"Zanzibar: Kwanini Tunasaili Kipengele cha Katiba?" Majibu!

Buchanan

JF-Expert Member
May 19, 2009
13,199
1,969
Kuna Makala iliyoandikwa na aliyejiita Charles Kayoka kwenye Gazeti la Nipashe la tarehe 18/08/2010 kuhusu kichwa cha habari kama kilivyo hapo juu. Ukitaka habari zaidi bonyeza hapa.

Hata hivyo napenda kujibu hoja alizotoa ndugu Kayoka kama ifuatavyo:

Magazeti wiki hii yamekuwa yakiandika kuwa mabadiliko ya 10 yaliyofanyika Zanzibar ya kuonyesha kuwa hiyo ni nchi iliyo na uhuru kamili na mipaka yanataka kuanzisha mgogoro wa kikatiba nchini.
Sioni kama kuna mgogoro wa kikatiba, ila waandishi wa habari wanataka kuyafanya tu mabadiliko haya kuwa ndiyo chanzo cha mgogoro wa kikatiba, badala ya kuiona Katiba ya Jamhuri ya Muungano yenyewe kama ndiyo tatizo.
Mimi sioni kama kuna tatizo katika maamuzi hayo ya Katiba kama ni tatizo, bali ni kuwa waandishi wa habari wameshindwa kuyajadili mabadiliko haya katika muktadha wake halisi.

Hapa ndugu Kayoka anajichanganya mwenyewe kwa kudai eti kuwa hakuna mgogoro wa Kikatiba huku akidai eti kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano ndiyo yenye tatizo! Sasa Katiba hiyo inakuwaje na tatizo wakati hakuna mgogoro? Ndugu Kayoka pia ameshindwa kuona kama kuna mantiki ya kuwa na nchi huru ndani ya nchi nyingine ni kitu kisichowezekana! Uhuru wa nchi hiyo uko wapi wakati nchi iko ndani ya nchi nyingine (Jamhuri ya Muungano wa Tanzania)?

Wiki mbili zilizopita Wanzanzibari walipiga kura kuamua kama waunde serikali ya umoja wa kitaifa au hapana; hatukuona kuwa ule ni uamuzi wenye athari kikatiba; lakini Katiba ya Zanzibar imekuwepo hapo miaka yote hiyo, zaidi ya miongo miwili.
Waandishi hatukujiuliza iweje kama Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano iwe na Katiba yake. Iwe na Rais wake, iwe na wizara zake na bajeti zake. Nadhani waandishi wangejiuliza haya yote wasingeona mabadiliko haya kama ni tishio katika Muungano, bali kuwa mchakato mzima wa kuunda Muungano ndio wenye matatizo.
Binafsi ninataka kuwakumbusha waandishi wenzangu kuwa, kabla ya kuundwa kwa Muungano, Zanzibar ilikuwa nchi kamili yenye hadhi ya Jamhuri na ilikuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa tangu Desemba 15, 1963. Iliingizwa siku moja na Kenya. Kumekuwa na dhana, pengine, kuwa kwa vile uhuru ule wa awali ulikuwa chini ya Waarabu basi haikuifanya Zanzibar kuwa nchi kamili. Sio Kweli, na mapinduzi ya Januari 1964 hayakuiondolea Zanzibar hadhi ya Jamhuri.

Kuwa na Katiba ya Zanzibar, Rais wa Zanzibar na bajeti ya Zanzibar hakumaanishi kwamba Zanzibar si sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ibara ya 34 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 inasema kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atatekeleza mambo yote ya Muungano na mambo yote yanayohusu Tanzania Bara. Kwa mantiki hiyo mambo yote yasiyo ya Muungano yanayoihusu Zanzibar yatatekelezwa na Rais wa Zanzibar. (Tazama Ibara ya 102 (1) ya Katiba ya JMT, 1977). Hapa tena mwandishi huyu anajikanyaga anapodai kwamba kabla ya Muungano Zanzibar ILIKUWA NCHI KAMILI. Sasa hivi ni nchi gani basi? Ukweli kwamba Zanzibar ilikuwa ni mwanachama wa UN imebaki historia na huwezi kuchukua historia hiyo na kuijengea hoja kwamba Zanzibar si sehemu ya JMT.

