Ya Mungu mengi ila Dunia ina mengi pia

wao ni wao

JF-Expert Member
Dec 23, 2022
1,181
2,771
Ndugu habari,

Tarehe 17/3 nilikuwa nchini Tanzania mkoani Dar es Salaam nilikokuja kuweka mambo sawa ili tarehe 18/3 niondoke kwenda Afrika kusini kwenye matibabu.

Ila hii tarehe nilishinda nyumbani kwa wazazi wangu wa kunizaa walipojenga kwa maana mimi sina nyumba hapa mjini.

Nilishinda ndani nikikumbuka mambo mengi ya hii tarehe ikiambatana na huzuni na furaha ila pia kuna muda nilitamani kucheka pekee yangu.

Hapa nyumbani nilikuwa na dada yangu aliyekuwa ananitake care mdogo wake, ila aliona hali niliyonayo akawa anasema mbona kama hauko sawa mdogo wangu au ndiyo unamkumbuka mzee?

Nikawa nacheka nasema hapana niko sawa dada, mara anitanie au ndiyo unataka kuniacha pekee yangu duniani?

Hili swali alilirudia mara tatu katika siku nzima tuliyospend wote hapa nyumbani kwa wazazi wetu walipojenga kabla hawajaitwa kwa Muumba.

Ila kiukweli hii siku nilikuwa na huzuni sababu nilipata bahati ya kuahidiwa mengi na Bwana yule na pia nilimtumainia ila akanirusha, hivyo ilikuwa siku ya mategemeo sana. Kuna muda nilisema pekee yangu yaani ingekuwa sasa hivi vyombo vya habari ni mimi tu , mwisho nikawa nacheka kicheko cha kujihurumia tu maana hali yangu kiafya sio nzuri.

Story zisiwe nyingi, Tarehe 19/04/2018 nilipokea simu mida ya jioni sana na namba ngeni ikiniuliza hivi;

Mpigaji: Hallo
Mimi: Habari
Mpigaji: Salama, naongea na mtoto wa mzee ... likatajwa jina la mzee wangu nikasema ndiyo mimi.

Akaendelea za siku, nikajibu salama akatia utani kidogo, umeacha kulewa kijana? Nikacheka kidogo nikajibu.

Mimi: Nimepunguza mzee mpaka hapo nilishatambua ni sauti ya nani na yeye pia alishajua kuwa nimemtambua ya kuwa yeye ni nani?

Mpigaji: Sasa rafiki yangu ... akataja jina langu akaendelea hivi kuna shida gani hapo kazini?

Mimi: Nikajaa kwenye line zake nikaeleza kwa kinagaubaga akasema sawa na pole sana, kwasababu kipindi hiko kulikuwa na kutoelewana kazini na mambo mengi ya ajabu ila ya kiutumishi.

Mpigaji: Ila akauliza ndugu ikiwa nitakupa cheo fulani je, utaweza kuwa muadilifu na hizo pombe kijana wangu?

Mimi: Nitaweza sana, hapo nikajikuta naanza kujitapa jinsi nilivyo na uwezo na hiyo chance ila pia nikawa naelezea kitaalamu baadhi ya mambo kuhusiana na hiyo chance.

Aliweza kunisikiliza na mwisho akawa ameniaga kwa kusema ipo siku nitatafutwa hivyo akakata simu.

Tulitumia takribani dakika kumi na tano kuzungumza na muhusika ila pia mimi muda huo wa jioni nilikuwa kidogo nimetia maji kidogo hivyo hata alivyoniahidi nafasi fulani ni pombe zilinifanya nijipambe, ila ukweli mimi sio muongeaji wala mtu wa majisifu.

Basi siku zikaenda na siku zikakata ile namba nikaisevu ila sikuacha hii habari nife nayo pekee yangu, nikampigia mke wangu nakumueleza A_Z akafurahi na kushangaa sana mimi kupigiwa simu na huyo bwana.

Nilimpigia mke wangu maana hakuwepo nyumbani alikuwa kwenye shughuli zake za kulijenga taifa huko Tunduma.

Basi kama ujuavyo sisi wanywaji na urafiki ni kitu hakiepukiki, basi haka kastory nikashare na rafiki yangu mmoja wa kitengo huko kunaitwa watu wasiojulikana.

Akafurahi sana na pia akasema siku ikipigwa simu kuwa tayari magazeti yashaambiwa kuhusu mimi itabidi nimkumbuke, nikacheka sana, nikasema usijali mimi ni ndugu yako.

