Gavana
JF-Expert Member
- Jul 19, 2008
- 33,635
- 8,954
ZANZIBAR: Fitna Adui wa Masikilizano na Umoja
Kutoka kwa Ibrahim Noor,
Kwenda kwa:
Walter Bogoya,
Generali Ulimwengu,
Mohamed Said
J Mihangwa,
Jarugum,
Juma Mwapachu,
Mtwangi,
P Karugendo,
Azavel Waitama,
Issa Shivji,
Chambi Chachage,
Nizar Visram,
Na Kwa Kila Linaemkhusu Kote Duniani
Balozi Ali Abeid Karume:
Si suala la nini mimi na wewe tunasema. Wala si suala la mpangilio wa vipindi vya kihistoria. Bali ni suala la nini kilifanyika na lini kilichofanyika kikaja kugeuzwa kwa makusudi na kwa madhumi ya kupotosha na kwa faida ya nani.
Na tuanze na mahala penye nganu za kusisimua na za kilele cha uwongo na nguvu za giza. Wapi? Pale Mkunazini penye yale yenye kuitwa mahandaki yanaoyosemekana yalikuwa yakitumika kuwekea watumwa katika hali ya mateso na unyama uliokithiri ambao hakuna binaadamu mwenye kujihishimu na kuuhishimu ubinaadamu wake na wa mwenzake ataweza kuuvumilia.
Soko la utumwa la Mkunazini lilifungwa rasmi tarehe 5 Juni, 1873. Miaka 18 baada ya soko hilo kufungwa, tarehe 12 May, 1891, ndipo wamishinari wa Kikristo waliweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa hospitali kwa ajili ya Wazungu na waliokuwa wakiishi mjini Zanzibar na kwa ajili ya wenyeji pia. Kwa mujibu wa maelezo ya jarida la CENTRAL AFRICA: A MONTHLY RECORD OF THE WORK OF THE UNIVERSITIES’ MISSION TO CENTRAL AFRICA, VOL. IX. 1891 lilochapishwa London na Wells Gardner, Darton, & Co.:
“A procession was formed from the church to the piece of ground on which the Hospital is to be built, which lies immediately behind the present Dispensary, whose windows overlook the old slave market.” (Msafara kutoka Kanisani kwenda kwenye kipande cha ardhi ambapo patajengwa Hospitali, ambayo ipo ubavuni mwa kituo cha afya, na madirisha yake yanachunguliwa palipokuwa na soko la watumwa).
Hospitali hiyo, (na kama ilivyokuwa hospitali ya Wafaransa ya skuli yako ambayo kwanza iliitwa St. Joseph School na baadae kuitwa Tumekuja), ilikuwa na ghala ya chini ya nyumba ambayo ikitumika kuhifadhia madawa katika mazingira ya joto. Kabla wapotoshaji kulibadilisha jengo la kihistoria, kulikuwa na viguzo vya kama futi tatu vyenye nafasi bapa juu yake, na nafasi kwa mtu kuweza kuzunguka baina ya viguzo.
Viguzo hivyo vilikuwepo mpaka katika miaka ya 70 na baada ya hapo vikavunjwa na badala yake wapotoshaji wakajenga baraza moja na kuweke minyororo yenye kutu. Mwenye kutaka kuiona picha asilia ya hivyo viguzo naomba awasiliane na mie nitampatia. Kwa mwenye kutaka ya ziada kuhusu hili nakuombeni muwasiliane na Professor Abdul Sheriff.
Mapango ya Mangapwani nayo pia yametiwa kwenye nguvu ya giza la wapotoshaji ukweli. Huenda ukawa unafahamu pale Mangapwani kuna sehemu mbili ambazo mara nyingi huwa zinachanganywa. Kuna pango la maji matamu ambalo inasemekana linatokezea baharini, na kuna hayo yenye kuitwa “mapango ya watumwa”. Wamiliki wa shamba na sehemu hio wameilalamikia Idara ya Mambo ya Kale na Makumbusho kuwa wanasema uwongo kukhusu sehemu hiyo ambayo huko nyuma ilikuwa inatumika kama ni sehemu ya itikadi ya kufugia majini.
Na hilo pango lenye mkondo wa maji pia linatumiwa kipropaganda kuwa wakifichwa watumwa, jambo ambalo si la kweli kabisa. Sababu ya kuwepo na kukuwa huo kijiji cha Mangapwani ni huo mkondo wa maji. Unawafichaje watu mahala ambapo wenyeji wake wanateremka mara nyingi kila siku kuchota maji yao ya kunywa, kupikia na kwa mengineyo hapo? Pili, wakifichwa watumwa kwenye mahala padogo hapo si watakwenda haja na kuyanajisi hayo maji pia?
