"Ni vyema pamoja na hoja na mijadala yetu ya kutafuta mustakbali wa Zanzibar tukubali ukweli, kwamba kimsingi tatizo sio Zanzibar, sio Wazanzibari. Kikwazo kikubwa cha Zanzibar ni Wazanzibari waliolewa na wanaopenda kuendelea na uraibu huo kwa vile unawapa andasa kwamba wanaishi maisha bora chini ya Zanzibar ya sasa iliyokosa muelekeo, inayonuka umaskini kama nchi na kila siku inazidi kudidimia. Aidha, tatizo ni Wazanzibari waliolala na kudhani kwamba tupo katika mapambano ya kisiasa wakati kumbe sote tumo kwenye jahazi moja la kutawaliwa na Mkoloni ambaye hana mapenzi na Wazanzibari sote kwa ujumla wetu lakini kawaaminisha hao wengine kwamba ati anatutawala kwa maslahi yao dhidi ya sisi wananchi wenzao tuliobakia ambao tumefanywa watuone ni mahasimu na maadui zao. Lakini, kikwazo kikubwa zaidi na cha hatari ni kila Mzanzibari aliyekata tamaa katika harakati za mageuzi. Anwar yupo gerezani na anapanda akishuka kortini tokea mwaka 1998, kwa tuhuma za kudhalilishwa kupita kiasi lakini hakukata tamaa. Na Mahathir, karudi katika siasa na kaiokoa nchi akiwa na umri wa miaka 92. Kaleta mageuzi yaliyowashinda vijana wa miaka 32, miaka 60 chini ya umri wake. Hakika katika hayo, Wazanzibari tunapaswa tutafakari, tujifunze na tuamke."
- Othman Masoud Othman
Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.