni haramu lakini alikuwa mtu mwema, tena kwa kule kujua kuwa sikula kitu tangu jana, akanitupia pande jema la nyama na vipande vidogo vidogo vilivyo vizuri kuliko vile alivyowatupia mbwa wengine. Hata nilipokwisha kula nikajaribu kurudi kuingia ndani ya duka, lakini hivi hakunikubalia, akasimama mlangoni na gongo mkononi, na hivyo nililazimika kuondoka kwenda kutafuta nyumba ingine.

Kwenda hatua chache mbele kulikuwa na duka la mchomaji mikate. Na wakati ule yule mwenye duka alikuwa akifungua kinywa, na ingawa sikuonekana na dalili ya kuwa na njaa mara akanitupia pande la mkate. Basi kabla sijalimeza lote kama vile wanavyofanya mbwa wengine, nikainamisha kichwa changu na kupungapunga mkia wangu kuwa ndiyo dalili ya shukrani, naye akafahamu, na akacheka. Ama kwa hakika ule mkate nilikua siutaki kabisa, lakini nikaona kama nikiukataa nitaonekana sina adabu, mradi nikaula taratibu ili aone kuwa nimeula kwa heshima. Na hivi pia akafahamu, tena nikamwona kama apendaye kuniacha nikae dukani mwake, basi nikakaa kitako nikitazama mlangoni, kuonyesha kwamba nataka niwe katika ulinzi wake wa hivi akakubali, tena alinizoeza kuingia hata ndani ya nyumba yenyewe, akanipa na mahali pa kulala, ambapo hapakuwa na kunikera.

Hisani nilizofanyiwa na mtu mzuri huyu zilikuwa nyingi sana. Na siku zote alikuwa na mapenzi nami, tena nikawa na sehemu ya chakula chake cha asubuhi, na cha mchana na jioni, nami upande wangu nikammiminia shukrani zangu zote na mapenzi, ambayo alikuwa na haki nayo kupata. Mradi nikakaa katika kumwangalia yeye tu, wala naye alikuwa hatoki nyumbani mwake bila kuwa na mimi pamoja naye, na kama akitukia kujitengeneza atoke nje, nami kumbe nimelala simwoni, ataniita, Rufas, Rufas, Rufas, kwani hilo ndilo jina alilonipa. Basi siku nyingi zikapita katika hali hii, hata siku moja akaja mwanamke kununua mkate. Katika kule kulipa kwake akatoa pesa nyingi, na kumbe vile moja ilikuwa mbaya, yule mchomaji mikate akaiona akakataa kuichukua, akataka ingine badili yake. Na yule mwanamke naye akaikataa vile vile akinena kuwa ile ni nzima kabisa, lakini yule mwokaji mikate hakukubali, kwani alijua kuwa hataweza kuipatia kitu. Mwisho wake akasema, Kwa hakika hii si nzima ni ya kubuni, na hata huyu mbwa wangu atakataa kuichukua. Mara pale akanita, Rufas! Rufas! Rufas Kusikia sauti yake tu, nikaruka juu ya meza ya bidhaa.

Yule mwokaji mikate akanitupia zile pesa mbele yangu, akisema, ‘Tazama kama iko moja iliyo mbaya.’ Nikatazama kila moja kwa makini: hata nilipoigundua nikaweka kiganja changu juu ya ile ya uwongo, na pale palenikamwangalia bwana wangu usoni ili kumwonyesha.

Basi yule mchomaji mikate akastaajabu mno kuona uhodari wangu, na yule mwanamke naye mwisho wake akasadikisha kuwa yule mtu alisema kweli; ndipo akatoa pesa ingine badili ya ile mbaya. Hata yule mwanamke alipokwenda zake, bwana wangu alifurahiwa sana ikawa ni kuwazungumzia majirani wote mambo aliyoyafanya, na kuongezea mengine zaidi kuliko yale yaliyokuwa.

Bila shaka wale majirani hawakusadiki habari zangu, nao walinijaribu mara nyingi kwa fedha mbaya walizozichanganya pamoja na nzima, lakini sikukosa kuzitambua na kuwashinda.

Mradi ikawa toka mwanzo wa asubuhi hata usiku lile duka hujaa watu waliojifanya kama wanunuzi wa mikate, kusudi yao ni kuangalia kama nilikuwa hodari kweli wa kutambua fedha mbaya kama hivyo nilivyotangaziwa. Sasa biashara ya mwokaji mikate ikavuma, hata mwenyewe akaona kuwa nilistahili taabu kusudi nimpatie fedha yeye.

Ama kwa hakika kulikuwa na wengi waliomwonea kijicho, na kwa hivyo walikuwa wakinichimbia kisima mimi, maana bwana wangu hakuniacha nitoke machoni pake. Hata siku moja, mwanamke ambaye hakupata kufika pale dukani, akaja kutaka mkate, na mimi nilikuwa nimejinyosha juu ya meza ya bidhaa kama ilivyokuwa desturi yangu. Akatoa thumuni sita akazitupa mbele yangu, na kumbe vile moja ilikuwa mbaya. Pale pale nikaiona, nikaiwekea kiganja changu huku nikimtazama yule mwanamke. Wakati nilipokuwa nikimtazama akainamisha kichwa chake, akanena, ‘Naam, barabara, hiyo ndiyo.’ Akasimama kuniangalia kisha akatoa thumuni ingine kulipa, halafu akatoka kwenda zake huku akinifanyia ishara nimfuate kwa siri.