Kwa hiyo basi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulikuwa ni kati ya nchi mbili zenye hadhi ya kimataifa, na kwa hiyo Muungano huu ni wa Kimataifa. Zanzibar haikuwa mkoa wala haijawahi kuwa mkoa, hata baada ya Muungano. Kilichotokea ni kuwa kwa vile hatukuwa na Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika, Katiba ya Tanganyika ikarekebishwa ili kuwa Katiba ya muda kwa matarajio kuwa kwama 1965, Katiba ya Muungano ingetungwa na baraza la wabunge. Hilo halikufanyika hadi mwaka 1977, miaka mitano baada ya kufariki Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Aman Karume.

Hii nayo ni historia kwamba Zanzibar ilikuwa ni nchi. Baada ya Muungano Zanzibar ikaacha kuwa nchi kamili huru bali ni sehemu ya JMT. Katiba ya Tanganyika kurekebishwa si tatizo kwani mambo hayo yalifanyika kwa makubaliano ya pande mbili ndio maana hakuna protest yoyote toka kwa viongozi wa Zanzibar juu ya mabadiliko hayo. Kumbuka kwamba Bunge pia lilikuwa na Wazanzibari.

Waandishi hatujiulizi, kwa nini Katiba ya Tanganyika ikatoholewa kuwa Katiba ya Muungano? Na Kwa nini Katiba ya Jamhuri haikurudishwa kama wenzetu wa Zanzibar walivyofanya mwaka 1984, kurudisha Katiba yao? Kwa nini Katiba ya Tanganyika iwe ndio hiyo hiyo Katiba ya Muungano?
Kuna tafsiri nyingi lakini moja la kukumbuka kuwa, katika mambo ya umoja wa kitaifa na muungano wa nchi kumekuwa na tabia ya wanasiasa kudhani kuwa "Umoja", "Muungano", na mikondo kama hiyo ya kikanda inaweza kutokomeza hisia za kitaifa na kikabila bila hata kukaa chini na kuongea na wahusika juu ya namna gani utaifa uwe mbele na hisia za ukabila na utaifa ziwekwe kando.
Hili lilijitokeza katika nchi za Kisovieti na kilichotokea baada ya perestroika ni kuwa watu walirudi tena kule kwenye ukabila, umajimbo. Na sisi tulifanya kosa hilohilo.

Sijui kwa nini mwandishi huyu anataka waandishi wenzake wajiulize maswali anayotaka yeye na si vinginevyo! Kwa nini hapendi tujiulize kwamba kwa nini tusiwe na "umoja kamili" kwa kuwa na Rais mmoja tu na Zanzibar ikabaki kuwa Mkoa kama vile Iringa? Hiyo si itaondoa ukabila zaidi kuliko ilivyo hivi sasa? Huko kurudi nyuma kunasababishwa na watu wachache ambao wanafikiri kwamba KUGAWANYIKA NDIO MAENDELEO! Wanathamini mipaka iliyowekwa na Wakoloni kuliko ile tuliyojiwekea sisi wenyewe!


Muungano haukuanza na mjadala wa namna gani tutaachana na siasa za kimajimbo na kikabila na kidini. Wanasiasa walidhani mifumo hii ya kijamii itakufa yenyewe au ingekufa kwa vile watu wangetambua kuwa Jamhuri ya Muungano ni muhimo kuliko umajimbo.
Na kwa sababu hiyo, wanasiasa wa wakati ule wa kuunga Muungano hawakutaka kuwashirikisha wananchi kuhusu uamuzi huu adhimu. Ndiyo maana Abdul Jumbe alitaka kuliweka hili suala sawa mwaka ule wa kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa. Lakini Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere na wenzake hawakulichukulia maanani na badala yake wale waliotaka kuujadili Muungano na kuufanyia marekebisho walifanyiwa kebehi au kufukuzwa madarakani.
Haikuwa sahihi. Tulifanya kosa la kutowashirikisha wananchi ambao, kupitia kura ya maoni, mijadala ya kitaifa, na kadhalika, tungeweza kusema aina gani ya Muungano tungeutaka.

