Habari
Waziri, Bodi watishiana
Mary Victor
Toleo la
273
19 Dec 2012
- Ni kuhusu TBS, maagizo yatolewa Dk. Kigoda aburuzwe kortini
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda anatuhumiwa kuibeba na hatimaye kushinikiza ipatiwe kazi ya kufanya ukaguzi wa magari nje ya nchi kampuni ambayo Bodi ya Shirika la Viwango nchini (TBS) iliikataa kwa sababu ya kutokidhi masharti na vigezo vya zabuni, Raia Mwema, limebaini.
Kutokana na hali hiyo, Bodi ya TBS imeiagiza menejimenti ya shirika hilo kumfikisha waziri huyo katika Mahakama ya Biashara, ili pamoja na mambo mengine, Mahakama hiyo ibatilishe uamuzi wa Dk. Kigoda unaodaiwa kuingilia mchakato wa zabuni wenye lengo la kupata kampuni makini zitakazofanya kazi hiyo ya ukaguzi wa magari yanayoingizwa nchini kutoka nchi za nje.
Kwa mujibu wa habari tulizonazo, kampuni ambayo Dk. Kigoda anadaiwa kuishinikiza Bodi ya TBS iipatie kazi ya ukaguzi wa magari nje ya nchi imetajwa kwa jina la W.T.M ambayo Agosti mwaka huu, ilisimamishwa na Bodi ya TBS kuendelea na majukumu yake ya ukaguzi.
Kati ya sababu za kuisimamisha kampuni kuendelea na majukumu yake ni pamoja na tuhuma zilizosababisha aliyekuwa Mkurugenzi wa TBS, Charles Ekerege, kusimamishwa kazi na pia kutokuwa na ufanisi katika utekelezaji na usimamiaji wa majukumu yake hayo.
Habari za uhakika kutoka ndani ya TBS zinasema uongozi wa Bodi ya Shirika hilo, umegomea shinikizo hilo la Waziri Dk. Kigoda kwa kuipatia kazi kampuni hiyo nje ya utaratibu wa zabuni, hali ambayo imeilazimu Bodi kuitaka menejimenti ya TBS kumfungulia mashitaka waziri katika Mahakama ya Biashara ili pamoja na mambo mengine iweze kutengua shinikizo hilo la waziri.
Vyanzo kadhaa vya habari hizi, vimeeleza kwamba uamuzi huo wa Dk. Kigoda umetokana na mambo mawili. Mosi, ni uwoga wa Waziri Kigoda kwa wabunge, na pili, ni kumpa upendeleo maalumu mmiliki wa kampuni hiyo, Mtanzania, ambaye anadaiwa kuwa mtoto wa kigogo mmoja ambaye amewahi kufanya kazi ndani ya shirika hilo.
Kampuni hiyo ya W.T.M ilikuwa katika orodha ya kampuni ambazo huko nyuma, chini ya Mkurugenzi Ekerege, zilipewa kazi ya kukagua magari nje ya nchi kabla ya kuyasafirisha kuja nchini, kama moja ya njia ya kudhibiti nchi kugeuzwa dampo la magari mabovu.
Hata hivyo, kampuni hiyo na baadhi ya nyingine, zinadaiwa kufanya kazi chini ya ufanisi, huku nyingine zikidaiwa kuwa kampuni hewa, na hivyo kulisababishia hasara kubwa shirika hilo, hali iliyoamsha mjadala mzito bungeni ambao ulisababisha kusimamishwa kwa Ekelege ili kupisha uchunguzi wa suala hilo.
Sakata hilo la kuwapo kampuni hewa na zinazofanya kazi ya ukaguzi wa magari chini ya ufanisi, ndiko kulikosababisha kung'olewa pia kwa aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami, na badala yake Rais Jakaya Kikwete kumteua Waziri Kigoda katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri aliyoyafanya Mei, mwaka huu.