Na mimi siku zote mawazo yangu yalikuwa katika kutafuta njia ya kuutegua uchawi niliologwa, na kwa kuona ile namna alivyoniangalia mwanamke yule, nafsi yangu ikaingiwa na tamaa, kuwa labda ametambua yaliyonipata, na hivi haikuwa uwongo.

Basi nikamwacha atangulie mbele kidogo, na mimi nilisimama mlangoni kumwangalia aendako. Na mara kwa mara alikuwa akigeuka nyuma kuniangalia, naye huniona nimesimama kumwangalia, nayeye huzidi kunipungia mkono nimfuate.

Wakati huu wote yule mwokaji mikate alikuwa akishughulika kuchoma mikate, akawa amesahau yangu yote, basi nikatoka taratibu kumkimbilia yule mwanamke, nikamkuta njiani.
 
Hata tulipofika nyumbani kwake, ambako kulikuwa mbali kidogo, akafungua mlango na kuniambia, ‘Karibu, karibu ndani, kwani hutojuta kamwe kwa kunifuata mimi.’ Nilipoingia ndani akafunga mlango na kunipeleka katika chumba kikubwa, kulikokuwa na kijana mwanamke mzuri akifanya kigwe.

Yule kiongozi wangu akanena, ‘Mwanangu, nimekuletea mbwa maarufu wa mwokaji mikate, anayeweza kutambua fedha na ghafi. Wafahamu kwamba siku ya kwanza niliposikia habari zake, nilikuambia kuwa nina yakini kuwa huyo lazima awe mtu kweli, aliyegeuzwa mbwa kwa uchawi. Na leo kwenda kwa mwokaji mikate kushuhudia mwenyewe habari hizo kumshawishi huyo mbwa kufuatana nami mpaka hapa. Je, sasa wasemaje?’

Kijana mwanamke akajibu, Kweli, mama, kisha akainuka na kuchovya mkono wake ndani ya gudulia la maji na kuninyunyizia mwilini, akinena, ‘Kama ulizaliwa mbwa, dumu kuwa mbwa kweli, lakini kama ulizaliwa mtu, basi kwa nguvu za maji haya, rejea umbo lako halisi.’ Na mara pale pale uganga ukateguliwa. Umbo la mbwa likanitoka nikawa kama sikuwa nalo kamwe, nikawa ni mtu niliyesimama mbele yake.

Nikashindwa kutoa shukrani kwa aliyeniokoa, nikajitupa miguuni pake na kubusu pindo za nguo yake, nikinena, ‘Nikushukuru namna gani kwa wema wako, na kwa haya uliyonitendea mgeni kama mimi?’ Tangu sasa ni mtumwa wako, nifanye kama unavyotaka!

Basi katika kule kueleza jinsi nilivyogeuzwa mbwa, nikamhadithia habari zangu zote, nikamaliza kwa kumtolea shukrani yule mama kwa furaha aliyoniletea.

Na yule binti yake naye akanena, ‘Sidi-Nouman, usitaje tena habari hizo. Kule kujulikana kuwa sisi tumekutumikia wewe yatosha kuwa malipo. Basi sasa na tuseme habari za mkeo Amina, ambaye namjua sana kabla ya kuolewa kwake, kwani najua kwamba alikuwa mchawi, na hata yeye ajua kwamba na mimi nilijifunza ufundi ule ule, kwa bibi yule yule mmoja. Na mara kwa mara tulikuwa tukikutana njiani wakati tukienda kuoga birikani, lakini hatukupendana wala hatukutakana usuhuba. Na kwa hayo yanayokuhusu wewe haitoshi kuwa basi nimeutegua uganga wake, ila sharti aadabiwe kwa uovu wake. Basi tafadhali kaa kidogo na mama yangu, uningojee, sasa hivi nitarudi.’

Mradi nikaachwa peke yangu pamoja na yule mama, nami nikazidi kumtolea shukrani yeye na binti yake.

Mama akajibu, ‘Binti yangu yu kama hivi umwonavyo, amehitimu sana uganga vile vile kama Amina, ila utastaajabu kuona jumla ya wema anaoufanya kwa maarifa yake, na kwa hivi ndio maana simwingilii kati na mambo yake, na la kama si hivyo, ningekuwa nimemkomesha kitambo.’ Basi alipokuwa akinena hivi, mara mwanawe akatokea amechukua chupa ndogo mkononi.

Akanena, ‘Sidi-Nouman, vitabu nilivyokuwa nikisoma sasa hivi, vimeniambia kuwa sasa Amina hayuko nyumbani, lakini atarudi punde hivi. Na kadhalika nimeona kuwa mbele za watumishi wake anajifanya kama mwenye wasi wasi mkubwa kwa kutokuwako wewe. Kisha ametangaza habari kuwa ulipokuwa ukila chakula pamoja naye, ulitukia kukumbuka kazi yako ya lazima uliyotaka uifanye kwa haraka nawe uliondoka nyumbani bila kufunga mlango na hivyo mbwa aliyepotea alitukia kuingia ndani, naye alilazimika kumfukuza kwa magongo.’