Hapa mwandishi hatoi sababu au Sheria ambayo inataka kwamba kabla ya kuungana lazima kuwe na mjadala! Au tuseme kabla ya kufanya jambo lolote la kitaifa lazima kuwe na mjadala! Ajiulize kwamba kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar, 1964 kulikuwa na mjadala wowote? Si tumeshuhudia kwamba baadhi ya Wazanzibari akiwemo Seif mwenyewe alidai kwamba Mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa ni "uvamizi?" Vivyo hivyo, Rais wa Zanzibar, Salmin Amour, aliingiza Zanzibar kwenye Jumuiya ya Nchi za Kiislam, OIC, bila kumshirikisha mwananchi yeyote wa Zanzibar, hatukuona malalamiko yoyote kutoka Zanzibar. Rais Mwinyi naye alitaka kuiingiza Nchi ya Tanzania bila kupitia kura za Maoni, hilo nalo kwa wapenda ushirikishwaji kutoka Zanzibar halikuwa tatizo kwao. Tatizo kwao ni Muungano! Mpaka sasa hatuoni kwamba kuna watu wanaojitokeza waziwazi kutaka mjadala kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar, kama yalikuwa ni halali au la! Waliohoji kuhusu Muungano inategemeana walikuwa wanahoji kuhusu nini hasa! Sidhani kama Karume sasa hivi atamsikiliza mtu yeyote anayetaka Pemba ijitenge na Zanzibar. Kwa hiyo Nyerere naye hakutaka kusikiliza maneno hayo ya kihaini!

Kwa maoni yangu ni kuwa hata uamuzi wa kuutengeneza Muungao nao ulikuwa wa haraka sana. Nchi nyingi za kiafrika wakati ule ndiyo kwanza zilikuwa zinapata uhuru. Wananchi wengi walikuwa hawana ufahamu wa kutosha juu ya serikali katika mfumo wa kimagharibi, tofauti na sasa; na wengi hawakuwa na elimu ya juu kama tulivyo sasa;
Kilichofanyika ni kuwaburuza tu. Hapo ndipo palikuwa mwanzo wa mgogoro wa kikatiba, kwa sababu wanasiasa wale hawakutafakari kuwa hapo baadaye kizazi kipya kitauangalia muungano huu na mchakato wa kuunda kwa jicho pevu zaidi na kuuliza maswali. Hicho ndicho kinachotokea zaidi.
Wanasheria watanisaidia hapa! Muungano ulianza na mkataba kati viongozi wawili wa kisiasa- Marais- Karume na Nyerere. Na kwa vile Muungano huu ulikuwa ni kati ya viongozi wa nchi, basi serikali ziliwakilishwa na serikali, sio vyama, ndizo zenye uwezo wa kuamua kuuza uhuru- sovereignty- na kuifanya nchi ikaingia kwenye Muungano.
Angalizo; Kumbukeni tulichokifanya kabla ya kuingia kwenye Jumuia ya Afrika Mashariki. Maraisi walikubali, lakini walitaka watu wajadili, tukajadili. Baadaye bunge likaidhinisha kwa sheria, na ndipo tukajiunga.

Kuundwa kwa Muungano kwa haraka kulitokana na tishio la Sultani Jamshid kurudi baada ya Mapinduzi. Kumbuka kwamba Serikali ya Zanzibar haikuwa na Jeshi imara la kuweza kupambana na Sultani ambaye aliikalia Zanzibar kwa miaka 100. Kwa hiyo ndio maana mjadala haukuwezekana. Kwa sasa hakuna sababu ya kurudi nyuma tena eti tuvunje Muungano kisha tuungane tena. Hayo ni mawazo potofu. Suala ni kuangalia kwamba tulikubaliana nini, kisha turekebishe pale ambapo tulisahau, kama kupo anyway!

Haiwezekani chama chochote kikajadiliana na chama cha nchi jirani na kuunda Muungano wa nchi bila rais, au bunge na wananchi kuupitisha. Hatukufanya hivyo wakati ule na kila tunapotaka kuwe na mjadala kuna watu wanaweka mguu.
Na kwa sababu mkataba ndio uliotumika kuongoza uundwaji wa Katiba ya Muungano, basi lazima tutambue kuwa sheria mama sio Katiba ya Muungano, tunaozungumzia Muungano. Sheria mama inakuwa Mkataba wa Muungano ambao unaweka bayana nini Tanganyika haki yake; na nini Zanzibar haki yake; na vipengele vile ndivyo tunavyokubali kuvitumia kutengenezea Katiba.

