Ahmed Rajab na Rais Mstaafu Jenerali Ibrahim Babangida

Hamid Rubawa

Member
May 23, 2018
72
202
Ahmed Rajab na Rais Mstaafu Jenerali Ibrahim Babangida

KAMA kuna mtawala wa kijeshi aliyewaweza Wanigeria basi alikuwa Ibrahim Badamasi Babangida (IBB) au “Maradona”, kwa umaarufu wake wa mitaani. Si bure kwamba alibandikwa lakabu hiyo ya jina la mchezaji soka maarufu wa zamani wa Argentina.

Sidhani kuwa kuna atakayesahau namna IBB alivyokuwa akicheza katika medani ya siasa za Nigeria, akiwapiga chenga Wanigeria wenzake, na hususan wanasiasa kwa miaka minane aliyokuwa madarakani (Agosti 27, 1985 hadi Agosti 27, 1993).

Alipokuwa Rais jina lake likitisha kushinda alivyo mwenyewe kwa umbo lake la wastani na kimo chake cha futi 5 na inchi 8. Chapa yake ni mwanya unaojitokeza kwenye meno yake ya mbele.

Asubuhi ya Jumamosi iliyopita ilinikuta njiani nikitokea Abuja, mji mkuu wa shirikisho la Nigeria, nikielekea Minna, mji mkuu wa jimbo la Niger. Gari niliyokuwa nikisafiria nayo iligeuka na kuwa kama Maradona wa zama zake kwani ikiyapiga chenga mashimo yaliyojaa barabarani.

Nilikuwa ninamuendea Babangida nyumbani kwake. Miadi yetu ilikuwa saa saba za mchana.

Ukitembea katika kurasa za maisha ya Babangida utakutana na mengi: umahiri wake, upole wake, ukarimu wake na jinsi anavyouthamini urafiki. Kwa hivyo, sikushangaa kwamba hakunitoa njiani nilipozungumza naye Alhamisi na kumwambia nikitaka kumhoji kwa ajili ya gazeti la Raia Mwema.

Alipokuwa Rais nilikuwa na mazoea ya kumtembelea ofisini mwake kwenye Ikulu ya Aso Rock kila nilipokuwa Abuja.

Siku zote akinipokea kwa uzuri nami hujiondokea nikiwa nimeokota mawili matatu katika mazungumzo yetu ama kuhusu siasa za Nigeria au za kwingineko.

Baada ya kuyaacha madaraka kwa kushinikizwa nilikutana naye mara mbili; mara moja nyumbani kwa rafiki yetu Abuja. Jina lake lilikuwa karibu linidondoke niulize yukoje Babangida pale mlango wa sebuleni ulipogonjwa na akaingia ndani.

Tulikula pamoja chakula cha mchana, tukapiga soga la kisiasa na alasiri ilipoingia akatuswalisha.

Mara ya pili ilikuwa London kwenye chumba cha hoteli aliyoshukia huyo rafiki yetu. Nilikuwa nishaanza kuwaaga waliokuwepo, mara mlango ukagongwa tukamuona Babangida ameingia.

Kuniona tu akanambia: “Ahmed, vipi unaanza kushuka kitumbo.”

Toka siku hiyo sikumshuhudia tena hadi Jumamosi iliyopita nilipomkuta ameketi sebuleni mwake, tabasamu ikichezacheza mdomoni. Aliponitupia jicho akaanza tena: “Naona unanenepa siku hizi.”

Nilimkuta akiwa kidogo dhaifu na nadhani akihisi maumivu ingawa hakunambia ila alinieleza tu kilichomsibu. Mgongo na miguu yakimpa taabu.

Nilipomuuliza tuna muda gani alinambia: “Muda wote uutakao. Sisi ni marafiki na lazima tusaidiane. Kama hatufanyi hivyo basi urafiki una faida gani? Na haya mahojiano yetu ni ya kihistoria kwa sababu hii ni mara yangu ya mwanzo kuzungumza na gazeti la Kiswahili.”

