SoC04 Akufaaye kwa Dhiki ndiye Rafiki

Tanzania Tuitakayo competition threads
Jun 25, 2023
45
31
Tanzania Tuitakayo, huweza kuja kwa kuwa na taifa moja ambalo ni rafiki zaidi ya ndugu (Special Relationship) kama urafiki (Special Relationship) uliopo kati ya mataifa yaliyoendelea zaidi duniani; USA na UK.

'Special Relationship' ni uhusiano wa kidiplomasia wenye nguvu, wenye umuhimu na wa kushibana sana kama ulivyo uhusiano kati ya Marekani na Uingereza, ambao ni uhusiano wa marafiki walioimarisha kwa pamoja Utamaduni wa Kimagharibi (Western Culture); Utamaduni wenye nguvu na unaotumika duniani kote leo hii; mfano, Lugha ya Kiingereza.

Enzi za kupigania UHURU wa Tanzania na Kusini mwa Afrika, Taifa la Tanzania halikuwa peke yake katika safari ya kupigania Uhuru tunaojivunia leo hii, bali liliungana na mataifa mengine huku taifa lililokuwa na 'Special Relationship' na Tanzania katika nyakati za kupigania Uhuru likiwa ni Afrika Kusini (Zuid Afrika)

Hivyo basi, ili kuijenga Tanzania Tuitakayo; Taifa la Tanzania linahitaji Taifa Rafiki wa Kweli la Kiafrika, ambalo tutashirikiana kweli na pamoja katika kuimarisha Utamaduni wa Afrika (African Culture) wenye nguvu na utakaotumika duniani kote ili iwe Tanzania Tuitakayo na yenye nguvu ya kuiongoza dunia; mfano, kupitia Lugha ya Kiswahili ambayo asili yake ni Pwani ya Afrika Mashariki.

Tafadhali tusome mashairi haya, yanayohusu Historia iliyopo kati ya Urafiki uliopo kati ya Tanzania na Afrika ya Kusini lakini pia Uhusiano Maalum wa Tanzania na Afrika ya Kusini.

TANZUID-AFRIKA

Enzi za Uhuru tangu, bado ipo kumbukumbu,
Solomoni Mahlangu, ya Morogoro Mazimbu,
Vidume wa bara langu, hawakucheza sasambu,
Kusini ya Afrika, rafiki wa Tanzania.

Soweto moja ya miji, ya Zuid-Afrika,
Tanzania Mbeya Jiji, la Soweto kadhalika,
Iko Soweto ya Mji, wa Moshi pasi na shaka,
Kusini ya Afrika, rafiki wa Tanzania.

Wangoni wa Tanzania, na Afrika Kusini,
Walifikia Songea, pale Ruvuma Mjini,
Sasa wamepazoea, wamesahau nyumbani,
Kusini ya Afrika, rafiki wa Tanzania.

Tangu Nyerere Mandela, Samia na Ramaphosa,
Wakuu hawajalala, urafiki kuutosa,
Pamoja twala chakula, upendo tusije kosa,
Kusini ya Afrika, rafiki wa Tanzania.

Kiswahili Tanzania, Kizulu kwa ndugu zetu,
Fahari twajivunia, kusini mwa bara letu,
SADC yazingatia, mawasiliano yetu,
Kusini ya Afrika, rafiki wa Tanzania.

Ni mataifa mawili, pacha ndugu marafiki,
Toka 'Nkosi Sikelel', hadi 'Mungu Ibariki',
Undugu wetu wa kweli, si ule wa kinafiki,
Kusini ya Afrika, rafiki wa Tanzania.

Kwetu tunayo singeli, ya kwao amapiano,
Za nchi zetu asili, zakuza mahusiano,
Kutengana siyo kweli, hayo si maridhiano,
Kusini ya Afrika, rafiki wa Tanzania.

Ni Nkosi Zwangendaba, nyumba nzuri ya wageni,
Na haiko kwa madiba, iko Songea shambani,
Inafanana haiba, na Afrika Kusini,
Kusini ya Afrika, rafiki wa Tanzania.

Nyimbo zetu za taifa, kama mawingu na anga,
Zafanana zake sifa, huimbwa kwa kujipanga,
Ni kwa timu za taifa, si Mamelodi na Yanga,
Kusini ya Afrika, rafiki wa Tanzania.

Walimu wa Kiswahili, tangazo wahitajika,
Kuwafunza Uswahili, Wazuid-Afrika,
Wajue pika ugali, na samaki wa kupaka,
Kusini ya Afrika, rafiki wa Tanzania.