Basi sasa nenda nyumbani kwako usikawie, wende ukangojee katika chumba chako mpaka Amina arudi. Aingiapo ndani, toka umlaki, na katika kustaajabu kwake kwa kukuona tena atajaribu kukimbia. Basi chupa hii nikupayo iweke tayari, ukimwona hivyo, mtie maji haya yaliyomo huku ukinena: ‘Pokea tuzo la makosa yako.’ Basi hayo tu, sina zaidi.’

Basi kila jambo likatokea sawasawa kama vile alivyotangulia kuniambia yule kijana mwanamke mchawi. Sikukaa dakika nyingi nyumbani mwangu mara Amina akaja, na katika kuingia kwake ndani chumbani, nikatoka kwenda kukutana naye, na ile chupa ya maji niliyopewa ninayo tayari mkononi.

Kule kuniona tu, akapiga ukemi kwa hofu na akataka kukimbia, lakini wapi! Amechelewa. Nikawa nimekwisha mtia maji usoni mwake huku nikinena maneno ya kichawi. Amina mtu akatoweka, na mahali pake alisimama farasi, naye ndiye yule uliyemwona nikimpiga jana.

‘Ewe, Jemadari wa Uaminifu, maadam sasa umekwisha sikia sababu ya kitendo changu, natumai kuwa Fahari Yako itanikubalia kuwa mwanamke yule mwovu, alistahili kutendewa ukali sana.’

Khalifa akajibu, ‘Sidi-Nouman, ama kwa hakika kisa chako ni cha ajabu, wala hakuna msamaha wa kusamehewa mkeo. Lakini nataka ukumbuke jinsi anavyoteseka kwa kugeuzwa mnyama, nami natumai kwamba hiyo adhabu aliyoipata, utaona kuwa yatosha.

Sikuamuru uende ukamshurutishe huyo kijana mwanamke mchawi atafute njia ya kumrudishia mkeo umbo lake la kibinadamu, kwa sababu najua kwamba wanawake wakianza kufanya uovu kama huu, ni vigumu kuacha kabisa, na nikifanya hivyo ni kama nikutakiaye akulipize kisasi kibaya zaidi, kushinda hivyo ulivyokuwa.
 
KISA CHA ALI KOGIA, MFANYI BIASHARA WA BAGHDADI





KATIKA enzi ya Harun Rashid, paliondokea mfanyi biashara mmoja aliyekuwa akikaa katika mji wa Baghdadi, jina lake Ali Kogia, ambaye hakuwa na mke wala mtoto, lakini nafsi yake radhi kabisa kwa faida kidogo anayopata katika biashara yake; tena alikaa kwa raha mustarehe katika ya nyumba aliyoachiwa na marehemu baba yake. Hata ikatukia kuwa kwa muda wa siku tatu mfululizo, kila akilala usiku huota kutokewa na mzee mmoja anayemshutumu kwa kutotekeleza jambo linalompasa kufanya Mwislamu mwema, kwa kuichelewesha sana safari yake ya kwenda Makka kuhiji.

Ali Kogia akafanya wasiwasi sana kwa ndoto hii, maana hakupenda kufunga duka lake na kufarakana na wanunuzi wake. Mradi akaifikiria sana safari hii, tena akajaribu kutoa sadaka ili kujituliza moyo wake kwa kuzidisha kutenda mema, lakini kila akifikiri aliona kuwa ile ndoto yamwelekezea ishara, ndipo sasa akaazimia kutoivunja tena safari.

Jambo la kwanza alilofanya aliuza mapambo yake ya nyumbani na vitu vyote alvyokuwa navyo dukani mwake, na akajiwekea akiba ya vitu kidogo tu vya kuuza njiani, na lile duka lenyewe nalo pia akaliuza; tena akapata na mpangaji wa nyumba yake kwa urahisi. Jambo ambalo hakuweza kulitengeneza vema ilikua ni mahali pa kuweka reale zake elfu za dhahabu alizopenda kuziacha asizichukue safarini.

Basi baada ya kufikiri sana, Ali Kogia akapata shauri aliloliona jema. Akatwaa zile reale zake akazitia ndani ya gudulia na juu yake akajaza mzaituni. Sasa, baada ya kuliziba vizuri lile akalichukua na kumpelekea mmoja wa marafiki zake, mfanyi biashara kama yeye. Akamwambia, ‘Ndugu yangu, labda umesikia kuwa karibu nitasafiri kwenda Makka pamoja na msafara, basi nimekuja kukuuliza kama utanifanyia hisani kuniwekea gudulia hili la zeituni mpaka nirudi.’ Mara yule mfanyi biashara akajibu, ‘Tazama, huu hapa ufunguo wa duka langu. Chukua ukafungulie, wende ukaliweke gudulia lako popote unapopenda. Nami nakuahidi kwamba ukirudi utakuja likuta papo hapo utakapoliweka.’
 
Baada ya siku chache Ali Kogia akapanda ngamia wake aliye mtwisha bidhaa, akafuatana na msafara, wakafika Makka mapema.