“Ingekuwa tunaishi zama zile za kupindua na kwa weledi wako wa kupindua huu ungekuwa wakati muwafaka wa kuipindua serikali ya sasa ya Nigeria” nilimwambia.

“Kwa nini ukasema hivyo?”

“Kwa sababu dunia imeshughulishwa na Donald Trump. Tena baadhi ya sababu zilizokufanya umpindue Rais Luteni-Jenerali Muhammadu Buhari 1985 bado zipo. Hali za maisha ni ngumu na Rais ni yuleyule Buhari. Na wewe ni gwiji wa kupindua.”

Babangida alicheka na akasema mambo yamebadilika sana tangu mapinduzi ya mwanzo Afrika yafanywe Misri mwaka 1952.

“Siku hizi umma unataka kushiriki katika siasa. Mapinduzi yamepitwa na wakati. Mwaka jana, 2015, watu hapa walikuwa wamechoka na ndiyo maana wakapiga kura kumuondosha kwenye madaraka Rais Goodluck Jonathan.”

Mnamo 1966, Babangida, akiwa na cheo cha Luteni, alishiriki kwa mara ya kwanza katika mapinduzi ya kijeshi.

Yalikuwa mapinduzi ya kupinga mapinduzi yaliyofanywa mapema mwaka huo na Jenerali Aguiyi Ironsi aliyeipindua serikali ya Waziri Mkuu, Sir Abubakar Tafawa Balewa. Ironsi aliuliwa na usukani akaushika Jenerali Yakubu Gowon.

Baada ya hapo, mapinduzi ya kijeshi yakamkolea Babangida na alishiriki katika takriban mapinduzi yote ya kijeshi ya Nigeria (Julai 1966, Februari 1976, Desemba 1983, Agosti 1985, Desemba 1985 and Aprili 1990).

Alilizima jaribio moja la mapinduzi lililofanywa na rafiki yake Kanali Buka Suka Dimka 1973.

Mapinduzi yaliyompa umaarufu ni yale yaliyompindua Buhari na yaliyomwezesha kuitawala Nigeria kwa miaka minane.

Kwa vile nilimtaja Trump, Babangida alimuelezea kuwa ni mtu mwenye kutisha.

“Kuhusu Afrika atahitaji kuwa na watu wenye ujuzi na wenye kuielewa Afrika na Ulimwengu wa Tatu wawe washauri wake,” alisema.

Nilimwambia kwamba Oktoba niliandika makala chini ya kichwa cha maneno kilichosema: “Kwa nini natamani Trump ambwage Clinton” (Raia Mwema, toleo la Oktoba 6, 2016). Nilimueleza sababu zangu na akazikubali.

Baada ya kurejelewa mfumo wa utawala wa kiraia, Babangida alijaribu mara mbili kutaka kupigania uchaguzi wa urais.

“Umesahau nini Ikulu hata ukawa na shauku ya kurudi tena?”

“Kuna kazi ambazo sikuzifanya na nyingine ambazo sikuzitimiza. Kwa mfano, dhana nzima ya ugatuzi ya kuifanya serikali kuu ya shirikisho isiwe na nguvu kubwa kama ilivyo sasa ili serikali za majimbo zipewe madaraka zaidi,” alisema.

“Si pahala pa serikali kuu kuendesha mambo ambayo yanaweza yakaendeshwa na makampuni ya watu binafsi.

“Serikali kuu ijishughulishe na sera ya nje, ulinzi, sera ya uchumi na usalama wa ndani ya nchi basi. Mengine yaachiwe biashara za kibinafsi ziyaendeshe.”

Moja ya mambo yaliyomkorofisha Babangida alipokuwa Rais ilikuwa namna ya kuleta mageuzi katika mfumo wa utawala kutoka wa kijeshi na kuufanya wa kiraia.

Madola ya Magharibi yakishikilia kwamba mfumo mpya usiweke kikomo cha idadi ya vyama vya siasa. Babangida akiamini kwamba pasiwe zaidi ya viwili.