Tuwafunze kuupika, wali kisamvu kwa nazi,
Kitoweo kubanika, kwa makuti ya mnazi,
Na mavazi sitirika, kama ya Kizimkazi,
Kusini ya Afrika, rafiki wa Tanzania.

Mihogo ya kuchemsha, kachumbari maridadi,
Loweka na kuiosha, kuondoa cyanide,
Kaanga chemsha pasha, twanga unga kwa juhudi,
Kusini ya Afrika, rafiki wa Tanzania.

Asali ya jabalini, na sharubati ya tende,
Maziwa kondoo tini, sukari hebu iende,
Utamu uso kifani, tuuonje tuupende,
Kusini ya Afrika, rafiki wa Tanzania.

Ulosema bia tamu, kuja hapa omba poo,
Tukuonjeshe utamu, wa maziwa ya kondoo,
Hautaishiwa hamu, utabeba kwenye ndoo,
Kusini ya Afrika, rafiki wa Tanzania.

Chakula cha Kiswahili, tukipeleke Durban,
Wakale mseto wali, kuku wa mambo ya Pwani,
Isiwashe pilipili, weka ile ya kijani,
Kusini ya Afrika, rafiki wa Tanzania.

Tunduma-Nakonde Boda, ndiyo hutuunganisha,
Magari kwa bodaboda, mizigo husafirisha,
Tunaipata faida, twafurahia maisha,
Kusini ya Afrika, rafiki wa Tanzania.

Zimbabwe nako Zambia, Botswana Msumbiji,
Angola na Namibia, ni salama yake miji,
Tupinge Xenophobia, dunia tuifariji,
Kusini ya Afrika, rafiki wa Tanzania.

MUNGU ndiye ngome yetu, ya upendo tulo nao,
SADC ndo chama chetu, umoja wetu na wao,
Hawa majirani zetu, chao chetu chetu chao,
Kusini ya Afrika, rafiki wa Tanzania.

Kiswahili Lugha yetu, chombo mawasiliano,
Utumwa hatuna katu, wa Lugha zenye mabano,
Miguu ina viatu, macho yaona maono,
Kusini ya Afrika, rafiki wa Tanzania.

Tukomeshe mauaji, kuwaua ndugu zetu,
Wawe ni wazamiaji, au mahasimu wetu,
Tuvikwe ya wema taji, tusifanane na chatu,
Kusini ya Afrika, rafiki wa Tanzania.

Na Zuid-Afrika, ni Afrika Kusini,
Nyumbani kwa Zulu Shaka, na asili ya Wangoni,
Nchi iloimarika, pande zote nje ndani,
Kusini ya Afrika, rafiki wa Tanzania.

Asante kwa kusoma pamoja nami shairi hili; swali ni je! Ile 'Special Relationship' ya nyakati za akina Hayati Mzee Nyerere na Hayati Mzee Mandela kati ya Tanzania na Afrika Kusini; nyakati za kupigania Uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika, bado ipo?

Jibu ni kuwa, kwa sasa uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Afrika Kusini ni kama uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Mataifa mengine yaani uhusiano wa kidiplomasia wa kawaida na si urafiki kama ndugu (Special Relationship).

Kama Tanzania na Afrika Kusini tulivyopambana pamoja na kuupata UHURU basi ndivyo tunavyotakiwa kupambana pamoja ili kuipata Tanzania na Afrika Tunayoitaka; Tanzania na Afrika yenye UHURU MAMBOLEO na yenye nguvu ya kuiongoza dunia kupitia Utamaduni wa Afrika (African Culture) ikiwemo Lugha ya Kiswahili.

Tanzania na Afrika Kusini tunavyo vingi sana tunavyofanana katika sanaa na utamaduni; lakini kubwa zaidi ni mfanano wa nyimbo zetu za taifa; NKOSI SIKELEL na MUNGU IBARIKI pamoja na mfanano wa baadhi ya maneno katika Lugha ya Kiswahili na Lugha ya Kizulu.

  1. Kiswahili (Mbuzi) - Kizulu (Imbuzi)
  2. Kiswahili (Nyama) - Kizulu (Inyama)
  3. Kiswahili (Kumi na Mbili) - Kizulu (Ishumi nambili)
  4. Kiswahili (Mafuta) - Kizulu (Amafutha)
  5. Kiswahili (Maji) - Kizulu (Amanzi)
Kwa kuhitimisha; Tanzania haiwezi kwenda kwenye Tanzania Tuitakayo ikiwa peke yake, inahitaji taifa rafiki wa kweli la kwenda nalo pamoja iwe mawingu, iwe mvua au iwe jua katika nyanja zote ambazo ni Afya, Elimu, Teknolojia, Utamaduni, Kilimo, Uchumi, Habari na Mawasiliano, n.k; kama ilivyo kwa mataifa ya Marekani na Uingereza.
 
