Zitto Kabwe: Adui, Rafiki, Kipenzi

Hussein Massanza

JF-Expert Member
Dec 26, 2012
918
1,994
Zitto Kabwe ni adui yao, akina nani hao? Ni rafiki yao, hao wenye uswahiba naye wapoje? Ni kipenzi chao, wasifu wa hao wanaompenda ni upi? Andiko hili linachambua kila kipengele katika muktadha mpana.

ADUI

Kunguni ni mdudu anayechukiwa sana na binadamu. Hawezi kuwa na jema hata kidogo. Huo wema wa kunguni umeanza lini? Ni mchokozi, msumbufu, mharibu starehe ya usingizi. Sisi tuliopitia maisha ya kulala na kunguni tunaelewa. Ambao hawajapitia, heri yao!

Wasifu huo ndiyo ukaibuka msemo wa "damu ya kunguni", anayesemwa au kujisema kuwa na damu ya kunguni maana yake anachukiwa na watu. Hana jema, kila atakalofanya, litageuzwa kwa uzuri wake kisha kupewa sifa mbaya. Lengo kuu ni kwamba aonekane mbaya kila siku.

Unamsifiaje mtu mwenye damu ya kunguni mbele za watu? Kama hutachekwa, basi na wewe utachukiwa. Utawekwa kapu moja na mwenye damu ya kunguni. Almasi ya mwenye damu damu ya kunguni ni chupa, dhahabu ni shaba.
Pamoja na kazi kubwa aliyofanya, akiongoza kamati yake ya Hesabu za Serikali (PAC) kusoma, kuchambua na kutafsiri makabrasha ya ripoti ya CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali) kuhusiana na skendo ya Tegeta Escrow, na kutoa mapendekezo.

Pamoja na kuukataa usingizi, kuamua kukesha akilinda ripoti ya PAC ili kuhakikisha haichakachuliwi kwa namna yoyote ile. Pamoja na ushujaa wa kuchambua madudu katika Akaunti ya Tegeta Escrow na kuwaumbua (naming and shaming) wahusika, bado damu ya kunguni ilidhihirika kuwamo ndani ya Zitto.

Kosa lake lilikuwa kuunga mkono muundo wa pendekezo (formulation), lililotolewa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge. Lililohusu namna ya kuishauri serikali (mamlaka ya uteuzi), kuchukua hatua za kumwajibisha Katibu Mkuu aliyesimamishwa, Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi.

Kabla ya Chenge, kila pendekezo liligonga mwamba, Spika Anne Makinda, alitaka lugha laini zaidi katika kuishauri serikali. Chenge alipotoa formulation yake, ikaungwa mkono haraka sana. Spika akaona ina nafuu kubwa. Zitto na Halima Mdee waliiunga mkono, wabunge wengi wa CCM wakashangilia.

Zitto akashauri, mapendekezo yaliyobaki ambayo yaliwagonga nyundo moja kwa moja, Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, yaandikwe kama Chenge alivyoshauri.

Spika Makinda akaona "mambo si ndiyo hayo", akakubali, wabunge wa CCM wakagonga meza kwa fujo. Spika akawauliza wabunge, sauti ya wengi ikasikika "ndiyoooo". Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, akashtuka, akasema hapana, "mnatuburuza."

Msimamo wa Mbowe ukaibua zogo bungeni. Wabunge wa upinzani, hususan wale wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wakamuonaZitto msaliti. Inakuwaje anakubali pendekezo la Chenge?

Zitto alishakuwa na sifa ya usaliti. Kwamba anakisaliti chama chake (Chadema) na upinzani kwa jumla. Kitendo kile cha kuunga mkono pendekezo la Chenge, akatafsirika kama "mja asili asiyesahau asili yake", alionekana amerudia zake za usaliti.

Chenge pia ni walewale wa damu ya kunguni, kwa hiyo hana jema. Pendekezo litolewe na Chenge? Haikuingia akilini kabisa kwa wapinzani! Kosa kubwa ni kwamba wapinzani badala ya kutathmini na kuona ubora au ubaya wa pendekezo la Chenge, wao wakamwangalia mtoa pendekezo, Chenge!

Laiti ‘msumari' wa Zitto kwa kugandamizia pendekezo la Chenge, ungepita, leo hii Waziri Mkuu na Masele nao wangekuwa tumbo joto. Haikuwa hivyo, wapinzani walimuona Zitto anasaliti kwa sababu hawaamini katika "baniani mbaya kiatu chake dawa", kwao Chenge ni baniani ambaye kiatu chake hakiwezi kuwa dawa, asilani, abadan!

