Adaiwa kumuua mpenzi wake kwenye makazi ya askari Kunduchi kisa wivu wa mapenzi

SteveMollel

JF-Expert Member
Jul 12, 2015
8,433
23,754
Kota za polisi, Kunduchi. Majira ya saa nane mchana leo hii..

Wakati mambo mengine yakiwa yanaendelea kama kawaida, watu walisikia kelele na purukushani kutoka kwenye ghorofa ya juu kabisa katika jengo la block G, chumba namba 30.

Kelele hizo hazikuwa za sherehe, ni mwanaume alikuwa anang'aka kwa sauti kubwa ya kwamba anataka mtoto wake! Anataka mtoto wake! Sauti kubwa, sauti ya amri.

Sauti ya mwanamke nayo ilipaza kutoka chumba hicho kumkambili mwanaume huyo ya kwamba mtoto huyo si wake.

Makelele hayo yakawafanya watu walokuwepo chini watazame huko juu kujua kwani kunani?

Pale chini ya ghorofa, umbali wa mita kadhaa, kulikuwa na kijana wa bodaboda, wateja wa genge lililopo karibu na pia watu kadhaa wanaoendelea na shughuli zao zingine. Watu hao wote waliacha waliyokuwa wanafanya wakaangaza macho yao kule juu kunapotokea kelele.

Kelele zile zikaendelea, kitambo kidogo, kama vile utani, dirisha likafunguliwa akatolewa mtoto mdogo, mtoto wa miezi kadhaa.

Mtoto huyo alikuwa ameshikiliwa na mwanamke ambaye ni mama yake mzazi, kufumba na kufumbua mtoto huyo akarushiwa nje kana kwamba mdoli!

Ni kheri wale watu waliokuwa wanaangaza hapo kwa kustaajabu, waliwahi kumnusuru mtoto yule kwa kumdaka, hata sasa mtoto anaendelea vema kabisa, anastaajabu tu yanayoendelea, mara ya mwisho mimi naondoka kwenye eneo la tukio alikuwa amehifadhiwa ndani ya bajaji, masikini ameketi anabung'aa.

Baada ya mtoto kurushwa, bado zogo likiwa linaendelea, kufumba na kufumbua, mwanamke naye akajitupa akitokea palepale dirishani!

Bahati mbaya alinguka vibaya sana, kichwa kiligota chini, damu zikamwagika.

Watu wakiwa wanastaajabu, wanajongea karibu kumtazama mwanamke huyu anayegugumia kifo, wakitazama kule dirishani alipotokea, mara bwana yule aliyekuwa anazoza naye kule juu akashuka ngazi akiwa ameshikilia kisu.

Anaujia mwili wa mwanamke yule huku naye akijikita kisu tumboni, analia kwa maumivu lakini haachi kujidunga, si mara moja wala mbili, damu zinamiminika lakini hajali!

Wale watu wachache waliokuwa wameusonga mwili wa mwanamke yule, kitendo cha kumwona bwana huyu anakuja, ameshikilia kisu, na tena akiwa anajidhuru mweyewe bila ya huruma, wote wakakimbia kujinusuru.

Mwanaume yule, kama vile maigizo, akamkita kisu mwanamke yule alokuwa amelala chini, si kisu kimoja wala viwili! Mpaka mwanaume mmoja jirani, alipojitosa kumshika bwana huyo mkono wenye kisu, tayari hali ya mwanamke ni mbaya sana.

Hajigusi, hajiwezi!

Aliwahishwa hospitali lakini kiukweli ni muujiza tu ndio unaweza kumwokoa dhidi ya kifo, si kingine.

Bwana yule naye akiwa anavuja damu, utumbo umetoka nje, alisaidiwa kutulizwa hapo chini, akapewa huduma ya upesi kuzuia damu nyingi zilizokuwa zinammwagika

Yupo amelala chini analalamika na kukoroma, maumivu makali, anataka kufa.

Kwa maelezo ya bwana huyo, akiongea na kukatakata kwa maumivu, yeye ametokea gongolamboto wala si mkazi wa hapo. Yeye alikuwa amekuja kumfuata mwanamke huyo hapo baada ya kupewa taarifa kwani alimtoroka na kuja kuishi na mwanaume mwingine ambaye ni askari. Mambo mengine kuyasema ni tabu, hasemi sentensi moja akaimaliza.

Baadae mume wa yule mwanamke alodungwa kisu, yaani askari, alifika katika eneo la tukio akiwa ameongozana na maaskari wenzake baada ya kupata taarifa ya majanga yalotokea nyumbani kwake, macho yake mekundu yanalenga machozi.

Akiwa na uchungu, alimfuata kwa shari bwana yule alokuwa amelala chini, bwana alomdunga visu mkewe, lakini watu wakamuwahi kumshika ili kuepusha shari.

Bwana huyo naye akawa anasema, nataka kumwona mwanangu, namtaka mtoto wangu! Yani hali ni tafarani. Polisi wengine wakiwa wanachukua maelezo kwa mashahidi.

Walimwondoa bwana huyo kando, gari likaja na kumbeba majeruhi yule kumpeleka mahali stahiki.

Update: Kufikia sasa, majira ya saa kumi na mbili kasoro jioni, habari zimetufikia ya kwamba mwanamke yule amefariki dunia. Hatujui kama bwana yule naye atapona ama lah?

Ujasiri aliounyesha kwa kuja kwenye nyumba ya watu, ndani ya kambi ya polisi, akiwa amepanda magari mawili mpaka kufika hapa, kwakweli ni wa aina yake.

Bila shaka alikuja hapa akiwa ameamua lake moja.

Moja tu.

Kweli ni huzuni.

Wanawake mtatuuua.

Nahangaika kuituma video hapa bila mafanikio..
 
Nimeogopa sana, sana! Kuna la kujifunza hapa lakini mambo yakienda mrama kwenye mapenzi hakuna haja ya kuuana jamani!

Mbona watu wako wengi sana kukatisha uhai kwa ajili ya mtu mmoja?
It’s not worth it.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom