Yanajirudia?

Yanajirudia?

DIZZO MTAWALA

JF-Expert Member
Joined
Aug 22, 2015
Posts
240
Reaction score
769
JE! ZILE SIKU ZINAJIRUDIA?

Muda kama huu, miaka mia moja iliyopita Tanganyika ilikuwa katika hali ya sintofahamu, kama ilivyo sasa. Wakati huo vita kuu ya kwanza ya dunia, vita mbaya kuwahi kutokea katika historia ya dunia, ilikuwa mwishoni, ingawa kwa Tanganyika tayari vita hiyo ilikwisha malizika tangun Juni 20, 1917. General wa vita wa kijerumani, Lettow von Vorbeck alikuwa amesalimu amri kwa Kamanda wa majeshi ya Uingereza, Horrace Byatt. Wakati huo Horrace Byatt akiweka makao yake makuu huko mjini Wilhemstat (Lushoto ya leo) kabla ya kuhamia Dar es Salaam mnamo january 1919.

Ingawa koloni lilikuwa chini ya utawala wa kijeshi, bado uhalifu ulikithiri. Watu walikuwa wakipotea na kutoonekana tena. Mfano, Askofu wa Zanzibar alipotelewa na mpishi wake aliyeitwa John Mbwana bin Benjamin Mngoma, Mbondei. Fununu zilikuwepo kwamba, watu waliokuwa wakionekana wana mapenzi na Ujerumani walichukuliwa kimyakimya na kupotea kabisa. Waingereza walipata wakati mgumu wa kutawala kwa sababu kuu tatu; moja hawakuwa na uzoefu wa kutawala koloni la Tanganyika, chukulia kwamba wasomi wa kiafrika waliokuwamo kwenye ofisi za kiserikali walikuwa wakizungumza kijerumani na Kiswahili, wakati waingereza wanazungumza kiingereza tu. Kwa hiyo, utawala mpya ulipata shida.

Kimantiki, sababu hiyo inaweza kufanana na sababu za kushindwa kwa serikali ya Tanzania ya awamu ya tano. Kabla ya awamu ya tano, watumishi wa serikali walizungumza lugha ya kistaarabu, waliongezewa mishahara kila mwaka kwa mujibu wa sheria, walipandfshwa vyeo na kupewa stahili zao mbalimbali. Serikali ya awamu ya tano ikaingia na ‘lugha’ mpya, hapa kazi tu. Hakuna kitu zaidi ya kazi tu.
Sababu ya pili iliyowapa waingereza wakati mgumu ni kukuta wenyeji wa kiafrika wengi, wazoefu ndani ya serikali, waozefu wa mazingira ya Tanganyika, wazoefu wa mji.

Pia walikuwemo mavetarni wa vita, waliopigana upande wa ujerumani. Hali hiyo iliwawia vigumu waingereza kutawala kwa amri. Ukjweli ni kuwa hawakuwa wazoefu wa mifumo ya kitanganyika, lakini kwa sababu ya ukoloni wakawa wakitoa amri bila kuwa na ujuzi wa mambo. Jambo hilo linafanana kabisa na mtindo wa serikali ya awamu ya tano. Vijana wengi walioteuliwa kwenye nafasi za uongozi hawana uzoefu, achilia mbali utashi wa kuongoza. Angalau, ukikosa uzoefu, basi uwe na utashi wa kuongoza, na ustaarabu pia. Lakini wateule wa magufuli ni watu wa kutoa amri, hata kwa mambo ya kitaaluma wasio na uwezo nayo. Hivyo ndiyo ilikuwa kwa wakoloni kiasi kwamba mambo yalikaribia kuwashinda. Nitaeleza.

