Tutangaze hali ya hatari mauaji ya albino
Faraja Mgwabati
Daily News; Sunday,December 14, 2008 @20:03
VITENDO vya mauaji ya albino nchini kwa imani za kishirikina, vimevuka mipaka na kulifanya jambo hilo siyo tena la kubembelezana, bali nguvu inahitajika kutumika kuondoa aibu hii.
Takribani albino zaidi ya 30 wameshauawa hadi sasa na dalili zinaonyesha mauaji hayatakoma leo wala kesho kwani hata wakati viongozi wakuu walipokuwa wakikemea mauaji hayo, kesho yake unasikia tena kuna mwingine ameuawa.
Viongozi wa serikali, wa dini, taasisi za kijamii, wanasheria na vyama vya kupigania haki za binadamu vya ndani na nje na hata wanahabari, wamelaani mauaji hayo, lakini haijasaidia.
Naamini sasa umefika wakati kwa serikali kutangaza hali ya hatari au kutangaza mauaji ya albino kuwa ni janga la kitaifa kwa kuwa usalama wa raia hawa wenye ulemavu wa ngozi upo mashakani, nao ni Watanzania kama wengine wanahitaji kuishi kwa usalama bila hofu.
Nasema hivyo kwa sababu siamini kama kukemea au kulaani au kutoa elimu kwa jamii pekee yake kunatosha, bali nguvu ya dola zaidi inahitajika kumaliza tatizo hilo.
Sioni sababu ya kuweka nguvu nyingi kwenye kuelimisha jamii kwa sababu hakuna mtu katika karne ya leo asiyejua kwamba kuua mtu ni kosa la jinai na adhabu yake ni kunyongwa.
Hivyo naamini kwamba wauaji wa albino wanajua wanachokifanya ila tu kwa sababu wamepumbazwa na ujinga wa waganga wa kienyeji ndiyo maana wanachukua jukumu hilo zito la kuua wenzao.
Sasa watu kama hawa siyo wa kucheka nao tena, bali ni kuwashughulikia kwa nguvu ya ziada tena ikibidi adhabu iwe kubwa zaidi ya wale wanaopatikana na hatia ya mauaji mengine kwa kuwa wanaoua albino wanadhamiria.
Ndani ya hali ya hatari, endapo itasikia albino ameuawa au usalama wake umetishiwa, ifanye msako wa nyumba hadi nyumba ikiwakamata wahusika wote wakiwamo waganga wa jadi wote wa eneo hilo.
Pia viongozi wa vijiji husika na hata wananchi ambao wanaweza kuwahisi wanahusika kwa namna moja au nyingine ili kupata ushahidi wa kutosha. Kwa kuendesha msako wa nyumba hadi nyumba bila shaka wahusika watakamatwa haraka, lakini pia wakishakamatwa wabanwe hadi wataje wanzao wote waliohusika wakiwamo waganga wa jadi wote wawekwe ndani.
Upelelezi wa kesi za wauaji wa albino ufanywe haraka ili wahusika wachukuliwe hatua haraka huku kesi hizo zitangazwe zaidi na vyombo vya habari ili kuwa fundisho kwa watu wengine.
Kikosi cha Operesheni Maalumu chini ya Kamanda Venance Tossi kinaweza kutumika kufanya kazi hiyo pamoja na kazi nyingine wanazozifanya kama za kukamata na kuchoma mashamba ya bangi.
Naamini bila kutumia nguvu mauaji ya albino yataendelea zaidi na tutakapokuja kushtuka ndugu zetu hawa watakuwa wamekwisha na hao waganga watahamia kwa watu wengine.
Baadaye wataanza kusema wanataka viungo vya Wazungu na wananchi wanaotaka utajiri wa haraka wataamini wataanza kuua Wazungu, itakuwa dhambi juu ya dhambi.
Tusisahau kuwa waganga wetu ndiyo walisababisha matukio ya uchunaji ngozi yaliyosababisha mauaji mengi ya watu hasa Mkoa wa Mbeya miaka michache iliyopita