Sasa bwana walisema wahenga sikio lilimponza kichwa. Uchaguzi wa 2020 mpaka unakaribia ile simu sikuwahi pigiwa mpaka ikawa inafika muda natamani nipige mwenyewe kuuliza huko kunani?

Wife akawa haishi kuniulizia vipi haujapigiwa au kuona taarifa za hiyo teuzi, nikawa nampoza kuwa usijali wakati wangu unakuja.

Ila nikajipa imani kuwa kama nimepigiwa simu kutoka lile jumba basi wananijua vyema, wacha nifanye jambo kwenye huu uchaguzi hakika siwezi angukia pua.

Doh salale, nikamshirikisha wife juu ya mimi kuutaka ubunge mkoa fulani, wife akagoma katu katu na ukizingatia yeye na mambo ya usalama anayaelewa kiasi chake akasema hiyo inaweza kusababisha ukose ile teuzi uliyoahidiwa.

Nikasema hapana lazima nifanye jambo kishingo upande wife akakubali ila akagoma kutoa hela za savings ili mimi nifanye jambo.

Hivyo nikazama benki moja mashuhuri hapa nchini nikavuta hela ya mkopo na pia nikamshirikisha jamaa yangu mmoja wa Iringa mwingi wa uwekezaji akakubali kunidhamini kwa milioni kadha wa kadha ukizingatia nilimpa ile story ya kupigiwa simu kutoka jumba kuu.

Hivyo akawa na uhakika sasa rafiki yake nimeula ni mwendo wa kusubiri tu mimi niingie huko ili aanze kutamba mwanaye niko majuu.

Mambo hayakuwa kama nilivyotaraji japo nilisapotiwa kwa maneno na historia ya mzee wangu kuwa sasa mimi ni mbunge hivyo ni mimi kuandaa kamati zangu vizuri.

Basi wajumbe hawakuwa upande wangu wala nini, walinipiga vibaya mno na hela zangu zikaenda bure ila nikasema basi haikuwa ridhiki.

Kazini watu walivyo wanafiki wakawa nikipita makoridoni ni full kujichekesha hata wale ambao mimi ni boss wao.

Wife akanisusa miezi miwili harudi home yupo zake tu kazini.

Dada yangu kipenzi naye alinikataza nikakaza shingo akawa akinipigia anasema dogo wewe jinga hivyo nikamlima block.

Ikawa ni mimi na bar, bar na mimi ukizingatia bwana mkubwa alitia mkwara mara ooh kwa wale walioacha kazi kwenda kuwania nafasi za ubunge wasijisumbue kurudi kazini, hivyo hata kazini sikwenda tena.

Kwenye vijiwe vya starehe wote wakanijua maana yakawa makazi yangu mapya ili nimalizie hela zilizobaki.

Rafiki yangu wa Iringa alinitangulizia milioni kadha wa kadha alipojua nimemwagwa basi akawa anapiga kunipa pole ila kama kuna kiasi kimebaki nimrejeshee aendeleze biashara naye nikamuona mzushi nikamlima block.

Kiukweli nilikuwa very frustrated maana kazini nako chokochoko zikaanza mara hela za kwenda kugombea nilizitoa wapi, wengine wakasema nimeiba kazini yaani tafrani ila na wivu pia.

Nilitengwa na kila mtu, tumaini pekee likawa ni kujipa imani kuwa labda ipo siku bwana yule atanipigia ili niwe kwenye ile nafasi.

Nikawa najisemea akipiga na nikawa kwenye hicho cheo wale wote wanaoninanga watanikoma maana nimechoka dharau mshenzi.

Basi muda kidogo bwana mkubwa akauruhusu watu walioacha kazi warejee kazini ila kwa mashariti kadha wa kadha, nikarejea nako nikakuta mambo si mambo. Nikavuliwa vyeo mshenzi nilivyokuwa navyo nikawa ni wa kawaida, waliokuwa ni majunior kwangu wakawa seniors wakati hata elimu hawanikaribii, ukizingatia na kazi nyingi mimi ndiye final sayer wao ila sasa sio hivyo tena.

Wiki mbili mbele nikiwa kazini nikala barua ya kunitoa mjini ikanitupa kijijini huko hata umeme hakuna ati nikawe boss wa huko.

Barua ilitoka moja kwa moja huko juu, nikaenda kishingo upande huku nasema naacha kazi siku si nyingi maana niendako ni njaa tu na shida ukizingatia na uzee huu ndiyo kwanza naishi kijijini sijawahi.