Kaimu Mkurugenzi wa TBS, Dominic Mwakangale, amethibitisha kuwapo kwa mgangano huo wa uamuzi kati ya Dk. Kigoda, Bodi ya TBS na Menejimenti yake.
Aidha, Mwakangale ambaye pia ni Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora ndani ya TBS, alikiri kupokea agizo la Bodi ya TBS, la kuitaka Menejimenti yake kumshtaki Dk. Kigoda katika Mahakama ya Biashara.
"Hatujakataa kutii agizo la Bodi (la kumfikisha Dk Kigoda katika Mahakama ya Biashara). Tulipopokea agizo lile tulimpelekea mwanasheria wetu, kwa hiyo hadi sasa hatujapata ushauri wake, na tunasubiri," alisema Mwakangale.
Raia Mwema lilifanya juhudi za kumtafuta Waziri Kigoda, ili pamoja na mambo mengine aweze kutoa ufafanuzi juu ya tuhuma hizo.
Juhudi hizo za kumpata Dk. Kigoda kwa njia ya simu yake ya mkononi zilifanikiwa juzi Jumatatu, baada ya ujumbe mfupi aliokuwa ametumiwa wiki iliyopita kuonyesha kwamba umemfikia.
Baada ya kupokea ujumbe wetu, Dk Kigoda aliomba apewe dakika tano mbele ili kutolea ufafanuzi suala hilo. Hata hivyo, Dk Kigoda hakuweza kujibu lolote hata baada ya dakika 30, na alipopigiwa na mwandishi wetu kumkumbusha juu ya ahadi yake hiyo, aliomba apewe muda zaidi akisema angejibu kupitia ujumbe mfupi wa simu yake ya mkononi.
"Naomba nikujibu baada ya dakika tano, nitakujibu kwa ujumbe mfupi wa simu (sms),"alisema Kigoda.
Mwakangale alizitaja kampuni ambazo zilikuwa kwenye mchakato wa mwisho wa zabuni ya kuomba kazi ya ukaguzi huo wa magari nje ya nchi, kabla ya Waziri Dk. Kigoda kuingilia kati na kushinikiza iingizwe pia katika orodha hiyo kampuni hiyo ya W.T.M. ni Japan Auto Appraisal- JAAI (Minato-Ku, Japan), Wilna International (Tokyo, Japan), Auto Terminal Japan Ltd (Japan), East Africa Automobile Services Co. Ltd (Watanzania wenye ofisi Japan).
Jabal Kilimanjaro na Auto Elect. Mech (Sharjah, U.A.E), Serengeti Freight & Forwarders Ltd (London, Uingereza), Unit 92 Thames (Industrial Park, Princess Margaret Road, East Tilbury-Uingereza).
Akielezea kwa nini kampuni ya W.T.M, inayomilikiwa na wazalendo haikuweza kuchaguliwa na menejimenti ya TBS, Mwakangale anasema: "Yapo masuala mengi, lakini kubwa zaidi kampuni hii imeshindwa kulipa fedha TBS kwa wakati."
Kabla ya Waziri Dk. Kigoda kuagiza kampuni hiyo ya W.T.M. iingizwe katika kampuni hizo zilizopatikana katika mchakato wa mwisho, habari zinasema kampuni hiyo ndiyo iliyokata rufani kwa Waziri huyo ikilalamikia hatua hiyo ya menejimenti na Bodi ya TBS kuiondoa katika orodha ya kampuni zilizoingia hatua ya mwisho.
Mmoja wa wajumbe wa Bodi mpya ya TBS aliyezungumza na gazeti hili kuhusu sakata hilo kwa sharti la kutotajwa jina lake kutokana na sababu za wazi kabisa, anasema:
"Sisi kama Bodi ya TBS, hatukukubaliana katika suala la kuipatia kampuni yenye tuhuma (W.T.M) na tayari ilishafungiwa tangu Agosti (mwaka huu) kutokana na utendaji usioridhisha. Mbali na hilo, yapo pia masuala mengine ambayo tusingependa kuyaweka wazi yaliyomfanya Waziri (Dk. Kigoda) avunje Bodi.