Sababu ya tatu iliyowapa waingereza wakati mgumu ni uchumi. Pamoja na kushinda vita lakini uchumi wa uiingereza uliyumba. Ndio wakati dola kubwa la uingereza, kubwa kuliko madola yote yaliyowahi kuwapo, lilianza kuanguka. Mwanzoni, ilionekana kama uchumi unakua, hadi kufikia mwaka 1924, kipindi kilichoitwa ‘Glorious years’, lakini baada ya hapo hakukuwa na cha maana. Ndio maana pamoja na Uingereza kutawala miaka zaidi ya 40 (1917 – 1961), lakini hawakuweza kujenga miundo mbinu mikubwa kama wajerumani waliotawalakwa miaka 20. (1884 – 1914). Wajerumani walijenga reli ya kati, reli ya kaskazini, bandari ya Dar es salaam, bandari ya Tanga, na kuanzisha mashamba makubwa ya Katani, Chai, Kahawa na Pamba ambayo leo yanaendelea. Walianzisha maboma na miji mingi kama Tabora, Dodoma, Lushoto, Mpwapwa, na kuijenga zaidi miji iliyokuwepo, Tanga, Dar es salaam, Moshi, Pangani nk. Kwa kifupi wajerumani waliifanya Tanganyika kama ndio kwao, kama makaburu walivyofanya Afrika kusini, wakati waingereza walikuja kama wageni wakijua muda wowote wanaweza kuondoka.

Wakati mgumu waliopata waingereza katika kipindi cha miaka miwili au mitatu ya awali, kulipelekea wazo la kutaka kuachana na Tanganyika, badala yake walikabidhi koloni hilo kwa India. Wazo la kuifanya Tanganyika kuwa koloni la India, liliwachefua sana waswahili. N kama vile waingereza walitaka kususa. Kimtazamo, Jambo hilo linashabihiana kabisa na kauli za Rais wa awamu ya tano, John Magufuli. Magufuli amewahi kunukuliwa akisema anatamani muda uishe apumzike. Amewahi pia kunukuliwa akisema, alijaribu tu kutaka kuwa Rais, maana yake hakuwa amekusudia. Ni kauli zinazoashiria kushindwa, kauli za mtu anayetaka kususia jambo.
Baada ya fununu za kuifanya Tanganyika kuwa koloni la India, wenyeji wa Tanganyika wenye asili ya Asia walikwisha kupanga kikao cha kushawishi mpango huo utekelezwe haraka, huko mjini Tanga, mji wa pili kwa umuhimu wakati huo.

Lakini siku mbili kabla ya kikao hiko, Desemba 17, 1919, Martin Kayamba na Ali bin Diwani waliitisha kikao cha watumishi wa umma wa kiafrika huko Tanga. Martin Kayamba, kitukuu wa mtawala wa zamani wa dola la usambaa, Chifu ‘Kimweri ya Nyumbai’ alikuwa karani mkuu wa mji wa Tanga, ambaye ana uzoefu wakufanya kazi hiyo huko Uganda na Kenya. Ali bin Diwani alikuwa Liwali, mtu wa kusikiliza na kutatua migogoro/kesi za kijamii. Baada ya kikao hiko, viongozi hao wa kiafrika walitoka na ujumbe wa kupinga mpango huo kwa kauli tatu; kwa mujibu wa Sir Horace Byatt aliyekuwa kiogozi wa serikali ya Tanganyika;

Moja, ‘sisi waafrika tunawahitaji wazungu kwa ajili ya maendeleo yetu, nchi yetu na watoto wetu.
Pili, ‘tumekubali kuwa chini ya utawala wa waingereza ili kwamba, tunaweza kupata haki, elimu bora, na uhuru zaidi kuliko utawala uliopita.
Tatu, ‘Sisi na ndugu zetu walioaga dunia, tulimwaga damu zetu wakati wa vita ya dunia ili waingereza watukomboe. (Wakati wa vita kuu ya kwanza ya dunia, wapo watanganyika waliopigana upande wa Ujerumani na wengine upande wa Uingereza).