Mradi ikawa kama hivyo wanavyofanya wasafiri wengine wakienda kuhiji, na yeye naye akaenda kutazama Alkaaba, na baada ya kutimiza sheria zote zinazohusu dini, akatoka kwenda kutoa bidhaa zake nje ili kuuza: akitumai kupata wanunuzi katika hao wanaopita njia.

Punde si punde wafanyi biashara wawili wakaja na kusimama mbele ya vile vitu vilivyopangwa; ikawa wanavigeuzageuza kuviangalia. Hata walipokwisha kuvitazama, mmoja akamwambia mwenziwe, ‘Laiti kama mtu huyu angekuwa na maarifa angevipeleka Kairo vitu hivi, ambako huko angepata bei nzuri kuliko hii atakayopata hapa.

Ali Kogia kusikia maneno yale, akaondoka akafunga vitu vyake, na badala ya kurudi kwao Baghdadi, akaungama na msafara mwingine uliokuwa ukienda Kairo. Huko Kairo kulimfurahisha sana, maana vitu vyake vyote alivyokuwa navyo aliviuza kwa mara moja, kisha akanunua na vitu vya Kimisri vilavyo azizi, ambavyo alikusudia kuvipeleka Damaskas kwenda kuuza. Lakini ule msafara ambao angefuatana nao kwenda huko ulikuwa hauondoki upesi ila baada ya majuma sita mengine, na kwà hivi ilikuwa uzuri kwake maana alipata nafasi ya kwenda kuangalia majengo ya mawe na miji mikubwa mikubwa iliyo kando kando ya mto wa Nil.

Alitamani sana kwenda Damaskas lakini mwisho wake akakumbuka kuwa yeye ana kwao Baghdadi, na mara pale pale ikamjia nia ya kurudi kwao kwa njia ya Aleppo, hata akiisha kuvuka mito ya Eufrati, ashike njia ya Tigris.

Lakini alipofika katika mji wa Mosul, Ali akasuhubiana na wafanyi biashara wa Kiajemi ambao walimshawishi kuandamana nao mpaka katika nchi yao, na hata Bara Hindi. Mradi ikawa hivyo, na miaka saba ikapita tangu alipotoka kwao Baghdadi. Wakati ule wote yule rafiki yake aliyemwachia lile gudulia alikuwa hamfikiri hata kidogo: si yeye wala si lile gudulia. Kwa kusema kweli ilikuwa bado mwezi mmoja tu, kabla ya kurudi Ali Kogia, ndipo yule mfanyi biashara alipokumbuka yote, kwa sababu siku moja mkewe alisema kuwa siku nyingi sana alikuwa hakula zeituni za namna yo yote, na kwa hivyo angependa kupata kidogo.
 
Mumewe akasema, ‘A! Kweli, umenikumbusha, miaka saba iliyopita kabla Ali Kogia hajakwenda Makka, alinipa gudulia la zeituni kumwekea. Lakini naona kwa muda wote huu lazima amekufa, kwa hivyo sioni sababu kwa nini tusile zeituni ikiwa twazipenda. Nipe taa niende nikazilete tuje tuzionje.’

Mkewe akamjibu ‘Mume wangu, nakusihi usifanye jambo lo lote

Baya! Japokuwa miaka saba imepita bila kupata habari za Ali Kogia, huenda akarudi kwa siku yo yote. Aibu ilioje akikuona umevunja uaminifu wako na kuvunja muhuri uiofungiwa gudulia! Basi nakuomba usisikilize maneno yangu, hasa na mimi sina hamu tena ya zeituni. Na pengine kwa hivi zilıvyokaa siku nyingi, zimeharibika wala hazifai tena. Na baada ya hivyo nina matumaini sana kuwa Ali Kogia atarudi; enhe! Akirudi itakuwaje? Basi nakusihi, heri uache.’

Yule mfanyi biashara ingawa alikuwa na busara, lakini alikataa kabisa kusikiliza shauri ya mkewe. Akatwaa taa na sahani akaenda dukani. Mkewe akamwambia, ‘Kama utakuwa mkaidi hivyo, haya shauri yako! Lakini kama halafu yakitokea mabaya usinilaumu mimi.’

Basi alipofungua lile gudulia akaona zeituni zote zilizu juu juu zimeoza, na kwa kutaka kuona kama zile za ndani zilikuwa nzuri akalisukasuka gudulia na kuzimimina nusu katika sahani, na reale za dhahabu nazo zikatoka kidogo.

Alipoziona zile reale kidogo tamaa ikamwingia. Akatazama ndani ya gudulia, akaona kumbe chini kulikuwa na dhahabu, Kisha akazirudisha tena guduliani, ndipo akarudi kwa mkewe.

Alipoingia chumbani akaita, akinena, ‘Mke wangu, ama maneno yako ni kweli, zile zeituni zimeoza, nami lile gudulia nimeliziba vizuri hata kama Ali Kogia akija hataweza kujua kama limeguswa.’

Mkewe akamjibu, Ama ungalifanya vizuri kunisadiki pale nilapokuambia, lakini sasa natumai kuwa hapana dhara itakayotokea.