Hapa hakuna Chama kilichoingia makubaliano na chama kingine bali ni Marais ambao walipewa ridhaa na wananchi wao, walikaa na kuzungumzia kuhusu kuunganisha nchi zao. Naomba nikujulishe kwamba Sheria mama ndio Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 na si Makubaliano ya Muungano, kwa sababu Makubaliano ya Muungano yalikuwa ya muda (interim) hadi hapo Katiba Mpya itakapoundwa. Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano iliundwa mwaka 1977 na ilijumuisha pia Makubaliano ya Muungano katika NYONGEZA YA KWANZA. Kipengele husika kinasema kama ifuatavyo: "During the period from the commencement of the union until the Constituent Assembly provided for in Article (vii) shall have met and adopted a Constitution for the united Republic (hereinafter referred to as the interim period) the united Republic shall be governed in accordance with the provisions of Articles (iii) to (vi)." Najua Professor Issa G. Shivji amewajaza ujinga baadhi ya watu, kwa maslahi yake binafsi, kudhani kwamba Hati za Muungano ziko juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977. (Niliwahi kuanzisha thread juu ya hili). Mtanisamehe wanafunzi wake mlioko humu, pamoja na mashabiki wa kuvunjika kwa Muungano, kama yeye (Shivji).

Sasa kama Zanzibar wamekubaliana kufanya serikali ya Umoja wa Kitaifa; na kuianisha Zanzibar vizuri zaidi kiutawala na kijiografia, mgogoro unatoka wapi kwa sababu mkataba wa Muungano, haujaikataza Tanganyika au Zanzibar, kuwa na Katiba zake na kuainisha mipaka ya mamlaka yake kiutawala.
Mgogoro ungetokea katika mambo yale ambayo mkataba wa Muungano uliorodhesha kuwa yashughulikiwe na serikali ya Muungano, na ndiyo yakaingizwa katika Katiba ya Muungano, na Zanzibar wakaamua kuyaweka katika katiba yao binafsi kama vile hayakutajwa kuwa mambo ya Muungano. Hakuna Katiba iliyovunjwa kwa maamuzi yaliyofanyika Zanzibar.
Ninahimiza kuwa ili haya mashaka yote yatoweke mambo kadhaa yafanyike. La kwanza ni kuanzisha mjadala wa kitaifa wa marekebisho ya katiba. Kwanza tutajadili kama tuwe na Katiba ya Tanganyika na ya Muungano na ya Zanzibar.
Pili tutairekebisha Katiba ya Muungano ili iondokane na viraka viraka, kama tunataka, baada ya majadiliano, kuendelea kuwa na Muungano. Tatu tutajadili kama tunaihitaji Muungano, na kama ndivyo uwe wa namna gani.
Na mwisho tungeirekebisha katiba kwa kuangalia kama tuna mambo ya kijamii, yangejadiiliwa wakati huo ili kuona kama yangefaa kuwa katika katiba au hapana
.

Hapa namkumbusha tena mwandishi huyu kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 iko juu ya Makubaliano ya Muungano ambayo yalikuwa ya muda (interim) kabla ya kuundwa kwa Katiba hiyo. Kama Wazanzibari walikuwa wanataka mjadala juu ya Muungano wangesema hivyo badala ya kukimbilia "kujitangazia uhuru" kisha baadaye kutaka tufuate yale ambayo tayari walishaamua kupitia Baraza la Wawakilishi. Tukiwafuata watakavyo, watabadilisha kipengele kingine halafu wanapiga kelele kwamba badilisheni Katiba ya Muungano simply kwa sababu wao wamebadili Katiba yao. Mwisho wa siku hatutakuwa na Muungano bali ni state of anarchy!
 
safi sana naona kama ataona hiyo kitu uvlivyomjibu basi ataelimika zaidi,
tatizo waandishi wa mashairi ya taarabu, wanataka kujifanya wachambuzi wa mambo ya katiba
 
Kuna mwandishi wa Raia mwema ameeleza ni jinsi gani wznz wamekuwa wanatumia maneno kujikanyaga. Eti kubadilisha katiba kwa mlango wa uani ni kuimarisha muungano. Kama ulivyoeleza hapo juu, ni jambo la kusikitisha kuwa znz wafanye mabadiliko ya katiba halafu ile ya muungano ifuate wanayotaka.
Imekuwa kana kwamba bila znz bara haiwezi kujiendesha. Ni kwa upuuzi huu ndio maana wamekuwa na kauli za koti likikubana.., mara tusipofanyiwa hivi tunajitoa katika muungano n.k. Lile la mafuta sasa halina nguvu maana ndio kilikuwa chanzo cha kuvunja muungano. Halina nguvu baada ya kusikia Mtwara na L.Tanganyika yapo.