Baada ya hapo, mitandao ya kijamii ikaingia kazini, Zitto alishambuliwa kwelikweli. Wachache waliojua ubora wa pendekezo la Chenge, walitetea kuwa Zitto alikuwa mjanja sana, mwenye akili akili za kimkakati kuunga mkono pendekezo la Chenge. Wengi hawakumwelewa, walimshambulia, walimponda.

Kama alichokisema Zitto, kingetamkwa na Tundu Lissu, hali isingekuwa mbaya kwa kiasi kile. Tatizo la Zitto ana damu ya kunguni. Alivyokuwa anatenda kazi yake kwa umahiri mkubwa, wasiomwamini walikuwa wanamfuatilia kwa umakini, wakiamini lipo eneo atateleza wamseme.

Zitto ni sawa na mchezaji mzuri asiyependwa. Kama ilivyowahi kutokea kwa Ryan Giggs, Manchester United au hata hapa Tanzania Haruna Niyonzima, Yanga, na wengineo, wakishika mpira, wanacheza vizuri sana, wanafanya mambo mengi makubwa yanayostahili pongezi lakini hawashangiliwi, ila kosa moja litasababisha azomewe kila upande. Kisa hawampendi, amewaudhi! Siku hizi Niyonzima hazomewi.

Wakati wa kuelekea kusomwa kwa ripoti ya PAC kuhusiana na Tegeta Escrow, pamoja na kuwepo kwa watu kumuunga mkono Zitto na kumtia moyo kwamba asiogope, wapo nyuma yake, wapo waliotamka bila kificho: "Zitto ni msaliti, muda utakapofika atapindisha ukweli ili kuwaokoa wachotaji wa fedha za Tegeta Escrow."

Kwao, Zitto na waliochota fedha za Escrow ni walewale. Kwa maana hiyo walitoa angalizo huku wakimfuatilia kwa makini mithili ya macho ya mashabiki kwa mchezaji mzuri wasiyempenda anapokuwa anachanja mbuga na kupiga chenga za maudhi uwanjani, wakisubiri akosee wamzoemee. Alipounga mkono tu pendekezo la Chenge, wakazomea, wakasema "si tulisema!"

Hata baadaye, ipo hoja iliibuka kwamba katika Tegeta Escrow, Zitto alitumiwa na makundi ya CCM kwa ajili ya mnyukano wa mbio za Urais 2015. Wapo waliosema ‘alishikishwa' kiasi kikubwa cha fedha na mzee Reginald Mengi ili kumwadabisha Muhongo kwa sababu wana bifu la vitalu vya gesi.

Hayo ni matokeo ya kuwa na damu ya kunguni, ufanya jema litageuzwa kuwa baya na ukitenda baya ndiyo kabisa. Katika mazingira kama hayo, wengi hujikuta wanayumba. Japo anajitahidi kubaki kwenye mstari, mara nyingi Zitto ameshayumbishwa na mashambulizi mpaka kujikuta anajibishana na wanaomchokonoa, au kutamka yasiyopendeza.

Zitto ni adui wa CCM, kwa maana ni mbunge mnoko. Kazi yake imeshaivua nguo serikali ya CCM mara kadhaa. Ni kiherehere, kwa sababu anafuatilia sana. Na akishafuatilia hana siri, haraka sana yataonekana mitandaoni, Twitter, Facebook na kadhalika kabla ya kufika bungeni.

Unoko wa Zitto unaosababisha asipendwe na CCM pamoja na serikali; Palipo na wizi au kashfa yoyote ile, lazima kivuli chake kitaonekana na atasema kuhusu skendo husika. Hali hiyo imesababisha aingie kwenye misukosuko mingi. Muwinda huwindwa!

Mwaka juzi, katika Bunge la Bajeti, kuelekea bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, Bodi ya Tanesco ilimsimamisha kazi, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu, William Mhando. Baada ya uamuzi huo, ikaibuka kashfa kuwa bodi ilifanya makosa ya kukiuka sheria ya manunuzi katika kununua mafuta ghafi.