Nikatia timu kijijini nako kumbe simu sishapigwa hivyo ni mwendo wa kufuatiliwa na watoto wadogo.

Yaani purukushani tupu, wife akanisamehe, akarudi nyumbani, nikamueleza hali halisi akawa ana namna akubali yamemkuta bwana yake.

Basi nikajipanga kulipa mikopo ya benki na kujiwekeza tena mpaka muda wa kustaafu ili nikaweke maisha yangu sawa.

Uzuri hela aliyokuwa nayo wife ambayo aligoma kuitoa ili nifanye kampeni ilikuwa ni nyingi kuzidi kiasi nilichokopa benki.

Hivyo tukakubaliana ile hela nikafanye namna nimalizane na watu wa benki alafu tuanze kujiwekeza kwa savings na investiments ndogo ndogo.

Hivyo mambo yakawa hivyo kwa msaada wa wife, maana ni muelewa sana kwenye hizi nyanja na Mungu ambariki mke wangu kipenzi.

Ukweli nilimchukia jamaa sana kwa kuhisi alikuwa ananichora hakuwa na nia ya kunipa hicho cheo ila nikamsamehe.

Ila yote yaliyonikuta najua alikuwa yeye ndiye muagizaji maana sina chembe ya shaka.

Utajiuliza kwanini alipopiga simu sikuwa na wasiwasi na vipi mbona nilivyojua ni yeye kwanini sikutetereka, ni kwasababu akiwa Waziri wa Uvuvi nimekutana naye sana kwetu akija na shida zake na pia mimi kwenda kwake maana alikuwa na dada yake mmoja nilitokea kumpenda ila haikuwa ridhiki yangu akanitemea mbali.

Hivyo nilimzoea sana mpaka kuna kipindi niliwahi kula bure pale hotelini kwake Chato kipindi nimeenda Geita kwenye shughuli zangu.

Nilikula bure baada ya siku ile kumkuta dada yake aitwaye (Kabula) akiwa amekuja sijui kujua hali ya maendeleo ya hoteli, hivyo hakuwa mgeni na mimi aliishia kusema muhudumie mgeni wangu yule.

Hivyo nilikula chakula ila badaye nikahitaji nimkule huyo dada mtu ila akanikatalia kata kata hivyo nilimaliza nikaondoka zangu.

Ile namba ninayo, mara ya mwisho niliipiga makusudi mwezi wa kumi na mbili ikapokelewa, nikakata sasa sijui watanitafuta japo siwaogopi. Mwenyewe nishajichokea sasa, sina cha kupoteza hata wakinipeleka popote labda wajiongezee gharama za mazishi siku zijazo.

All in all keep resting, bwana wewe ungenipa cheo leo sipo hapa jukwaani niko zangu mitaa fulani nakula kiyoyozi huku namtabiria Yanga apigwe.
 
mbona husomeki mkuu?Sasa Kama kazi unayo unashindwa kukaa kwenye kiyoyozi ucheki gem?
Mzee kiyoyozi naweza kukaa kwangu na kwetu kote hakuna shida .

Ila raha niwe najua mimi ni mtu mwenye cheo fulani ambacho mkianza kulialia kuhusu nchi yetu lazima mnitaje basi hapo ndiyo furaha ya mimi kuwa kwenye kiyoyozi sio sasa kiyoyozi napata ila nikiwa na vyeo mshenzi .

Isitoshe sipo bongo kwa sasa nipo kwenye matibabu kwa madiba na siruhusiwi kupata kiyoyozi kutokana na hali ya gonjwa langu .
 
Halafu we mlevi mi mlevi mwenzio kama nakujua, japo hatujuani.
Kama ni wale wakuingia ofisini na simu unakabidhi mapokezi basi hakika unanijua maana hao ndiyo nilikuwa nalewa nao na bado nalewa nao .

Au una biashara kubwa kubwa kama akina Glenn namjua nje ndani japo hanijui ila mbali na hapo umenifananisha mkuu
 
Kama ni wale wakuingia ofisini na simu unakabidhi mapokezi basi hakika unanijua maana hao ndiyo nilikuwa nalewa nao na bado nalewa nao .

Au una biashara kubwa kubwa kama akina Glenn namjua nje ndani japo hanijui ila mbali na hapo umenifananisha mkuu
Bila shaka Mkuu!....Nimekufananisha.
 
Back
Top Bottom