Maneno haya hayakumpata sana yule mfanyi biashara kama vile yalivyompata yale mengine. Mradi usiku kucha akawa anafikiri namna ya kuzichukua zile dhahabu na namna ya kuja kumwambia Ali Kogia, kama akirudi kutaka gudulia lake. Hata asubuhi yake akaondoka kwenda kununua zeituni mpya, kisha akatwaa zile kuukuu akazitupa na kuchukua reale za dhahabu akazificha; ndipo akalijaza tena lile gudulia kwa zeituni mpya alizonunua. Kuisha kufanya hivi akaliziba akaenda kuliweka pale pale lilipowekwa na Ali Kogia.

Baada ya mwezi mmoja Ali Kogia akarudi tena Baghdad na kwa kuwa nyumba yake ilikuwa ingali ina wapangaji akaenda kufikia katika nyumba ya wageni. Hata asubuhi kulipokucha akatoka kwenda kumtazama rafiki yake yule mfanyi biashara, ambaye alimpokea kwa wema na maneno mengi yakimtoka kustaajabu. Baada ya kupita dakika chache kwa kuulizana na Ali Kogia akamwambia rafiki yake amkabidhishe gudulia lake alilompa zamani kumwekea.

Yule rafiki akasema, ‘Naam, hapana budi. Nafurahi kwa kuwa nimeweza kuwa na manufaa kwako. Basi huu hapa ufunguo wa duka langu, chukua wende ukafungue, nawe utaliona pale pale ulipoliweka.’

Ali Kogia akachukua gudulia lake akaenda nalo chumbani kwake kule alikofikia, akalifungua. Akatia mkono wake kwa nguvu mpaka chini ya gudulia, lakini reale hazikuwamo; mradi nafsi yake ikatumai kuwa zimo. Basi akatoa sahani katika vyombo vyake vya safari akamimina zeituni, lakini vile vile hakuona kitu. Kuona hivi akastuka na kutetememeka kwa hofu akawa hana la kusema maskini, kisha akainua mikono yake juu, akashukuru akinena, ‘Alhamdulilalhi! Hivi kweli rafiki yangu wa tangu zamani aweza kunifanyia uovu kama huu?’

Akatoka haraka sana kwenda kule nyumbani kwa rafiki yake na akamwambia, ‘Rafiki yangu, nadhani utastaajabu kuniona nimerudi tena, maana zile reale elfu za dhahabu nilizotia ndani ya gudulia hili chini ya zeituni hazimo. Labda umezikopa kwa kusudi kufanyia biashara yako, ikiwa ni hivyo vema, hapana neno, ila nataka unipe cheti cha stakabadhi, nawe utaweza kunilipa taratibu.’

Yule mfanyi biashara aliyekuwa akiyatarajia maneno kama haya alikuwa ameyaweka tayari majibu yake. Akasema ‘Ali Kogia, pale uliponiletea lile gudulia la zeituni mimi nililishika? Mimi najua kuwa nilikupa ufunguo wa duka kwenda kufungua duka langu kisha ukalichukua wewe mwenyewe kwenda kuliweka mahali ulipopenda. Je! Kwani hukuliona hali ile ile ulipoliweka? Kama ulitia dhahabu ndani yake lazima ziwemo hata sasa; lakini mimi sijui habari yo yote ila najua kwamba uliniambia kuwa lina zeituni. Basi sadiki haya nikuambiayo, lakini mimi sikuligusa kabisa.’

Ali Kogia akawa bado anajaribu kila njia kumfanya mfanyi biashara aseme kweli. Ndipo akamwambia, ‘Ama mimi napenda amani, na kwa hivi nitasikitika sana kama ikinilazimu kufanya ukali. Basi nakuambia tena, fikiri sana heshima yako. Lakini kama nitakata tamaa ya kupata reale zangu, itanilazimu kwenda kushtaki.’

Mfanyi biashara akajibu, Ali kogia, wasema kuwa ni gudula la zeituni ndilo uliloliweka kwangu. Kweli ulilileta lakini kisha uliliondoa mwenyewe. Hivi sasa waniambia kwamba lilikuwa na reale elfu za dhahabu na hivyo wataka nikurudishie! Kwani hapo kwanza wewe ulinitajia habari za reale hizo? Ama mimi kwa nafsi yangu hata kule kujua kuwa gudulia lako lilikuwa na zeituni sikujua maana hukunionyesha, nitakuja jua ya dhahabu? Nhu, makubwa haya! Ila yana nafuu kidogo kwa kuwa hudai lulu wala almasi.’ Basi tafadhali nenda zako wasije watu wakanijalia dukani pangu.’

Wakati huu hawakukusanyika watu wapitao njia tu, lakini hata wale majirani wafanyao biaslara walijazana kusikiliza ugomvi, na kwa mara wakijaribu kuwapatanisha. Lakini kwa neno la mwisho alilosema yule mfanyi biashara, lilimfanya Ali Kogia kueleza sababu ya ugomvi wao, ndipo akawahadithia habari zote, nao wakamsikiliza mpaka mwisho. Kisha wakamwuliza yule mfanyi biashara kana alikuwa nalo la kusema.

Yule akakubali kuwa kweli aliweka gudulia la Ali Kogia dukani mwake, ila alikataa kuwa aliligusa, na tena akaapa kuwa hivyo vilivyokuwamo ndani yake alivijua kwa kuambiwa na mwenyewe Ali Kogia, halafu akawataka wote waliokuwapo washuhudie matusi aliyotukanwa na Ali Kogia.