Ikabainika kuwa pamoja na makosa ambayo Mhando anatajwa kuwa nayo, yapo maelezo kuwa tofauti yake na bodi, ilisababishwa na yeye kupinga ukiukwaji wa makusudi wa sheria ya manunuzi. Kwamba mshindi wa zabuni ananyimwa halafu anapewa aliyeshindwa.

Zabuni imetangazwa, makampuni kadhaa yamejitokeza kuwania tenda. Kila moja inatangaza ofa yake, baadaye baada ya kupima vigezo kampuni moja ikashinda. Ajabu iliyopewa tenda ikawa kampuni tofauti na ile iliyoshindaa. Hiyo ni kashfa, na kulikuwa na sura ya wazi kwamba rushwa ilichukua nafasi.

Zitto akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) wakati huo, akamwandikia barua Spika Makinda, kuomba kamati yake iruhusiwe na bunge kuhoji pande zote mbili, Mhando na bodi ya Tanesco.

Haraka sana picha likageuka; Ikaelezwa kuwa Zitto alihongwa na makampuni ya mafuta kwa ajili ya kumtetea Mhando. Hali ilikuwa mbaya sana mpaka akaita mkutano na waandishi wa habari kujitetea lakini haikusaidia. Ilisababisha mpaka baadhi ya wabunge kuomba uongozi wa POAC uondolewe.

Spika Makinda alipoiagiza Kamati ya Ngwilizi (Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi) kufanya uchunguzi, ikabainika Maswi na Muhongo, walisema uongo kwa lengo la kushawishi bajeti yao ipite na kuwadhibiti waliokuwa wakiipinga kwa kupitia kashfa ya ununuzi wa mauta ghafi.

Kipindi hicho, Zitto alitoka kwenye mstari, alimtumia SMS Maswi akamwambia: "Maswi sijawahi kugombana na wewe kwa kuwa nakuheshimu sana. Tuhuma ambazo wewe na waziri wako mnazitoa dhidi yangu ni uongo, uzushi na za kupikwa.

"Mwambie waziri wako na wewe binafsi, sijawahi kushindwa vita ya kulinda credibility yangu, sipendi ujinga hata kidogo, mimi nina uhuru wa kusema ninachokiamini, sina bei, tupambane tu tuone nani ataumia."

Maswi na Muhongo walionywa na bunge wakati huo, ila baada ya matokeo ya sasa katika skendo ya Tegeta Escrow, tayari Maswi ameshasimamishwa kazi, Muhongo anaendelea kuvutiwa ‘uradi kwa tasbihi'. Swali nani ameumia? Majibu yapo wazi.

Siri moja, ukiwa mtu halisi hutafeli hata mara moja. Vita ya Maswi na Muhongo upande mmoja na Zitto upande wa pili, inanipa majibu kuwa mkweli ameendelea kuwa imara pamoja na misukosuko yote. Mzushi, pigo moja tu, leo yupo chali. Kwa hapa Zitto ni halisi zaidi.

Zitto akaichachafya serikali ya CCM; Alimtaja Waziri wa Fedha wakati huo, Mustafa Mkullo kwamba ni fisadi, kisha akalinyooshea kidole Baraza la Mawaziri kwamba lilihongwa ili kulifuta Shirika Hodhi la Rasilimali za Mashrika ya Umma (CHC) kwa sababu za kifisadi.

Mawaziri wakawa wakali, wakamtaka Zitto athibitishe, yeye aliwasilisha uthibitisho wake na kuanzia hapo ikawa kimya. Mawaziri walinywea! Haihitaji kutumia darubini kujua kuwa Zitto ni adui wa Baraza la Mawaziri kwa sababu alisema lilihongwa. Mawaziri hawawezi kumpenda. Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri ni Rais, kwa maana hiyo JK hawezi kumfurahia.

Mkullo alisema Zitto anatumika na kwamba anahongwa. Zitto akatoa uwanja huru, kila mmoja aruhusu kuchunguzwa ikibainika yeye (Zitto) amewahi kuhongwa, atajiuzulu uenyekiti wa POAC, ubunge na ataacha siasa.

Akamtaka Mkullo kutangaza kuwa tayari kuuacha uwaziri endapo itathibitika amehusika na ufisadi akiwa Waziri wa Fedha. Mkullo alinywea lakini ripoti ya CAG ya mwaka 2012, ilimng'oa Mkullo pamoja na mawaziri wengine saba.