Sasa twende kwenye taji la uwongo kukhusu soko la watumwa la Mkunazini. Sijui kama unajua, na kama wasomaji wengine humu wanajua, kuwa soko la watumwa lilikuweko Zanzibar kwa miaka 40 tu, si kwa makarne kama wanavyodai wanapropaganda, na lilihamishwa mara nne; la mwisho hapo Mkunazini lilikuweko kwa muda wa chini ya mwaka kabla ya kufungwa kabisakabisa. Masoko yote hayo pamoja na biashara ya utumwa katika pwani nzima ya Afrika Mashariki na Zanzibar, haijapatapo kumilikiwa na Waarabu wala na watawala wa Zanzibar wenye asili ya Kiomani.
Kwa taarifa yako na ya wasomaji wengine, soko la Mkunazini lilitolewa zawadi na kupewa Reverend Edward Steere, mkubwa wa The Universities’ Mission to Central Africa. Aloitoa zawadi hiyo (ambae naamini hujapata kumsikia), ni Likhimidas Ludha ambae alikuwa wakala wa Jeiram Sewji. Zawadi hiyo ilitolewa na kusajiliwa rasmi tarehe 20 Agosti, 1874.
Balozi, nakuomba unisikilize katika hili. Tatizo kubwa lililotukumba ni kuamini jambo au mambo ambayo hatuna ilimu nayo lakini yamebuniwa kwa lengo la kutufitnisha wenyewe kwa wenyewe. Ukizingatia kwa kituo utaona hakuna aliyesalimika katika hili na muhanga wa mwanzo ni wasomi. Kwanini wasomi? Kinyume na watu wengi wa kawaida, wasomi wanapenda kusoma vitabu, makala, kuangalia videos, na katika tabia hiyo nzuri huwa ni wepesi pia kudanganyika pengine kuliko watu ambao si wasomi, khasa khabari hizo za uzushi na propaganda wakiwa wanazisoma mara kwa mara.
Hii ni khatari kubwa kwetu sote. Kwa Zanzibar, kwa Tanganyika, kwa majirani zake wanane, kwa baina ya Afrika Kaskazini ya Jangwa la Sahara, na Kusini ya Jangwa hilo. Hii pia inakhatarisha Umoja wa Bara la Afrika, na Zanzibar imegeuzwa donda lenye kunuka baina ya Waafrika-Waarabu na Waafrika wengineo. Pia ni janga baina ya Waislam wenyewe kwa wenyewe waliopo Zanzibar na siasa zao za mpasuko ambazo shina lake ni huo mzizi wa fitina na upotoshaji ulio kubuhu; baina ya Waislam na Wakristo, baina ya wenye dini na wasiokuwa na dini. Na ni janga baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nchi ya Oman na majirani na wahisani wake.
Hata dunia imetiwa kwenye upotoshaji huu. Watalii wengi wanaotembelea Zanzibar hupelekwa pale Mkunazini penye Chuo Kikuu (Open University) Huru cha kukhitimu uwongo wa giza la uwongo kwa gharama ya Dola 5 za Kimarekani.
Leo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuna vyama vya siasa ambavyo takriban kwa ujumla wao, vimesimama juu ya mihimili ya ideologia ambayo ni mihimili ya Muungano na Mapinduzi ambayo imesimama kwenye nyumba iliojengwa juu ya mchanga na kwa nguvu za nyumba ya buibui.
Ni kisingizio cha kuivamia na kuikandamiza Zanzibar kwa kutumia sababu ya kuikomboa kutokana na utumwa. Usisahau ulishindwa kujibu ni wangapi kati ya watu 14 akiwemo baba yako ambae alikuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, ambae anatokana na kizazi cha watumwa au utumwa.
Na wewe Balozi unagombea Uraisi wa Zanzibar katika hali ambayo ni khatari kwako (na kwa wagombea walio kama wewe na kwenye vyama vyote vya siasa) na zaidi kwa Zanzibar na kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; ni khatari kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki; ni khatari kwa SADCC; ni khatari kwa majirani wanane muhimu wa Tanzania; ni khatari kwa Umoja wa Afrika (AU); ni khatari kwa ubinaadamu kwa jumla. Na ni khatari zaidi kwenye futi sita chini ya ardhi ambazo sote zinatusubiri.
Tuamke tujenge nchi zetu kwa matufali madhubuti yasiyo na uwongo na chuki kubwa za kupandikiza. Tulijenge Bara la Afrika badala ya kulialia na kulalamika kusokwisha kwa kujitafutia uhalali wa kiutawala kwa kuwasukuma wengine kwenye haramu zisizowakhusu au zenye kuwakhusu wote pamoja na wengi pia - Waarabu, Waafrika, Wahindi, Wakristo, Waislam, na wenye kuamini dini za kienyeji.
Tuamke kabla hatujamalizwa.
Mvunja nchi ni mwananchi!

