Baada ya kushuhudia utawala wa kibeberu wa serikali ya Tanganyika uliojaa dhulma, madhila na idhilali ambazo zimefanya hata roho za Kizanzibari kuwa hazina thamani, na Wazanzibari kuweza kuuliwa kama mijusi, Mzanzibari yoyote mwenye akili zake timamu ni lazima ataona kuwa hakuna njia iliyobakia ya kuuondosha utawala huo wa kibeberu ila kudai Uhuru. Jee kuna Mzanzibari yoyote ambaye amefurahishwa na idhilali za kutawawaliwa na serikali ya Tanganyika?
Kabla ya kuendelea zaidi, nataka kutafautisha jambo moja muhimu, nalo ni kuwa Wazanzibari hatukutawaliwa na Watanganyika, yaani watu wa Tanganyika, bali tumetawaliwa vibaya na serikali ya Tanganyika ambayo pia Imewatawala Watanganyika wenyewe kwa njiya nyingi zilizo mbaya kwao pia. Kwa hivyo hatuna kinyongo na ndugu zetu wa Tanganyika, bali tuna matatizo na serikali iliyowatawala na wao pia na kuwatendea mengi ya dhulma.
Tujiulize nini maana ya kutawaliwa? Nchi yoyote ikinyimwa moja tu katika mambo yake muhimu yenye kuendesha na kuihami nchi, na jambo hilo likawa linaendeshwa na serikali ya nchi nyingine, basi nchi hiyo huwa imetawaliwa.
Jambo la kwanza lenye kuashiria kutawaliwa kwa nchi ni kuwa sukani za kiuchumi, kama vile utozaji wa ushuru juu ya bidhaa zinazoingia na kutoka nchini huwa hazipo mikononi mwao. Hatamu hizi za kiuchumi wa Zanzibar zimedhibitiwa na serikali ya Tanganyika.
Pili, Iwapo mambo ya usalama wa nchi na raia hayamo katika mikono ya nchi hiyo bali yanaendeshwa na nchi nyingine, basi nchi hiyo imetawaliwa. Mambo ya Polisi na ya kijeshi yote Zanzibar yanaongozwa na serikali ya Tanganyika.
Tatu, iwapo mipaka imeondoshwa na watu wa nchi tawala wanaweza kuingia Na kutoka bila ya kizuwizi chochote, basi nchi hiyo imetawaliwa. Watanganyika ni zaidi ya milioni thalathini, na Wazanzibari hawafiki milioni moja. Kuweza Watanganyika kuingia na kuishi Zanzibar bila ya kikwazo chochote si kutawaliwa tu, bali kuna hatari ya kubadilisha maumbile hasa ya wakaazi, mila, dasturi, tabia na hadi lugha ya watu wa nchi hiyo iliyotawaliwa.
Nne, Iwapo nchi imenyimwa sauti katika mambo ya nje na ikawa inasikika sauti ya serikali ya nchi yenye kutawala tu, basi nchi hiyo, bila shaka, imetawaliwa. Zanzibar ilikuwa na kiti chake katika Umoja wa Mataifa, na tokea kutawaliwa na serikali ya Tanganyika imenyimwa kiti hicho na badala yake kuna kiti kimoja tu: kila cha nchi iliyotawala, na amri zote za kidiplomasia hutoka kwa watawala wa Tanganyika.
Tano, iwapo hata chama kinachotawala nchini hakiruhusiwi kumuweka mtu waliyemchagua wengi wao kuwa ndiye mtetezi wao wa uraisi wa nchi yao na badala yake wakapewa mtu aliyechaguliwa na watawala, basi si chama hicho pekee, bali nchi yenyewe huwa imetawaliwa.
Sita, na iwapo wananchi hata wakimpa mtetezi wa upinzani zaidi ya asilimia thamanini ya voti zao ili awe raisi wao mpya, na serikali ikafanya kila mazingaombwe na ghilba na kumpa ushindi aliyeshidwa, basi nchi hiyo huwa imetawaliwa.
Iwapo katika mambo sita tuliyoyataja, ni jambo moja tu katika hayo linapatikana Zanzibar, basi nchi hiyo huwa imetawaliwa; tena imetawaliwa kwa dhulma kubwa ya utawala wa kibeberu. Lakini utawala wa serikali ya Kitanganyika haukutawala kibeberu jambo moja tu katika haya tuliyoyataja. Serikali ya Tanganyika inatawala Zanzibar katika mambo hayo sita na zaidi ya hayo. Jee ni kweli kuwa Wazanzibari waliuondisha utawala wa Kiingereza ili, kwa hiyari zao wajitie katika utawala dhalimu na wa serikali ya Tanganyika? Iwapo Wazanzibari, kweli, hawakujitia katika utawala dhalimu wa serikali ya Tanganyika, bali wametendewa hayo bila ya ridha zao, basi umefika wakati si wa kutafuta njia gani za kuutengeneza muungano, bali umefika wakati wa kudai UHURU.
Ni wazi kabisa kwa kila Mzanzibari kuwa tulionao si muungano. Hakuna muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Zanzibar imetoka katika utawala wa Kiingereza na imetiwa katika utawala wa Serikali dhalimu ya Tanganyika bila ya ridhaa ya wananchi ama wa Zanzibar au wa Tanganyika. Utawala wa Kiingereza ulikuwa si mzuri, lakini utawala huu wa serikali katili ya Tanganyika ni muovu kupindukia kiasi. Mtawala yoyote anayewaingilia raia na kuwauwa kama kwamba si binadamu, basi utawala huo ni lazima upingwe na uondoshwe. Kwa hivyo, ni lazima Zanzibar idai UHURU wake. Hakuna njia nyingine itakayofaa. Kama hamsadiki, basi tuwe tayari kuoneshwa idhilali kubwa zaidi na mauwaji ya raia wengi zaidi bila ya kupata natija yoyote.
Uhuru unaweza kupatikana bila ya shaka yoyote. Lakini ni wajibu wa kila Mzanzibari mwenye akili timamu aliweke hilo mbele. Awe hataki tena kingine ila kujitawala wenyewe. Iwe nyimbo yetu ni hiyohiyo moja tu: Tunadai UHURU wetu, na hapana shaka yoyote, UHURU utapatikana iwapo Lengo la Wazanzibari walio wengi ni hilohilo moja. Ni wachache tu waliofikiria kuwa Muingereza na nguvu zake alizokuwa nazo kuwa siku moja ataondosha utawala wake; hakuna aliyefikiria kuwa makaburu wa Afrika ya Kusini na nguvu za kijeshi walizokuwa nazo kuwa siku moja watawacha ueberu wao na kukubali matakwa ya watawaliwa.
Kuanzia leo, nawaomba wenzangu wenye kuyakubali haya, wasilitumie tena jina la "TANZANIA" badala yake watumie jina la TANGANYIKA. Kulitumia jina la "Tanzania" ni kukubali kuwa kweli tuna muungano na hatukutawaliwa, na pia tuzipaze sauti zetu za kuidaia Zanzibar UHURU wake.