Kabla ya kung'oka, mawaziri walikuwa wabishi, Zitto akaanzisha mchakato wa kukusanya saini 70 ili zihalalishe hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu. Mambo kabla hayajawa mabaya sana, Mkuu wa Nchi aliwaondosha mawaziri wote waliokumbwa na kashfa. Je, huyo si adui wa serikali ya CCM?

Ni Zitto aliyetimuliwa bungeni mwaka 2007 kwa sababu ya kupeleka bungeni hoja ya Buzwagi, akimtaja aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, kusaini mkataba kimagumashi, kinyume hata na agizo la Rais, aliyetaka isisainiwe mikataba mipya ya madini mpaka kwanza ile ya awali ipitiwe upya.

Zitto akaonekana mbeya, kizabizabina, aliyekusudia kuivua nguo serikali na kumharibia ulaji Karamagi, akasimamishwa kuhudhuria vikao vya bunge. Hii ni kuthibitisha kuwa Zitto ni adui wa CCM na ubunge wake umekuwa mwiba kwa maovu ndani ya Serikali ya CCM.

Mwaka 2008, baada ya hotuba ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alipotangaza kujiuzulu, Zitto aliomba muongozo kwamba kwa mujibu wa Katiba, Waziri Mkuu anapojiuzulu na Baraza la Mawaziri linavunjika, kwa maana hiyo mawaziri wote hawana kazi. Mawaziri walimzomea, walimuona mnoko, anayechonga sana. Walipinga! Hawakujua wanapinga Katiba.

Ni Zitto ambaye alishawekewa sumu kwenye maziwa, akaokolewa na simu ya marehemu Amina Chifupa, aliyemwambia asiendelee kunywa, ni sumu. Akatibiwa Hospitali ya Rufaa, Bugando, Mwanza. Ni Zitto aliyenusurika kifo kwa ajali kadhaa, ikiwemo zilizotajwa kusukwa!

Ni adui wa wapinzani, maana anaonekana ni msaliti, anayetumiwa na CCM kudhoofsha upinzani nchini. Zilishatolewa ripoti kadhaa (japo hazikuwahi kuthibitishwa), zikionesha namna Zitto alivyo na ukaribu na Usalama wa Taifa pamoja na Serikali.

Taarifa kwamba Zitto ni msaliti wa upinzani, zilianza tangu mwaka 2008. Maneno hayo yameendelea kuchukua nafasi mpaka leo. Sura hiyo imemfanya Zitto kuonekana kibaraka, mamluki wa CCM. Wasambazaji wa maneno haya walifaulu, ila hawakuweza kummaliza.

Hiyo ndiyo sababu ya Zitto anapokuwa kwenye wakati muhimu zaidi kushughulikia mambo nyeti kwa taifa, badala ya kuungwa mkono kwa asilimia 100, wapinzani wanakuwa wanamtolea macho, wakivizia akosee wamzomee!
Uthubutu wake wa kutaka vyama vyote vya siasa vinavyopata ruzuku serikalini vikaguliwe na kusisitiza kwamba havijakaguliwa, uliongeza kasi ya kuonekana msaliti wa upinzani na kwa chama chake (Chadema). Akawa adui mkubwa wa wapinzani. CCM nayo ikazidi kumuona mnoko, adui, ukaguzi-ukaguzi nini?

RAFIKI

Zitto ni rafiki wanamageuzi, wanaoamini
katika fikra huru za kisiasa. Wanaopenda siasa za mawazo huria pasipo kubanwa na vyama. Hii ndiyo sababu wale wanaoonekana vimbelembele, kuongeaongea, kuzozazoza bila kukistahi chama chao cha CCM, kama Deo Filikunjombe, Kangi Lugora na wengineo, ni marafiki hasa wa Zitto.

Anne Kilango Malecela (CCM), aliwahi kuniambia kuwa anampenda na kumwamini sana Zitto kwa sababu ni mwanasiasa mwelewa asiye na katikati. Kilango: "Kama Zitto anaona kitu hakipo sawa, atasimamia hivyo mpaka mwisho."
January Makamba aliwahi kumzungumzia Zitto: "Ni mwanasiasa ambaye sitapata shida kufanya naye kazi kwa sababu anapenda ushirikiano. Anapokuwa na hoja yake, huzungumza na wabunge wa vyama vyote bila kubagua, ndiyo maana mara nyingi hoja zake huungwa mkono na wengi."