Watanganyika wamechoka na wanataka kwenda mbele, wznz wameulizwa sana swali moja, JE mnataka muungano au mumeuvunja?? Hawsemi, wanajiumauma.
Serikali tatu ni mzigo kwa bara na hiyo slogan wabara wanasema hapana, ni njia ya wznz kutaka ubara kwenye mafao!
Je,wznz lini mtaomba kura ya maoni kuhusu muungano? wabara hawana haja ya kura ya maoni kwa vile kuwepo muungano ni jambo jema, lakini ukivunjika hawana cha kupoteza. Na kama kipo cha kupoteza Wazanzibar tuambieni ni kipi hicho?
 
Hivi katiba ya Zanzibar ni mojawapo ya mambo ya muungano? Nadhani watu (hasa sisi watanganyika!) mara nyingi tunasahau kuwa muungano wetu ni kwa baadhi ya mambo tu!
 
Mwandishi wa makala hiyo ni wale ambao JK aliwaita Makanjanja. Unaona kabisa huyu anaandika kwa kutumia kifua na si akili. Anashindwa kutofautisha MUUNGANO na SHIRIKISHO. Na naona wengi hawana weledi wa jambo hilo. Katika Muungano tunapata Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yenye nia kwa Ufupi TAN - ZAN - IA. Kihistoria hizi zilikuwa nchi mbili huru ambazo ziliamua kuungana na kuwa nchi moja na si shirikisho. Sasa wafahamu kuwa wanaporejea neno Jamhuri katika ufafanuzi wa nchi ya Zanzibar wanamaanisha kuwa nchi ya Tanzania inakufa; na zinarejeshwa Zanzibar na Tanganyika. Hili uhitaji kuwa mwanasheria kulifahamu. Hii ni simple logic. Sasa hapa ndipo kuna tatizo. Na hata uchaguzi wa oktoba 2010 una utata na katika mazingira haya ni batiri. Maana wananchi wa nchi ya Zanzibar hawawezi kumchagua mbunge au Rais ambaye atatumikia Tanzania bara (yaani Tanganyika). Kumbuka kimantiki baada ya kuwa na Nchi ya Zanzibar, huwezi tena ukawa na nchi ya Tanzania ( nchi mbili kwa wakati mmoja). Jambo hili ni zito na utambuzi wake ndio unatuonyesha kuwa watawala wetu hata nchi wanayoiongoza na Katiba waliyokula kiapo kuilinda hawavifahamu. Hapa kuna suala la Legitimacy na Legality. Kisheria Baraza la Wawakilishi linaweza kubadili kipengele chochote cha Katiba ya Zanzibar lakini hawana mamlaka ya kufuta au kubadili Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. kufanya hivyo ni kuvunja Katiba . Jambo ambalo mwandishi wa makala ya gazeti hilo anajaribu kulisaili wakati akifikiri kuwa analitolea ufafanuzi.
 
Hivi katiba ya Zanzibar ni mojawapo ya mambo ya muungano? Nadhani watu (hasa sisi watanganyika!) mara nyingi tunasahau kuwa muungano wetu ni kwa baadhi ya mambo tu!

Ni kweli Katiba ya Zanzibar in itself si suala la Muungano per se lakini baadhi ya mambo ya Muungano yako kwenye Katiba ya Zanzibarna ya Muungano eg kwamba Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sio "nchi kamili huru," Mahakama ya Rufani, etc.
 
Ni kweli Katiba ya Zanzibar in itself si suala la Muungano per se lakini baadhi ya mambo ya Muungano yako kwenye Katiba ya Zanzibarna ya Muungano eg kwamba Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sio "nchi kamili huru," Mahakama ya Rufani, etc.