Serikali iliona wazi hasira za watumishi, na kama mpango huo ungetekelezwa, damu ingemwagika. Hata hivyo, Martin Kayamba alianza kupata wasiwasi juu ya waafrika wenzake. Aliona waafrika wanavyotaabika na hatima yao inavyoendelea kuwa hatarini. Leo, hatima ya wapinzani wa serikali ipo hatarini.
Ndipo ilipofika mwezi machi,1922, kayamba akaanzisha chama cha wafanyakazi kilichoitwa Tanganyika Territory African Civil Servants Association (TTACSA), hiki ndicho chama cha kwanza cha kutetea wafanyakazi kwenye kurasa za historia ya Tanganyika. TTACSA ililenga kuwainua watanganyika wa kiafrika. Wanachama wake walikuwa watumishu wa umma, wasomi waliojifunza lugha ya kiimgereza, pamoja na wasio wasomi. Katika jengo la chama kulitolewa elimu ya kiingereza, jiografia na historia. Lengo la kufundisha masomo hayo ni kuwawezesha watanganyika waweze kwenda sambamba na mabadiliko ya nyakati.

Kayamba alihimiza sana umoja huku akiinadi kauli mbiu aliyobuni; ‘Umoja ni Nguvu’, kauli mbiu iliyotumiwa na vyama vyote vya kiharakati vilivyofuata hadi hii leo. Kulikuwa na michezo ndani ya TTACSA ili kuvutia vijana wadogo kushiriki shughuli za chama. Matawi ya chama yalifunguliwa sehemu mbalimbali ndani ya Tanganyika, kuanzia Pangani, Tukuyu na Dar es Salaam. Mwaka 1924, huko mjini Bukuba, kulifunguliwa chama kilichoitwa Bukoba-Bahaya Union kama muendelezo wa TTACSA. Tawi la TTACSA la mjini Dar es Salaam, lilifunguliwa na Mwalimu Cecil Matola, mtu maarufu mwenye ushawishi mkubwa kwa watumishi wa umma ndani ya Dar es Salaam. Cecil Matola, mwalimu wa shule ya serikali ya Dar es Salaam, msomi wa misheni ya Kiungani, Fundi selemala wa zamami katika mashamba ya chai huko Kenya, mtu wa ukoo wa kichifu wa kabila la Uyao,Ndiye aliyekuja kuanzisha chama cha African Union (AA) mnamo mwaka 1929. Wanachama wengi wa TTACSA, akiwamo Cecil Matola waliamua kuanzisha chama cha AA, baada ya kukubali wazo la Rawson Watt, aliyetokea Mombasa, Kenya. Martin Kayamba alibaki na TTACSA yake hadi mwaka 1945, kama chama cha kutetea wafanyakazi.

Huko Dar es salaam, chama cha AA, pamoja nakufanya harakati kadhaa, lakini zaidi kilikuwa ni chama cha ‘wala bata wa mjini’. Ingawa Katiba ya AA ilikataa ubaguzi na kutaka waafrika wote waungane, lakini kimatendo kilibaki kuwa chama cha wanaojiweza kiuchumi. Watu wa hali ya chini walikuwa watumishi wa kwenye shughuli za chama, kufanya usafi, kugawa vinywaji kwa wakubwa, na kuwakuna videvu. Ada ya kiingilio na ada ya mwaka zilikuwa kubwa, na za kiwango tofauti. Viongozi walilipa shilingi ishirini kwa mwaka, wanachama wengine wenye nguvu shilingi kumi, na wanachama wanyonge shilingi tano. Wakati huo zilikuwa ni fedha nyingi.