Kwa wanamageuzi, Zitto amekuwa kielelezo cha uswahiba naye kutokana na kumbukumbu ya alichokifanya katika skendo ya Buzwagi, saini za kumng'oa Waziri Mkuu, Tegeta Escrow na kadhalika.

Ni hao ambao wamekuwa wakijiuliza, kama Zitto ni mamluki, mbona ni yeye ambaye amekuwa mstari wa mbele kuanzisha hoja nzito za kuitikisa Serikali? Hata katika Tegeta Escrow, naye alitajwa kupokea mgawo, swali: Ni mtu gani anayeweza kula rushwa halafu akamuumbua aliyempa?

KIPENZI

Zitto ni kipenzi cha wasanii hasa wanamuziki wa kizazi kipya. Ndiye mwanasiasa ambaye jina lake linasikika kwenye nyimbo nyingi, kuliko mwingine yeyote. Vilevile watoto wa shule na vijana vyuoni, wanampenda na kumchukulia kama kioo cha maisha yao yajayo, kwa wale wanaoota kuwa wanasiasa.

Mpango wake wa kupigania haki za wasanii na kufanikisha kuzifanya kazi za sanaa kuwa biashara rasmi inayotambulika serikalini, iliongeza chachu kwa wasanii kumpenda, ingawa hata kabla, alikuwa kipenzi chao.

Haiba yake, ndiyo sababu ya wanamuziki Bwana Misosi, Ben Pol, Jay More, Roma, Kala Jeremiah na wengine wengi kumuimba katika nyimbo zao.

Mradi aliouanzisha wa Kigoma All Stars "Leka Dutigite", kusaidia wanamuziki wa Mkoa wa Kigoma kujiunda pamoja kama kampuni na wote kuunganishwa kwenye Shirika la Hifadhi ya Jamii la NSSF, hivyo kuwezesha kupata bima ya afya, ni pointi nyingine iliyofanya wasanii wampende zaidi.

Ukiwa bungeni, utajionea jinsi watoto wanavyompenda Zitto. Wanapokwenda bungeni kwa ajili ya ziara ya kujifunza (study tour), wanapomuona Zitto huchanganyikiwa. Humkumbilia, kumkumbatia na kupiga naye picha. Wanampenda! Ni kipenzi chao!

By Luqman Maloto
 
Hakika zitto ni kijana msomi uwezo wake na weledi wake n wakutukuka.ameonyesha njia na nia na kuwa mfano wa kuigwa kwa wanasiasa wasomi hasa vijana.hakika bwana huyu amaeonyesha uwezo wake na kukubalika bila ya unafiki mkubwa kwa makundi yote ya siasa upinzani na hata chama tawala wanajua huyu jamaa ni akili kubwa na kwa ukwel uliowazi n kuwa huyu ni miongon mwa hazina ghali sana na tunu iliyotukuka kwa taifa letu.amezongwa na mengi amepitia magumu na machungu mengi amejizzolea pia maadui wengi kutoka pande zote bali amesimama imara bila kutetereka na mwishowe maadui zake wameishia kupata aibu.lakin mh zitto asikate tamaa kwan afaham kuwa mti mzuri ndo hurushiwa mawe.mh zitto endelea kutekeleza wajibu wako kwa jamii kuitoa jamii gizan na umaskin uliokithiri endelea kutekeleza wajibu wako kwa weledi,hekima,busara uadilifu na kutenda haki uliomkubwa wwe ni hazina na tunu iliyotukuka kwa taifa letu songa mbele.kazana huko mbele banapo uzima uliongoze taifa letu la tanzania na kulirudisha kwenye mstari ulionyooka wa uadilifu na haki
alluta continua
alluta continua
alluta continua
mapambano yanaendelea katika
kufuta ujinga
umaskini
ufisadi na ubadhirifu
Kupata huduma bora za kiafya
Upatikanaji wa maji safi na salama
NAOMbA KuWasilisHA
 
