Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 22,454
- 32,980
View: https://youtu.be/msgve8ZwfHE?si=U_4RF703Qpe3nSpU
Ally Sykes ndiye aliyechora kadi ya TANU na kuchagua rangi na nembo yake.
Rangi alizochagua zilikuwa, nyeusi kuwakilisha taifa la Kiafrika na kijani ardhi ya Tanganyika.
Mfano wa kadi ya TANU ulitokana na kadi yake ya Tanganyika Legion.
Baada ya kumaliza kuichora ile kadi, aliwaendea Tanganyika Standard Newspapers ili wamchapishie.
Kutoka mfukoni mwake mwenyewe alichapisha kadi 1000 za kwanza na akitumia fedha za TAGSA alichapisha kadi nyingine 2000.
Kadi nambari 1 ilitolewa na Ally Sykes kwa rais wa TANU, Julius Kambarage Nyerere na Ally aliweka sahihi yake kama afisa aliyeitoa.
Ilipendekezwa kwamba kadi chache za mwanzo lazima zipigwe mnada na fedha zitakazokusanywa zitiwe kwenye hazina ya chama.
Abdulwahid, Ally, Dossa Aziz, Rupia na wengine walipanda dau kununua kadi hizo.
Ally alimshinda kaka yake Abdulwahid kwa bei akapata kadi ya TANU nambari 2; Abdulwahid alipewa kadi nambari 3; Dossa Aziz kadi nambari 4; Phombeah kadi nambari 5; Dome Okochi, mmoja wa wale wazalendo kutoka Kenya katika TANU alipata kadi nambari 6 na Rupia kadi nambari 7, Bibi Titi kadi nambari 16; Iddi Faiz Mafungo kadi nambari 24; Iddi Tosiri kadi nambari 25.
Hizi kadi za TANU kwa kuwa zilikuwa za rangi ya kijani washabiki wa Yanga wakajinasibisha na TANU wakidai TANU ni Yanga na ni chama chao.
Bahati mbaya Sunderland wao wakivaa rangi nyekundu na rangi nyekundu ni rangi ya bendera ya Uingereza.
Club ya mpira iliyopigania uhuru wa Tanganyika ni Young New Strong Football Club kutoka Tabora.
Juhudi za kuihuisha TANU zilikuja mwaka 1955 mwaka mmoja baadae kupitia Young New Strong Football Club - kilabu ya kandanda iliyoanzishwa miaka mingi nyuma ambayo ilikuwa maarufu pale mjini.
Wanachama wa kilabu hiyo baadhi yao ndiyo walikuwa waasisi wa African Association mwaka wa 1945, mashuhuri miongoni mwao walikuwa Fundi Mhindi na Maulidi Kivuruga.
Mwenyekiti wa kilabu hiyo alikuwa Juma Mrisho, mcheza kandanda mashuhuri kwa siku zile.
Shaaban Mohamed Silabu na Bilali Rehani Waikela walikuwa Katibu na Naibu Katibu.
Mzee Waikela ndiye aliyenisomesha historia hii.