Kwa sababu hiyo alijitwika mwenyewe dhima ya kuviunda vyama hivyo. Ingawa mwaka 1989 alihalalisha uundwaji wa vyama vya siasa, kufikia 1992 alivipiga marufuku vyama vyote na akaviasisi viwili vipya, kimoja kikielekea “kidogo mrengo wa kushoto” na kingine kikielekea “kidogo mrengo wa kulia.”

Huo ndio mwongozo alioutumia kuunda chama cha Social Democratic Party (SDP) na cha National Republican Convention (NRC).

Katika kipindi hicho siasa za Nigeria zilikuwa zi moto. Upinzani dhidi ya Babangida ulizidi na Aprili 22,1990 alikosewa chupuchupu kupinduliwa na Meja Gideon Orkar.

Wakati wa jaribio hilo la mapinduzi, Babangida alikuwa katika Kambi ya Dodan Barracks, Lagos, kulikokuwako makao makuu ya majeshi na makazi ya rais.

“Walipokuwa wakikwita Maradona uliona ni sifa au wakikukejeli?”

“Niliridhia kwani ndivyo Wanigeria wanavyofanya mambo yao. Siku zote huwapa viongozi lakabu. Waliniona nachelewesha mchakato wa majeshi kuacha madaraka na kuwapa raia utawala wakaona kuwa nawapiga chenga, na siku zile mpigaji chenga mkubwa duniani katika soka alikuwa Maradona. Kwa hivyo, mwandishi habari mmoja akanibandika lakabu hiyo na ikaniganda.”

“Ulipoyaacha madaraka akaingia Chifu Ernest Shonekan kuongoza serikali ya mpito haikuchukua muda, nikikumbuka ilikuwa miezi mitatu tu Jenerali Sani Abacha akampindua. Ulikuwa Misri wakati huo, ulihisi nini uliposikia kuhusu mapinduzi hayo?”

“Nikwambie kweli nikitaraji kuwa Abacha atafanya kitu kama hicho, nadhani alikuwa halipendi wazo la serikali ya mpito.”

“Ukimtilia shaka baada ya wewe kuondoka madarakani au kabla?”

“Nikimtilia shaka hata nilipokuwa Rais. Kulikuwa na nyendo za hapa na pale na harakati nyingi. Na watu wakisema kwamba yeye ndiye atayenirithi, kwa hivyo mtu akisikia habari kama hizo huanza kujiona kuwa kweli atakuwa mrithi.”

“Kwa hivyo ulimwacha kwenye wadhifa wake wa waziri wa ulinzi ukijua kwamba atapindua?”

“Kwa makusudi niliamua kumwacha aendelee kuwa waziri wa ulinzi kwa sababu nikihisi kuwako Abacha katika serikali kutawapa moyo raia kwamba hapatofanywa mapinduzi. Lakini Abacha alitushangaza sote.”

“Hamza al-Mustapha, mlinzi wa Abacha, anasema kuwa anaandika kitabu cha kumbukumbu zake na atawataja waliomuua Abacha na Abiola. Na ni watu hao hao. Unasemaje?”

“Sina la kusema tusubiri tuone yeye atasema nini.”

Hatimaye uchaguzi wa urais ulifanywa Juni 12, 1993. Mgombea wa chama cha SDP alikuwa Moshood Abiola na wa NRC alikuwa Bashir Tofa.

“Ninaikumbuka siku ya uchaguzi wa urais 1993. Ilikuwa Jumamosi na milango ya saa kumi na moja za alasiri, mtu wa karibu sana na wewe alinipigia simu kunambia kwamba Abiola anashinda na akanitaka nimpe maoni yangu ya nini cha kufanya.

Lakini kulikuwa hakuna cha kufanya isipokuwa kumtangaza kwamba ndiye mshindi. Kwanini hamkutaka awe mshindi na alikuwa rafiki yako?”

“Kweli alikuwa rafiki yangu mkubwa lakini nikijua kwamba akiwa Rais atapinduliwa tu. Alikuwa na uhasama na majeshi na majeshi yalikuwa hayamtaki awe amiri jeshi wao.”