Umeelezea vizuri kwa upande mmoja wa mazuri
Kipi kilipelekea awe adui (wa chama chake na wafuasi wa chadema na kwa upande mwingine awe rafiki wa CCM na wafuasi wao )
Nianzie kampeni za 2010 ambapo nilianza fuatilia mchango wa Zitto kwa Chama chake
Nakumbuka kipindi hicho kwanza Zitto hakuudhuria uzinduzi wa kampeni za chadema pale jangwani huku anafahamu ushiriki wake ungeongeza hamasa kubwa kwa Chama chao na mgombea wao wa urais Dr Slaa
Pia ni kipindi hicho hicho akawa anapamba vichwa vya magazeti ya Chama cha mapinduzi uhuru na mzalendo moja ya habari ninayoikumbuka alisifu kwamba JK amejenga Uchumi imara(hii haikuwa njema kwa chama chake ambacho kinamgombea anaeshinda na hasimu ambaye yeye Zitto anamsifu )na pia coverage yake TBC televisheni ilikuwa kubwa na hasa pale alipotangaza kugombea urais wa Chadema 2015,hii ilikuwa inaharibu attention ya wanaounga mkono mgombea wa Chama Chake
Zaidi aliripotiwa na ----------- kufanya mawasiliano ya karibu na afisa usalama Jack Zoka ambayo tafsiri ya wafuasi wa Chadema yalilenga kuhujumu matokeo ya uchaguzi wa Chama chao
Baada ya kampeni kuisha akawa ameongeza wafuasi wa CCM ambao hata humu walionesha kushabikia chochote Zitto anachofanya(kwa hili pia lazima wafuasi wa chama chake watilie shaka.
Kauli zake humponza (kumbuka kipindi cha Lwakatare)
Hayo ni machache ambayo mimi mtu wa mtaani ni siye na chama nimeyaona
 
sendeka aliomb mwongozo kwasababu alikuwa hataki pinda awajibishwe
 
Umeelezea vizuri kwa upande mmoja wa mazuri
Kipi kilipelekea awe adui (wa chama chake na wafuasi wa chadema na kwa upande mwingine awe rafiki wa CCM na wafuasi wao )
Nianzie kampeni za 2010 ambapo nilianza fuatilia mchango wa Zitto kwa Chama chake
Nakumbuka kipindi hicho kwanza Zitto hakuudhuria uzinduzi wa kampeni za chadema pale jangwani huku anafahamu ushiriki wake ungeongeza hamasa kubwa kwa Chama chao na mgombea wao wa urais Dr Slaa
Pia ni kipindi hicho hicho akawa anapamba vichwa vya magazeti ya Chama cha mapinduzi uhuru na mzalendo moja ya habari ninayoikumbuka alisifu kwamba JK amejenga Uchumi imara(hii haikuwa njema kwa chama chake ambacho kinamgombea anaeshinda na hasimu ambaye yeye Zitto anamsifu )na pia coverage yake TBC televisheni ilikuwa kubwa na hasa pale alipotangaza kugombea urais wa Chadema 2005,hii ilikuwa inaharibu attention ya wanaounga mkono mgombea wa Chama Chake
Zaidi aliripotiwa na ----------- kufanya mawasiliano ya karibu na afisa usalama Jack Zoka ambayo tafsiri ya wafuasi wa Chadema yalilenga kuhujumu matokeo ya uchaguzi wa Chama chao
Baada ya kampeni kuisha akawa ameongeza wafuasi wa CCM ambao hata humu walionesha kushabikia chochote Zitto anachofanya(kwa hili pia lazima wafuasi wa chama chake watilie shaka.
Kauli zake humponza (kumbuka kipindi cha Lwakatare)
Hayo ni machache ambayo mimi mtu wa mtaani ni siye na chama nimeyaona

wacha uongo wewe, Siku ya uzinduzi wa Kampeni Jangwani nilikuwepo, na Zitto alikuwa miongoni mwa wazungumzaji wakuu, na alizungumza
 
Zito mzuri na mbaya pia. Mzuri kama ulivyompamba mbaya ni kuwa hawezi kutofautisha nyumbani kwake na nyimbani kwa jirani
 
home boy Zitto was my role. mode 2007 lkn gafla nikaanza kutomwamini japo najua na naamini ni mtu anayefanya jambo kwa umakini mkubwa.

yapo mengi mazur na yapo mabaya pia. ameshindwa kusimamia hoja ya akaunt nje
 
wacha uongo wewe, Siku ya uzinduzi wa Kampeni Jangwani nilikuwepo, na Zitto alikuwa miongoni mwa wazungumzaji wakuu, na alizungumza