Kama ilivyo CCM ya awamu ya tano, chama cha AA hakikuangaika na maslahi ya watanganyika. Mara moja viongizi wao waliwahi kuomba kuongezewa mshahara ili wafanane na mishahara wahindi, lakini Gavana Donald Cameron akawatolea nje, hawakupambana zaidi. Enzi hizo mishahara mikubwa wanakula wazungu, mishahara ya kati wanakula wahindi halafu waafrika wanafikiriwa, hata kama kazi zinafanana. Na ilipotokea fursa ya kuongeza elimu walianza wazungu, kisha wahindi haalfu waafrika wanafikiriwa. Hata hivyo, bado waafrika hao waliokuwa serikalini walijiona bora kuliko waafrika wengi waliokuwa wakivuja jasho mjini. Walikuwa wamefungwa minyororo ya dhahabu. Je! Vijana wa CCM hawafanyi haya haya leo hii?

Ukiacha mishahara, makazi ya watu yaligawanywa pia. Serikali ilitenga eneo jipya la Kariakoo kuwa makazi mapya ya waafrika, pamoja na Ilala. Wahindi walitakiwa kukaa Upanga na Kisutu, huku wazungu wakikaa Masaki na Oysterbay. Ole wako mswahili ukutwe masaki nyakati za jioni ukizurura. Sheria ya uzururaji iliwaathiri wavuja jasho wengi waliokuwa wakizunguka usiku na mchana kutafuta riziki huku na kule, kitu ambacho Rais Magufuli alitaka kukirudisha.
Miaka ya 1930 – 1939, ilitawaliwa na makundi makubwa mawili ndani ya chama cha AA, ambayo uhasimu wao uliongezeka baada ya kifo cha mwanzilishi na Rais wa kwanza wa AA, Mwalimu Matola aliyefariki Machi, 1931. Kundi moja lilitaka kufanya chama kiwe cha wanyonge, leo kuna wajamaa uchwara ndani ya CCM. Kundi la pili lilitaka chama kiwe cha watu wenye hadhi. Hawa wa kundi la pili, walikuwa na kauli yao kwamba; “Ni vizuri kusaidiana kwenye misiba na mazishi, lakini si kwa fedha za chama”. Leo tuna CCM ya awamu ya tano inayokula fedha za rambirambi.Mambo yanajirudia.

Hilo kundi la pili ndio lilikuwa la viongozi, wengi wao wakiwa wafanyakazi lakini pia wafanyabiashara na watu maarufu na wenye ushawishi mjini, ‘watu hatari’. Mathalani, Zibe Kidasi, huyu aliwahi kuwa kiongozi wa jumuai iliyoitwa ‘Beni Ngoma’ wakati wa utawala wa kijerumani. Beni ngoma iligawanyika katika makundi mawili hasimu, kundi la Arinoti na Marini. Makundi haya yalijihusisha na shughuli mbalimbali za kijmii kama burudani, lakini pia uhalifu. Makundi yote mawili, Arinoti na Marini yalimiliki vikosi vya kijeshi. Zibe Kidasi alikuwa Brigedia Jenerali wa kundi la Arinoti, na katika serikali alikuwa mhariri - mhakiki wa nyaraka za serikali. Mtu mwingine ‘hatari’ alikuwa makamu wa Rais wa kwanza, Mzaramo Ramadhani Ali, aliyewahi kuwa Rais wa kundi la Marini kundi hasimu la Arinoti. Ramadhan, mfanyabiashara maarufu na ‘Alwatan wa mjini’, alikuja kuwa Rais wa ‘Wazaramo Union’. Hawa ni mfano wa vingozi wa makundi ya kihalifu waliojazana kwenye serikali ya awamu ya tano, wakitumia nafasi zao kuendeleza uhalifu wao, huku wakimsifia Rais na kuonea wapinzani ili kulinda nafasi zao serikalini.