“Kwa nini?”

“Kwa sababu ya alivyokuwa. Majeshi yalihisi kwamba alitumia rushwa kufika alipofika kisiasa na pia akishukiwa kwamba kwa sababu ya uhusiano wake na kampuni ya simu ya Marekani ya ITT angeweza kutumiwa na dola la nje. Kwa hivyo, kulikuwa na wasiwasi kuhusu usalama.”

“Ni wakati gani ulipwaya ukijihisi uko chini katika maisha yako?”

“Pale umma ulipoanza kuandamana, wanafunzi, vyama vya wafanyakazi na wananchi kwa jumla. Maandamano hayo yalikuwa kitisho kwa umoja na uthabiti wa taifa.”

“Ulihisi watu wamekuandama wewe binafsi?”

“Ndiyo na nilihutubu kwenye bunge nikiyaambia mabaraza ya bunge kwamba kama wakihisi mimi ndiye tatizo basi nilikuwa tayari kuyaacha madaraka.”

“Na watu wakikwita dikteta.”

“Nilijaribu kujitathmini na kujipima kirazini; na ndiyo, kweli nilikuwa dikteta.”

“Na nini kilikuwa kilele cha furaha yako.”

“Mafanikio yetu. Tuliijenga Abuja na miundombinu mingine juu ya kuwa hatukuwa na fedha nyingi. Hata hivyo tuliweza kuuendesha uchumi vizuri. Siku zile tukiuza pipa moja la mafuta kwa dola za Marekani $12. Na uchumi wetu ulistawi na kukua 1991/1992.

Ukilinganisha na fedha alizokuwa akipata Rais Obasanjo, sisi tulikuwa hatuchumi hivyo. Katika mwisho wa utawala pipa hilohilo moja likiuzwa kwa dola za Marekani $100.

Alichokuwa akichuma Obasanjo kwa mwaka mmoja ndicho nilichokuwa nikichuma kwa miaka yote minane ya utawala wangu.”

“Kadhalika kulikuwa na malalamiko mingine kuhusu utawala wako.”

“Ndiyo kwamba tulikuwa hatuheshimu utawala wa sheria.”

“Na kwamba mkifunga magazeti na hata kuwaua watu kama Dele Giwa.”

Dele Giwa alikuwa mhariri na mmoja wa waasisi wa gazeti la kila wiki la Newswatch. Siku moja aliletewa barua ya bomu na alipoifungua bomu likamripukia.

“Watu walitoa hukumu kuhusu kadhia ya Dele Giwa hata kabla ya uchunguzi kufanywa. Lakini sisi tuliunda Kamati ya Uchunguzi na kesi ilisikilizwa mahakamani mpaka kwenye mahakama ya rufaa na vyombo vyetu vya usalama havikupatikana na hatia yoyote.”

“Unahisi vipi kuhusu mauaji ya Mamman Vasta aliyehukumiwa kifo kwa uhaini wa kupanga kukupindua. Huyu alikuwa rafiki yako, mlisoma pamoja na mlikuwa pamoja.”

“Kuna sehemu ya kadhia hiyo ambayo hukuipata. Uvumi ulipoanza kuenea kwamba alikuwa akipanga kupindua alinipigia simu na akanambia anataka kuja kuniona ofisini mwangu lakini lazima pia awepo rafiki yetu mwengine, J Nasko (Jenerali Gado Nasko).

Walipokuja alinambia kwamba akitaka Nasko awe shahidi na kwamba mkewe alikuwa akilia akimwambia alisikia tetesi hizo na akamtaka anijie kunieleza kwamba si kweli.

“Nikamwambia kuwa mimi sikuamini kuwa kulikuwa na mpango kama huo na ndio maana sikumwambia kitu. Nikasema kwamba kama kulikuwa na mpango wa kupindua basi wao wawili ndio waliohusika kwa sababu hata jina la Nasko likitajwa isipokuwa langu kwa sababu siwezi kujipindua mwenyewe.

