Superman
JF-Expert Member
- Mar 31, 2007
- 5,695
- 1,696
- Thread starter
- #321
Napendekeza kuwa vipaumbele katika Uchaguzi wa 2010 viwe kama vifuatavyo;
- Katiba: Katiba ya nchi ina mapungufu mengi na makubwa. Katiba ndio dira ya uongozi na ustawi wa jamii huru. Katiba haiwezi kutungwa kwa matakwa ya wachache wenye mahitaji ya kujitwalia kila lililo bora katika nchi. Katiba ni lazima ijenge usawa na haki kwa watu wote bila kujali nafasi zao katika jamii. Katiba lazima ijenge heshima kwa wananchi kati yao na kwa nchi yao. Katiba ni lazima ijenge uwajibikaji. Serikali ijayo ihakikishe kuwa wananchi wote wenye uwezo wa kushiriki katika kuandaa na kutunga Katiba wanashirikishwa (kwa kuchagua) katika utungaji wa Katiba ya nchi. Kuachia kundi la wanasiasa wachache kutunga Katiba ni kunyima haki na kuondoa usawa muhimu kwa Taifa.
- Afya: Jinsi gani serikali ijayo itakavyohakikisha afya za wananchi wake zinaboreshwa. Hii inahusu zaidi mapambano ya nguvu dhidi ya Malaria, maambukizo ya ukimwi, na magonjwa mengine, uboreshaji na uongezaji wa hali na idadi ya hospitali/zahanati, madaktari, vitendea kazi na dawa baridi
- Elimu: Jinsi gani serikali ijayo itakavyo hakikisha elimu inatolewa kwa wote wenye kuihitaji ili kuondokana na ujinga na kuongeza uwezo wa uzalishaji, ubunifu na kuepukana na umasikini. Wananchi wenye elimu nzuri wanaweza kuliingizia taifa mapato makubwa kwa kutumika katika juhudi za maendeleo na pia kukodisha wataalamu kwa nchi zinazohitaji utaalam huo.
- Miundombinu: Serikali ijayo inahakikisha vipi kuwa barabara, njia za reli na usalama wa majini zinaboreshwa na kuwa za viwango vya juu ili kuwezesha unafuu wa uchukuzi wa mazao ya kilimo na urahisi wa usambazaji wa huduma za jamii ikiwemo ulinzi na usalama, elimu na afya na kadhalika. Vile vile, ili kuwezesha kupunguza ajali zinazoligharimu Taifa kutokana na upotevu wa maisha ya wananchi wake, upungufu wa nguvu kazi kutokana na muda wa matibabu na hata kupunguza uwezo wa wahusika kwenye ajili hizo kuzalisha kwa kiwango kizuri kama inavyotakiwa.
- Kilimo cha kisasa: Kwa kuwa Taifa lina ardhi nzuri yenye rutuba na ukubwa wa kutosha, serikali ijayo ifanye jitihada kuhakikisha ardhi hiyo inatumika vizuri katika uzalishaji wa mazao ya kilimo na biashara ili kuwezesha nchi kuzalisha chakula cha kutosha na kuongeza pato la Taifa kutokana na kilimo. Kwa kutumia kilimo, wakulima wataweza kujikimu na hali ngumu ya maisha kwa kuweza kuhakikisha ustawi wa familia zao na kujemga Taifa huru zaidi lenye kujitosheleza kwa chakula na bidhaa nyinginezo za mashambani. Vile vile kilimo kitapunguza tabia ya watu kuwa wachuuzi kwa bidhaa zinazozalishwa nje ya nchi.
- Viwanda: Serikali ijayo itakuwa na mpango gani wa kuanzisha viwanda vya usindikaji wa mazao ya wakulima na uzalishaji wa bidhaa nyingine za majumbani, maofisini na sehemu nyingine kama zinavyohitajika na jamii? Kwa kukuza viwanda, serikali itaweza kuhakikishia wakulima soko la mazao yao, kuongeza ushindani na bidhaa za nje, kuongeza ajira kwa watu wake na kuongeza pato la Taifa. Vile vile, viwanda vitaifanya nchi iwe na heshima duniani kwa kuwa na watu wenye ujuzi na ubunifu na wenye kipato kinachoridhisha zaidi.
- Ulinzi na Usalama: Serikali ijayo inatakiwa iwe na uwezo wa kuhakikisha kuwa mali na hali za watu wake zinalindwa kila wakati ili kuwawezesha kuzalisha zaidi, kufurahia mafanikio yao na kujenga uzalendo kwa nchi yao. Nchi salama ina uwezo mkubwa zaidi ya kukua kiuchumi na kujenga jamii yenye umoja.
- Ushirikishwaji wa Umma: Tanzania itajengwa na watanzania. Serikali ijayo ihakikishe kuwa watanzania wa rika zote, wenye uwezo wa kushiriki katika ujenzi wa Taifa wanashirikishwa ipasavyo katika kuamua, kujenga na kufurahia matunda ya nchi yao.
- Na mengine yoyote kama yatakavyochangiwa na wengine.
Du! Recta ulikuwa wapi muda wote huu toka jana?
Kwa kweli nondo zako ni makini sana na zimekamilika.
Hata hivyo ukipenda kuboresha zaidi unakaribishwa.
Hii issue ya Ulinzi na Usalama, unaweza ukaielezea kwa undani zaidi?