Ali Kogia akamshika mkono na kumwambia, ‘Hayo umeyataka mwenyewe, na maadam waniambia niende nikashtaki, vema nitashtaki tuone kama utathubutu kusema tena maneno yako mbele ya Kadli.

Basi kama Mwislamu mwema alivyo, yule mfanyi biashara aliambiwa asikatae shauri hiyo ya kwenda kwa hakimu, naye akakubali. Kisha akamwambia Ali Kogia, ‘Ama hivyo vizuri, kwani ndipo tutakapojua upesi yupi aliye na haki.’

Basi watu wawili hawa wakajipeleka wenyewe mbele ya Kadhi, na Ali Kogia akaanza kuhadithia habari zake. Halafu Kadhi akamwuliza ni mashahidi gani alionao. Ali Kogia akajibu kuwa yeye hakujishughulisha kwa hayo maana alidhania kuwa ni rafiki yake, na tangu hizo siku alimjua kuwa ni mwamnifu.

Yule mfanyi biashara naye kwa upande wake, akasema habari zake, tena akataka aape kiapo cha dini na kusema: ‘Si kwa kuwa sikuiba reale za dhahabu tu, lakini hata kule kujua kuwa zilikuwamo ndani ya gudulia sikujua kabisa. Kadhi akamruhusu aape, alipokwisha kuapa yule Kadhi akamnadishia kuwa hana hatia.

Ali Kogia akafanya ghadhabu kwa kupata hasara kama ile, akaanza kubishana juu ya hukumu iliyokatwa, akisema kuwa atakata rufaani, ili hukumu yake ihukumiwe tena na mwenyewe Khalifa, Harun Rashid. Lakini yule Kadhi hakumsikiliza maneno yake, ila alikuwa radhi kabisa kuwa hayo aliyohukumu ndiyo yaliyokuwa haki.

Mradi hukumu ikapita, na yule mfanyi biashara akarudi kwake kwa furaha na Ali Kogia akarudi katika chumba chake kule katika nyumba ya wageni kuandika barua ya kuomba msaada wa Khalifa. Hata asubuhi yake akatoka akaenda kujiweka katika njia aliyokuwa akipita Khalifa akitoka kusali sala ya adhuhuri, akatoa barua yake akampa jemadari anayetangulia mbele ya Khalifa, ambaye kazi yake ilikwa ni kupokea barua, hata wakifika nyumbani huzitoa akampa bwana wake. Na humo ndimo Khalifa Harun Rashid anamozisomea kwa makini sana.

Basi kwa vile Ali Kogia alivyojua desturi hii, akamfuata Khalifa mpaka katika ukumbi wa jumba lake kungojea majibu. Baada ya dakika chache jemadari akamtokea na kumwambia kuwa Khalifa amesoma barua yake, na kisha amechagua na wakati wa kubarizi naye kesho asubuhi. Halafu yule jemadari akauliza na anwani ya yule mfanyi biashara, ili naye apate kuitwa.

Basi ikawa kwa siku ile ile usiku, Khalifa na Jaffari, waziri wake mkuu, pamoja na Marur, mkuu wa matoashi, wote watatu wakajigeuza mavazı kama ilivyokuwa desturi yao, wakatoka kwenda kutembea mjini.

Hata walipokuwa wakipita katika njia moja, mara Khalifa akasikia sauti zalizomfanya kuchungulia katika dirisha lililokuwa wazi na akaweza kuona mpaka uani; akaona watoto kumi au kumi na mbili wakicheza katika mbaamwezi, basi akajibanza pembeni kwenye giza, akiwatazama.

Mmoja aliyekuwa hodari kupita wote akawaambia wenziwe ‘Tuchezeni mchezo wa Kadhi, mimi nitakuwa Kadhi, na ninyi mniletee mfanyi biashara aliyemwibia Ali Kogia reale elfu za dhahabu!’

Maneno ya yule mtoto yakamkumbusha Khalifa ile barua aliyoisoma asubuhi, hata akapenda kungoja kusudi apate kuwangalia watoto jinsi watakavyofanya.

Basi mchezo ule uliokusudiwa kuchezwa uliwapendeza sana watoto wengine, kwani nao walisikia maneno mengi juu ya mashtaka na hukumu iliyotolewa, basi mara pale wakapangana. Kadhi akakaa katika kiti chake kwa makini, na huyo aliyekuwa jemadari akampeleka kwanza Ali Kogia, anayeshtaki, na halafu akampeleka mfanyi biashara aliyeshtakiwa.

Ali Kogia kufika mbele ya Kadhi akajiinamisha chini, kisha akainuka na kuanza kueleza yake neno kwa neno; akamaliza kwa kumsihi Kadhi amsaidie ili asipate hasara kubwa ya mali kama ile.

Kadhi alipokwisha kusikiliza maneno yake, akamgeukia mfanyi biashara wa uwongo, na kumwuliza kwa nini hakumlipa Ali Kogia reale zake anazosema.

Mfanyi biashara wa uwongo akatoa sababu zake, vile vile kama alivyotoa mfanyi biashara wa kweli kumwambia Kadhi wa Baghdadi, na kadhalika akataka aapishwe kuwa amesema kweli.

Yule Kadhi mtoto akamwambia, ‘Ngoja kwanza, kabla hatujafika kuapishana, nitapenda kuliona hilo gudulia na zeituni zake. Kisha akauliza, Je! Ali Kogia, gudulia lako unalo? Na alipoona kuwa hanalo, Kadhi akamwambia, ‘Nenda kalichukue, ulete.’ Basi yule aliyejifanya kuwa Ali Kogia mara akatoka, kisha akarudi akajifanya kama anayeweka gudulia chini, mbele ya Kadhi, akisema kuwa lile ndilo gudulia lake alilompa mshtakiwa kumtunzia. Na kwa kutaka kujua kweli hasa, Kadhi naye akamwuliza mfanyi biashara kama analikumbuka kuwa ndilo gudulia lile lile. Basi kule kunyamaza kwake yule mfanyi biashara, kulionyesha kuwa anaungama kweli; ndipo Kadhi akaamuru lile gudulia lifunuliwe, Ali Kogia akasogea karibu kama atakaye kufunua kifuniko, na yule Kadhi mtoto naye akajifanya kama achunguliaye ndani ya gudulia.

Akasema kwa kustaajabu, ‘Lo, zeituni hizi nzuri namna gani ama nitapenda kuonja moja.’ Akajifanya kama atoaye moja na kutia mdomoni mwake, na kusema, ‘Kwa hakika ni nzuri kabisa, lakini naona ajabu sana kuwa zeituni za miaka saba kuwa nzuri namna hii! Na atumwe mtu akawaite wachuuuzi wa zeituni, tusikie watasemaje!

Mara pale pale watoto wawili wakapelekwa mbele ya Kadhi kama kuwa wao ndiyo wachuuzi wa zeituni, na Kadhi akasema nao. Akawaambia, ‘Niambieni kweli, zeituni zaweza kuwekwa kwa miaka mingapi hata zisioze, zikafaa kuliwa?’

Wale wafanyi biashara wakajibu, ‘Seyid yetu, ijapokuwa zitatunzwa sana haziwezi kukaa zaidi ya miaka mitatu bila kuoza. Kwani huwa hazina tamu tena na rangi yake hukwajuka, hazifai kitu tena ila kutupwa tu. Kadhi mtoto akawajibu, ‘Ikiwa hivyo msemavyo ndivo tazameni gudulia hili, mniambie hizo zeituni zilızomo ndani yake zimekaa miaka mingapi.’

Wafanyi biashara wakajifanya kama wanaozitazama na kuzionja halafu wakamwambia Kadhi kuwa zeituni ni nzuri kabisa, kisha ni mpya. Kadhi mtoto akawaambia, ‘Mmepotea, Ali Kogia asema kuwa tangu azitie ndani ya gudulia hilo yapata miaka saba.’

Wafanyi biashara wa zeituni wakanena, ‘Tunakuhakikishia kuwa zeituni hizi ni za mwaka huu, na kama utapenda kuwauliza wafanyi biashara wote wanaokaa Baghdadi, hakuna hata mmoja atakayekanusha maneno yetu.’

Yule mfanyi biashara aliyeshtakiwa kusikia hivi, akafunua kinywa chake kama atakaye kubisha, lakini Kadhi hakumpa nafasi, akamwambia, ‘Nyamaza, mivi we!’ Kisha akasema, ‘Mchukueni mkamnyonge.’ Basi mchezo ukaisha, na watoto wakapiga makofi kwa furaha, huku wakimwongoza mdhalimu kwenda kunyongwa.
 
Harun Rashid akastaajabu sana kuona hekima ya mtoto jinsi alivyohukumu kwa akili mashtaka ambayo yeye mwenyewe atayahukumu kesho. Akamwuliza waziri mkuu ambaye naye pia alistaajabu vile vile kama yeye mwenyewe, ‘Hivi kuna hukumu ingine kupita hi? Mimi sioni ingine!’

Waziri akajibu, ‘Ikiwa kweli mambo ni kama haya tuliyoyasikia, Seyid yangu, mimi naona vizuri ufuate mfano wa mtoto huyu katika njia za hoja na katika kukata hukumu yako.’

Khalifa akamwambia, ‘Haya basi! Itunze sana nyumba hii na kesho uniletee yule mtoto aje ahukumu mashtaka haya mbele yangu. Na yule Kadhi pia aitwe ili aje ajifunze kazi yake kwa kumsikia mtoto atakavyohukumu. Tena upeleke mtu kwa Ali Kogia akamwambie kesho aje na gudulia lake la zeituni na wachuuzi wawili wa zeituni na wao pia waweko.’ Kuisha kusema hivi, Khalifa akarudi nyumbani kwake.

Hata asubuhi kulipokucha waziri akaondoka nyumbani alikowaona wale watoto wakicheza, na kumuita bibi mwenye nyumba pamoja na watoto wake. Punde si punde watoto watatu wakatokea, ndipo waziri mkuu akauliza, ‘Yupi aliyekuwa Kadhi katika mchezo wenu wa jana usiku?’ Yule aliyekuwa mkubwa na mrefu uso wake ukambadilika kwa hofu, lakini juu ya hivyo akaungama kuwa ni yeye, na pale pale mama yake akawa na wasiwasi mkubwa. Ndipo waziri akasema kuwa amepata amri kumchukua mtoto mbele ya Khalifa.