Kulikuwa pia na maveterani wa vita ya kuu ya dunia, akina Kleist Sykes, katibu mkuu wa kwanza wa chama. Alikuwapo Mzee Sudi, huyu alikuwa mweka hazina wa chama. Pamoja na wazazi wake kuwa watumwa waliotoka Congo enzi za biashara ya utumwa, lakini yeye alijiinua na kuwa mfanyabiashara mkubwa mjini, akimiliki nyumba kadhaa.
Vuguvugu la kutafuta uhuru lilianza miaka ya 1950, baada ya kusikia tetesi kutoka baraza la umoja wa mataifa lilosimamamia makoloni yalipo chini ya uangalizi maalum, Tanganyika ikiwemo. Makoloni mengine yalikuwa Cameroon, Palestina, Western Togo, Samoa, New Guinea, Ruanda – Urundi (Rwanda na Burundi), Somaliland. Funufnu hizo zilimfikia mwalimu mmoja, mwanaharkati, msomi wa elimu ya magharibi aliyekuwa akifundisha shule ya misheni ya Pugu, aliyeitwa Julius Kambarage Nyerere. Hata hivyo kazi haikuwa nyepesi. Mwaka 1954, Nyerere na wenzake walikibadili chama cha TAA (AA ya zamani) na kuwa TANU na kuanza rasmi harakati za kupigania uhuru.

Serikali ya kikoloni ilifanya kila jitihada za kukabiliana vuguvugu la kisiasa lilokuwa likisambaa kote Tanganyika mithili ya moto wa msituni. Jitihda hizo zilikuwa ni pamoja na kukitangaza chama cha UTP (United Tanganyika Party) kilichokuwa kikiongozwa na wazungu. Serikali iliitangaza UTP kama chama cha wote, kisichojali matabaka ya rangi wala ukabila. Pia serikali iliweka sheria ngumu za kuwazuia watumishi wa umma kujihusisha na TANU, walipiga marufuku matendo au maneno yenye lengo la kukosoa serikali.

Mwaka 1957, serikali ilimzuia Nyerere kufanya mikutano ya hadhara. Hatahivyo zuio hilo liliondolewa baada ya kipindi kidogo kwa sababu ya ziara ya umoja wa mataifa (UNO) nchini Tanganyika. Serikali ya Magufuli ilipiga marufuku mikutano ya kisiasa, kwa namna ileile iliyofanywa na wakoloni. Wakati wakolini walimuhofia Nyerere, Serikali ya Magufuli inawahofia wapinzani. Ilifika wakati, waingereza waliomba serikali ya Marekani isimruhusu Nyerere atmbee nje ya jengo la makao makuu ya Umoja wa Mataifa kwa zaidi ya masaa 24, wakihofia Nyerere anaweza kupanga mapinduzi akiwa Marekani. Haitoshi, serikali ililazimisha chuo cha Mt. Francis kimfukuze kazi Nyerere, lakini Nyerere kabla ya kufukuzwa akaamua kuepusha shari kwa waajiri wake dhidi ya Serikali ya wakolini, akaacha kazi kwa hiari.

Gavana Edward Twining aliyekuwa kiongozi wa serikali ya Tanganyika alikuwa akimchukia mno Nyerere. Kama leo, Magufuli anavyowachukia viongozi wa upinzani. Edward Twinning alimuita Nyerere ‘gaidi’,mbaguzi wa rangi, na mroho wa madaraka. Hata hivyo Nyerere alikazia kwamba ‘hatupambani na watu weupe’ bali tunapambana na ukoloni. Na kwa itikadi hiyo, alipata marafiki ‘wazungu’ waliomsaidia, akiwamo Marion the Lady Chesham. Gavana Twinning alifanya kila mbinu ya kumlazimisha Nyerere aanze mapambano ya vurugu ili apate sababu ya kuungwa mkono kimataifa. Aliwabambikizia kesi viongozi wa TANU, akiwamo Nyerere aliyefunguliwa kesi ya ugaidi. Lengo likiwa ni kuwajaza hasira viongozi wa TANU ili wahamasishe vurugu, waonekane ni waasi. Leo, serikali ya magufuli inafanya kila mbinu kuwajaza hasira viongozi wa vyama vya upinzani kama mtego wa kutaka kuwaingiza kwenye kufanya vurugu.