Ziliungana nchi mbili na kuwa nchi moja. Kiutawala kuna mambo ya Muungano na yasiyo ya muungano. Hapo uliwekwa utaratibu wa kuyahudumia kwa kuwa kuunda Serikali ya Baraza la Mapinduzi kwa upande wa iliyokuwa nchi ya Zanzibar na Upande wa iliyokuwa nchi ya Tanganyika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa ufupi baada ya Muungano Zanzibar iliongozwa Baraza la Mapinduzi kwa masuala ambayo si ya Muungano; na hadi leo na Serikali hiyo kujulikana kama Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ). Lakini pia kwa masuala hayo Kuliwekwa Baraza la Wawakilshi kutunga Sheria. Kwa utaratibu huo haikumaanisha na hata leo haimaanishi kuwa na vyombo hivyo basi ni kuwa na Uhuru wa kijamhuri. Naona tafsiri zinazotolewa na viongozi wetu hasa kwa upande wa Zanzibar japokuwa kwa jazba na ukali zinatupotosha na haziitakii mema Tanzania. Machoni mwa Wazanzibari walio wengi na ambao wamezaliwa ndani ya Tanzania (Maana wakati wa Muungano Zanzibar ilikuwa na watu takriban laki tatu, wengi wao wameishatangulia mbele ya Haki) inaonekana kuwa kuna Nchi ya Zanzibar na Nchi ya Tanzania. Hili ni tatizo kubwa na ni matokeo ya upotoshaji uliofanywa kimakusudi. Lakini nataka niwasifu waasisi wa mkanganyiko huu kwa kufanya "timing" nzuri ya kura za Maoni kuhusu uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar. Maana hata watawala wetu hawawezi kulisemea la kuvunja katiba kwa kuchelea kuwa mataifa makubwa wataona kuwa kuna njama za kupinga hoja ya Serikali ya umoja wa kitaifa. Hapa kunaitajika wapambanuzi waweze kutofautisha nia njema ya Kuunda Serikali ya Umoja wa kitaifa na nia mbaya ya kuvunja muungano.
 
Ni kweli Katiba ya Zanzibar in itself si suala la Muungano per se lakini baadhi ya mambo ya Muungano yako kwenye Katiba ya Zanzibarna ya Muungano eg kwamba Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sio "nchi kamili huru," Mahakama ya Rufani, etc.

So kisheria Zanzibar wanaweza kubadili katiba yao kadri wapendavyo. Katiba ya Zanzibar haiwazuii kufanya hivyo! Zanzibar inayo sovereignty kwa mambo yasiyo ya muungano.
 
Kisheria Baraza la Wawakilishi linaweza kubadili kipengele chochote cha Katiba ya Zanzibar lakini hawana mamlaka ya kufuta au kubadili Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. kufanya hivyo ni kuvunja Katiba .

Ni kweli BLW haliwezi kubadili katiba ya JMT na ninavyojua hawajafanya hivyo!
 
Ni kweli BLW haliwezi kubadili katiba ya JMT na ninavyojua hawajafanya hivyo!
Kwa kubadili kipengele kinachohusu Masuala ya Muungano ambacho kinakinzana na Kipengele cha jambo hilo katika Katiba ya JMT tayari wameingilia mamlaka ambayo si yao. Hapo kuna Tatizo. Kisheria Katiba ya zanzibar inatokana na Katiba ya JMT. Kwa tafsiri ya haraka kipengele hicho cha Katiba ya Zanzibar ambacho kimefanyiwa mabadiliko kwa vile kinakinzana na Kipengele ndani ya katiba Mama basi kitakuwa "Null and Void"
 
Kwa kubadili kipengele kinachohusu Masuala ya Muungano ambacho kinakinzana na Kipengele cha jambo hilo katika Katiba ya JMT tayari wameingilia mamlaka ambayo si yao. Hapo kuna Tatizo.

Katika hili wameingilia mamlaka ya nani? Nilidhani wanayo 'mamlaka' kamili ya kubadili katiba yao.

Kwa tafsiri ya haraka kipengele hicho cha Katiba ya Zanzibar ambacho kimefanyiwa mabadiliko kwa vile kinakinzana na Kipengele ndani ya katiba Mama basi kitakuwa "Null and Void"

Kwa kuzingatia jibu la hapa juu, ingekuwa 'null and void' endapo BLW lingefanya mabadiliko hayo kwenye katiba ya JMT kwa sababu halina mamlaka hayo.
 
Ni kweli BLW haliwezi kubadili katiba ya JMT na ninavyojua hawajafanya hivyo!

Kama hawajavunja Katiba ya JMT, 1977 (wewe unatumia lugha kwamba hawajabadili) unafikiri kwa nini Wazanzibari wanataka Katiba ya JMT ibadilishwe iendane na mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar, 1984?
 
Back
Top Bottom