Ni sawa, akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki.

Hapohapo tuwaze zaidi kuwafaa hao marafiki ili tufae kuwa marafiki zao. Sijui kama tunaelewana!

Japan ni rafiki wa karibu kila nchi anazozitengenezea magari hadi hivi leo.

Marekani ni rafiki azifaaye nchi zinazohitaji teknolojia zake za ulinzi na kadhalika.

Uarabuni ni rafiki wao woote wanaotumia mafuta.

Uchina na bidhaa za viwandani.

Kimsingi tuoende kuwekeza kwenye kujitengeneza kuwa marafiki bora kwa kutafuta tutakachowafaa jamii ya ulimwengu kuliko kuwaza watufae wao.

Ni kama msemo maarufu kuwa usitafute mume bora tu, jipange kuwa mke bora na vice versa: usitafute mke mwema tu, jipange haswa kuwa mume afaaye kwanza. Ova.
 
Asante sana ndugu yangu kwa maoni na mawazo haya mazuri. Najua umepitia shairi langu mwanzo mpaka mwisho; Kuna sehemu nimeandika: "Chakula cha Kiswahili tukipeleke Durban." sijasema chakula cha Kizulu kiletwe Dar es Salaam.

Hii maana yake ni kwamba, kwenye urafiki maalum 'Special Relationship' tunaangalia tulichobarikiwa zaidi ili tuweze kuwafaa wenzetu pia kwa hicho; mfano, kutokana na ardhi nzuri na bora tuliyobarikiwa nayo ifaayo kwa kilimo maana yake tunao uwezo wa kumlisha rafiki yetu au kuwalisha marafiki zetu.

Ninaposema Tanzania ni Rafiki wa Afrika Kusinj, maana yake tunaangalia Historia pia inasemaje? Nyakati za kupigania Uhuru wa Mataifa ya Kusini mwa Afrika, Tanzania ni Taifa lililowafaa sana marafiki zetu kwa kuwapa ufadhili wa mambo kadha wa kadha ukiwemo ufadhili wa hifadhi pale Mazimbu Morogoro, Tawi la Chuo Kikuu cha SUA; Solomon Mahlangu.

Hii inaamisha kuwa; 'Special Relationship' ni win win situation na wote mnanufaika; si kuwa tegemezi. Kuwa tegemezi ni Ukoloni Mamboleo, yaani unatawaliwa bila kujua.
 
Karibuni na asanteni nyote mnaoendelea kunipigia kura, kushukuru na kuwasilisha maoni yenu katika andiko hili.
 
Asante sana ndugu yangu kwa maoni na mawazo haya mazuri. Najua umepitia shairi langu mwanzo mpaka mwisho; Kuna sehemu nimeandika: "Chakula cha Kiswahili tukipeleke Durban." sijasema chakula cha Kizulu kiletwe Dar es Salaam.

Hii maana yake ni kwamba, kwenye urafiki maalum 'Special Relationship' tunaangalia tulichobarikiwa zaidi ili tuweze kuwafaa wenzetu pia kwa hicho; mfano, kutokana na ardhi nzuri na bora tuliyobarikiwa nayo ifaayo kwa kilimo maana yake tunao uwezo wa kumlisha rafiki yetu au kuwalisha marafiki zetu.

Ninaposema Tanzania ni Rafiki wa Afrika Kusinj, maana yake tunaangalia Historia pia inasemaje? Nyakati za kupigania Uhuru wa Mataifa ya Kusini mwa Afrika, Tanzania ni Taifa lililowafaa sana marafiki zetu kwa kuwapa ufadhili wa mambo kadha wa kadha ukiwemo ufadhili wa hifadhi pale Mazimbu Morogoro, Tawi la Chuo Kikuu cha SUA; Solomon Mahlangu.

Hii inaamisha kuwa; 'Special Relationship' ni win win situation na wote mnanufaika; si kuwa tegemezi. Kuwa tegemezi ni Ukoloni Mamboleo, yaani unatawaliwa bila kujua.
Nnaona, tumeelewana vizuri
 
Back
Top Bottom