Masikini mama yake, akauliza, ‘Je! Ndiyo anataka kuninyang’anya mwanagu nini?’ Lakini waziri akamtoa hofu kwa kumhakikishia kuwa atarudishiwa mwanawe baada ya saa moja, na akamwambia laity kuwa angejua sababu aitiwayo mwamawe, ama nafsi yake ingekua radhi kabisa. Kwa hivi akawa na nguvu, ndipo akamvika mwanawe nguo safi kisha akamtoa kufuatana pamoja na waziri wakaenda.

Mtoto alipopelekwa mbele ya Khalita alikuwa na hofu na wasiwasi kidogo, lakini Khalifa akataka aanze kumweleza sababu ya kumtumia mtu kuitwa. Akamwambia kwa upole, ‘Karibu mwanangu! Karibu, nadhani ni wewe uliyekuwa mwamuzi wa mashtaka ya Ali Kogia na mfanyi biashara jana usiku. Nilikusikia kwa bahati tu wakati nilipokuwa nikitembea, nami nilipenda sana namna ulivyoendesha hukumu. Na leo utamwona Ali Kogia wa kweli na mfanyi biashara wa kweli. Basi kaa kitako karibu nami.

Khalifa akakaa kitako katika kiti chake cha enzi, na yule mtoto akawa wa pili wake; na wale watu wanaoshtakiana wakaingizwa ndani ya chumba cha baraza. Basi katika kule kuamkia kwao walijitupa chini kifudifudi mmoja mmoja, huku wakigusa kwa vipaji vyao zulia lililotandikwa chini ya kiti cha enzi. Hata walipoinuka, Khalifa akawaambia, ‘Sasa semeni maneno yenu. Na huyu mtoto atawahukumia haki na kama kutakuwa na mengineyo zaidi, hayo nitayatazama mwenyewe.’

Ali Kogia na mtanyi biashara wakaanza kusema maneno yao mmoja mmoja, lakini mfanyi biashara alipotaka aape kiapo kile kile alichoapa kwanza mbele ya Kadhi, mtoto akamzuia, na kumwambia, ‘Kabla hayo hayajafanyika lazima kwanza nione hilo gudulia la zeituni.’ Ali Kogia kusikia vile, akalipeleka gudulia kwa Khalifa, na kulifunua. Khalifa akatwaa zeituni moja kuonja, kisha akawaamrisha na wale wafanyi biashara wa zeituni walio stadi, waonje vile vile. Kisha halafu wakasema kuwa zeituni ni nzuri, tena ni mpya, nazo ni za mwaka ule ule. Yule mtoto akawaambia kuwa Ali Kogia amesema kuwa ni miaka saba tangu alipozitia ndani ya gudulia lile; lakini wao walishikilia kusema vile vile kama walivyojibu wale watoto siku ile ya mchezo wao.

Wakati huu yule mfanyi biashara aliyeshtakiwa akaona imemkalia vibaya akajaribu kutoa hoja za kujitetea. Lakini yule mtoto alikuwa na akili sana hata mwisho wake akaamuru anyongwe. Ndipo halafu akamgeukia Khalifa kumtazama, na kunensa ‘Ewe Jemadari wa Uaminifu, huu sasa si mchezo ila ni kweli tupu na hivyo ni mahali pako wewe Seyid yangu kumhukumu, wala si mimi.’ Mradi Khalifa akasadikisha kuwa yule mtu alikuwa mwivi akawaamuru wamwondoshe wakamnyonge, na hayo yakatimizwa, lakini baada ya kuungama makosa yake na kuonyesha mahali alipoficha reale za Ali Kogia. Baada ya haya, Khalifa akamwamuru na yule Kadhi ajifunze namna ya kuhukumu haki kama vile alivyofanya yule mtoto. Ndipo halafu yule mtoto akarudishwa kwao, baada ya kupewa mfuko wa reale elfu za dhahabu kuwa ndiyo zawadi yake.
 
FARASI WA UCHAWI​







SIKU moja ilikuwa siku kuu ya Mwaka Mpya, ambayo ndiyo iliyokuwa siku kuu kubwa kuliko zote katika milki ya Ajemi. Siku hiyo mfalme alishinda kutwa katika mji wa Shirazi akitazama michezo ya ajabu, iliyofanywa na raia zake kwa kuienzi siku kuu.

Jua lilipokuwa likichwa na mfalme alipokuwa karibu kuwapungia mkono watu wake ili warudi makwao, mara ghafla akatokea Mhindi mbele ya kiti chake cha enzi ameongozana na farasi mwenye tandiko na hatamu za fedha, na ukimwangalia wamuona kama farasi kweli.

Akasema hali amejiangusha chini kifudifudi, ‘Seyidyi yangu, ingawa nimechelewa kufika mbele yako, lakini naweza kuhakikishia kwamba katika hayo mambo ya ajabu uliyoyaona mchana huu, hapana yawezayo kulingana na farasi huyu. Seyid, utakubali kumwangalia?’

Mfalme akajibu, ‘Simwoni na kitu, ila naona ni werevu wa kuiga tu kama wa kweli, na fundi aliye stadi aweza kumfanya zaidi ya huyo.’
 
Back
Top Bottom