"Hata hivyo, tumeiagiza menejimenti (ya TBS) ilifikishe suala la Waziri Mahakama ya Biashara. Kinachofanywa na Waziri ni kutokana na hofu ya kuwaogopa wabunge, ndiyo maana baadhi yao wanafanya uamuzi unaokinzana.
"W.T.M , ni kampuni ya Mtanzania, taarifa ambazo tunazo, ni kwamba mama wa mmiliki wa kampuni hiyo ambaye kwa sasa ni marehemu, alikuwa ni mtumishi wa TBS kwa miaka kadhaa iliyopita. Kijana huyo anapewa kazi hii kama heshima kwa marehemu mama yake mzazi.
"Hivyo basi kijana huyo ndiye aliyeanza kazi ya kukagua magari nje ya nchi hadi pale TBS ilipoamua kumsimamisha Agosti mwaka huu kutokana na ufanisi wa shughuli zake kuwa mdogo, na pia kuchelewesha malipo pamoja na masuala mengine.
"Baada ya kusimamishwa , aliamua kukata rufaa kwa Waziri , ndipo Dk. Kigoda alipoiagiza TBS kuwa mfanyabiashara huyo arudishwe kwa kutumia taratibu za zamani. Menejimenti ya TBS ilipoleta suala hili kwenye Bodi, tulilikataa kutokana na kwamba kwa sasa hatutumii taratibu hizo za zamani katika utoaji wa zabuni za Serikali.
"Kwa kuwa tayari tulishatangaza tenda (zabuni) kwa kampuni kuomba kazi hiyo, yeye (W.T.M) hakuomba, na kwa kuwa amechelewa asingeweza kuomba tena...zipo taarifa ambazo Bodi ilizipata kwamba amekuwa akitoa vyeti nchini Uingereza kwa waagizaji magari nchini pasipo magari hayo kukaguliwa.
"Yapo baadhi ya magari ya wafanyabiashara wakubwa yameingizwa nchini kwa utaratibu huo. Kwa misingi hiyo, Bodi iliona hakukuwa na sababu ya kumrudisha mtu wa namna hiyo."
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Deo Filikunjombe , alipotakiwa kuzungumza mgogoro huo mpya baina ya Waziri na Bodi ya TBS, alisema:
"W.T.M ni kampuni mbovu haifai hata kupewa kazi tena na TBS. Kwanza ni kampuni ambayo ilishafungiwa kukagua magari. Namheshimu sana Dk. Kigoda, lakini katika hili nitamshangaa sana kama anaikingia kifua kampuni yenye tuhuma lukuki kwa kushindwa kusimamia majukumu yake ipasavyo."
Dk Kigoda, mara tu baada ya kukabidhiwa wizara hiyo, alichukua hatua kadhaa, zikiwamo za kumsimamisha aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Ekelege ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake kuhusu uendeshaji wa shirika hilo. Hadi sasa, uchunguz huo bado unaendelea.
Aidha, Dk Kigoda ndiye aliyevunja iliyokuwa Bodi ya TBS, chini ya Mwenyekiti, Oliva Mhaiki. Wajumbe wengine wa Bodi hiyo na maeneo wanayowakilisha yakiwa kwenye mabano, ni pamoja na Donald Chidowu (Katiba na Sheria), Rashid Salim (Viwanda na Biashara Zanzibar), Dk Bertha Maegga (Afya na Ustawi wa Jamii), Odilo Majengo (Viwanda na Biashara) na Profesa Ntengwa Mdoe (Chuo Kikuu cha Sokoine- SUA).
Wengine ni Peter Machunde (Taasisi ya Sekta Binafsi -TPSF), Dk. Godfrey Mariki (Tume ya Ushindani wa Bidhaa-FCC), Suzy Laizer (SME's), Elpina Mlaki (Fedha na Uchumi) na George Simbachawene (Mbunge wa Kibakwe, sasa Naibu Waziri, Nishati na Madini