“Nilijaribu kumkinga lakini ripoti za usalama tulizokuwa tukizipata zilionyesha kwamba mimi nilikosea. Kwa hivyo, nikaamrisha awekwe kwenye kizuizi cha nyumbani. Na akajaribu kutoroka. Sasa kama huna hatia kwanini utataka kutoroka kutoka kwenye kizuizi cha nyumbani kwako mwenyewe?

“Kwa bahati mbaya alihukumiwa kwa sheria ya 1979 ambayo hukumu kwa kosa la uhaini ni kuuliwa kwa kupigwa risasi.”

“Kwani hukuwa na nguvu za kumsamehe au kumpunguzia hukumu?”

“Nilikuwa nazo lakini lakini ingekuwa hatari ningefanya hivyo.”

“Unajua mjane wake anasemaje? Anasema kwamba wewe ndiye uliyempa Vasta mke kwa sababu ndiye uliyetia saini ya ndoa yake na wewe ndiye uliyetia saini amri ya kuuliwa kwake. Ni maneno mazito hayo.”

“Ngoja nikwambie kitu. Kuna msichana mmoja mdogo anasoma kwenye skuli yetu. Huja huja hapa nyumbani kuogolea kwenye bwawa. Siku moja alinambia kwamba kasikia kuwa mimi ni rafiki wa babu yake.

Nikamuuliza nani babu yake. Akanambia Mamman Vasta. Nikamjibu kwamba kweli alikuwa rafiki yangu mkubwa. Halafu akataka kujua kilitokea nini. Nilimwambia asubiri mpaka akue, atasoma na atafahamu.

Nitamwambia nini msichana wa miaka 12? Lakini kukwambia kweli aliponiuliza swali hilo nilihisi vibaya. Sikuwa na raha hata kidogo.

“Una matumaini kwa Nigeria chini ya Buhari? Itategemea Ahmed. Kipindi chake ni cha miaka minne na kutokana na uzoefu wangu hawezi kuibadili nchi katika kipindi hicho. Lakini nina matumaini mema kuhusu Nigeria na kwa kizazi kijacho.”

“Siku moja nilipokuwa ofisini mwako Ikulu uliniuliza nikitoka Nigeria nitaelekea wapi.

Nilipokujibu na kukutajia kwamba nitaonana na Rais nchi hiyo uliruka na ukanambia ‘ya nini kwenda kumuona kisirani yule’. Alikufanya nini hata ukanambia hivyo/‘

Babagida aliangua kicheko halafu akasema:

“Siku ile nilikuwa bado sijawahi kukutana naye lakini nilipata habari zake kutoka kwa mtu aliyekuwa karibu naye. (Babangida akanitajia jina la mtu huyo) lakini baadaye nilipomuona Rais yule alinieleza kwanini alilazimika kutawala kwa mkono wa chuma na nilibadili maoni yangu juu yake.”

“Viongozi gani wenzako wa Kiafrika unaowakosa na unaowatamani?”

“Utashangaa lakini ni Jerry Rawlings (aliyekuwa Rais wa Ghana), Félix Houphouët-Boigny (wa Côte d’Ivoire) akiipenda sana Nigeria na nisimsahau Hosni Mubarak (wa Misri). Tukiheshimiana.”

Zamani Babangida aliwahi kunambia kwamba nikienda kwake nisisahau kuungalia mlango wa Kizanzibari aliopewa zawadi na Rais mstaafu Dk. Salmin Amour.

Kwa hivyo, Jumamosi iliyopita nilimwacha akiketi nilipomkuta nikaenda nje kwenye msikiti wa nyumbani kwake kuuangalia huo mlango wenye asili moja na mimi.

Screenshot_20230823-135515_Gmail.jpg
Screenshot_20230823-135538_Gmail.jpg
 
Ila Ahmed Rajab ni jasusi wetu,kapenya ikulu nyingi Sana,hata mwalimu zilikua zinaiva sana
 
Back
Top Bottom