Ok kipi nikuthibitishie ujue kwamba nilikuwepo ,nidanganye ili iweje,kwa uthibitisho muulizeZitto mwenyewe hata kwa pm.,kama wewe unasema ulikuwepo hizo kampeni za uzinduzi Jangwani 2010 na Zitto akaongea basi itakuwa ulikuwa ndotoni mkuu. Nakumbuka waliongea ni pamoja na Mpendazoe ,Shibuda,Mabere Marando,Mbowe ...na G Solo ali rap na kila mmoja alisimama pale uwanjani(niliudhuria kama observer)
 
Umeelezea vizuri kwa upande mmoja wa mazuri
Kipi kilipelekea awe adui (wa chama chake na wafuasi wa chadema na kwa upande mwingine awe rafiki wa CCM na wafuasi wao )
Nianzie kampeni za 2010 ambapo nilianza fuatilia mchango wa Zitto kwa Chama chake
Nakumbuka kipindi hicho kwanza Zitto hakuudhuria uzinduzi wa kampeni za chadema pale jangwani huku anafahamu ushiriki wake ungeongeza hamasa kubwa kwa Chama chao na mgombea wao wa urais Dr Slaa
Pia ni kipindi hicho hicho akawa anapamba vichwa vya magazeti ya Chama cha mapinduzi uhuru na mzalendo moja ya habari ninayoikumbuka alisifu kwamba JK amejenga Uchumi imara(hii haikuwa njema kwa chama chake ambacho kinamgombea anaeshinda na hasimu ambaye yeye Zitto anamsifu )na pia coverage yake TBC televisheni ilikuwa kubwa na hasa pale alipotangaza kugombea urais wa Chadema 2005,hii ilikuwa inaharibu attention ya wanaounga mkono mgombea wa Chama Chake
Zaidi aliripotiwa na ----------- kufanya mawasiliano ya karibu na afisa usalama Jack Zoka ambayo tafsiri ya wafuasi wa Chadema yalilenga kuhujumu matokeo ya uchaguzi wa Chama chao
Baada ya kampeni kuisha akawa ameongeza wafuasi wa CCM ambao hata humu walionesha kushabikia chochote Zitto anachofanya(kwa hili pia lazima wafuasi wa chama chake watilie shaka.
Kauli zake humponza (kumbuka kipindi cha Lwakatare)
Hayo ni machache ambayo mimi mtu wa mtaani ni siye na chama nimeyaona

ukumbuke PIA yeye ndiye aliyetembea maeno mengi na Dr. Slaa kama mgombea uraisi akimpigia kampeni kuliko mbuge yeyote CDM
 
ukumbuke PIA yeye ndiye aliyetembea maeno mengi na Dr. Slaa kama mgombea uraisi akimpigia kampeni kuliko mbuge yeyote CDM

Binafsi naandika yale niliyoyashuhudia na kusoma magazetini kama raia wa kawaida kabisa .hayo ambayo sina hakika nayo siwezi yakubali ama kuyakataa kwa sababu sifahamu.
Hivi kuna uhusiano kati ya I'd yako na chama cha ACT na je kuna uhusiano wowote kati ya Zitto na. chama kipya cha siasa ACT?
Binafsi simchukii Zitto ila nafuatilia nyendo na kauli za wanasiasa kadri niwezavyo
 
Binafsi naandika yale niliyoyashuhudia na kusoma magazetini kama raia wa kawaida kabisa .hayo ambayo sina hakika nayo siwezi yakubali ama kuyakataa kwa sababu sifahamu.
Hivi kuna uhusiano kati ya I'd yako na chama cha ACT na je kuna uhusiano wowote kati ya Zitto na. chama kipya cha siasa ACT?
Binafsi simchukii Zitto ila nafuatilia nyendo na kauli za wanasiasa kadri niwezavyo

hakuna uhusiano wowote mkuu na hicho chama.
wengi pia tunasoma na kusikia habari kutoka katika vyombo mbalimbali vya habari, bila kusahau vipo vyombo vya "udaku" pia.hivyo Nivema kufuatilia habari kwa kina ili kupata uhakika wa jambo husika.
 
zito ni mwanasiasa wa KISASA, aliyethubutu kufanya siasa kama kazi ya kutumikia wananchi, mda wote amekuwa akisimamia kilicho sawa hata kama watu wote watampinga.....
ni mwanasiasa mzalendo na aliyejaa uchungu na nchi yake.....
MUNGU AKULINDE ZITO ILI TUZIDI KUNUFAIKA WANYONGE......
 
Back
Top Bottom