Viongozi wa upinzani, wakiziruhusu hasira zao ziwafanye wachochee vurugu, vyombo vya dola vinaweza kufanya mauaji ya Raia, halafu Magufuli atapata sababu ya kuwafungulia kesi viongozi wa upinzani. Je! Haya hayatokei leo?
Wakuu wa wilaya wakati wa ukoloni, kama ilivyo hawa wa leo, walikuwa wakiwapelekea mahakamani ‘machifu’ (viongozi wa kijamii) waliounga mkono juhudi za TANU kwa sababu za kupika. Lakini wapi, serikali ya kikoloni ilishindwa. Katika chaguzi mkuu wa Agosti 1960, TANU ilishinda viti 70 kati ya 71 vya baraza la uwakilishi/Bunge.

Wanasema, Historia haiwezi kubadilika, inaweza kurekebishwa. Matendo ya serikali ya awamu ya tano dhidi ya vyama vya upinzani yanatia kinyaa. Ni kama vile kuna matabaka miongoni mwetu kama ilivyokuwa wakati wa ukoloni. Serikali imewekeza nguvu nyingi kwenye kulinda madaraka kuliko kujenga nchi ya watu wenye umoja na mshikamano, misingi tuliyowekewa na baba wa taifa. Serikali inatumia nguvu kubwa kugawa wananchi na kuondoa uzalendo. Matokeo yake ni kujenga jamiiya watu wasio na muda wa kufikiria hatima ya nchi. Watu wasioona haja ya kuitetea nchi yao ndani na nje, watu wepesi, wasioona vigumu kuisaliti nchi kwenye nyakati ngumu kwa sababu uhuru wao wa kisiasa unaibwa na serikali. Nawasilisha.
 
Mkuu asante maana umenikumbusha mbali enzi nipo O' Level nasoma na yule kijana mzee wa Lumumba, Kifupi Jiwe hawezi kuyajua haya sabb wakati huo alikuwa kwao
 
Very well documented.

Ukoloni ni falsafa, fikra na matendo, na wala siyo rangi. Hata kama ni raia wa Tanzania, mweusi tii, halafu unafanya waliyoyafanya waingereza wakati wa ukoloni, wewe ni mkoloni. Huna tofauti na wakoloni wote waliotangulia.

Baba na babu zetu walipigana kuuondoa ukoloni wa mtu mweupe barani Afrika. Sisi tuna wajibu mkubwa na mgumu zaidi wa kupigana na kuwaondoa wakoloni wa sasa, ambao ni weusi wenzetu.
 
Aisee nimejitahidi nimemaliza kuisoma natamani Magufuli nayeye angeisoma na wale magavana wake akina Bashite.

Mungu akubariki mleta uzi
 
Hongera sana Mkuu Dizzo, nimefarijika sana kumbe wenye akili bado wapo nchi hii. Hili andiko nimelichukua nitalihifadhi kwa rejea zangu za baadaye. umeroa darsa zuri sana. Umeichambua vizuri sana awamu ya 5 ya Magufuli, kwa muktadha wa kihistoria. Hongera sana!!
 
Maneno Mazito sana haya.

"Matendo ya serikali ya awamu ya tano dhidi ya vyama vya upinzani yanatia kinyaa. Ni kama vile kuna matabaka miongoni mwetu kama ilivyokuwa wakati wa ukoloni. Serikali imewekeza nguvu nyingi kwenye kulinda madaraka kuliko kujenga nchi ya watu wenye umoja na mshikamano, misingi tuliyowekewa na baba wa taifa. Serikali inatumia nguvu kubwa kugawa wananchi na kuondoa uzalendo. Matokeo yake ni kujenga jamiiya watu wasio na muda wa kufikiria hatima ya nchi. Watu wasioona haja ya kuitetea nchi yao ndani na nje, watu wepesi, wasioona vigumu kuisaliti nchi kwenye nyakati ngumu kwa sababu uhuru wao wa kisiasa unaibwa na serikali"
 
Back
Top Bottom